Wajibu wa Mzazi Kama Mwalimu wa Kwanza wa Mtoto
Tafiti nyingi za
mazingira ya kujifunzia zimeendelea kusisitiza kuwa elimu bora kwa mtoto huanzia
nyumbani. Kuwepo kwa mazingira rafiki ya kielimu nyumbani kunampa mtoto nafasi ya
kukua kiufahamu na humuandaa vyema kujifunza
kabla hajaanza shule rasmi.
Kimsingi, mzazi ndiye mwalimu
wa kwanza anayemwezesha mtoto kujifunza vizuri. Mtoto hujifunza kutembea, kuongea,
kujilisha, kazi za nyumbani na kadhalika kwa msaada wa mzazi. Ikiwa mzazi atatambua
wajibu wake kama mwalimu wa mtoto na akautekeleza ipasavyo, kazi ya mwalimu shuleni
hurahisishwa.
Tutazame maeneo manne
muhimu yanayoweza kukusaidia wewe kama mzazi kutekeleza wajibu wako kama
mwalimu wa mwanao katika mazingira ya hapo hapo nyumbani.
Mfatufie vifaa vya kujifunzia
Mtoto anahitaji kuchangamshwa
kiakili, kimwili, kihisia na kimahusiano tangu anapozaliwa. Anapochangamshwa
mapema, ufahamu wake hujiweka tayari kujifunza hata kabla hajakutana na mwalimu
wake shuleni.
Ili aweze kuchangamshwa
ipasavyo, anahitaji vifaa muhimu vya kujifunzia. Kwa mfano, unaweza kuhakikisha
mtoto anapata rangi na penseli za kuchorea, makaratasi na madaftari ya
kuandikia, CD/DVD za katuni na hadithi mbalimbali, majarida na vitabu vya
watoto, kamba za kuruka, vizibo/vifaa vya kuhesabia pamoja na vifaa vingine
anavyoweza kuvitumia kuifanya akili yake ijifunze ubunifu.
Wazazi wengi, hasa wa
mijini, hutumia fedha nyingi kuwanunulia watoto vifaa vilivyotengenezwa tayari
kama ‘magari’, mipira, ‘ndege’, ‘simu’, ‘samani za nyumba’ na kadhalika. Hata
hivyo, vifaa hivi vina hatari ya kumnyima mtoto fursa ya kukuza ubunifu na kupata
ujuzi wa kutengeneza vitu vinavyoendana na mahitaji yake.
Mletee malighafi rahisi
kama maboksi, mkasi na gundi yatakayomsaidia kutengeneza vitu halisi anavyovihitaji.
Kwa kufanya hivi, mtoto hukuza uwezo wa kufikiri na kuhalisisha kile
anachokifikiri.
Mtoto akijifunza kuandika. Picha @Jielewe |
Mjengee hamasa ya kujielimisha
Hamasa ni nguvu
inayomsukuma mtu kuwa tayari kuweka juhudi katika kutimiza malengo
aliyojipangia. Mzazi, kama mwalimu wa kwanza wa mtoto, unao wajibu wa kumjengea
mwanao hamasa kubwa ya kutaka kujifunza.
Kwa mfano, ili kukuza
hamasa yake, waweza kumjenga kisaikolojia aweze kuamini kuwa anao uwezo na anaweza.
Imani kuwa anaweza ni muhimu sana na itakuwa nguzo yake anapojifunza.
Waweza pia kumpa mifano
ya namna elimu na maarifa vinavyoweza kumsaidia mtu kutatua matatizo
yanayomkabili. Mwonesha fursa zilizoko mbele yake kwa kuzihusianisha na
mafanikio yake darasani. Mpe mifano ya wanasayansi maarufu waliogundua mambo
makubwa yaliyobadili maisha ya watu.
Msimulie habari za
wanasheria maarufu watetezi wa haki za watu wanyonge, madaktari wanaookoa
maisha ya watu, walimu, wabunifu wa majengo maarufu, mainjinia wa barabara, waandishi
wa habari na kada nyinginezo. Masimulizi haya hujenga hamasa kubwa inayomwongezea
mtoto shauku ya kuelimika.
Wakati mwingine
masimulizi yanayotanguliza fedha dhidi ya maarifa yanawakatisha tamaa watoto
kujibidiisha kielimu. Ikiwa unataka mwanao apende elimu mwoneshe vile elimu
hiyo ilivyo muhimu pengine kuliko pesa.
Fuatilia maendeleo yake
Mtoto anahitaji kile
anachokifanya kitambuliwe na kimfurahishe mzazi wake. Anapojua kuwa unafuatilia
mafanikio yake, atajitahidi kujibidiisha zaidi ili aendelee kujiletea sifa. Mpe
fursa ya kujisikia fahari kwa kutambua jitihada anazofanya katika masomo.
Fanya mawasiliano na
walimu wake shuleni kujua anaendeleaje. Anapogundua unafuatilia yanayoendelea
shuleni kwake, atajua unamthamini na atahamasika kufanya utambue anavyoweza.
Ni kweli wakati
mwingine waweza kukutana na taarifa usizozipenda shuleni. Labda kiwango chake
cha kufaulu hakifanani na matarajio yako. Hakuna sababu ya kumkatia tamaa.
Badala ya kumsimanga na kumwonesha namna alivyo ‘kilaza’, onesha imani kubwa uliyo
nayo kwake. Mhakikishie unajua anavyoweza kufanya vizuri zaidi.
Kadhalika, tambua maeneo
mahususi aliyoonesha uwezo wake na ikiwezekana shiriki shughuli zake nyingine
anazozipenda. Anapoona unathamini mambo anayoyapenda hata kama si ya kitaaluma,
hatakuwa tayari kukuangusha kwa mambo anayojua unayatarajia kwake ikiwemo
taaluma.
Wakati mwingine watoto
hushindwa kufanya vizuri kwa sababu hatuwapi msaada wanaouhitaji. Jenga
utaratibu wa kumsaidia kitaaluma. Kaa nae jioni, uliza amepewa kazi gani ya
kufanya nyumbani. Mpe msaada lakini usimlemaze akawa tegemezi. Kwa kufanya
hivyo, utamfanya awe na shauku kubwa ya kukuthibitishia alivyo na uwezo.
Mzoeze kufuata ratiba ya siku
Familia nyingi hazina
mazingira yanayomwezesha mtoto kujifunza kwa utulivu. Mfano ni pale watu wazima
wanaoishi na mtoto wanapotumia muda mwingi kutazama televisheni na kusikiliza
redio kwa namna inayowazuia watoto kufanya kitu kingine tofauti.
Katika mazingira
mengine, watoto hupotelea kwenye michezo mingi isiyodhibitiwa huko mitaani tena
bila uangalizi wa wazazi. Mambo haya hayawezi kumsaidia mtoto kujifunza.
Hakikisha mazingira ya nyumbani kwako yanampa mtoto fursa ya kujisomea bila
usumbufu.
Vile vile, msaidie
kupangilia mambo yake kulingana na umri. Utamaduni wa ratiba unajengwa. Anaporudi
kutoka shuleni, kwa mfano, ajue atacheza
kwa muda gani, ataoga saa ngapi, wakati upi atafanya kazi za nyumbani, kufanya
ibada ya pamoja, kusimuliwa hadithi ya kitandani na kulala.
Sambamba na ratiba isiyobadilika
badilika, fanya juhudi za kumpunguzia majukumu mengine yanayoweza kuwa kikwazo
cha kujifunza. Ingawa kushiriki kazi za mikono ni muhimu sana kwa ukuaji wa mtoto, jitahidi kutambua ni
wakati gani kazi hizi zaweza kuwa kikwazo.
Msingi wa elimu bora
hauanzii shuleni na mtoto hawezi kupenda shule hivi hivi bila juhudi zako
mzazi. Ukitimiza wajibu wako, utashangaa atakavyojifunza kwa urahisi.
Soma Jarida la Maarifa kwenye gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi. Niandikie kwa bwaya@mwecau.ac.tz
Maoni
Chapisha Maoni