Sababu za Watu Kufanya Uchaguzi Mbaya wa Kazi
Uchaguzi
wa kazi ni maamuzi anayoyafanya mtu kuanzia pale anapopata wazo la kazi
anayotaka kuifanya mpaka anapostaafu. Haya ni maamuzi anayoyafanya mtu kutimiza
ndoto zake kimaisha tangu anapokuwa masomoni; anapoomba kazi kwa mara ya kwanza
na kuipata; anapobadilisha kazi na hata pale anapofikia umri wa kustaafu kazi.
Maamuzi
haya yanaposhindwa kukidhi matarajio na kumfanya mtu asifurahie kazi yake,
tunaweza kusema, hapo anakuwa amefanya uchaguzi mbaya wa kazi. Uchaguzi wa
namna hii unaweza kusababisha mtu asiyotumie uwezo wake wote kazini, hali
inayoweza kuleta kutokuridhika na kazi.
Kwa
kuwa kutokuridhika na kazi kunaweza kusababisha mtu aache kazi, au aendelee kufanya
kazi yake kwa manung’uniko, makala haya yanaangazia sababu tano kubwa zinazochangia
watu kufanya uchaguzi mbaya wa kazi.
Kukidhi matakwa ya soko
Mwenendo
wa soko ni sababu moja kubwa inayoathiri maamuzi ya kazi anayoyafanya mtu. Kwa
kawaida, kazi zinazohitajika kwenye soko la ajira ndizo zinazowavutia watu
wenye ndoto za kuajiriwa.
Hata
hivyo, changamoto ya kuongozwa na soko ni pale mahitaji ya soko yanapobadilika ghafla
kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya kisera.
Hivi
sasa, kwa mfano, karibu kila chuo kikuu hapa nchini kina program za ualimu. Kwa
sababu ya mahitaji makubwa ya walimu mashuleni, wanafunzi wengi huona ni
afadhali wasomee ualimu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kuajiriwa
mara baada ya masomo.
Huko
tuendako, hata hivyo, wahitimu wa ualimu wanaweza kuwa wengi kuliko mahitaji
halisi tutakayokuwa nayo wakati huo. Katika mazingira kama hayo, wahitimu wengi
wa ualimu watalazimika kutafuta ajira nyinginezo nje ya ualimu. Hali hii inaweza
kuleta changamoto kwa wanafunzi walisomea ualimu kwa lengo la kupata ajira
mapema.
Pamoja
na umuhimu wa kuongozwa na mahitaji soko la ajira kufanya maamuzi, ni vyema
kufikiri itakuwaje ikiwa hapo baadae soko la ajira halitahitaji ujuzi wako.
Kukidhi matarajio ya watu
Kuna
kazi ambazo jamii huziheshimu kuliko nyinginezo. Mfano, kazi zenye kuhitaji
ujuzi na maarifa maalum ambayo si watu wengi wanaweza kuwa nayo, huheshimika
zaidi kuliko kazi zinazotegemea ujuzi wa jumla.
Aidha,
mtu anayefanya kazi kama hizi huchukuliwa kama mtu mwenye hadhi ya pekee kwenye
jamii na watu humpa heshima kama mtu mwenye ujuzi maalum.
Kwa
kuwa binadamu kwa hulka yake anapenda heshima, ni rahisi kazi za namna hii kuwa
chaguo la watu wengi hasa wasioutambua wito wao. Mara nyingi watu hawa hujikuta
wakitamani kukidhi matarajio ya jamii kwa kuchagua kazi wanazojua zinaheshimika.
Hata
hivyo, mara nyingine, mtu anapofanya kazi kukidhi tu matarajio ya jamii anaweza
kuishia kukosa furaha ya kazi hasa nyakati za changamoto.
Unapofanya
kazi isiyoendana na wito wako, inakuwa rahisi kubaini unafanya kitu kisichokidhi
matarajio yako binafsi mambo yanapokwenda kinyume na matarajio yako. Hali ya
kuchoka huweza kusababisha kuacha kazi na kutangatanga kutoka kwenye kazi moja
kwenda nyingine.
Kuiga waliofanikiwa
Kuna
kijana mmoja alivutiwa sana na kazi za wakili mmoja aliyekuwa maarufu mwishoni
mwa miaka ya tisini. Kwa sababu ya mafanikio makubwa aliyokuwa nayo wakili
huyo, kijana yule aliamua kusomea sheria.
Baada
ya kusomea sheria na hatimaye kufanya kazi za uhakimu kwa zaidi ya muongo
mmoja, bado kijana yule anasema hajafikia mahali akajisikia utoshelevu wa kazi.
Majuzi nilikutana naye akijaribu kufanya mipango ya kusomea kitu kingine kama
jitihada za kutafuta utoshelevu.
Si
jambo baya kuvutiwa na kujifunza kwa watu tunaofikiri wamefanikiwa kwenye kazi
zao. Hata hivyo, unapoiga maamuzi ya mtu mwingine unahitaji kuchukua tahadhari.
Kila
mtu ana upekee wake. Mtu anaweza kufanya vizuri kwenye eneo fulani la utaalam
lakini hiyo isimaanishe kuwa na wewe ukifanya kitu hicho hicho utafanikiwa. Jitahidi
kuuelewa upekee wako na elekeza nguvu zako huko.
Kupata kipato kikubwa
Upo
ukweli kwamba moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kutuwezesha kumudu
maisha yetu. Kwa sababu hiyo, kazi zenye uhakika wa kipato kikubwa, huwa
zinawavutia watu wengi kuliko kazi zenye heshima lakini hazina kipato kikubwa.
Si
wakati wote, hata hivyo, suala la kipato huwa ni sababu iliyokamilika kueleza
kwa nini tunafanya kazi. Yapo mazingira ambayo kazi inaweza kuwa na kipato
kikubwa lakini haimfanyi mtu atumie uwezo na ujuzi wake kikamilifu.
Inapotokea
mtu analipwa vizuri lakini haoni namna gani kazi hiyo inakwenda sambamba na vipaji
na haiba yake, ni rahisi mtu huyo kuanza kujisikia kudumaa na hivyo kukosa
furaha ya kazi.
Pamoja
na kipato, angalia na sababu nyingine kama namna ujuzi, maarifa na uzoefu wako
unavyotumika ikiwa utafanya kazi unayoichagua.
Ufaulu hafifu na uchumi duni
Katika
mazingira yetu, kiwango cha ufaulu ndicho kinachoamua hatma ya mtu. Mtu mwenye
ufaulu mkubwa wa masomo kwa kidato cha nne au cha sita ndiye anayekuwa na
nafasi nzuri zaidi ya kufanya uchaguzi unaokidhi ndoto zake kuliko mwingine
mwenye ufaulu usioridhisha.
Zipo
kazi ambazo ili mwanafunzi apate nafasi ya kuzisomea na kuzipata, anahitaji
kuwa na ufaulu mkubwa. Hizi ni zile kazi zenye kuchukuliwa kuwa nyeti mfano
udaktari, sheria na uinjinia.
Ndio
kusema, ufaulu dhaifu unaweza kuzima ndoto za mtu na kumfanya achague fani
ambazo awali hakuwahi huzifikiria. Mtu, kwa mfano, anaweza kuamua kusomea
sayansi ya udongo, si kwa sababu anaipenda lakini ndiyo inayopatikana kwa
kutumia matokeo aliyonayo.
Pia,
uwezo mdogo wa kiuchumi unaweza kuzima ndoto za maisha ya watu wengi. Jitihada
za kupata mkopo wa elimu ya juu huchangia wanafunzi wasio na uwezo kufanya maamuzi yasiyozingatia matamanio yao.
Ingawa ni kweli uchaguzi mbaya wa
kazi unaweza kumgharimu mtu, bado hata hivyo, kuna nafasi isiyo na kikomo ya
kurekebisha maamuzi yaliyokwisha kufanywa. Lililo muhimu ni kujua kile unachokihitaji.
Maoni
Chapisha Maoni