Mambo ya Kufanya Unapotafuta Kazi

INGAWA inafahamika kuwa wapo wahitimu, tena wengi tu, ambao hufanya maamuzi ya kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata darasani kujiajiri wenyewe, kwa maana ya kubadilisha maarifa na ujuzi walionao kuwa bidhaa pasipo kumtegemea mtu aitwaye mwajiri, bado tunajua kuwa wahitimu wengi, kadhalika, huchagua kutafuta ajira. Kwao, huona ni rahisi kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao kwa njia hiyo.
Makala haya yanasaili mambo yanayoweza kumsaidia mhitimu anayetafuta ajira kupata taarifa zinazohusiana na namna bora ya kuwasiliana na mwajiri kwa matumaini ya kupata ajira anayoitegemea.

Dhana ya soko la ajira


Mhitimu anayeamua kutafuta ajira ili kuendesha maisha yake, kimsingi tunaweza kusema, anaingia kwenye soko liitwalo la ajira. Na kama yalivyo masoko mengine, soko hili ni uwanja unaowakutanisha watu wenye mahitaji ya aina mbili yanayotegemeana kwa karibu. Mmoja akiwa na bidhaa ya ujuzi na weledi, lakini akiwa na hitaji la kujipatia kipato kwa kutumia ujuzi au maarifa anayoamini anayo. Huyu ni mtafutaji kazi. Mwingine, si tu anao uhitaji wa ujuzi na weledi huo ili kutafuta majibu ya changamoto za kazi zake lakini anazo pia raslimali za kuulipia. Huyu anaitwa mwajiri. Pande hizi mbili zinahitajiana na kutegemeana kwa maana ya hitaji la mmoja huwa ni jawabu la mwingine.

Inapotokea mahitaji ya pande mbili hizo, yaani mwajiriwa na mwajiri yakakutana hapo tunasema kuna kuajirika, employability. Kwa maana nyingine, mtafutaji kazi anatarajiwa kuonyesha ujuzi na uwezo wa kutumia maarifa aliyonayo katika kutatua changamoto za kikazi zinazomkabili mwajiri, kwa weledi unaotakiwa. Na mwajiri mtarajiwa naye kwa upande wake, anapaswa kuonyesha uwezo wa kukidhi mahitaji ya kiuchumi aliyonayo mtafutaji kazi, ambaye ni mwajiriwa mtarajiwa.

Kutokana na ukweli kwamba waajiriwa hutofautiana ujuzi na uwezo huo, na kwa sababu uwezo wa waajiri kadhalika hutofautiana, na kwa kuwa haiwezekani kila mwenye ujuzi anakidhi mahitaji ya mwajiri, hapa ndipo ushindani wa soko la ajira unapojitokeza. Kwa hiyo ni jukumu la mtafuta kazi kujiandaa ipasavyo kiujuzi na kiweledi ili kuweza kushindana vyema katika soko la ajira.

Kufuatilia habari za ajira unayoitafuta

Mtafuta kazi anawajibika kufuatilia kwa karibu taarifa za nafasi za kazi kupitia vyanzo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti, tovuti zilizoandaliwa maalumu kwa ajili hiyo kama hii, pamoja na njia nyingine za kupeana taarifa kama Twita na kadhalika.

Vile vile, Wizara ya Kazi na Ajira ina kitengo maalumu kiitwacho Wakala wa Huduma za Ajira, TaESA ambao pamoja na majukumu mengine hutoa huduma ya ushauri na takwimu juu ya masuala ya ajira kwa waajiri na watafutaji kazi, kusambaza taarifa za soko la ajira kwa wadau mbalimbali pamoja na kuunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, ni jukumu la anayetafuta kazi kutafiti na kujua nafsi za kazi zinazotangazwa ili kuelewa matarajio halisi ya mwajiri wake mtarajiwa na hivyo kujaribu kuonyesha namna anavyokidhi matarajio hayo kupitia wasifu wake binafsi na barua ya maombi ya kazi.

Kuandaa nyaraka zinazohitajika

Pamoja na maandalizi ya kiujuzi anayopaswa kuyafanya mtafuta kazi, ili kushindana vyema, ni busara kuandaa nyaraka zitakazokusaidia kutambulisha ujuzi na uwezo ulionao.



Picha: @bwaya

 Nyaraka hizo ni pamoja na:
1) wasifu/maelezo binafsi (curriculum vitae)
2) vyeti na nyaraka nyingine za kitaaluma
3) barua ya maombi ya kazi
4) barua za kupendekezwa na watu wanaoaminika.

Nyaraka hizi ndizo zinazokutambulisha kwa mwajiriwa wako mtarajiwa pasipokukutana na wewe. Kwa kuwa nyaraka hizi hutumika kufanya maamuzi ya ama kukuita kwa usaili au kukuacha, upo umuhimu mkubwa wa kuziandaa kwa umakini mkubwa.


Kundaa wasifu binafsi (curriculum vitae)


Wasifu binafsi ni maelezo yanayoeleza ujuzi, maarifa, uzoefu na weledi alionao mtafuta kazi anaoamini utamvutia mwajiri kumwita kwenye usaili na hatimaye kumwajiri. Katika kuandaa maelezo haya, ni vizuri kuelewa mahitaji mahususi ya mwajiri mtarajiwa kama tulivyojadili katika makala iliyopita.

Katika kuandika wasifu binafsi, mambo saba ni ya muhimu kuzingatia:

1) Taarifa za msingi za mtafuta kazi 

Weka taarifa kama vile majina yako kamili, jinsia, hali ya ndoa, tarehe ya kuzaliwa, utaifa na njia muhimu za mawasiliano. Taarifa nyingine zaweza kuwa muhimu lakini zisizo na ulazima wa kufahamika. Hizi ni kama kabila, dini, idadi ya watoto, mitazamo au ufuasi wa kisiasa, malengo na kadhalika.
Mfano:
        Name:
        Nationality: Tanzanian
        Permanent Residence: 
        Birth date: 
        Marital status: 
        Postal Address: 
        Mobile: +255(0) 754 870 815
        E-Mail: bwaya@mwecau.ac.tz

Taarifa kama mahali pa kuzaliwa, majina ya wazazi na kazi zao yanaweza kuonekana kwenye cheti cha kuzaliwa ambacho ni kawaida kuambatanishwa, kwa hiyo nazo hakuna sababu ya kuzitaja.


2) Sifa za kitaaluma

Anza na ngazi ya juu zaidi iliyofikiwa mpaka ngazi ya chini. Uandikaji unaotumika zaidi ni kuonesha tunuku ya kitaaluma (mfano cheti, Stashahada, shahada nk) ikifuatiwa na taasisi ya kitaaluma iliyotoa tunuku hiyo na mahali ilipo (mfano shule, chuo na kadhalika) pamoja na mwaka ulipotolewa.
Mfano;             
                          2013-2016: Shahada ya Sanaa katika Stadi za Mazingira
                                                   Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge  

Kwa kawaida, sifa hizi huwa ni zile zinazohusiana na mafunzo ya ujuzi yatolewayo kwa ngazi ya chuo, lakini inapotokea ngazi hiyo haina sifa nyingi, basi si vibaya kuonyesha angalau mpaka ngazi ya Cheti cha Elimu ya Sekondari na Cheti cha Juu cha Elimu ya Sekondari.


  3) Uzoefu na historia ya kuajiriwa.

Hapa mwombaji huonyesha ajira alizowahi kuzifanya, tangu apate ujuzi aliouonyesha kwenye kipengele cha 2) hapo juu, iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea kwa kueleza kwa kifupi majukumu aliyofanikiwa kuyatekeleza huko alikowahi kupita.

Uzoefu huu, huandikwa kwa mtiririko wa aina ya kazi iliyowahi kufanywa, kuanzia ya hivi karibuni zaidi au uliyonayo, taasisi husika pamoja na mwaka wa kuanza na kumaliza kazi hiyo.

Ni hapa ndiko mwomba kazi ataonyesha alichowahi kukifanya au kusababisha kitokee kwenye kazi alizowahi kufanya. Mwajiri kwa kawaida huvutiwa zaidi na mwombaji anayeonyesha namna alivyoweza kuleta ufanisi huko alikokuwa kwa matumizi ya maneno kama "kuzalisha/kuongeza (ufanisi)", "kupunguza/kuondoa (changamoto)", "kubuni", "kuanzisha", "kusababisha", "kubadili", "kuchangia mabadiliko", "kuwezesha", na kadhalika.

Kwa mhitimu ambaye hajawahi kuajiriwa, hapa anaweza kuonesha mafunzo aliyowahi kuyafanya kwa vitendo pamoja na kazi za kujitolea na jinsi zilivyomfanya alete tofauti fulani kama mwenzake aliyewahi kuajiriwa.

4) Ujuzi na weledi

Baada ya kuonyesha uzoefu wa kikazi alionao, mwombaji huonyesha aina ya ujuzi na weledi aliowahi kuupata kupitia shughuli, warsha, makongamano na kadhalka yalivyomsaidia kuongeza ujuzi mwepesi unaomsaidia "kuzalisha", "kukuza", "kubuni", "kuanzisha", "kusababisha", "kubadili", "kuchangia mabadiliko", "kuwezesha", na kadhalika. Kama ilivyo ada, ataonyesha mahali, mwaka, shughuli husika na malengo yake kwa mtiririko wa kuanzia hivi karibuni mpaka yale ya zamani.

5) Machapisho na tafiti

Kama kazi inayoombwa inahusiana na masuala ya taaluma na elimu (mfano ualimu, ukufunzi, tafiti, uhadhiri na kadhalika), mwombaji huonyesha machapisho na tafiti alizowahi kuzifanya na kuziandika. Hapa, ataonyesha jina la chapisho, mwaka lilipochapishwa. Lengo ni kuonyesha kwamba ameshiriki katika kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili jamii, pamoja na kuchangia maarifa yaliyopo.

6) Tuzo au heshima alizowahi kupewa mwomba kazi. Hapa ndiko iliko fursa ya kuonyesha namna mwombaji alivyowahi kutambuliwa katika ajira zilizopita kwa kuonyesha tuzo za kutambua mchango wake katika kazi zake. Si lazima iwe kazini tu, yaweza kuwa katika masomo, lakini tuzo zenyewe zapaswa kuwa tofauti na zile tunuku za kitaaluma moja kwa moja.
Mwajiri huvutiwa na mtu anayeweza kuonyesha namna jitihada zake zilivyoweza kuwafanya watu kuona matokeo ya kazi zake na kuamua kumtuza, au kumtambua kwa namna moja au nyingine.

Maneno kama, "nilishinda", "nilituzwa", "nilitambuliwa", nilizawadiwa" na kadhalika, kwa sababu ya shughuli, majukumu, jitihada zilizowahi kufanywa, yanamwongezea mwombaji nafasi ya kukubalika.

Ni vigumu kutamani kumwajiri mtu aliyefanya kazi kwa miaka 10 mahali, na hajawahi kutambuliwa kwa chochote.

7) Orodha ya wadhamini

Taja watu wanaoaminika wanaoweza kutoa ushuhuda wa uwezo na weledi wa mwombaji. Hapa, mwombaji ataorodhesha angalau watu watatu wanaomfahamu vizuri iwe kwa kumfundisha au kufanya nae kazi wakiwa na nyadhifa zinazotambulika. Ni vizuri kuwasiliana nao kabla ya kuwataja kwa kuwa wanaweza kuulizwa pasipo mwombaji kujua. Na wakati mwingine ni vyema kuwaomba kukuandikia barua ya utambulisho ukazitumia inapolazimika.

Dokezo muhimu

Wasifu binafsi hubadilika kulingana na mahitaji ya mwajiri (ujuzi na uzoefu unaohitajika) na hivyo huboreshwa kukidhi mahitaji. Ni muhimu kukumbuka kwamba uandishi wa maelezo binafsi hutegemeana na matarajio mahususi ya mwajiri na ari ya mwombaji wa kazi katika kujieleza. Maelezo yanayovutia, yenye kina kwa kiasi, pamoja na nyaraka nyinginezo zinazotakiwa, huongeza uwezekano wa kumshawishi mwajiri kuona umuhimu wa kumwajiri muhusika.

Kadhalika, ni vyema kuelewa kwamba mwajiri au yeyote anayepitia maombi, hana muda mrefu wa kusoma "kitabu" cha maelezo binafsi ya mwombaji. Hivyo, ni vizuri kuandika kwa ufupi kwa kutumia maneno sahihi katika kueleza uwezo wako ipasavyo.

Soma namna ya kuandika barua ya kuomba kazi hapa


Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz   

Maoni

  1. Ndugu Bwaya uzidi kubarikiwa na muumba, vijana wengi sana hata wahitimu wa vyuo vikuu
    hawawezi kabisa kuandika barua za kuomba kazi.Shida wengi wao wanajifanya wajuaji hata kujifunza hawataki.

    JibuFuta
  2. Asante sana ndugu Mlambo kwa kusisitiza umuhimu wa kila mwanajamii kutoa mchango wake kutatua tatizo tulilonalo. Ni kweli vijana hawajapata fursa ya kujifunza mambo haya wanayoyahitaji. Tuwasaidia wale wenye nia ya kujifunza kupata fursa hiyo pale tunapoweza.

    JibuFuta
  3. Umeongea fact mkuu wahitimu wanahitaji msasa kama huu lasivyo wataziona taaluma zao ni mizigo vichwani mwao

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging