Mambo ya Manne ya Kufanya Mtoto Akusikilize, Akuheshimu
Msomaji
mmoja wa safu hii aliniandikia hivi majuzi akidai mwanae hamsikilizi. Kwa
mujibu wa mzazi huyu, pamoja na kufanya jitihada za kumwelekeza mwanae mambo
muhimu ya kimaisha, bado kijana wake huyo haonekani kusikiliza. Anasema, kadri
anavyomwadhibu mwanae, ‘ndivyo anavyozidi kuwa mkaidi…’
Mzazi
huyu, inavyoonekana, amepoteza mamlaka yake kama mzazi. Mamlaka kimsingi ni
uwezo wa kusema kitu na kikasikika bila kulazimika kutoa adhabu. Unapokuwa na
mamlaka maana yake unayo nguvu ya ushawishi inayomfanya mtoto awe tayari
kukuiga, kukusikiliza, kukuelewa na kufanya kwa hiari yake yale unayomwelekeza.
Ni
ukweli ulio wazi kuwa ushawishi wa mzazi kwa mtoto wake hauji hivi hivi.
Ushawishi ni matokeo ya jitihada za muda mrefu zinazofanywa na mzazi ili kuwekeza
katika uhusiano na mwanae tangu mapema. Tutazame maeneo manne yanayoongeza
ushawishi wa mzazi kwa mtoto.
Kushiriki anayoyapenda huongeza kuaminika PICHA: Sayuni |
Kuaminika
Mamlaka
yako mzazi kwa mwanao yanategemea kiwango cha imani alichonacho kwako.
Kukuamini maana yake, kwanza, hana mashaka na nia yako njema kwake na pili, anaamni
anayo nafasi ya pekee kwako kama mzazi wake.
Kwa
kawaida, mambo madogo madogo sana ndiyo humfanya mtoto aongeze imani yake
kwako. Kwa mfano, kutumia sehemu ya muda wako kwa ajili yake kwa kufanya
mazungumzo na matembezi naye, kufurahia yale mema yanayomgusa zaidi, humfanya
mtoto akuamini. Kuaminika kunakwenda sambamba na vile unavyoonesha kumthamini
kama mtu anayestahili heshima.
Msimamo usioyumba
Hakuna
kitu kibaya kama kutokueleweka unataka nini. Kutokueleweka kunakotokana na
kubadilika badilika, kunatuma ujumbe mbaya kuwa huna uhakika na usahihi wa kile
unachokidai kwake. Hali hii ya kutokutabirika kwako humfanya atake kuendelea
kujaribu bahati yake kwa sababu tayari ana wasiwasi na mamlaka yako kama
wazazi.
Ili
kujihakikishia mamlaka ni muhimu kuwa na msimamo wa pamoja na mzazi mwenzako.
Kupingana wazi wazi na msimamo na maamuzi ya mzazi mwenzako mbele ya mwanao huwapunguzia
mamlaka yenu kama wazazi na ni kutengeneza mazingira ya kujaribiwa kwa mamlaka
yenu mara kwa mara.
Kuishi unayoyasema
Mtoto
hujifunza zaidi kwa yale unayoyafanya kama mzazi kuliko yale unayoyasema.
Mamlaka yako kama mzazi yanategemea na namna maneno yako yanavyooana na yale unayoyafanya.
Mtoto anapokuona ukifanya yale yale unayomzuia yeye anakupunguzia alama za
ushawishi wako kwake.
Hakikisha
unaishi maneno yako. Tenda unayoyasisitiza. Unapomwambia ashukuru anapopewa
kitu, kuwa mfano kwa kuwa mtu wa shukrani. Unaposisitiza aombe msamaha, jitahidi
kuonesha mfano kwa kuomba msamaha pale unapojikwaa.
Mstahi anapokosea
Unafanya
nini pale unapogundua mwanao amekosea? Unamkemea kwa ghadhabu tu kwa sababu ni
mtoto? Ni vizuri kuelewa kuwa watoto, kama sisi tulio watu wazima, wanatamani
sana kutendewa kwa staha. Unapomtendea kwa staha unamfanya ajione analo deni la
kukulipa heshima unayostahili.
Hakuna
sababu ya kumkemea mtoto kupita kiasi hata kama unajua ni kweli amekosea.
Hakuna sababu ya kumvunjia heshima kwa kumdhalilisha mbele ya rafiki zake.
Unapofanya hivyo, ni rahisi kujenga kisasi cha utoto. Usipomstahi mwanao,
unapoteza mamlaka yako kwake.
Kwa
ujumla, mamlaka yako kama mzazi ni zao la maisha yako yanayohalalisha
kusikilizwa. Ukijenga uhalali kama mzazi, hutalazimika tumia nguvu nyingi
kutafuta ushiwishi kwa mwanao.
Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamis kwa makala kama hizi. Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz
Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFutaChapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFuta