Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -2
PICHA: Shutterstock
|
Katika makala yaliyopita
tuliona mbinu tatu unazoweza kuzitumia kuelewa mambo unayojifunza. Kwanza, ni ‘njaa’
inayokusukuma kuelewa. Unapokuwa na ari ya kuelewa jambo, mara nyingi,
utahamasika kulielewa bila kutumia nguvu nyingi.
Pili, tuliona ni muhimu
kutengeneza picha kubwa ya jambo unalojifunza kabla hujaanza kujifunza undani
wa mambo madogo madogo ndani ya picha hiyo.
Kwa mfano, unaposoma
aina za vyakula, lazima kwanza uelewe vyakula. Uelewa wa jumla wa vyakula
utakurahisishia kazi ya kuchanganua aina zake kwa sababu tayari unayo rejea utakayoitumia
kuelewa zaidi.
Mbinu ya tatu ni kukihusisha
kitu unachokisoma na mambo unayoyafahamu tayari. Unaposoma aina za vyakula, kwa
mfano, lazima uwe unafikiria vyakula mbalimbali unavyovifahamu katika mazingira
yako.
Unapojaribu kuhusianisha
kile unachokisoma na maisha yako ya kila siku, unaurahisishia ubongo wako kazi
ya kupokea kuliko kuingiza kitu kipya kisichohusiana kwa vyovyote vile na kile
kilichopo kwenye ufahamu tayari.
Katika makala haya, tunaendelea
na mbinu nyingine tatu zinazoweza kukusaidia kuyaelewa na kuyamiliki maarifa.
Jitathmini kadri unavyosoma
Nakumbuka kuna wakati
tulikuwa tukisoma darasani usiku. Mwenzetu mmoja alitoka nje kujinyoosha apunguze
usingizi kabla hajaendelea na mkesha.
Bwana mmoja aliyekuwa
anapenda masihara aliamua kwenda kubadilisha ukurasa wa kitabu ambacho mwenzetu
huyu alikuwa anakisoma. Baada ya dakika kadhaa, mwenye kitabu alirudi na
kuendelea kusoma kwenye ukurasa ule ule uliobadilishwa bila yeye kujua.
Ndivyo wanavyosoma
wanafunzi wengi. Wanatumia muda mrefu kusoma bila kutathmini kile
wanachokisoma. Hili ni kosa kubwa kwa mtu mwenye kiu ya kuelewa.
Bila kufanya tathmini,
unaweza kuingiza mambo mengi kichwani lakini hujui yanakwenda kuhifadhiwa
kwenye eneo gani ubongoni mwako. Kama tulivyosema, ni vyema kinachoingia kwenye
ubongo wako kielekezwe kwenye eneo linalohusika ili iwe rahisi kukitumia.
Jifunze kujifanyia
tathmini kadri unavyosoma. Jiulize namna gani kile unachokisoma kinahusiana na
mambo unayoyafahamu.
Tuchukulie unasoma aina
za vyakula vinavyosaidia kujenga mwili. Kadri unavyosoma yaliyoandikwa,
unahitaji kujiuliza namna gani hicho unachokisoma kinaleta maana.
Je, kinafanana na kitu
gani unachokijua tayari? Kama tulivyokwisha kusema, maarifa tunayojaribu
kuyaelewa yanahusiana na mambo tunayokutana nayo kila siku. Kama huuoni uhusiano
huo maana yake ufahamu wako haupati kitu. Rudia tena.
Lakini pia, kadri
unavyosoma jiulize namna gani hicho unachokisoma kinatofautiana na kile
unachokijua. Mambo gani unayoyasoma yanayopingana na yale unayoyafahamu tayari?
Ipo kanuni ya ujifunzaji
inayosema, ‘kama unachokisoma hakijakufanya usielewe, basi huelewi.’ Maana yake
ni kuwa kuelewa ni matokeo ya kuondoa hali ya kutokuelewa inayojitokeza kadri
unavyoingiza maarifa mapya kwenye ufahamu wako.
Kwa hiyo unapoendelea
kusoma, ni muhimu kutathmini namna gani maarifa hayo mapya yanavyokosoa uelewa
uliokuwa ili ubaini maarifa mapya unayoyapata.
Tumia vyanzo tofauti
Wanafunzi wengi hupenda
njia ya mkato katika kujifunza. Wanapopata maandishi rahisi yanayowasaidia
kujibu mtihani, mfano madesa, wanaishia hapo. Mazoea haya, hata hivyo,
huwafanya ‘waegeshe’ maarifa kwa sababu inakuwa vigumu kuyaelewa kwa undani
wake.
Ikiwa unapenda kuwa na
uelewa mzuri wa jambo unalojifunza, ni muhimu ujenge mazoea ya kutumia vyanzo
tofauti vya maarifa. Kwa mfano, soma vitabu vingi vinavyoelezea jambo hilo
hilo. Baada ya kusoma kitabu cha kwanza, tafuta kitabu kingine kinachoelezea kitu
kile kile.
Uzoefu unaonesha kwamba
wakati mwingine unaposoma jambo lile lile kwenye kitabu kingine, akili inaweza
kukudanganya kuwa tayari unaelewa na hivyo huna sababu ya kuendelea.
Usidanganyike.
Ukweli ni kwamba kila
kitabu kina namna tofauti ya kuelezea jambo hilo hilo. Kupitia tofauti hizi za
uwasilishwaji wa maarifa, uelewa wako utaimarika zaidi.
Lakini pia, katika
kusoma vitabu vilivyoandikwa na waandishi tofauti uwezekano ni mkubwa utakutana
na mkanganyiko wa maarifa. Kile ulichokisoma kwenye kitabu cha awali sicho
kinachoonekana kwenye kitabu cha pili.
Mkanganyiko wa namna hii
si jambo baya. Mkanganyiko ni afya katika kujifunza. Bila mkanganyiko itakuwa
vigumu kupanua uelewa wako.
Unapokutana na
mikanganyiko chukulia hiyo kama fursa ya kubaini maeneo unayohitaji kupata msaada
wa mwalimu wako au mwanafunzi mwenzako mwenye uelewa zaidi.
Uzuri ni kwamba siku
hizi teknolojia imerahisisha ujifunzaji. Ukiingia kwenye mtandao wa YouTube,
kwa mfano, unaweza kupata video mbalimbali zinazofafanua jambo ulilolisoma
kwenye vitabu. Katika kutazama video hizi, uelewa wako utaimarika zaidi kwa
sababu mule utakutana na michoro, maelezo ya picha ambayo kwa hakika
yataimarisha uelewa wako.
Sambamba na kutumia
vitabu na namna nyingine za kuhifadhia maarifa, usiache kumsikiliza mwalimu.
Mwalimu hufundishwa namna ya kurahisisha maarifa yaendane na mazingira yako.
Kazi ya mwalimu ni
kupunguza ugumu wa lugha ya vitabuni ili iendane na lugha unayoielewa zaidi.
Mwanafunzi mwenye tabia ya kumsikiliza mwalimu kwa makini, kwa kiasi kikubwa,
anajipunguzia kazi ya kutafsiri maarifa ambayo wakati mwingine yanawekwa kwenye
isiyoeleweka kwa urahisi.
Wafundishe wengine
Kama tulivyotangulia
kusema, huwezi kuwa na uelewa mzuri wa jambo kama bado hujalifanya liwe sehemu
ya maisha yako. Usipoweza kuyamiliki maarifa unayojifunza, hayatakusaidia.
Ili uweze kuyamiliki
maarifa, lazima ufanye kazi ya kuyatumia katika maisha yako halisi. Hatua ya
kwanza ya kutumia maarifa yako ni kuwafundisha wengine.
Unapowafundisha watu
wengine unafanya mambo mawili kwa pamoja. Kwanza, unalazimika kutafuta lugha
nyepesi kuelezea jambo ambalo wakati mwingine ulitumia siku nzima kulieleza.
Huwezi kumfundisha mtu
kwa kutumia maneno yale yale yaliyotumika kwenye kitabu. Lazima utatumia maneno
yako mwenyewe yatakayomsaidia mwenzako kuelewa. Kufanya hivi kutakusaidia wewe mwenyewe
kuelewa kwanza.
Pili, katika
kuwafundisha wengine utabaini maeneo ambayo bado hukuyaelewa vizuri. Haya ni
maeneo ambayo pengine hukutumia muda wa kutosha kuyaelewa au yalikuwa na ugumu
zaidi ya maeneo mengine.
Kupitia kuwafundisha
wengine utaweza unajirahisishia kazi ya kuyaelewa maeneo hayo ‘korofi’ na
kuyashughulikia kwa wakati.
INAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni