Umuhimu wa kutofautiana ili kujenga mahusiano imara

Kwa wale wafuatiliaji wenzangu wa tamthlia isiyopendwa na wengi, Isidingo the Need, mtakuwa mmeona mgogoro wa kimahusiano kati ya Rajesh Kumar na mkewe Priya. Wawili hawa wamejaliwa mtoto mmoja wa kike, Hiranya, ambaye si mtoto wa kuzaa wa Rajesh. Sasa ikafika mahali mwanaume huyu akatamani kuwa na mtoto ‘wa kumzaa mwenyewe’. Priya hayuko tayari kupata mtoto mwingine. Anadhani  kilicho muhimu kwa sasa ni kumlea mtoto wao na sio kuongeza majukumu ya malezi.
Kuona hivyo Rajesh anang’aka. Iweje kupata mtoto iwe shughuli ya kubembeleza kiasi hicho wakati ukweli unajulikana kwamba hana mtoto wa kumzaa? Akafikia kuhisi huenda tatizo si mtoto bali yeye, na kwamba Priya hataki kuzaa nae. Wazo hilo linachafua vibaya hali ya hewa mule ndani na hatimaye jamaa anaamua kukimbia nyumba kwa muda ili apate nafasi ya kupunguza mawazo.

Hapa tunaona chanzo cha matatizo mengi ya kimahusiano. Kutokuwa tayari kuyatazama mambo kwa mtazamo wa mwenzako. Kushindwa kukubali kwamba na mwenzako naye ana haki ya kufikiri na kuamua kwa uhuru kama wewe na kwamba kudhani anachofikiri mmoja kinaweza kuwa sheria kwa gharama ya uhuru na matakwa ya mwenzake si jambo linaloweza kuboresha mahusiano. 

Katika mfano nilioutoa, Rajesh na Priya wanajikuta wakinuniana na kuingia kwenye mgogoro kwa sababu wote wawili au mmoja wao hataki kuvaa viatu vya mwenzake. Rajesh hajafanikiwa kuelewa kuwa mke wake anafikiri tofauti na hataki kukubali tofauti hiyo. Kwake tofauti ni matusi. Hataki mjadala. Anachotaka yeye ni mtoto. Hataki kusikia Priya anafikiri kuweka bidii zaidi kwenye kazi yake ya Upolisi wala kujikita kwenye majukumu ya malezi ya mtoto wao wa pekee ambaye ni mgonjwa. Anadhani kile anachokitaka yeye kinastahili kuungwa pasipo hoja. Ndio tabia ya wanaume wengi wanaodhani kuwa kiongozi wa familia maana yake ni kumnyima mwanamke uhuru wa kufikiri.

Priya naye kwa upande wake anashindwa kuelewa mume wake angetamani fahari ya kuwa na mtoto wa kumzaa mwenyewe. Haelewi kwamba ndani ya Rajesh ipo shauku ya kuwa na mtoto wa kiume katika nyumba hiyo ambayo kwa mujibu wa maelezo yake ‘idadi ya wanawake imezidi ile ya wanaume’. Sasa kwa sababu kila mmoja anaamini yeye ndiye anayefikiri vizuri kuliko mwenzake, mambo yanaharibikia hapo na mawasiliano yanakatika. Ugomvi na kukimbia nyumba vinafuata.
Hapo utashangaa. Ingawa karibu sisi sote tunapenda sana kueleweka, inakuwaje hatufanyi jitihada za kusikiliza na kuwaelewa wa upande wa pili? Kwa nini tunataka tueleweke kwa tusiotaka kuwaelewa?  
Tofauti hazikwepeki
Wafuatiliaji wa mahusiano wanasema hatuwezi kujipa fursa ya kuelewa upande wa pili kama sisi wenyewe ndani mwetu kuna namna fulani ya ubinafsi unaotokana na hisia za kutokujiamini. Wanasema, mwenzi anayejiamini ni mwepesi zaidi kuelewa upande wa pili na kwa kawaida hajisikii kutishwa na mawazo tofauti. 

Sasa unaweza kujiuliza, ‘Kutokujiamini tena? Yule Rajesh uliyemtaja hivi punde hajiamini?’ Jawabu ni ndio, Rajesh wa Isidingo hajiamini. Angejiamini asingekuwa na sababu ya kutoroka mawazo tofauti kutoka kwa mkewe. Angejipa nafasi ya kuelewa hoja za upande wa pili na kuwa tayari kupokea majibu asiyoyapenda bila kuathiri uhusiano wao.
Sasa hulka hii ya watu kutokutaka kuwaelewa wengine na kulazimisha wengine wawaelewe wao unaweza kuiona hata kwenye mahusiano ya kawaida kabisa. Angalia namna tunavyopokea maoni tofauti kwenye mitandao ya kijamii. Inakuwa kama tunapoandika mambo fulani hatutarajii wasomaji kuona dosari. Hii ni dalili ya kutokujiamini. Huwezi kujiamini na ukashindwa kusikia upande wa pili usiofurahisha masikio. 

Unajisikia vizuri kujua anakupenda ulivyo Picha Na thegrio.com
Ndivyo ilivyo kwenye mahusiano. Tofauti ni jambo la lazima. Na kwa asili binadamu tumezaliwa na tofauti zinazotutambulisha.  Tumekulia kwenye mazingira tofauti, malezi tofauti, sehemu tofauti, imani tofauti na vingine vingi tofauti. Hiyo pekee ingetosha kutufanya tuelewe wenzi wawili hawawezi kufanana kwa mengi. Mtafanana dini, lakini hamtafanana mitazamo. Mtafanana mitazamo kadhaa, lakini sio misimamo. Maisha ndivyo yalivyo. Pamoja na ukweli kwamba ipo hulka ya kibinadamu ya kuvutiwa  na wale wanaofanana nae, lakini bado katika hali halisi tofauti zetu na watu huwa ni nyingi kuliko kufanana. 

Nakumbuka kisa kimoja cha maswahiba wangu. Mmoja mshika dini mzuri mwingine hakuwa anachukulia masuala ya imani kwa uzito unaostahili. Unaweza kumwita mpagani. Sasa kila ilipofika Jumapili, ilikuwa ni kawaida kwa mke ambaye ndiye alikuwa kama kiranja wa imani pale nyumbani kugomba kwa sababu mume hakuona umuhimu wowote wa kwenda kanisani. Na mke hakuwa tayari kumwona mume akiendeleza uzembe huo wa kiroho, wakati huo huo mume hakuwa tayari kuona anabadilishwa. Matokeo yake wakajikuta katika mazingira ya ugomvi usioisha. 

Ilibidi wasaidiwe kuelewa umuhimu wa kutambua, kukubali na kuchukuliana na tofauti zao. Mke akatambua kumbe yapo mambo hayawezi kubadilishwa kwa jitihada hata kama ni kweli yanayopiganiwa kubadilika yana manufaa. Akatambua kumbe tabia huwa haibadilishwi kirahisi tena kwenye mazingira ya shinikizo na kwamba jitihada za kumbadilisha mwenzi huishia kujenga ‘mazingira ya uasi’ yasiyoweza kujenga mahusiano yenye afya. Alikubali kumpokea mume wake katika hali hiyo hiyo ya upagani asioupenda.

Hatima yake, kwa kuona sasa anapendwa bila masharti, mume alibadilika na kuona thamani ya maisha ya kiroho. Upendo usio na masharti ukageuka kuwa shinikizo jepesi la mabadiliko.Tunachokisema ni kwamba kutaka mpenzi wako awe vile unavyotaka wewe, atende upendavyo wewe ni udhaifu wa kihaiba unaoweza kukuza tofauti zaidi kati yenu.

Tunaweza kuzipokea na tofauti na kuzivumilia

Kama kuna mambo tunapaswa kujiuliza kabla ya kuhusiana na mtu ni ikiwa tunaweza kumpokea vivyo hivyo alivyo pasipo matarajio ya mabadiliko yoyote. Kwamba alivyo mchumba wako ndivyo atakavyoendelea kuwa isipokuwa akiweza kubadilika bila shinikizo. Uelewe hivyo na upime kama umelipokea hilo ipasavyo. Na kubadilika, kama kupo kuje bila jitihada za ‘kujaribu kubadilisha’. 

Kwamba kama rafiki yako wa kike leo anapenda mtindo fulani wa mavazi, nywele au maisha, upendo wako kwake una maana ya kumpokea alivyo bila nia fichi ya kuja kumgeuza awe upendavyo wewe baadae. Huko ndiko kumpenda mtu pasipo masharti. Kumpokea umpendaye bila kutishwa na tofauti fulani fulani  zinazokufanya utarajie mabadiliko ndio upendo wenyewe. Ni kuweza kuendelea kumpenda mtu unayejua anakoroma bila mpango wa kuja kumbadilisha baadae. Huo ndio upendo wa dhati.

Tunapoyasema haya hatumaanishi watu huwa hawabadiliki kabisa. Hapana. Na wala hatumaanishi kwamba ukiingia kwenye mahusiano hubadiliki. Hapana. Yapo mambo yanayoweza kuzungumzika kirahisi na yakambadilisha mpenzi wako bila matatizo. Na haya ni rahisi kuyatambua kwa kupima mwitikio na mwelekeo wa mazungumzo. Na kwa kawaida, yanapozungumzwa hayasababishi upinzani mkali wala uzito wa mawasiliano. Hayo yanaweza kubadilishwa.

Lakini yapo mengine mengi ambayo hata kama tusingependa kuyaona kwa wenzi wetu, njia pekee tunayoweza kuitumia kukabiliana nayo si kujaribu kuyabadilisha bali kuyavumilia kwa maana ya kuyaona kwa macho ya kuwaruhusu wenzi wetu kuwa vile walivyo pasipo hofu wala shinikizo la kukataliwa. 

Na inapokwepo haja ya kubadilika, mtu pekee unayeweza kumbadilisha upendavyo na kwa wakati wowote ni wewe ama kubadili mtazamo wako kwa tabia hiyo usiyoipenda au wakati mwingine inapobidi kubadilisha tabia yako iendane na tabia inayokukera. 

Kwa mfano badala ya kukazana 'kumbadilisha' mume wako mwenye mazoea ya kuvua soksi na kuzitupa tupa bila utaratibu hapo sebuleni, pengine ni muhimu kukubali kuwa hivyo ndivyo alivyo. Ikubali tabia hiyo na ivumilie. Na unaweza kushangaa kitendo hicho cha kumpokea vile alivyo, kinaweza kumfanya akabadilika kirahisi kuliko kutumia nguvu nyingi kutengeneza mabadiliko kwa njia za ugomvi na shari.


Uamuzi wa mabadiliko ni wako

Najua zipo tofauti za kitabia zisizovumilika. Kuna yale yanayoitwa makosa makubwa yasiyovumilika. Naelewa kadhalika yapo maamuzi ya msingi katika mahusiano ambayo mmoja anaweza kudhani ni ya lazima kufanyika hata kama hakuna ridhaa ya upande wa pili. 

Katika mazingira kama hayo wachambuzi wa mambo haya wanadhani ni muhimu kupima gharama za kujaribu kubadilisha kisichobadilika kwa kuzilinganisha na gharama za kubadilika mwenyewe. Kwamba kipi chepesi, kuacha kubadilisha/kuamua kwa gharama ya kubadilika mwenyewe/kuvumilia au kujaribu kubadilisha kwa gharama ya mahusiano? Kwamba kipi muhimu, kufanya lolote bila kujali athari zake kwenye mahusiano, au kufanya lolote kulinda mahusiano hata ikibidi kuachana maamuzi yasiyokubalika upande wa pili?

Hatima ya yote, tofauti zetu za maoni na mitazamo si jambo baya. Ni afya. Mahusiano yenyewe tunayoyajadili yanawezekana kwa sababu ya uwepo wa tofauti za kijinsia. Mume na mke. Tofauti hiyo ndiyo nguvu ya mahusiano ya watu wawili. Kwa nini sasa hatuwi tayari kupokea tofauti nyinginezo? Kwa nini tunapendana kwa matarajio ya kubadilika? Je, sisi ni wakamilifu kiasi cha kuhitaji kitu kikamilifu, tabia kamilifu na mtu mkamilifu? Tunaogopa nini? Kuna shida gani kwa mfano watu wawili wenye imani tofauti kuheshimu tofauti zao bila kuathiri mahusiano yao? Je, hawawezi kuchagua kuishi pamoja kwa kutambua tofauti iliyopo kati ya imani zao na wao wenyewe na kutenganisha imani hiyo na mahusiano yao? Hawawezi kuvumiliana kwa kuheshimu imani zao tofauti na bado wakapendana kwa dhati?
christianbwaya@gmail.com

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia