Mwaka Mmoja Bila Mama, Mkono wa Mungu Haujatuacha…
Nakumbuka mwezi Juni 2002, nikiwa mwanafunzi wa sekondari, eneo
ni stesheni ya gari moshi (treni) mjini Singida nikiwa ninarudi nyumbani
nikitokea Dodoma. Ilikuwa ni safari ya kuunga unga iliyoanzia Dar es Salaam kupitia
Dodoma na kisha Singida.
Wakati huo tulikuwa tunaondoka Dodoma saa nne asubuhi,
Singida tunafika saa za jioni kuanzia saa kumi na moja hivi tukiwa taabani kwa
uchovu wa kukaa kwenye mabehewa yaliyoonekana kuhangaika mno kupita kwenye
mataruma katikati ya vichaka ya Dodoma na Singida. Jioni hiyo ninayoikumbuka
vyema tulichelewa kidogo na hatimaye tulifika Singida stesheni saa kumi na
mbili unusu hivi za jioni.
Ile tu treni inafunga breki namwona mama yangu akiangaza angaza
macho kujua nilikuwa kwenye behewa lipi. Mama alikuwa amefika stesheni hapo
kunipokea. Nilifurahi kupita maelezo. Siwezi kuwa na maelezo sahihi yanayoweza
kukidhi furaha ya kulakiwa na mama baada ya kuwa mbali naye kwa muda fulani.
Mama alikuwa na tabia ya kuhakikisha anafanya mapokezi ya
nguvu kila mara aliposikia narudi nyumbani. Kilichopendeza zaidi ni jioni ya
siku ya mapokezi. Ilikuwa kawaida tumbo kustushwa na mapochopocho ya kila
namna.
Mazungumzo kwa kawaida yalikwenda mpaka usiku wa manane. Huo ndio ulikuwa wakati wa ‘sayu’, neno la Kinyaturu lenye maana ya salaam ndefu zinazofanyika watu wawili wanapokutana aghalabu baada ya kuachana kwa muda mrefu. Mama hakuwa mwongeaji kivile lakini alijua nini cha kusema.
Mazungumzo kwa kawaida yalikwenda mpaka usiku wa manane. Huo ndio ulikuwa wakati wa ‘sayu’, neno la Kinyaturu lenye maana ya salaam ndefu zinazofanyika watu wawili wanapokutana aghalabu baada ya kuachana kwa muda mrefu. Mama hakuwa mwongeaji kivile lakini alijua nini cha kusema.
Sadaka ya muda wake
Kwa kawaida, nilipofika nyumbani kuwasalimia, mara zote alinihimiza kwenda
kijijini nikamsalimie babu na bibi. Mama alikuwa ‘mtoto’ wa kwanza kwa babu
yangu. Na kwa namna fulani walimtegemea. Alijisikia furaha sana nikifunga
safari kwenda kuwasalimia wazee wale. Na mara nyingi sikusubiri anikumbushe. Najua
wazee wale, kwa sasa, wanamkosa sana.
Mama alikuwa na tabia ya kutoa sadaka ya muda wake
kuhakikisha anakuwa sababu ya furaha kwa watu wake wa karibu. Nakumbuka Mungu
aliponizawadia mtoto miaka kadhaa iliyopita, mama aliomba likizo kazini kwake
kuja kunisaidia kumtunza mke wangu kwa majuma mawili. Kwake, familia ilikuwa na
nafasi ya kwanza, mengine yalifuata. Ninamkumbuka kwa kuheshimu sana maisha ya
kifamilia.
Mwalimu asiye na cheti
Nakumbuka
matukio mengi kwenye miaka ya themanini katikati nikiwa na kati ya miaka minne
na sita. Enzi hizo watoto tuko watatu tu pale nyumbani. Ilikuwa ni kawaida mimi
na mdogo wangu anayenifuata ‘kubanana naye’ jioni kushuhudia akisonga ugali. Alituimbia
nyimbo za Sunday School zilizotufundisha maisha ya Ukristo kwa lugha ya kitoto. Baba naye,
baada ya chakula, alifanya kazi ya kutusimulia hadithi za biblia.
Nilipoanza kujifunza kuhesabu na kusoma kabla sijaanza shule,
jikoni ndiko kulikuwa mahali pa kufanyia
mazoezi ya kuhesabu. Mama alikuwa na kazi ya kuvumilia kusikiliza. Kwa hakika utoto
ulikuwa mtamu karibu na mama. Pamoja na ukweli kuwa hakuwa na elimu kubwa ya
darasani, alijitahidi kutujengea mazingira ya kujifunza.
Uandishi na kazi za
mikono
Nakumbuka miaka ya 90 mwanzoni nikiwa nasoma madarasa ya
mwanzo shule ya msingi, baba yetu alikuwa masomoni kwa miaka kadhaa. Kila
alipomwandikia baba barua, mama alinihimiza na mimi niandike barua kwa baba.
Alinifundisha kusimulia matukio ya pale nyumbani kwa maandishi. Utamu wa kuandika
barua mara kwa mara wakati mwingine ulinifanya nimkumbushe lini hasa tungemwandikia
baba barua tena. Najua Mzee Bwaya anakumbuka barua zangu.
Si elimu tu. Mama alitufundisha kufanya kazi za ndani bila
kujali jinsia. Ni kweli kwa Wanyaturu ni kama mwiko fulani hivi kwa wanaume
kuingilia kazi za wanawake. Kwetu hapakuwa na namna. Nyumbani alikuwa mwenyewe
na alihitaji msaada wa shughuli ndogo ndogo.
Mbali na kufagia, kudeki, kuosha vyombo, mimi na mdogo wangu
wa kiume anayenifuata, Fortunatus, tulikuwa na jukumu la kuteka maji kwa kutumia
toroli. Mama alikuwa na namna yake ya kutufanya tujisikie fahari kufanya kazi
hizo. Na kweli ni kama tulishindana na mdogo wangu kusukuma toroli kwa lengo la
kutafuta ‘ujiko’ kwa mama. Leo hii sioni shida kufanya kazi zinazoonekana kuwa
ni za kike kwa sababu ya mama.
Kunyenyekea
Mama hakuwa mkamilifu lakini alijitahidi kuishi Ukristo. Hakuwa
mchoyo wa msamaha tulipomkosea na alipogundua amekosea hakusita kuomba msamaha.
Hapa ninakumbuka kisa kimoja.
Siku moja, nikiwa kidato cha tatu, nimerudi nyumbani nikakuta
baadhi ya nakala za gazeti la Rai zilizokuwa zimehifadhiwa kwa kumbukumbu zimenyofolewa
baadhi ya kurasa zake. Baba yetu ni mtunzaji mzuri wa magazeti ya zamani na
vitabu. Ametufundisha kwa vitendo kuheshimu maandishi labda kwa sababu ya ualimu
wake.
Basi. Baadae nikagundua aliyechana magazeti hayo ni mama.
Aliyatumia kuwafungia zawadi wageni wake akijua hatuyahitaji tena. Hakujua kuwa
wakati mwingine huwa tunasoma magazeti ya mwaka uliopita.
“Sasa umefanya nini mama?” niliuliza kwa mchanganyiko wa hasira na
wasiwasi wa kuogopa kumkwaza. Alikuwa mpole mpaka mtu unaogopa kumchokoza. Uzuri
alijua namna ya kushughulika na mtu aliyekasirika.
“Sifee ougansamehe he
baba wane!” aliniomba msamaha kwa Kinyaturu.
Kweli kauli kama hizi zenye ubinadamu hunifanya nimkumbuke mara nyingi sana. Sana. Na sababu kubwa ni vile alivyojua kutumia maneno ya Kinyaturu kuwasilisha ujumbe muhimu kila tulipowasiliana. Alipenda kuniita Sife, jina langu la ukoo. Sife ni jina la babu yangu aliyemzaa bibi upande wa mama. Kwake, ilikuwa ni heshima kunitambua kama babu yake mzaa mama.
Kweli kauli kama hizi zenye ubinadamu hunifanya nimkumbuke mara nyingi sana. Sana. Na sababu kubwa ni vile alivyojua kutumia maneno ya Kinyaturu kuwasilisha ujumbe muhimu kila tulipowasiliana. Alipenda kuniita Sife, jina langu la ukoo. Sife ni jina la babu yangu aliyemzaa bibi upande wa mama. Kwake, ilikuwa ni heshima kunitambua kama babu yake mzaa mama.
Mazungumzo ya mwisho
Jumamosi ya terehe 3 Oktoba, 2015 alinipigia simu jioni.
Alikuwa akinitakia heri nikijiandaa kutetea tasnifu yangu siku ya Ijumaa ya
Oktoba 9, 2015 Chuoni Mlimani.
Nakumbuka kauli yake kwangu, “Mungu amekusaidia sana baba yangu na mpaka
hapo ameshakufikisha mbali sana. Mimi najua Mungu ana kusudi na wewe babu…na
hata kwa wadogo zako umekuwa mfano mzuri!” Alikuwa na matarajio makubwa
sana kwangu na kwa kweli alikuwa sehemu ya motisha ya mengi niliyoyafanya.
“Unajua mama mmenisaidia s’saana kutimiza ndoto zangu nyingi.
Sasa ni zamu yangu.” alicheka aliposikia hivyo. Sikujua nilisema kisichowezekana.
Mazungumzo ya Jumamosi hiyo ndiyo yalikuwa ya mwisho.
Siku kama ya leo mwaka jana
Alituacha usiku wa Jumanne tarehe 6 Oktoba, 2015 akiwa
amelazwa kwa masaa matatu tu katika Hospitali ya Mkoa wa Singida. Mungu
alimchukua masaa machache baada ya kutapika na kuishiwa nguvu akiwa kazini
akiwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu waliokuwa wakilelewa
katika kituo kimoja mjini Singida. Mungu peke yake anajua kwa nini aliamua
kumchukua katika kipindi hiki tulipokuwa tunamhitaji sana.
Umepita mwaka mmoja lakini haikuwa rahisi kukubaliana na
ukweli kwamba ametuacha. Namshukuru Mungu, hata hivyo, kwa kutupitisha katika
kipindi hiki kigumu cha mwaka mzima bila mama. Haikuwa rahisi lakini Mungu
amekuwa faraja yetu. Mwaka mmoja bila mama, bado mkono wa Mungu haujatuacha. Hata sasa Mungu ametusaidia.
Kaka Bwaya [Christian], Mungu ni faraja pekee na iliyo kuu kwa wanadamu wote. Umenikumbusha miaka 16 iliyopita nilipompoteza pia mama yangu kipenzi. Hakika, kuna mama mmoja tu na huyo akiondoka basi. Tumaini la pekee ni kuwa tunaye BABA MFARIJI wa wote. Barikiwa sana
JibuFutaAsante sana ndugu Noverty kwa maneno mazito. Mungu ni faraja yetu.
JibuFutaMungu azidi kuwafariji na kuwapa neema ya kuishi katika ile misingi ambayo mama aliwajengea
JibuFutaMaoni haya yameondolewa na mwandishi.
JibuFutaAsante sana Monica kwa maneno ya faraja. Mungu ni mwema.
JibuFutaMungu ni mwema
JibuFuta