Muhtasari na Hitimisho, 'Kanuni zinazoongoza mahusiano na migogoro ya wanandoa'

TANGU tulipoanza mfululizo wa makala za mahusiano, jambo kubwa nililojaribu kulionesha ni nafasi ya mahitaji ya hisia katika kuimarisha au kuvuruga mahusiano. Na msingi wa haya yote ni kusema kwamba mahusiano hayana miujiza. Mahusiano yanaongozwa na kanuni za kawaida sana ambazo ukifanikiwa kuzitambua na kuzitumia utapunguza kama sio kuondoa matatizo mengi. Kwa mhutasari, ningependa tuyapitie mambo makuu yaliyojitokeza katika mjadala wetu kwa kuyaweka katika makala moja inayojitegemea.

Kanuni zinazosimamia mahusiano

Kwanza kabisa tuliona kwamba mahitaji ya kihisia yanatofautiana kijinsia. Anachokihitaji mwanamke sicho anachokihitaji mwanaume. Tuliona kwamba mwanamke kwa kawaida anatamani kupendwa na kujisikia kuwa na nafasi ya kwanza katika maisha ya mwanaume, wakati mwanaume anatamani kuona hadhi na uwezo wake kama mwanaume utambuliwa. Maana yake ni kwamba mwanaume na mwanamke wanatafsiri upendo kwa lugha tofauti. Mke anauona upendo kama mahaba, ukaribu na mpenzi wake, wakati mume anauona upendo kama heshima na kutambuliwa.

Tulisema, watu wawili wanapoanza mahusiano, kwa kawaida, mahusiano hayo huwa ni kwa sababu mahitaji haya ya kihisia yanashughulikiwa kwa bidii. Mwanaume ambaye kwa tamaduni nyingi ndiye huanzisha mahusiano hujitahidi kutumia kila njia anayoweza ili kumfanya mwanamke ampendaye ajisikie kupendwa. Jitihada hizo humfanya mwanamke naye kuwa na mazingira sahihi ya kuwa na ujasiri wa kujibu upendo na urafiki anaoupata kwa kumfanya mwanamme naye ajisikie mfalme. Hii ndiyo hali ya kuwezeshana  inayowafanya watu wawili waendelee kujisikia ule ukaribu kihisia.
Wenzi wa ki-Naijeria wakionekana furahia kudumu kwa mapenzi yao.  Picha na Christian Krarup

Na kwa mujibu wa tafiti, tuliona, mapenzi huanza kubadilika pale mambo mengine yanapoingilia utegemeano huo iwe kwa kujua ama kutokujua. Tuliona, kwamba mara nyingi mwanaume ambaye ndiye chanzo cha duara la utegemeano wa kimapenzi, hujikuta katika mazingira ya mashinikizo mengine ya kimaisha na kusahau jukumu la kumfanya mke wake kuendelea kujisikia kuwa kipaumbele chake. Hali hiyo inapotokea, mwanamke hujikuta hapati yale mahitaji ya kihisia aliyoyatarajia kwa mume wake. Sasa kwa wanawake wengi, hiyo yaweza kuwa sababu ya kunyong'onyea kihisia na hivyo kujikuta akishindwa kuwa na ujasiri wa kumtimizia mume wake mahitaji yake. Hapo ndipo ulipo msingi wa kutokuelewana.

Tunaposema kutokuelewana, tumaanisha ile hali ya kutokuwepo kwa mvuto wa kiashiki kati ya wenzi/wapenzi ambao ndio huwa dalili ya kwanza ya mahusiano yenye matatizo. Hii ikiwa na maana kwamba mmoja wapo anapoanza kuhisi havutiwi kimapenzi vya kutosha na mpenzi wake na hivyo kuanza kuhisi anahitaji 'msaada wa nje' ya ndoa, hiyo ndiyo hali tunayoiita kutokuelewa. Ni kule kuanza kushindwa kufunguka moyo, kushindwa kuwasiliana mioyo, na kwa hakika ni kule kuanza kufungiana mioyo.

Tuliona, kukosekana kwa mvuto huo wa kimapenzi, huweza kusababisha kukosekana kwa ukaribu unajengwa kwenye misingi ya urafiki wa wapenzi husika. Hapa tukiwa na maana kwamba ishara rahisi ya kuanza kutokuelewana ni pale mmoja wapo anapoanza kukosa ujasiri wa kuwa karibu na mwenzake kimazungumzo, kimawasiliano au kimwili. Mahusiano ya namna hii huendelea kuwepo kwa kutegemezwa na ahadi tu na sio vinginevyo. Hali hii ndiyo mgogoro wenyewe. Na inapofikia hapo, unaweza kushangaa wapenzi wanatamani kuongea lakini hawana ujasiri wa kuongea. Na wakiongea wanazungumza mambo yasiyowahusu. Wanatamani kuwa karibu lakini hawawezi kwa sababu ya shuku ya utayari wa mwenzake.

Vyanzo vikuu vya matatizo ya mahusiano

Katika sababu kadhaa zinazosababisha kutokuelewana, moja wapo kubwa tuliyoiona ni namna wapenzi wanavyoanzisha mahusiano yao. Kwamba unaingia kwenye mahusiano ukitegemea nini, hiyo yaweza kuwa sababu kubwa ya mgogoro mbele ya safari. Tuliona wapo wapenzi wanaoingia kwenye mahusiano kwa sababu zisizo za kimapenzi. Hapa kuna mambo kama pesa, fursa, sifa za marafiki na mashinikizo mengine ikiwamo kupata ujauzito. Wengine wanaingia kwenye mahusiano wakiwa na taarifa zisizosahihi kuhusu ndoa na mahusiano. Hizo zote zaweza kuchangia kukatishwa tamaa na uhalisia wa mabo unapoingia kwenye mahusiano na hatimaye mambo kuweza kwenda mrama.

Ili kupunguza uwezekano wa matatizo, tuliona pengine ni muhimu kijana kujikagua vya kutosha kujiridhisha kama anaelewa kwa nini anaingia kwenye mahusiano. Na si tu kujikagua mwenyewe, pengine pia ni muhimu kujihakikishia kwamba na mwenzake anaelewa sababu inayomsukuma kuingia kwenye mahusiano. Kwa kufanya hivyo, wawili hao watakuwa wamepunguza mazingira ya kuhitilafiana pasipo sababu.

Kingine tulichokiona, ni kwamba mabadiliko ya maisha yanayoongeza msongo wa mawazo ni sababu moja wapo. Hapa tulizungumzia hatari ya fikra maarufu kwamba usawa wa kijinsia una maana ya kufanana kijinsia. Fikra hizi zinazoweza kufaa kwenye harakati za usawa katika jamii, hazina nafasi kwenye ndoa na mahusiano tunayoyazungumzia. Wachambuzi wa mambo ya mahusiano wanafikiri kwamba wanawake wanapoanza kuamini kuwa wanaweza kuwa sawa na wanaume, na wakati mwingine kwamba hata bila wanaume wanaweza, basi misuguano ya kimahusiano huwa si jambo la ajabu katika mazingira haya.

Namna bora ya kukabiliana na changamoto hii, tuliona ni kwa wanaume kuelewa changamoto hii ya mashinikizo yanayowakabili wanawake na kuwasaidia kupita salama kwenye kipindi hiki cha mpito wa haki za kijamii. Wanawake pia kwa upande wao, wanahitaji kuelewa ugumu unaowakabili wanaume katika kubadili majukumu yao yaliyozoeleka. Kutegemea mabadiliko ya ghafla ni kutengeneza shinikizo jingine ambalo halitatatua changamoto iliyopo.

Kadhalika, tuliona lipo suala la hisia za wivu. Mke au mume, kwa kutokujiamini kwake, anaweza kujikuta anaanza kuhisi kutishiwa nafasi yake na kitu au mtu mwingine. Hali hii ya kuwa na mashaka mashaka na kuishi bila kujiamini sio nzuri na haijengi mahusiano. Tulisema, na hapa tunarudia, kwamba ingawa inaaminika huwezi kumpenda mtu bila kumwonea wivu, wachunguzi wa mahusiano wanasema wivu hauwezi kwenda pamoja na mapenzi. Ni wajibu wa wapenzi kushughulika na hisia zao za kutokujiamini ili waweze kuweka mazingira ya kufurahia mahusiano yao.

Ukiacha suala la wivu, tumeona namna kutokujifunza kuzielewa, kuzikubali na kuzichukulia tofauti zetu kunavyoweza kuleta matatizo. Kilichozungumzwa hapo ni kuona jinsi tofauti zetu zilivyo jambo jema tukijifunza kuzitumia kwa faida na kuziona kama fursa ya kukua kimahusiano. Na suala la kuweza kuvaa viatu vya wapenzi wetu linawezekana kama sisi wenyewe tunajiamini na hatutishwi na tofauti za mtazamo, imani na tabia walizowazo wapenzi wetu.

Sasa ipo dhana kwamba watu wanaposhindwa kuelewana, maana yake hawakuwa watu sahihi. Tuliona kwamba jambo hili si kweli. Hakuna mtu sahihi kwenye mahusiano bali kanuni sahihi. Tulichokisema ni kwamba mwanaume yeyote anaweza kuishi na mwanamke yeyote ikiwa wataweza kutambua na kufanyia kazi kanuni rahisi kabisa za mahusiano. Kanuni moja kuu ni kutambua na kuyajibu mahitaji ya mwenzake kunakomfanya na yeye ahamisike kuyatambua na kuyajibu mahitaji yako. Rahisi zaidi kusema kuliko kutekeleza. Hata hivyo, hili linawezekana katika mazingira ambayo wapenzi wanayo nia ya dhati ya kubaki waminifu kwa kuyapa mahusiano yao kipaumbele.

Hoja kuu tuliyoijenga ni kwamba mahusiano yote huanza kwa njia ya nasibu. Mvuto unaoanzisha mahusiano hutegemeana na mwonekano wa mwili lakini pia hisia zinazojenga ukaribu au maamuzi. Tuliona kwamba uzuri wa mtu ni suala la mtazamo unaojengwa na imani za jumla za jamii zinazotengeneza matarajio fulani. Vigezo vya uzuri vinavyomvuta mtu kwa mwingine ni mambo ya kimtazamo tu yanayoweza kubadilika kadri watu wawili wanavyoendelea kukutana na kuhusiana.

Na katika kuthibitisha hayo, tuliona, hata watu wanaojikuta kwenye mahusiano kwa sababu moja au nyingine, wanaweza kuanza kupendana kama wapenzi wengine kwa dhati kabisa. Kwa hiyo suala la mtu sahihi kwenye mahusiano halipo. Ni imani tu ambayo mara nyingi ina ubinafsi fulani ndani yake na ni mbinu fulani za kukwepa kuwajibikia changamoto zetu. Mtu akishindwa kuwekeza vya kutosha na akaanza kuhisi mzigo unamleema, anaishia kujiaminisha, "ah, nililamba dume. Huyu si mtu sahihi kwangu', jambo ambalo tuliona si kweli.

Katika kuhitimisha mfululizo huu, suala kuu lilijitokeza katika kuboresha mahusiano ni gharama. Namna gani wapenzi wako tayari kulipa gharama za kujenga mahusiano yao hilo ndilo la kwanza na la msingi. Ni kwa kiwango gani kila moja anachukua hatua za kuwekeza vya kutosha kwenye mahusiano badala ya kusubiri matunda ya mahusiano bora? Ni kwa kiasi gani wapenzi wanakuwa tayari kujifunza mambo ya mahusiano? Je, ni kweli kwamba mahusiano huja yenyewe bila kujifunza?

Namna gani kila mmoja anabadili mtazamo wake na kujiona mwenye wajibu wa kujitolea katika kuboresha mahusiano yake badala ya kutafuta njia za mkato? Kwa sababu ukweli ni kwamba namna gani kila mmoja anatambua changamoto za mahusiano zinazotokana na aina ya majukumu anayoyafanya, imani za kidini alizonazo, utamaduni wake, na matarajio ya jumla ya jamii, yote hayo yanamua kwa kiasi kikubwa aina ya mahusiano tunayokuwa nayo.

Nawashukuru sana wasomaji wa blogu hii kwa mrejesho mzuri nilioupata tangu nilipoanza kuanzia mfululizo huu majuma kadhaa yaliyopita. Nimepata maoni mengi ya kuboresha kazi zangu, nimepata maswali mengi mazuri ambayo nitajitahidi kuyajadili kadri muda utakavyoruhusu. Lililo muhimu nililojifunza ni kwamba wasomaji wengi wanaamini kwamba mahusiano bora, pamoja na changamoto zake, yanawezekana. Hilo ndilo jambo la kutia moyo.

Mfululizo wa makala hizi umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na maandishi mbalimbali aliyowahi kuyasoma mwandishi, kwa kuongezea na uzoefu binafsi pamoja na mahojiano aliyoyafanya na watu kadhaa walio kwenye ndoa/mahusiano. Hata hivyo, yaliyoandikwa yanafaa kuwa taarifa za jumla na sio ushauri mahsusi wa nini cha kufanya katika kukabiliana na matatizo halisi. Msomaji anawajibika kwa maamuzi anayofanya, na hivyo anashauriwa kuonana na wataalamu wanasihi kwa msaada mahsusi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?