Mwaka Mmoja Bila Mama, Mkono wa Mungu Haujatuacha…

Nakumbuka mwezi Juni 2002, nikiwa mwanafunzi wa sekondari, eneo ni stesheni ya gari moshi (treni) mjini Singida nikiwa ninarudi nyumbani nikitokea Dodoma. Ilikuwa ni safari ya kuunga unga iliyoanzia Dar es Salaam kupitia Dodoma na kisha Singida.

Wakati huo tulikuwa tunaondoka Dodoma saa nne asubuhi, Singida tunafika saa za jioni kuanzia saa kumi na moja hivi tukiwa taabani kwa uchovu wa kukaa kwenye mabehewa yaliyoonekana kuhangaika mno kupita kwenye mataruma katikati ya vichaka ya Dodoma na Singida. Jioni hiyo ninayoikumbuka vyema tulichelewa kidogo na hatimaye tulifika Singida stesheni saa kumi na mbili unusu hivi za jioni.


Ile tu treni inafunga breki namwona mama yangu akiangaza angaza macho kujua nilikuwa kwenye behewa lipi. Mama alikuwa amefika stesheni hapo kunipokea. Nilifurahi kupita maelezo. Siwezi kuwa na maelezo sahihi yanayoweza kukidhi furaha ya kulakiwa na mama baada ya kuwa mbali naye kwa muda fulani.

Mama alikuwa na tabia ya kuhakikisha anafanya mapokezi ya nguvu kila mara aliposikia narudi nyumbani. Kilichopendeza zaidi ni jioni ya siku ya mapokezi. Ilikuwa kawaida tumbo kustushwa na mapochopocho ya kila namna. 

Mazungumzo kwa kawaida yalikwenda mpaka usiku wa manane. Huo ndio ulikuwa wakati wa ‘sayu’, neno la Kinyaturu lenye maana ya salaam ndefu  zinazofanyika watu wawili wanapokutana aghalabu baada ya kuachana kwa muda mrefu. Mama hakuwa mwongeaji kivile lakini alijua nini cha kusema. 


Mama yangu, Magdalena, Mama Christian 
Sadaka ya muda wake

Kwa kawaida, nilipofika nyumbani kuwasalimia, mara zote alinihimiza kwenda kijijini nikamsalimie babu na bibi. Mama alikuwa ‘mtoto’ wa kwanza kwa babu yangu. Na kwa namna fulani walimtegemea. Alijisikia furaha sana nikifunga safari kwenda kuwasalimia wazee wale. Na mara nyingi sikusubiri anikumbushe. Najua wazee wale, kwa sasa, wanamkosa sana.

Mama alikuwa na tabia ya kutoa sadaka ya muda wake kuhakikisha anakuwa sababu ya furaha kwa watu wake wa karibu. Nakumbuka Mungu aliponizawadia mtoto miaka kadhaa iliyopita, mama aliomba likizo kazini kwake kuja kunisaidia kumtunza mke wangu kwa majuma mawili. Kwake, familia ilikuwa na nafasi ya kwanza, mengine yalifuata. Ninamkumbuka kwa kuheshimu sana maisha ya kifamilia.

Mwalimu asiye na cheti

Nakumbuka matukio mengi kwenye miaka ya themanini katikati nikiwa na kati ya miaka minne na sita. Enzi hizo watoto tuko watatu tu pale nyumbani. Ilikuwa ni kawaida mimi na mdogo wangu anayenifuata ‘kubanana naye’ jioni kushuhudia akisonga ugali. Alituimbia nyimbo za Sunday School zilizotufundisha maisha ya Ukristo kwa lugha ya kitoto. Baba naye, baada ya chakula, alifanya kazi ya kutusimulia hadithi za biblia.

Nilipoanza kujifunza kuhesabu na kusoma kabla sijaanza shule, jikoni ndiko kulikuwa mahali pa  kufanyia mazoezi ya kuhesabu. Mama alikuwa na kazi ya kuvumilia kusikiliza. Kwa hakika utoto ulikuwa mtamu karibu na mama. Pamoja na ukweli kuwa hakuwa na elimu kubwa ya darasani, alijitahidi kutujengea mazingira ya kujifunza.

Uandishi na kazi za mikono

Nakumbuka miaka ya 90 mwanzoni nikiwa nasoma madarasa ya mwanzo shule ya msingi, baba yetu alikuwa masomoni kwa miaka kadhaa. Kila alipomwandikia baba barua, mama alinihimiza na mimi niandike barua kwa baba. Alinifundisha kusimulia matukio ya pale nyumbani kwa maandishi. Utamu wa kuandika barua mara kwa mara wakati mwingine ulinifanya nimkumbushe lini hasa tungemwandikia baba barua tena. Najua Mzee Bwaya anakumbuka barua zangu.

Si elimu tu. Mama alitufundisha kufanya kazi za ndani bila kujali jinsia. Ni kweli kwa Wanyaturu ni kama mwiko fulani hivi kwa wanaume kuingilia kazi za wanawake. Kwetu hapakuwa na namna. Nyumbani alikuwa mwenyewe na alihitaji msaada wa shughuli ndogo ndogo.

Mbali na kufagia, kudeki, kuosha vyombo, mimi na mdogo wangu wa kiume anayenifuata, Fortunatus, tulikuwa na jukumu la kuteka maji kwa kutumia toroli. Mama alikuwa na namna yake ya kutufanya tujisikie fahari kufanya kazi hizo. Na kweli ni kama tulishindana na mdogo wangu kusukuma toroli kwa lengo la kutafuta ‘ujiko’ kwa mama. Leo hii sioni shida kufanya kazi zinazoonekana kuwa ni za kike kwa sababu ya mama.

Kunyenyekea

Mama hakuwa mkamilifu lakini alijitahidi kuishi Ukristo. Hakuwa mchoyo wa msamaha tulipomkosea na alipogundua amekosea hakusita kuomba msamaha. Hapa ninakumbuka kisa kimoja.

Siku moja, nikiwa kidato cha tatu, nimerudi nyumbani nikakuta baadhi ya nakala za gazeti la Rai zilizokuwa zimehifadhiwa kwa kumbukumbu zimenyofolewa baadhi ya kurasa zake. Baba yetu ni mtunzaji mzuri wa magazeti ya zamani na vitabu. Ametufundisha kwa vitendo kuheshimu maandishi labda kwa sababu ya ualimu wake.

Basi. Baadae nikagundua aliyechana magazeti hayo ni mama. Aliyatumia kuwafungia zawadi wageni wake akijua hatuyahitaji tena. Hakujua kuwa wakati mwingine huwa tunasoma magazeti ya mwaka uliopita.

 “Sasa umefanya nini mama?” niliuliza kwa mchanganyiko wa hasira na wasiwasi wa kuogopa kumkwaza. Alikuwa mpole mpaka mtu unaogopa kumchokoza. Uzuri alijua namna ya kushughulika na mtu aliyekasirika.

“Sifee ougansamehe he baba wane!” aliniomba msamaha kwa Kinyaturu. 

Kweli kauli kama hizi zenye ubinadamu hunifanya nimkumbuke mara nyingi sana. Sana. Na sababu kubwa ni vile alivyojua kutumia maneno ya Kinyaturu kuwasilisha ujumbe muhimu kila tulipowasiliana. Alipenda kuniita Sife, jina langu la ukoo. Sife ni jina la babu yangu aliyemzaa bibi upande wa mama. Kwake, ilikuwa ni heshima kunitambua kama babu yake mzaa mama.

Mazungumzo ya mwisho

Jumamosi ya terehe 3 Oktoba, 2015 alinipigia simu jioni. Alikuwa akinitakia heri nikijiandaa kutetea tasnifu yangu siku ya Ijumaa ya Oktoba 9, 2015 Chuoni Mlimani. 

Nakumbuka kauli yake kwangu, “Mungu amekusaidia sana baba yangu na mpaka hapo ameshakufikisha mbali sana. Mimi najua Mungu ana kusudi na wewe babu…na hata kwa wadogo zako umekuwa mfano mzuri!” Alikuwa na matarajio makubwa sana kwangu na kwa kweli alikuwa sehemu ya motisha ya mengi niliyoyafanya.

Unajua mama mmenisaidia s’saana kutimiza ndoto zangu nyingi. Sasa ni zamu yangu.” alicheka aliposikia hivyo. Sikujua nilisema kisichowezekana. Mazungumzo ya Jumamosi hiyo ndiyo yalikuwa ya mwisho.

Siku kama ya leo mwaka jana

Alituacha usiku wa Jumanne tarehe 6 Oktoba, 2015 akiwa amelazwa kwa masaa matatu tu katika Hospitali ya Mkoa wa Singida. Mungu alimchukua masaa machache baada ya kutapika na kuishiwa nguvu akiwa kazini akiwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu waliokuwa wakilelewa katika kituo kimoja mjini Singida. Mungu peke yake anajua kwa nini aliamua kumchukua katika kipindi hiki tulipokuwa tunamhitaji sana.


Umepita mwaka mmoja lakini haikuwa rahisi kukubaliana na ukweli kwamba ametuacha. Namshukuru Mungu, hata hivyo, kwa kutupitisha katika kipindi hiki kigumu cha mwaka mzima bila mama. Haikuwa rahisi lakini Mungu amekuwa faraja yetu. Mwaka mmoja bila mama, bado mkono wa Mungu haujatuacha. Hata sasa Mungu ametusaidia

Maoni

  1. Kaka Bwaya [Christian], Mungu ni faraja pekee na iliyo kuu kwa wanadamu wote. Umenikumbusha miaka 16 iliyopita nilipompoteza pia mama yangu kipenzi. Hakika, kuna mama mmoja tu na huyo akiondoka basi. Tumaini la pekee ni kuwa tunaye BABA MFARIJI wa wote. Barikiwa sana

    JibuFuta
  2. Asante sana ndugu Noverty kwa maneno mazito. Mungu ni faraja yetu.

    JibuFuta
  3. Mungu azidi kuwafariji na kuwapa neema ya kuishi katika ile misingi ambayo mama aliwajengea

    JibuFuta
  4. Maoni haya yameondolewa na mwandishi.

    JibuFuta
  5. Asante sana Monica kwa maneno ya faraja. Mungu ni mwema.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging