Namna ya Kutambua Kazi ya Wito Wako
Kuna
mawazo yanapandikizwa kwenye fahamu za vijana kuwa mafanikio hayaji bila mtu kufanya
aina fulani ya kazi. Wahubiri wa mawazo haya wanapima tija na heshima ya kazi kwa
mizani ya kipato.
Mtazamo
huu, kwa kiasi kikubwa, unachochewa na
mfumo wa kibepari unaotukuza faida anayopata mtu binafsi dhidi ya manufaa mapana
ya jamii. Katika mfumo huu, mtu anaweza kufanya kazi yoyote almuradi inamnufaisha
yeye binafsi.
Mawazo
kama haya ya kuweka mbele fedha, kwa kweli, yanakwenda kinyume na utamaduni
wetu wa kijamaa unaopima ufanisi wa mtu kwa kutazama mchango alionao katika
kuwasaidia wengine.
Tunafahamu,
kwa mfano, wazee wetu wengi waliitumikia jamii yetu kwa uadilifu lakini walistaafu
wakiwa watu wanaoishi maisha ya kawaida. Heshima yao haikuwa namna
walivyojitengenezea himaya zao za kimaslahi, bali namna walivyoweza kutumikia
wito wao.
Kizazi
hiki cha sasa kinaanza kuupa mkono utamaduni huo. Vijana wa mjini wanasema, ‘sasa
tunapambana na hali zetu.’ Kila mtu anapigania maslahi yake kwa kutumia njia zozote
halali na haramu.
Mwelekeo
huu umefanya watu wavamie kazi zisizo za wito wao kwa sababu tu zina harufu ya
kuwaharakishia mafanikio ya kifedha. Watu hawa hujikuta wakifubaza uwezekano wa
kufanikiwa kinyume na matamanio yao. Sababu ni kufanya kitu sahihi lakini kisichokuza
ile mbegu inayoishi ndani yao.
Katika
makala haya, naiita mbegu hii wito, na ninapendekeza mbinu nne unazoweza kuzitumia
kuibaini na kuikuza kupitia kazi unayoifanya.
Kitu gani kinakugusa?
Kila
mtu analo eneo la maisha linamvutia kulifuatilia kwa karibu. Kuna kitu ambacho
ukikisikia kinazunguzwa mahali moyo wako unasisimka. Unapokuwa kwenye
mazungumzo na watu wengine, masikio yako yanasikia kitu hicho hata kama watu
wengine hawakisikii. Unanunua vitabu, unafuatilia televisheni na mitandao na
karibu kila unachokifanya kinazunguka zaidi kwenye eneo hilo hilo.
Unapoendelea
kusoma hapa tayari kuna kitu kinakujia kichwani. Inawezekana ni matatizo fulani
ya watu, hitaji fulani unalofikiri jamii yetu inalo au ubunifu fulani unaoamini
bado jamii haijauona.
Pia,
huenda ni masuala ya teknolojia. Inawezekana ni mfumo fulani wa maisha, imani
au fikra katika jamii unazofikiri ungepewa nafasi ungezibadilisha. Chochote kile
kinachogusa fikra zako, hicho ndicho kinachoweza kuwa wito wako. Ukifanya kazi
zinazogusa eneo hilo unaweza kufanya vizuri zaidi.
Unajitambulisha na kitu gani?
Kwa
kawaida, kuna vitu tukivifanya vikaleta matokeo fulani tunajisikia fahari. Kila
mtu ana eneo lake akilifanya vizuri anajisikia kuridhika. Kuna watu wanajisikia fahari wanapotetea haki
za watu; wengine kufundisha; wengine uandishi; kubuni vitu vipya; kuongoza
wengine; kushauri, kuendesha biashara, kutaja kwa uchache.
Kile
kinachokuletea ufahari, mara nyingi, utapenda kujitambulisha nacho. Utatumia
muda mwingi kukielewa kuliko unavyofanya kwenye maeneo mengine.
Nina
rafiki yangu daktari mzuri lakini mara zote hujitambulisha kama mwandishi. Mazungumzo
yake mengi hujikita kwenye uandishi kuliko udaktari na sisi tunamtambua kama
mwandishi kuliko daktari. Hii ndiyo sifa ya wito. Unaweza kufanya kazi nyingine
lakini kinachokupa hali ya utoshelevu kikawa kitu kingine kabisa.
Jiulize,
kitu gani ukikifanya vizuri unajisikia fahari? Je, watu wanakusifia na
kukutambua kwa kitu gani? Ukiweza kuuoanisha uwezo huo na kazi unayoifanya itakuwa
rahisi kupata mafanikio makubwa zaidi.
Unayatazamaje mafanikio?
Mafanikio
ni dhana pana isiyo na jibu moja. Kila mtu ana namna yake ya kutafsiri kile
kinachoitwa mafanikio. Wapo wanaochukulia mafanikio kama uwezo wa kujikusanyia mali.
Hawa huridhika wanapokuwa wamefikia kiwango cha kujitosheleza na vitu
vinavyowawezesha kuishi maisha mazuri.
Wengine
mafanikio yao ni umaarufu katika jamii. Vitu vinavyowafanya wajulikane ndivyo wanavyovichukulia
kama mafanikio. Wengine wanakwenda mbali zaidi. Hawaridhiki na fedha wala
umaarufu bali mamlaka. Wasipopata madaraka yanayowapa nguvu ya kuwatawala
wengine, bado hawajisikii kufanikiwa.
Pamoja
na hao, wapo pia wanaopima mafanikio yao kwa namna wanavyotatua matatizo ya
watu wanaowazunguka. Hawa, hawaishii kuridhika na maisha mazuri bali kuona maisha yao yanagusa watu wengine.
Tafsiri
ya mafanikio uliyonayo, ni kiashiria kimojawapo cha wito ulionao katika maisha.
Wito wako hutengeneza mtazamo fulani wa mafanikio. Ukiweza kuoanisha tafsiri uliyonayo
ya mafanikio na kazi unayoifanya uwezekano ni mkubwa kuwa kufanya vizuri zaidi.
Maamuzi gani unayafurahia?
Kipimo
cha juu cha wito ni aina ya maamuzi unayoyafanya. Kuna nyakati unaweza kufanya
maamuzi ambayo si kila mtu anaweza kukuelewa lakini wewe mwenyewe ukawa na
amani na kile unachokifanya.
Kuna
kijana aliwahi kuacha kazi yenye kipato kikubwa ili akafanye kitu alichoamini
kinabeba thamani yake. Aliacha kazi ambayo watu wengi wangetamani kuipata na
akaenda kuanzisha biashara. Mtu wa namna hii kwa vyovyote anakuwa na wito wa
ujasiriamali ndani yake. Ili wito huo ukamilike inakuwa ni lazima afanye
maamuzi magumu.
Jiulize,
umewahi kufanya maamuzi gani yaliyobadili mwelekeo wa maisha yako? Ikiwa kuna
maamuzi unatamani kuyachukua ukiamini yatabadili maisha yako, huo inawezekana
ndio wito wako.
Wito hubeba mafanikio yako
Mafanikio
katika kazi mara nyingi hujipua kama mbegu inayoota kwenye wito alionao mtu. Kila
mtu ana mbegu yake. Kwa mfano, hata tungependa kujiajiri si kila mtu anaweza. Wapo
watu ambao hata wangewezeshwa kujiajiri bado hawatafanya vizuri. Kujiajiri si
wito wao.
Kadhalika,
si kila mtu anaweza kuajiriwa. Kuna watu wana wito ndani yao wa kutengeneza
mifumo inayoajiri watu wengine. Wito wao ni kusimamia mawazo yao na kuyageuza
kuwa ajira. Ndio maana ni muhimu kuutambua wito wako.
Unapoutambua
wito wako unajiweka kwenye nafasi ya kujitoa kikamilifu kwenye eneo lililobeba
thamani yako. Hutajaribu kufanya vitu vingi kwa sababu unajua iliko thamani
yako na wapi pa kuelekeza nguvu zako.
nimejielewa zaidi..Asante sana.
JibuFutaUjumbe umetembea katika hisia zangu. Mi ni mwalimu mwanafunzi katika masomo ya chemistry & biology. Lakini naishi na ndoto za kuwa muigizaji na mtunzi wa vitabu vya stori kama tamthiliya na makala mbalimbali. Tayari nimeanza michakato ya kukamilisha ndoto hizo, ualimu ninaosomea nataka kuutumia namna hii sasa sijui nitakuwa upande gani baada ya kuoanisha ninachosomea na ndoto zangu!
JibuFuta