'Usawa wa kijinsia' unavyoweza kuharibu mahusiano

Wanawake wanatafuta haki ya kuwa sawa na wanaume. Na wamefanikiwa. Katika makala haya tunajaribu kuonesha hatari ya wanawake kudhani wanaweza kuwa sawa kijinsia na wanaume na bado waweze kuwa na mahusiano imara na wanaume. Ni salama zaidi kwa wanawake kuelewa kwamba usawa wa kijinsia haumaanishi kufanana kwa wanaume na wanawake. Ingawa ni kweli tunapigania usawa wa fursa, bado twapaswa kutambua haitawezekana wanaume wakageuka kuwa wanawake na wanawake kadhalika wakageuka kuwa wanaume.
__________________________________________________________________________
NIOMBE msamaha kwa wasomaji wanaopenda kusoma kila kitu kwenye makala moja. Sikudhani kwamba ingewezekana kufanya hivyo kufuatia uzito wa suala lenyewe la mahusiano. Badala yake, niliamini kwa kuzungumzia suala moja moja, kidogo kidogo, suala baada ya jingine, ningeweza kugusia masuala mengi yanayoweka msingi wa tunachojaribu kukijadili kwenye mfululizo huu.

Vile vile nishukuru kwa mwitikio mzuri nilioupata tangu mfululizo huu uanze. Nimepata mrejesho mzuri sana kuwahi kupata tangu nianze kublogu. Kilichonisisimua zaidi ni utayari wa wasomaji wangu wengi kunishirikisha uzoefu wao wa kimahusiano na hivyo kunipa fursa adimu ya kujifunza tena na tena. Nawashukuru sana.

Kwa mhutasari tu, tunaweza kusema kwamba mahusiano bora ni matokeo ya utayari wa wenzi kulipa gharama za kujua na kujibu mahitaji ya mwenzake. Mahusiano bora si matokeo ya kukutana na 'mtu sahihi' anayekufanya uwe na furaha by default, bali jitihada za kutenda jambo sahihi kwa wakati. Jitihada hii ndiyo kipimo cha kijana anayetaka kuingia kwenye mahusiano. Kijana asiye tayari kujitoa kuelewa na kushughulikia mahitaji ya mwenzake, hayuko tayari kuingia kwenye mahusiano.

Katika makala ya leo nitaanza kujadili, kama nilivyoahidi, sababu za watu wanaopendana kuanza kupishana na hatimaye kujikuta wakishindwa kuwasiliana ipasavyo, hali ambayo ndio daraja la migogoro ya kimahusiano.

'Usawa wa kijinsia' katika ndoa hauwezekani

Sababu ya kwanza, ni kueleweka vibaya kwa dhana ya 'usawa wa kijinsia'. Najua hatari ya kuzungumzia suala tete kama usawa wa kijinsia kwa 'mtazamo hasi'. Nitaomba uvumilivu. Ni ukomavu kusoma mawazo usiyoyapenda kwa utulivu na kwa nia ya kuelewa kinachozungumzwa kisha uamuzi wa usahihi au upotofu wa kinachosemwa ukabaki kuwa haki yako mwenyewe.

Harakati za usawa wa kijinsia zinaelekea kufanikiwa. Jamii imebadilika, na hatimaye sasa wanawake wengi wanakwenda shule tofauti na ilivyokuwa hapo zamani. Shule zimewasaidia akina mama wengi kupata kazi za maana zilizokuwa nadra sana kuzipata siku za nyuma. Iwe kwa upendeleo maalum, au kwa uwezo halisi unaoneshwa na akina mama, ni wazi kuwa uhalisi wa nadharia ya usawa wa kijinsia imeaanza kuonekana. Na ni jambo jema kabisa tena la kupiganiwa na kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo.

Usawa wa kijinsia au ni utofauti wa kijinsia? Picha: developmentdiaries.com
Hata hivyo dhana hii ya 'usawa wa kijinsia' inaleta dosari pale inapovuruga namna wanawake wanavyohusiana na wanaume. Mwanamke, aliyeiva 'haki za wanawake' anapoanza kuamini kuwa 'yuko sawa na mwanaume' kwenye ndoa yake, anahatarisha si tu hisia za mwanaume, bali hata usalama na uhai wa ndoa yake. Nitaeleza.

Katika enzi za 'ujima' wanawake, ambao wengi hawakuwa na elimu, walikuwa watu wa kukaa nyumbani. Majukumu makubwa ya mwanamke yalikuwa ni kulea familia kwa maana ya kuwatunza watoto, mume pamoja na kuweka mazingira ya nyumba katika hali inayofaa. Hiyo ndiyo ilikuwa 'ajira' kuu ya mwanamke iliyoshuhudiwa na wanaume wengi wa sasa.

Ni mwanaume, ambaye kimsingi jamii ilimpendelea, ndiye aliyekuwa na jukumu la kutafuta mkate wa kila siku. Ndiye aliyekuwa na wajibu wa kuhakikisha familia yake inakula na kushiba. Kama kingekosekana chakula ndani ya nyumba, yeye ndiye aliyekuwa na majibu. Hapakuwa na ambiguity ya majukumu. Mwanaume ni mtafutaji, mwanamke ni mlezi wa watoto. Waswahili wengi tulilelewa  hivyo.

Pamoja na matatizo ya mfumo huo wa ujima, bado mfumo huo ulimwezesha mwanaume kupata ile 'heshima' ambayo tulikubaliana ndiyo hitaji la msingi la kihisia la mwanaume wa kawaida na ulimfanya mwanaume kujisikie 'in total control', na hivyo 'kile kiburi' cha uanaume kililishwa ipasavyo.

Mwanamke naye, kwa kuwajibika na shughuli za nyumbani muda wote, aliweka mazingira sawia ya kumtuliza 'mzee' akirudi nyumbani na stress za kutafuta mkate. Kwa kukaa nyumbani, nguvu zake zote aliziwekeza kwenye mahusiano na mume wake, watoto wake na majirani. Kwa namna hiyo, aliweza kumfanya mzee awe na utulivu wa moyo awapo kwenye mihangaiko yake kazini.

Ingawa ni kweli wapo wazee walioa wanawake wengine, hiyo ilikuwa kimila kuliko ilivyokuwa kimahitaji. Na ilipokuwa kihisia, suala lilikuwa utamaduni wa wanawake kuamini mahusiano huja bila kujishughulisha. Kwa hakika si kila kilichofanywa zamani kilikuwa sahihi na lakini angalau yalikuwepo matarajio fulani ya kijinsia yaliyofanya mambo yakawa shwari kwenye ndoa na ikawa nadra watu kupishana kiasi cha kupeana talaka.

Matarajio ya wanawake na wanaume yamegeuzwa

Hivi sasa ni kwamba 'maendeleo' yametufanya tusijue kwa hakika nani anatakiwa kufanya nini kwenye familia. Mwanamke anatarajia mwanaume awe kama mwanamke na yeye mwanamke anajifikiria kama mwanaume. Mwanaume naye kwa upande wake anatarajia mwanamke awe 'empowered' kiasi cha kutosha kutafuta mkate wa kila siku ili 'kwa pamoja wasaidiane kulisha familia' tofauti na ilivyo kuwa zamani wakati naye anashindwa kuwa 'kama mwanamke' kwa majukumu ya nyumbani.

Sasa ilivyo, ni kwamba mwanamke huyu, anayeshughulika na kazi sawa sawa na mwanaume, anayechoka na stress za kazi kama alivyo mwanaume, anatamani anaporudi nyumbani akutane majukumu yote yamefanywa. Bahati mbaya ni kwamba anaporudi nyumbani anajikuta akibaki kuwa 'mwanamke' yeye peke yake, maana mwanaume ndio kwanza anaurudia uanaume wake kinyume na matarajio yake. Wakati mwanamke aliyechoka na kazi kama mume wake anatamani mme wake amsaidie kuingia jikoni, kuosha vyombo na kupeleka maji jikoni,  mume ndio kwanza anatamani ashike gazeti kujipumzisha akisubiri kula chakula kilichoandaliwa na mwanamke akalale. Stress.

Matokeo ya mwanaume kugoma kuwa kama mwanamke nyumbani, wakati anatamani mwanamke awe kama mwanaume kazini, yanamfanya amfanye mwanamke ajisikie hapendwi. Kumbe na yeye kwa upande wake, pamoja na kutamani kuwa sawa na mwanaume kazini, bado amejizidishia matarajio kwa kutaka kisichowezekana kwa wanaume wengi ambao hawako tayari kugeuka kuwa wanawake katika mazingira ya nyumbani.

Katika kujaribu kutatua mkanganyiko huu, wakati mwingine imebidi wasichana wa kazi watafutwe. Wasichana hawa, ambao hujikuta katika mazingira ambayo wenye nyumba wote ni 'wanaume', na hivyo kuwa ndio wanawake pekee kwenye nyumba. Wanaolea watoto, wanafua nguo zote, wanapika, wanafanya karibu kila kitu. Matokeo yake mwanaume huanza ku-appreciate majukumu ya 'mwanamke' huyu ambaye sasa anakuwa kama 'mwanamke pekee' kwenye nyumba, hali inayomfanya mwanamke halisi kuanza kuona tofauti ambayo mwisho wake ni majeraha.

Usawa wa kijinsia si kufanana kijinsia

Usawa wa kijinsia kwa mazingira haya unawafanya wanaume wakose mwelekeo na bila wao kujua  hujikuta wanahitaji wasichokijua. Mke anayetafuta kupanda ngazi ya mafanikio ya kikazi anajikuta anasahau majukumu yake ya 'asili', hali inayojenga matarajio yasiyowezekana kwa mwanaume ambaye naye anaishia kuwa frustrated.

Hizi frustrations ndizo zinazopunguza mawasiliano ya mioyo wa wenzi, na hivyo kuwa chanzo cha kila mmoja kupunguza ari ya kujishughulisha kuelewa na kujibu mahitaji ya mwenzake. Hili likitokea, ni rahisi mengineyo kama wivu, hasira, na hata michepuko kutokea. 

Katika mazingira haya ya usawa na haki za wanawake, pengine ni vyema wanawake kutambua kwamba usawa wa kijinsia haumaanishi kufanana kwa wanaume na wanawake. Hii ikiwa na maana kuwa ni salama zaidi wanawake kutambua tofauti yao na wanaume kihisia (emotional differences).

Ingawa ni kweli tunapigania usawa wa fursa, shule, kazi na kadhalika, bado twapaswa kutambua haitawezekana wanaume wakageuka kuwa wanawake na wanawake kadhalika wakageuka kuwa wanaume. Tutambue mahitaji ya wanaume hayafanani na yale ya wanawake.

Wakati tunahakikisha akina mama wanapata fursa sawa na wanaume, pengine ni wakati wa kutambua kwamba katika ndoa, hiyo nadharia ya usawa wa kijinsia haifanyi kazi, na inapotokea ikafanya kazi matokeo yake huwa si ya kufurahisha sana.

Tunahitaji 'smooth transition'?

Pengine tunahitaji mabadiliko ya taratibu. Tuanze na hatua ya kwanza ya kutambua mahitaji tofauti ya kijinsia. Kutambua tofauti hizo kuwasaidie wanawake kupunguza matarajio yao kwa wanaume. Kwamba ni kuzidi kiasi kutarajia usawa ulio kinyume na imani za wanaume.  Mwanaume aliyelelewa akimwona mama yake  kambeba mtoto mgongoni,  hawezi kujikuta kambeba mtoto mgongoni kwa kisingizio cha 'maendeleo ya kijinsia'. Ni makosa kutarajia yasiyowezekana.

Kadhalika, ni vyema wanaume kuelewa enzi zinawadai kuwa sensitive zaidi na mahitaji halisi ya mwanamke kuliko ilivyokuwa kwa baba zao. Wanawake wa enzi za 'usawa wa kijinsia' wana stress nyingi mno. Kazini wanapambana kufikia 'kimo' cha wanaume, na nyumbani wanapambana kurudi kwenye asili ya jinsia yao. Ni vizuri kuelewa mahitaji yao katika mazingira haya na kuwasaidia kuelewa kinachowakabili.

Vinginevyo, enzi hizi zimekuja na mzizi mpya wa matatizo ya kimahusiano. Ukizitambua na kuzifanyia kazi mapema, unaweza kupunguza matatizo. Katika makala yanayofuata, tutaangalia kwa kina wivu na jinsi wivu usiposhughulikiwa unavyoweza kuharibu mahusiano.

Msingi wa hoja ya leo unajengwa kwa kutumia nadharia ya John Gray, mwandishi wa kitabu cha 'Why Mars and Venus Collide'.
Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?