Tunapambana na UKIMWI kwa kupambana na utu wa watu wanaoishi na VVU?

Hivi majuzi nilipata fursa ya kushiriki mradi unaojaribu kudhibiti maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI kwa kuwasaidia watu wanaoishi na virusi hivyo kukabiliana na hali hiyo ambayo kwa hakika hugeuza kabisa maisha yao. Fursa hii adhimu ilinifungua macho kuona kile ambacho sikuwahi kukiona kwa muda mrefu. Nisingependa kutoa takwimu za tafiti za majumuisho zinazojaribu kuonesha hali ikoje kwa ujumla bali takwimu za hali halisi niliyoiona kwa macho yangu.
__________________________________________________________________________
KWA MAJUMA kadhaa, nilikuwa kwenye mazingira ambayo karibu kila ninayemwona alikuwa anahitaji huduma ya kukabiliana na virusi vya UKIMWI. Na kwa wastani, kila siku niliwaona watu wanaokaribia mia moja (100) wanaotafuta huduma hizi za kitabibu. Na kwa utaratibu ulivyokuwa, ni kwamba mtu asingeweza kurudi kwa mara ya pili katika kipindi cha mwezi mzima. Maana yake ni kwamba kwa mwezi mzima, kila siku watu wapya wasiopungua mia moja , bila kujirudia rudia, iliwabidi kutafuta msaada kuokoa maisha yao kwa usiri mkubwa.

Kwa hakika wengi wa watafuta huduma hawa walikuwa ni watoto na vijana waliojikuta na maradhi haya kwa kuzaliwa. Ni vijana yatima, wengine waliachwa na wazazi wao wangali wachanga. Wanasimuliwa wazazi walifariki kwa maradhi ya UKIMWI. Wengi wao wanatoka kwenye jamii masikini sana. Hawana uwezo wa kupata elimu wala huduma za msingi za kila siku. Wengine wanaishi maisha ya kunyanyaswa, kuonekana hawana maana yoyote kwenye jamii na wanapuuzwa.

Siku moja wapo ya juma, vijana waathirika wenye umri wa kati ya miaka 12 – 20 hukusanyika kupata msaada wa namna ya kukabiliana na hali zao, ambazo, kwa hakika wengi wao wamezaliwa nazo. Nasoma orodha ya wanaojiandikisha. Imefikia 112 ukiacha waliongia bila kujiandikisha.
Mmoja wao ambaye ndio kwanza amemaliza kidato cha sita katika shule inayoitwa ya vipaji maalum na kushinda mtihani kwa Daraja la kwanza Alama Tano katika Fizikia, Kemia na Hisabati, ananiambia, “hata sijui nilifaulu vipi bro…maana nimesoma kwa tabu na adha kubwa. Ndugu wananitenga na kuniona sina haki ya kusoma”, anasita na kumalizia, “wananiona ni wa kufa kesho tu”.

Wote hawa pamoja na kuishi na VVU, wana haki ya kujisikia sawa na mtu mwingine yeyote. Picha: @bwaya
Jamii bado inaamini mtu mwenye virusi vya UKIMWI anasubiri siku ya maziko. Ni suala la muda tu. Tunasahau kwamba hata bila virusi hivyo, ni suala la muda tu kwetu sote.
Kijana huyu anayeonekana ni mwerevu lakini aliyekata tamaa anasema, “Naishi maisha ya usiri mno. Sipendi mtu yeyote ajue kuwa nina VVU”.

Usiri huu unaweza kuelezwa kwa namna nyingi. Mojawapo ni kwamba waathirika wanajua kabisa kwamba jamii inahusisha VVU na vitendo vya uzinzi na uasherati. Kwamba huwezi kupata virusi hivi isipokuwa kwa zinaa. Hakuna binadamu anapenda kuhusishwa na tabia zisizofaa na kukubalika. Kwa hiyo waathirika wanaamua kukaa kimya wasionekane watu wasio na maadili.

Lakini kwa kuwatazama vijana hawa na watoto kwa mamia wanaoletwa na wazazi kupata huduma, ninajiuliza mantiki ya imani hii iliyojichimbia mizizi kwenye akili zetu. Kwa kumwona kuwa mwasherati na mzinzi, tunamtendea haki kijana huyu aliyejikuta na maradhi ya UKIMWI? Anajisikiaje anapotafakari namna alivyojikuta na virusi hivi?

Vijana wa namna hii, wengi wao walihudhuria matibabu kwa muda mrefu wakiamini wanatibiwa matatizo ya kifua, vipele na kadhalika. Mmoja aliniambia, “Nilijua anatibiwa aleji’. Wanapopewa taarifa za kuugua maradhi ya UKIMWI wengi wanakata tamaa na kila kitu kwenye maisha. Na kinachowakatisha tamaa zaidi ni kwa sababu sisi wenyewe tunawachukulia kama watu wasio sawa na sisi. Kwa sababu ni wazinzi, basi gharama wanatakayolipa ni kuwatenga. Hivyo wanajificha na hawasemi hali zao.

Wengine shauri ya kukataa tamaa na maisha na kuchoka kujifikiria kama watu wasio sawa na wengine, wanaamua kujipa haki ya kuwa sawa na wenzao kwa kufanya ngono zembe na watoto wenzao ambao nao, masikini, wanajifunza ngono. Matokeo yake wazazi wasioathirika wanajikuta wanamlea mtoto mwenye virusi vya UKIMWI. Haya ni matokeo ya kuwafanya waathirika wa virusi vya UKIMWI wajione kama watu wa daraja la kubaguliwa. Watu wajiosawa na watu wengine.

Tunavyowaadhibu wanaoishi na virusi vya UKIMWI

Juzi juzi nikimsikiliza mama mmoja, mama wa makamo mtu mzima, ananiambia, “Wakati nina ujauzito wa mwanangu wa tatu, ndipo nilipogundua nimeambukizwa na virusi vya UKIMWI. Nimekuwa nikifikiri ilikuwaje nalia tu na sipati jibu”. Huyu ni mfano wa akina mama wengi, ‘walioletewa’ virusi vya UKIMWI nyumbani bila habari.
Ananiambia, “Katika hali hii ya kukata tamaa, unaenda kanisani ambako ndiko ungetegemea kupata faraja na utulivu wa moyo, unaposikia mchungaji anavyozungumzia UKIMWI kama laana….unajikuta ukiongeza msongo wa mawazo.”

Tunachojifunza ni kwamba tabia ya kuchukulia mambo kwa mtazamo wa jumla ina gharama kubwa. Kudhani tunapoufanya UKIMWI uonekane ni ‘gonjwa hatari na laana’ ni kuwasaidia watu kuachana na tabia mbovu ni kupotoka. Kujua hatari ya tabia haijawahi kuwa sababu ya kukwepa hatari hiyo. Tafiti za mabadiliko ya tabia zinaonesha hivyo.

Pengine ni wakati sahihi tuanze kuuelewa ukweli kwamba UKIMWI ni ugonjwa kama magonjwa mengine. Tangu miaka ya 2004, mgonjwa wa UKIMWI akitumia vizuri dawa za kudhibiti virusi hivyo, anaweza kuishi maisha ya kawaida kama mtu mwingine yeyote. Muhimu ni kutumia dawa kwa usahihi na kwa wakati. Na ilivyo hivi sasa, tofauti pekee ya mtu mwenye virusi hivi na watu wengine ni matumizi ya dawa. Maisha yake ni sawa na maisha ya mtu mwingine yeyote.

Nakumbuka msichana mmoja alipata kuniambia, “Mchungaji aliposikia mchumba wangu ana virusi vya UKIMWI alitutenganisha. Hakutaka kusikia ndoa baada ya hapo”. Huu ni ushahidi kuwa tunahitaji uelewa sahihi wa masuala haya. Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anaweza kuwa na mahusiano na mtu asiye na virusi hivyo bila kumwambukiza. Na hata wakitaka kupata mtoto, inawezekana kabisa mama akabeba ujauzito bila kumwambukiza mumewe wala mtoto atakayezaliwa. Mambo yamebadilika.

Ni lazima kuwatenganisha wenzi wawili wanaotaka kuoana kwa kutumia sababu, “yule ni mgonjwa” kama wao wenyewe hawaoni ugonjwa huo kuwa tatizo? Kwa nini tunawabagua watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI? Tunadhani kuwa na virusi vya UKIMWI ni kukosa haki ya mahusiano kama alivyonisimulia mama mmoja anayeishi na virusi hivi, “Mume wangu alipogundua nina virusi vya UKIMWI nay eye hana, alianza vituko. Alinifukuza”.

Kuwanyima watu wenye virusi vya UKIMWI haki ya kuhusiana na watu wengine si kuwatenga na watu wawapendao? Tunawatumia ujumbe gani? Kwamba kwa kuishi na virusi vya UKIMWI wanakuwa si sawa na binadamu wengine? Kwa hakika kumfanya mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI aonekane ni mtu wa tofauti na watu wengine si kumsaidia. Sana sana tunamfanya ajinyanyapae mwenyewe na matokeo yake ni kuchukua hatua madhubuti za kuwarubuni wengine wawe kama yeye.

Ni kweli wapo wengi tu walioambukizwa virusi vya UKIMWI kama matokeo ya tabia. Na wakati mwingine wasingependa ionekane hivyo. Lakini je, tunayo sababu ya kuwafanya wajione kuwa raia daraja la mwisho 'wanaosubiri kifo'? Bwana mmoja siku moja ananiambia, "hata sijui ofisini walijuaje. Kila mmoja amenibadilikia. Nahisi kusemwa kila wakati na sijiamini kabisa. Na hii imeathiri sana ufanisi wangu kazini". Ndivyo ilivyo. Tumejihesabia haki  kupita kiasi na kuwaona wanaoishi na virusi vya UKIMWI kama watu 'waovu' kuliko sisi. Tunawafanya waishi maisha ya usononi na usiri uliopitiliza. Maisha ya kukata tamaa. Matendo haya wanawasaidiaje?

Mapambano dhidi ya UKIMWI yasiwe unyanyapaa

Siku ya Wajibu wa Blogu. Picha: www.blogactionday.org
Tunapopambana na virusi hivi kwa kampeni za hadharani, tunazungumziaje UKIMWI? Tuwasaidieje watu wenye virusi vya UKIMWI kujisikia kuwa sehemu ya jamii? Kuzungumzia UKIMWI kama laana inayowahusu wezi wa wake za watu kunasaidia kutatua chochote? Matokeo yake mazungumzo hayo yanamfanya mtu anayeishi na virusi hivyo ajijengee mtazamo hasi, ajilinde kwa kujificha na wakati mwingine afanye vitendo asivyotarajia kama namna ya kutafuta kuwa sawa na wengine. Hali hii haimsaidii yeye wala jamii kwa ujumla.

Katika kuadhimisha siku ya wajibu wa blogu Duniani, pengine tutafakari kwa kina namna tunavyoweza kuwafanya waathirika wa UKIMWI kujisikia kuwa watu wanaostahili usawa na haki kama watu wengine. Pengine ni muhimu tuwaone kama watu wengine wanaougua maradhi haya kama wanavyougua wengine. Kama ambavyo mgonjwa wa sukari hajifichi, kwa hofu ya kunyanyapaliwa, ni vyema tuweke mazingira yanayowafanya wenzetu wanaotumia dawa za kudhibiti virusi vya UKIMWI kujiona kuwa bado ni sawa na watu wengine. Kwa kufanya hivyo, tunawasaidia kugeuza imani, mitazamo na tabia zao kwa ujumla na hivyo kuwafanya waishi maisha ya furaha, amani na yenye matumaini. Si ndoto. Inawezekana.

christianbwaya@gmail.com

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?