Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi
PICHA: Shutterstock |
Nakumbuka siku ya kwanza kusikia neno ‘cell’
nikiwa kidato cha kwanza haikuwa kazi rahisi kupata picha kamili. Mwalimu wetu
aliandika ubaoni, ‘cell is a basic unit
of life.’ Niliduwaa. Sikujua anamaanisha nini zaidi ya kutazama kamusi
kujua maana ya maneno aliyoyatumia.
Mwalimu alirudia maneno hayo hayo kuweka
msisitizo, na kisha akatafsiri kwa Kiswahili. Alisema, ‘maana yake ni hivi kuna
kitu kidogo kisichoonekana kwa macho kwenye miili yetu kinachofanya tuishi. Mmeelewa?’ Kwa kweli hatukuwa na namna nyingine zaidi ya
‘kuelewa’ na tukaitikia, ‘ndiyo!’
Mwalimu alifurahi na akatupa muda tunakili sentensi
hiyo kwenye madaftari yetu. Tulifanya hivyo ingawa ni wazi hatukuwa tukielewa
anaongelea nini.
Kazi iliyofuata ilikuwa ni kukariri sentensi hiyo
bila kuelewa ina maana gani. Tulifikiri kukumbuka ndio kuelewa.
Mtihani ulipokuja tulijibu vile vile bila kukosea
na mwalimu alitupa alama za juu kwa kurudia kile kile alichokuwa
ametukaririsha. Lakini ukweli ni kwamba hatukuwa tumeelewa ‘tulichomeza.’
Changamoto
ya ufundishaji
Huu ni mfano wa namna ufundishaji unavyochangia
kwa kiasi kikubwa kufanya maarifa yanayokusudiwa na mtalaa yakose maana kwenye
maisha halisi ya wanafunzi.
Tunasoma vitu vingi tusivyoviona kwenye maisha
yetu ya kila siku. Matokeo yake tunaishia kukumbuka na kufaulu mitihani kwa
kiwango cha juu lakini thamani yetu kimaarifa ikibaki vile vile.
Tunamaliza shule lakini hatujui tunawezaje
kutumia maarifa hayo kubadilisha maisha yetu kwa sababu ukweli ni kwamba
hatuoni uhusiano wa wazi kati ya kile tulichojifunza shuleni na maisha yetu ya
kila siku.
Ikiwa tunataka kubadili hali ya mambo, mahali pa
kuanzia ni kuwekeza kwenye maandalizi madhubuti ya walimu. Kama nilivyoeleza kwenye
makala yaliyopita, mwalimu ndiye anayebeba dhima ya elimu.
Bila mwalimu
aliyeandaliwa vyema, hatuwezi kuona matunda ya sera nzuri za elimu, mitalaa
mizuri, madarasa bora na hata vifaa bora vya ujifunzaji na ufundishaji.
Mwalimu aliyeandaliwa vyema na kufuzu kazi ya
kutafsiri mtalaa katika maisha ya mwanafunzi, anaweza kuibua na kuchochea
udadisi kwa mwanafunzi wake.
Jitihada
za wadau
Katika makala yaliyopita, tulitumia mfano wa
mradi wa Next Generation Leaning (NGL) unaoendeshwa na Shirika la Opportunity
Education Foundation kujifunza namna mwalimu anavyoweza kuifanya kazi hii kwa
ufanisi.
Tuliona kanuni mbili. Kwanza, mwalimu anahitaji
kumfanya mwanafunzi aone namna gani kile anachofundishwa darasani kinagusa
maisha yake ya kawaida. Kujua uhusiano uliopo kati ya maudhui anayojifunza na
maisha yake, kunamfanya athamini maudhui husika na hivyo kuwa na ari ya
kujifunza.
Pili, mwalimu anahitaji kumjengea
mwanafunzi uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu maudhui anayojifunza.
Kanuni hii inamsaidia mwanafunzi kupunguza utegemezi kwa mwalimu na hivyo
kujenga hali ya kujiamini kuwa anaweza kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji.
Kukuza ujuzi
Kanuni ya
tatu ni kumtarajia mwanafunzi kutumia maarifa yake kujitengeneza ujuzi.
Mwanafunzi wa NGL si tu anahitajika kujibu maswali ya kufikirisha, bali kuonyesha
ujuzi mahususi.
Mathalani,
baada ya mwanafunzi kujifunza namna mimea inavyotengeneza sukari kwa kutumia
mwanga wa jua, lazima aoneshe anavyoweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto
anazokabiliana nazo katika mazingira yake.
Hali
halisi katika shule zetu ni tofauti. Mwalimu humtarajia mwanafunzi kukusanya na
kukariri maarifa. Kipimo cha ujifunzaji ni kwa kiwango gani mwanafunzi huyu anajua
kutoa maelezo sahihi ya nadharia za kitaaluma.
Mwanafunzi
anayesoma mada ya Uchafuzi wa Mazingira, kwa mfano, anatarajiwa kukusanya,
kukariri na kuelewa maelezo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira.
Mwanafunzi
huyu mwenye taarifa nyingi kuhusu uchafuzi wa mazingira bado anaweza kuvumilia
kuishi na takataka zilizo karibu na makazi yake bila wasiwasi. Kwa mtindo huu,
uelewa wa uchafuzi wa mazingira hajaweza kumsaidia kuona tatizo na kulitatua.
Kwa
mwanafunzi huyu uchafuzi wa mazingira ni ‘mambo ya shule’ yasiyohusiana na
maisha yake halisi ambayo hata hivyo yanaweza kumsaidia kufaulu mitihani yake
vizuri.
Katika
zama hizi za ukuaji wa mawasiliano, maarifa ya kila namna yanaweza kupatikana.
Mtu yeyote mwenye ujuzi wa namna ya kutumia mtandao wa intaneti anaweza
kutafuta na kupata chochote anachotaka kujifunza.
Kuendelea
kusisitiza kwenye kumbukumbu ya maarifa kimsingi si kumtendea haki mwanafunzi.
Maarifa hayapaswi kuwa lengo la elimu. Tunahitaji kuongeza thamani kwa kwenda
mbele ya maarifa.
Ujuzi ni maarifa
yanayozalisha
Badala ya
mwalimu kumjazia mwanafunzi maelezo mengi, anahitaji kulenga katika kukuza uwezo wa mwanafunzi
kutumia maarifa anayoyapata katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto halisi
zinazomkabili.
Uwezo huu
unaitwa ujuzi. Mtu mwenye ujuzi kwa hakika anaweza kufanya vitu vinavyoonekana
kama ushahidi kuwa amejifunza maudhui fulani.
Kwa mfano,
katika kufundisha mada ya uchafuzi wa mazingira, mwalimu asiishie kumjaza
mwanafunzi nadharia na maelezo mengi yanayohusiana na uchafuzi.
Badala
yake, aende hatua moja mbele kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuona matatizo
yanayofanana na kile anachojifunza na kujaribu kutafuta majibu yanayolingana na
kiwango chake cha uelewa. Huko ndiko kutumia maarifa kujipatia ujuzi, kanuni
muhimu sana ya mradi wa NGL.
Mwalimu
wa NGL, kwa mfano, mbali na kuhakikisha
mwanafunzi anahusianisha kile anachojifunza na maisha yake, anatarajiwa kukuza
ujuzi wa mwanafunzi kwa kufundisha katika namna inayochochea utafutaji wa
majibu.
Ufanisi
wa somo unapimwa kwa namna mwanafunzi anavyoweza kutazama nje ya darasa na
kubaini matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa kutumia maarifa aliyonayo.
Mwanafunzi ashirikiane na wenzake
Tunafahamu
kuwa wanafunzi hutofautiana uwezo. Wapo wanafunzi wenye uelewa mkubwa wa mambo
kuliko wengine.
Kadhalika,
kila mwanafunzi ana namna yake bora zaidi ya kujifunza. Wapo, kwa mfano,
wanaojifunza kwa kusikia, wengine kwa kutazama, wengine kwa kufanya.
Kwa
kuzingatia ukweli huo, mradi wa NGL unayo kanuni ya nne inayomtaka mwalimu kumwezesha
mwanafunzi kujifunza akishirikiana na wenzake.
Kupitia
majadiliano, mwanafunzi anapata nafasi ya kusikiliza uzoefu na uelewa wa
wenzake ambao kwa hakika unaweza kuwa tofauti na wa kwake.
Pia, kwa
kuwa majadiliano haya yanafanyika katika mazungumzo ya kawaida na marafiki, mwanafunzi
anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufurahia kile anachokisoma.
Ingawa
walimu wetu wamekuwa wakifundishwa mbinu hii ya kuwashirikisha wanafunzi katika
ujifunzaji, mara nyingi utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi.
Walimu
wengi, kwa mfano, hupata shida kujua ni wakati upi mwanafunzi ashirikiane na
wenzake na anaposhirikiana na wenzake afanye nini. Matokeo yake walimu
huendelea kutumia mbinu za kimazoea zinazowanyima wanafunzi fursa ya kushiriki
kwenye mchakato wa ujifunzaji.
INAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni