Iweje waliotulia hawaolewi, aolewe huyu asiyetulia?

Si mara zote uhusiano wa ndoa ni matokeo ya upendo kama inavyotarajiwa. Yapo mahusiano mengi tu ya ndoa ambayo kimsingi ni arrangements za watu kujipatia mahitaji mengine kabisa yasiyohusiana na mapenzi. Katika makala haya, tunajaribu kuonesha kwamba si kila mwanamke aliyeolewa maana yake ni kuwa anafaa na kadhalika, si kila asiyeolewa maana yake ni kuwa hafai.
__________________________________________________________________________
SWALI kutoka kwa msomaji wangu mwingine linasomeka kama ifuatavyo:


“I dont believe all wives are wife material (Siamini wanawake wote wanafaa kuoelewa). Wapo wanaoolewa kwa kuwa Mungu alipanga iwe hivyo and you people call it lucky (wengine wanaita bahati ). 
And there are single ladies single mothers who are so obedient and mannered but not married. (Kuna wanawake na akina mama hawajaolewa na bado wana heshima na tabia njema) So kuolewa ni tabia njema ya mwanamke au mipango ya Mungu???” anamaliza.

Nakushukuru sana msomaji wangu kwa kufuatilia blogu yetu. Mrejesho kutoka kwa wasomaji ni sehemu ya uhai wa blogu. Shukrani sana. Sasa twende moja kwa moja kwenye swali lako:

Sababu za wanaume kuoa hazifanani

Si mara zote uhusiano wa ndoa ni matokeo ya upendo kama inavyotarajiwa. Yapo mahusiano mengi tu ya ndoa ambayo kimsingi ni arrangements za watu kujipatia mahitaji mengine kabisa yasiyohusiana na mapenzi. Ndoa zimeanza kuwa 'fursa' za kujinufaisha kibinafsi na zinameanza kupoteza dhana halisi ya mahusiano. Ndoa zimeanza kuchukuliwa kirahisi kama ubunge na udiwani unaopatikana hata kama huwapendi wapiga kura.

Aina mpya ya usaliti wa mahusiano. Picha theheraldng.com 
Wapo watu huoa ili waweze kupata uhamisho wa kikazi ‘kumfuata mwenzi’. Wapo wanaooa fedha na elimu na hawafikirii kingine chenye maana 'takatifu' ya ndoa. Wengine wanaoa kupata ‘watumishi wa ndani’ watakaosaidia kupika, kufua, kusafisha nyumba na kadhalika. Wengine wanawachukulia wanawake kama ‘viwanda’ vya kuwazalia watoto. Wapo wanaooa ili kupata ‘heshima’ ya marafiki au jamii kwamba jamaa siku hizi kaoa. Wanataka kufikia matarajio ya wengine. Zote hizo ni ndoa na zaweza kuwa halali.

Kwa hiyo tunaweza kusema kwa hakika, wapo wanaume tena wengi tu huoa si kutafuta utoshelevu wa kihisia kwenye ndoa. Hawana habari na kujua na kujibu mahitaji ya‘mwenzi’ na wala hawafikirii namna ya kuwekeza kwenye ndoa ili kadhalika waweze kupata mahitaji yao ya kihisia. Badala yake, ndoa kwao ni nyenzo ya kujipatia 'raslimali watu' itakayowafaa kwa shughuli nyinginezo, wakijua kuwa mahitaji yao ya kihisia watayakidhi kupitia michepuko.

Si kila anayeolewa ni ‘wife material’

Kwanza haiwezekani kila mwanamke awe wife material. Tofauti ya malezi, imani, mitazamo na mambo mengine kibao, kama usawa wa kijinsia unaopiganiwa siku hizi, vyote hivyo vimewafanya wanawake wasikidhi vigezo vya kuoleka achilia mbali kuolewa kwa sababu ya kuwa na sifa za kuolewa. 

Na kama tulivyoona katika aya zilizopita, yapo mazingira ya kutosha kuwafanya wanawake kuolewa kwa sababu nyinginezo nje ya ‘kuwa na sifa za kuolewa’. Pengine wanacho kile kinachotafutwa na baadhi ya wanaume wanaojali ‘mengineyo’ zaidi ya upendo. Hivyo wanaolewa kama bidhaa, vitu, viwanda, wafanya kazi na kadhalika. 

Ndio maana unaweza kushangaa wanawake wajeuri, wazinzi, wababe, wasiopenda kwa dhati, bado wanaweza kuolewa kwa sherehe kubwa tu. Kwa nini? Ni kwa sababu wanaume wanaowaoa wanaotafuta bidhaa. Kwa wanaume wa jinsi hii wala usishangae wanawake wenye nidhamu, unyenyekevu na maadili wakaonekana si lolote.

Umejiwekea mazingira ya kukutana na ‘waoaji’?

Kwa upande mwingine, wapo wanawake wazuri, werevu, waadilifu, waaminifu na kila aina ya sifa njema hawaoelewi. Pamoja na sababu nyinginezo, huenda hawajajiweka katika mazingira ya kuonana na waoaji! Tulisema huko nyuma watu huhusiana na wale wanaowajua. Kadri unavyoonana na watu ndivyo wanavyokujua na vetting yao kwako unaweza kuzaa matokeo.  

Sasa kama mwanamke kwa sababu moja au nyingine haonani na watu, iwe kwa aibu, kazi nyingi, dharau na kadhalika, inaweza kumwia vigumu sana kuonekana. Kujenga urafiki unaoweza kuelekea kwenye mahusiano serious kunaanzia kwenye kukutana. Hukutani na watu, hata kama unafaa, unajiharibia mwenyewe na baadae unalalamika 'huna bahati'.

Wengine pamoja na uzuri na ‘utakatifu’ walionao, hawajijengei taswira nzuri kwa wanaume ‘waoaji’. Chukulia mfano wanawake wabishi, wenye majigambo, wasiojua kusikiliza, wanaoamini wanajua kila kitu, watetezi wa usawa wa kijinsia uliozidi mipaka na kadhalika. Hawa hata kama wanao uzuri wa nje, wanaweza kujikuta wakiwa ‘bidhaa’ ya wanaume wakora wanaotafuta michepuko na sio mahusiano ya kudumu. Na wakiolewa, hujikuta wakiangukia kwenye kundi la wanaume wanaowachukuliwa wanawake kuwa njia ya kufikia malengo yao mengine ya kimaisha.

Ndio kusema, si kila mwanamke anayeolewa basi ni mwadilifu, na si kila asiyeolewa hafai. Kinachogomba ni umeolewa kwa sababu gani? Umependwa kwa sababu mwanaume anaamini unaweza kujibu mahitaji yake ya kihisia, au umeolewa kama nyenzo ya mwanaume huyo kufikia malengo yake mengine ya kimaisha? Je, hujaolewa kwa sababu hufai, au umeshindwa kujikutanisha na wanaume ‘waoaji’ na kuwathibitishia unavyoweza kujibu mahitaji yao ya kihisia?

Si kila aliyeolewa, ameolewa kwa bahati na mipango ya 'mungu’. Kadhalika kwa wasioolewa. 
Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Uislamu ulianza lini?