Chimbuko la wivu na athari zake katika mahusiano

Umewahi kuhisi unaachwa na mtu unayetarajia kumwoa au kuolewa nae? Umewahi kutamani kuwa na 'access' na simu au barua pepe ya mwenzi wako ili angalau ujisikie kutulia moyoni? Umewahi kujisikia vibaya mwenzi wako akizungumza na mtu mwingine hata kama hukuwa na ujasiri wa kumwambia? Umewahi kumchukia mtu na hata kupambana nae kwa siri au wazi sababu tu umehisi anahatarisha uhusiano wako? Kama lolote kati ya hilo linaelezea hali yako, basi makala haya yanakuhusu.
Najua wapo, tena wengi tu, wanaoamini ni vigumu kutenganisha hisia za wivu na mapenzi. Wanaamini huwezi kumpenda mtu bila kumwonea wivu. Kwamba kiasi kidogo cha wivu kinathibitisha upendo kwa unayempenda. Lakini ni hisia hizo hizo za wivu ndio zimekuwa chanzo cha maumivu ya moyo, majeraha, talaka na hata vifo vya watu tunaoambiwa ni 'wapenzi'. Haya hayawezi kuwa matokeo ya upendo hata kidogo. Wivu umesababisha watu wasiwe na amani na mahusiano yao. Wivu umesababisha watu wawe na hasira, ghadhabu na uchungu, wakati mwingi, kwa mambo yasiyokuwepo. Wapo waliofikia kugombana na watu wasiohusika kwa sababu tu wanahisi kuingiliwa kwenye mahusiano. Wivu si hisia zinazoweza kuleta faida hata kama wengi tumekuwa tukiamini hivyo.
Wivu ni ugonjwa wa nafsi isiyojiamini

Kuhisi mtu unayempenda anaweza kuwa na hisia za kimapenzi na mtu mwingine sio jambo la kujivunia. Kutokumwamini mpenzi uliyenaye na kuhisi kuna mtu mwingine anahatarisha, threaten, uhusiano wenu haiwezi kuwa afya ya mahusiano. Ni ugonjwa unaohitaji tiba.

Ingawa wakati mwingine hisia hizi huwa sahihi, wakati mwingi huwa ni hisia tu zisizokuwepo. Ni hisia za kutokujisikia salama na kutokujiamini. Ninapokuwa na hisia za wivu, mara nyingi hili ni tatizo langu kuliko linavyoweza kuwa la huyo ninayeugua kwa ajili yake. Mahusiano yenye tishio la wivu, kuhisiana, kupekuana, na kadhalika, hutegemea na namna gani mtu aliye kwenye mahusiano asivyojiamini kwa maana ya kuwa na nafsi isiyotulia kumwezesha kujiamini na kuwaamini wengine.

Wivu ni hisia za ubinafsi zisizo na chembe ya upendo. Picha Na Jamie
Malezi ndio msingi wa kutokujiamini. Si kazi nyepesi kwa mwenzi aliyekuzwa bila kujiamini kujisikia salama nafsini. Hajiamini na hawaamini wengine. Na hii hujidhihirisha sana kwa watoto wa miaka kati ya mwili na sita. Kwa sababu bado wanakuwa hawajajifunza kushindana, watoto wa umri huu huwa ni wepesi kujisikia kutishwa, threatened mzazi anapomsifia au kumwonesha upendo mtoto mwingine. Huwa hawajajenga uwezo wa kujiamini na hivyo hushindana na chochote kinachofikiriwa kuhatarisha umiliki wao. Wasiposaidiwa kujiamini kadri wanavyokua, watoto hawa huwa hawabadiliki. Hukua na hisia hizo hizo za ubinafsi na hofu ya mahusiano. Wanapoingia kwenye mahusiano, ndio hawa ambao hushindwa kuamini kwamba wanaweza kupendwa kama watu wengine. Na hata wanapopendwa, huhisi lolote linaweza kutokea wakati wowote. Hujenga mahusiano yaliyojaa hofu. Kwa hiyo tunaweza kusema kutokujiamini ndio hasa wivu wenyewe.

Watafiti wengine wanakubaliana kwamba wivu ni matokeo ya imani batili kuhusu mapenzi na mahusiano. Wivu ni imani. Umewahi kusikia watu wanasema, "Hakuna mwanaume anaweza kuwa mwaminifu! Hawa wanaume waangalie tu!" "Hawa wanawake waone hivi...hata ufanyeje hawawezi kutulia kwenye ndoa!" Haya ni matokeo ya imani zilizojikita kwenye akili ya mtu na ndizo zinazopalilia hisia za kutokujiamini, na hivyo kujenga taswira isiyokuwepo.

Ukweli ni kwamba unapoamini hakuna mtu anaweza kuwa mwaminifu kwenye ndoa hata ufanyeje, unajenga matarajio yanayoweza kutengeneza uhalisia usiokuwepo. Imani kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa mwaminifu huathiri mtazamo wako na hivyo huwezi kumwamini mkeo anaposafiri kikazi kwa siku kadhaa. Unajenga hofu unaposikia mumeo anakwenda kazini kwa zamu ya usiku. Na ubaya wa imani hizi zinazojengeka kwenye ufahamu humtafuna mtu ndani kwa ndani hivyo hata usiposema ulivyo na wasiwasi, lakini unajua unavyopata tabu moyoni kwa kujua lolote linawezekana kutokea. Hakuna uhusiano wowote unaweza kuleta utimilifu wa furaha inayotarajiwa katika mazingira haya ya hofu na mashaka.

Wivu na mapenzi haviendi pamoja

Hisia za wivu zikishakomaa ndani kwa ndani huhamia kwenye hatua inayoweza kuonekana wazi.  Hapa tunasema hisia zinahama kutoka kuwa mtazamo na imani hasi na kuwa tabia. Katika hatua hii mtu huanza kuchukua hatua za kujihami katika kukabiliana na tishio linalohisiwa. Hapa tunazungumzia mbinu za kuanza kuchunguza mwenendo wa mwenzako kwa siri.  Kuanza kumfuatilia kujua mambo yake ya faragha. Kuanza kuonesha wasiwasi wako waziwazi.

Katika hatua hii mtu huanza kupekua simu kwa siri, kupekua kompyuta kujua kurasa zisizoperuziwa au hata kuuliza uliza kwa wengine mwenendo wa mwenzake. Katika hatua hii, kadhalika, mtu huanza kufanya majaribio ya kupambana na kile kinachohisiwa  kutishia uhusiano wake. Huanza kuthubutu kuanza kuwapigia simu watu anaohisi ndio tatizo. Mchanganyiko wa hasira, wasiwasi, hofu na uchungu humfanya adhamirie kupambana na watu anaowahisi iwe kwa maneno au hata kwa matumizi ya nguvu. Anahama kutoka kuumia moyoni, hadi kupambana.

Katika mazingira haya, hatuwezi kusema kinachokusukuma ni upendo. Huwezi kumpenda mtu kwa dhati wakati huo huo ukimfuatilia kwa karibu kwa matarajio ya 'kukusanya ushahidi' usijenga mahusiano yenu. Wivu, kama tulivyoona, ni matokeo ya kutokujiamini. Ni udhaifu. Na kwa hakika huwezi kupenda kama wewe mwenyewe hujiamini. Tafiti zimethibitisha hivyo. Kwamba kadri unavyompenda mwenzi wako, ndivyo inavyokuwa vigumu kuhisi 'kuibiwa'. Kwa hiyo kuhisi hisi 'kunyang'anywa' si dalili ya upendo. Ni dalili ya tatizo lako la kutokujiamini.

Tunaweza kukabiliana na wivu

Unapopata hisia za wivu, jambo la kwanza la kufahamu ni kwamba bado hujaweza kujiamini ipasavyo. Hujaweza kujipenda mwenyewe. Tafuta msaada wa kitaalamu uweze kujiamini na kujipenda mwenyewe kwanza kabla ya kusubiri mtu mwingine akupende kwa kiasi unachotaka. Na kuna ukweli fulani kwamba ni mara chache unaweza kumbadilisha mwenzako. Kumbe kwa kutokujiamini na kujipenda, unajiwekea mazingira ya kuteseka unapoingia kwenye mahusiano.

Kwa lugha rahisi kabisa, hisia za wivu maana yake ni kutokuamini watu. Una mashaka na tabia za watu. Unaamini uko sahihi, wengine wanakosea. Badilika. Tafuta msaada uweze kuwaamini watu. Itakusaidia kuepuka kuteseka kwa mambo yasiyokuwepo kwa sababu tu huwezi kuwaamini watu. Kutokuamini, ndiyo wivu wenyewe.

Ni kweli kuwa wakati mwingine hisia za wivu huwa hisia za hali iliyopo. Kwamba ni kweli yupo mtu wa tatu katika mahusiano yenu. Kama mwanadamu unajisikia vibaya. Lakini dawa si wivu wa kiwango cha kupambana na mshindani wako.  Katika mazingira hayo, wakati mwingine tatizo huwa ni wewe. Ndio. Huenda hujalipa gharama ya kumfanya mpenzi wako ajisikie kupendwa na kuthaminiwa. Huenda umemfanya ajisikie kutumika kama daraja la mtu kufikia malengo mengine ya kimaisha. Badilisha mtazamo wako. Tafuta msaada wa kukufanya ujisikie mwenye wajibu wa kuleta mabadiliko kwenye mahusiano yako. Wivu haukusaidii kutatua matatizo yako.

Wivu usikufanye upambane na mtu asiyehusika. Hasira ni kiburi. Hasira, tunaambiwa haijawahi kutenda haki. Itakugharimu kukarabati mahusiano kwa kuongeza duara la mapambano na mtu wa tatu. Pambana na mwenzi wako kwa kumpa haki yake. Kama una hakika analo tatizo la kuvutwa na vya nje, kabiliana naye abadilike. Tafuteni msaada wa kitaalam kushughulikia mahusiano yenu. Hamna haja ya kupambana na mtu wa tatu ambaye kimsingi mmemkaribisha wenyewe.

Wivu ni sumu mbaya katika mahusiano. Unapojisikia hatari ya kumpoteza mpenzi wako, unapojisikia unatumia nguvu nyingi kuliko anazotumia yeye, maana yake ni kwamba bado hujampenda. Ni hatari ya hisia zako, na za mwenzako. Unajeruhi hisia zao mara nyingi kwa jambo lisilokuwepo. Unajikuta unachukua hatua zinazoongeza majeraha hata baada ya kushughulikia tatizo lenu. Upendo wa kweli hauhesabu gharama. Upendo hauna masharti. Unapompenda mtu, hufikirii yeye anafanya nini. Na unapofanya hivyo, mara nyingi, unamsababisha kubadilika.

Kabla hujafanya maamuzi ya kuhusiana na mtu, jitathimini. Jichunguze mwenyewe kwanza. Je, unajiamini? Unaamini wengine? Unafikiri nini kuhusu kupenda na kupendwa? Je, mahusiano ni kulipa gharama au kutarajia kutendewa? Kama huna hakika, tafuta msaada ndipo uweze kuingia kwenye mahusiano. Vinginevyo, utamjeruhi huyo unayetaka kuhusiana nae, utajijeruhi mwenyewe, na zaidi, utajeruhi wengine. Kwa sababu wivu, imethibitika, ni jaribio la kumtumia umpendaye kudhihirisha ulivyo na mtazamo hasi nafsi yako mwenyewe. Ishughulikie.

christianbwaya@gmail.com

Maoni

  1. Napendezwa na mafundisho yako maana yananijenga kwa kiasi kikubwa..napenda kuulza kama kuna machapisho ya vitabu au majarida kwa mada unazotoa

    JibuFuta
  2. Asante.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?