Mambo Matano Yanayoweza Kukusaidia Kupata Muda wa Kuwa Karibu na Mtoto

Wazazi wengi wanapenda kuwa karibu na watoto  kwa lengo la kuwajengea mazingira ya kujifunza. Changamoto, hata hivyo, ni kukosa muda wa kutosha kufanya hivyo.

Kwa mfano, ni kawaida kwa wazazi kutoka nyumbani alfajiri na kurudi usiku wakati ambao tayari watoto wameshalala. Matarajio makubwa ya kikazi yamekuwa kipaumbele na hivyo tunatumia muda mwingi kufanya kazi ambazo kimsingi ndizo zinazotusaidia kuwatunza watoto wetu. 

Hata hivyo, majukumu  yetu haya muhimu yanatufanya wakati mwingine tukose muda wa kuwasaidia watoto kihisia, kiufahamu na hata kimahusiano kama tunavyotamani.

Makala haya yanajadili hatua tano za kuchukua ili kukusaidia mzazi kupata muda wa kuwekeza katika malezi ya watoto wako.


Wazazi wakifurahia kuwa pamoja na mtoto. PICHA: nepsych.com
Fahamu watoto wanakuhitaji

Wazazi wengi wanafikiri wakiweza kuhakikisha watoto wao wamekula vizuri, wamelala mahali salama, wamevaa vizuri, wana afya njema, wameenda shule bora na wanapata mahitaji mengineyo muhimu, basi wamemaliza.

Lakini pamoja na umuhimu wa mahitaji haya, ni vizuri kutambua kuwa watoto wanakuhitaji wewe zaidi. Wanahitaji upatikane uweze kuwasikiliza kujua hisia, wasiwasi, matumaini yaliyonayo, uongee nao kujua maisha yao binafsi, siri zao na mengine ambayo hawawezi kuwaambia watu wengine.

Fikiria jambo hili. Ukiweza kupata dakika kumi tu kwa siku kukaa na mwanao umsikilize na kumpa nafasi ya kuhusiana na wewe, maana yake kati ya masaa 168 uliyonayo kwa juma, utakuwa umefanikiwa kuwa na mwanao kwa muda wa siku 27 tu pale atakapokuwa anafikisha umri wa miaka 12/13! Ni hatari kuyafanya malezi kuwa ‘kazi ya ziada’ inayofanywa pale muda unaporuhusu.

Kupangilia vipaumbele

Mgawanyo wa masaa 24 tuliyo kila siku unategemeana na vipaumbele tulivyonavyo. Kanuni ni rahisi. Raslimali isiyotosha huelekezwa kwenye maeneo ya kipaumbele. Kwa mfano, tunapoweka kazi mbele, ni wazi tutaelekeza sehemu kubwa ya muda katika kufanya kazi. Vile vile, katika mazingira hayo tunalazimika kupunguza muda wa kufanya mambo yasiyo ya muhimu.

Ndio kusema, kutambua umuhimu wa kupatikana kwa mwanao kunaenda sambamba na kufanya jitihada za kuhakikisha unapangilia muda wako uweze kupata muda wa kuwa na mwanao. Muda hutengenezwa. Kuweka kipaumbele katika familia, kutakufanya uepuke mambo mengine yasiyo ya lazima ili uweze kupata muda mzuri wa kuwa na familia yako.

Kwa mfano, badala ya kupitia kwenye maeneo yanayokukutanisha na marafiki zako kwa mazungumzo yasiyo ya lazima baada ya kazi, unaweza kwenda nyumbani moja kwa moja na hivyo kupata muda wa kuwa na familia yako.

Weka malengo ya kifamilia

Jaribu kuwahusisha watoto na mwenzi wako katika kutengeneza utaratibu wa utakaozingatia matarajio ya kila mwanafamilia. Unapokuwa na mpango wa kifamilia unaoeleweka inasaidia kuwafanya watoto kujua shughuli gani ya kifamilia wanaweza kuitazamia.

Kwa watoto wengi, kwa mfano, kukumbuka sherehe za kuzaliwa, mahafali, siku ya wazazi shuleni na matembelezi ni mambo yanayoweka kumbukumbu ya kudumu katika maisha yao. Unapokumbuka kuingiza mambo haya ya wanao katika mipango yako, inawasaidia watoto kuona unajali mambo yao.

Kadhalika, shughuli zenye malengo ya kifamilia ni mfumo wa uwajibikaji katika familia unaosaidia kukukumbusha mzazi kutenga muda kwa ajili ya kukidhi matarajio ya watoto.

Usihamishie ‘ofisi’ nyumbani

Hii ni changamoto kwa wafanyakazi wengi. Ni kweli wakati mwingine tunakosa kabisa muda wa kumaliza majukumu yetu kazini na hivyo kulazimika kwenda nayo nyumbani. Lakini, hata hivyo, yapo mazoea ya kupoteza muda kazini wakati mwingine bila sababu za msingi.

Kwa mfano, wafanyakazi wengi huweza kutumia muda mwingi kwa soga zisizo na tija wawapo kazini. Teknolojia imefanya iwe rahisi ‘kuishi’ kwenye mitandao ya kijamii bila ulazima. Matokeo yake, hatukamilishi majukumu ya kazi kwa muda uliopangwa na hasara ya upotevu huu wa muda hufidiwa kwa kukosekana nyumbani.

Sambamba na kutokuhamishia kazi za ofisi nyumbani, ni muhimu kukumbuka wajibu wako kama mzazi uwapo nyumbani. Watoto wanahitaji kukaa na mzazi na sio mzazi anayeendelea kuwa polisi, meneja, mwalimu au injinia awapo nyumbani.

Tenga muda maalum kwa familia

Fikiria kutumia siku za mwisho wa wiki kwa ajili ya familia yako. Katika mazingira ambayo siku tano za juma zimekuweka mbali na nyumbani, kuendelea na ratiba nyingine siku za mwisho wa wiki ni kuwanyima watoto haki yao ya msingi.

Dhamiria kuwa siku za Jumamosi na Jumapili ni maalum kwa ajili ya kukaa na watoto na mume/mke wako badala ya kutoka na marafiki au kwenda kwenye shughuli nyinginezo zinazoendelea kukuweka mbali na familia. Unapokuwa nyumbani unawapa watoto wako muda wa kutosha kukufurahia kwa mazungumzo na michezo ya pamoja.

Kadhalika, waweza kufikiria kuwapeleka watoto matembezini nje na nyumbani kama vile kwenye maeneo maalum kwa michezo ya watoto, fukwe za bahari, kwenye bustani na maeneo ya wazi, hotelini na hata maeneo ya ibada kadri ya matakwa na matamanio ya watoto.

Fuatilia jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila siku ya Jumanne.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?