Vyuo Vikuu Vinawajibika Kukuza Ujuzi wa Wahitimu Wake



Kukosekana kwa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ni moja wapo ya sababu kubwa zinazochangia ukosefu wa ajira unaoendelea kuwa tatizo hapa nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo ya uanangezi mjini Dodoma wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema waajiri wengi wamekuwa wakilalamika kuwa vijana wengi wanaoingia kwenye soko la ajira wanakosa ujuzi unaohitajika katika kazi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ukosefu huu wa ujuzi wa kazi huwalazimu baadhi ya waajiri kufungua milango ya ajira kwa wafanyakazi wenye sifa kutoka nje ya nchi.
Katika mazingira ambayo wahitimu kati ya 800,000 na 1,000,000 wanaingia kwenye soko la ajila kila mwaka hapa nchini, habari za vijana wanaotafuta kazi kukosa ujuzi unaohitajika ni lazima zipewe uzito unaostahili.
Uamuzi wa serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine wa ajira, kama Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuandaa program hiyo maalumu ya kukuza ujuzi itakayofanyika katika maeneo ya kazi ni sehemu ya ufumbuzi wa tatizo kubwa tulilonalo.
Waziri Mkuu alinukuliwa na Mwananchi akisema, “Kwa pamoja tuliazimia kuandaliwa kwa miongozo ya kitaifa ya kusimamia mafunzo ya vitendo kwa wahitimu na mafunzo ya uanagenzi lengo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa maeneo ya kazi yana ubora unaohitajika.”
Programu hiyo ya miaka mitano inayolenga kukuza ujuzi kwa takribani watu milioni 4 tayari imeshawafikia vijana 11,340 katika fani mbalimbali kupitia vyuo vya mafunzo vya umma na binafsi.
Takwimu
Kilio cha kukosekana kwa ujuzi miongoni mwa watafuta kazi ni cha muda mrefu. Ripoti ya Utafiti wa Ajira na Kipato ya mwaka 2012, iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa mwezi Julai 2013, inathibitisha kauli ya Waziri Mkuu kuwa watafuta kazi hawakidhi vigezo vya ajira.

Kwa mfano, wakati kwa mwaka 2011/12 zilikuwepo nafasi za kazi 126,073 nchini kote, ni wafanyakazi wapya 74,474 tu ndio walioweza kuingia kwenye soko la ajira kwa kipindi hicho. Nafasi za kazi zipatazo 45,388 hazikuweza kujazwa sababu mojawapo ikiwa ni waombaji kukosa sifa.

Aidha, Baraza la Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa ushirikiano na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) liliwahi kufanya utafiti ulioonesha kuwa zaidi ya nusu ya watafuta kazi wenye shahada katika nchi za Afrika Mashariki, hawakidhi vigezo vya kuajiriwa.

Kwa Tanzania, utafiti huo ulibaini kuwa ni asilimia 39 tu ya wahitimu ndio waliokuwa na ujuzi unaokidhi vigezo vinavyohitajika na wajiri wao.

Somo kwa vyuo vyetu

Tunaipongeza serikali kwa hatua hiyo ya kutengeneza program ya mafunzo ya ujuzi kazini inayolenga kurekebisha upungufu wa mafunzo yasiyokidhi mahitaji ya soko la ajira yanayotolewa na vyuo vyetu.
Ni dhahiri mafunzo ya uanagenzi yanamsaidia mtu ambaye tayari yuko kazini kujifunza kwa vitendo namna anavyoweza kuboresha ujuzi wake wakati huo akiendelea na kazi.
Ufanisi wa mpango muhimu kama huu, kwa hakika, unategemea ushirikiano wa karibu na waajiri. Badala ya kuwaadhibu vijana kwa kukosa ujuzi unaohitajika kazini, waajiri wajione kama wadau muhimu wenye wajibu wa kushiriki kurekebisha kasoro za kimfumo.
Hata hivyo, mzizi wa tatizo hili la ukosefu wa ujuzi kwa wahitimu unaanzia kwenye vyuo vyetu ambavyo ndivyo vyenye wajibu wa kuwajenga vijana kiujuzi ili kuwawezesha kuajirika au kujiajiri.
Pamoja na tofauti ndogo ndogo, mfumo wa vyuo vyetu katika kuwaandaa vijana wanaoingia kwenye soko la ajira unafanana. Msisitizo umekuwa kwenye maarifa ya jumla yanayotolewa na watu ambao kazi yao kubwa ni kuzalisha maarifa badala ya kutumia maarifa hayo kutatua changamoto.
Hivi sasa, kwa mfano, mhadhiri ambaye hajawahi kuwa mwalimu wa sekondari, ndiye anayepewa kazi ya kuwaandaa walimu watakaokwenda kufanya kazi ambayo yeye mwenyewe hajawahi kuifanya.
Mhadhiri huyu anaweza kuwa na ufaulu wa juu katika nadharia za ualimu, lakini hana ujuzi wa hali halisi ya ualimu shuleni. Hatuwezi kutegemea mhadhiri huyu aweze kuwapika wanafunzi wake kuwa walimu walioiva kiujuzi kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kuishi kile anachokifundisha.
Matokeo ya utaratibu huu ni kuzalisha wahitimu wanaothamini maarifa kuakisi matarajio ya wahadhiri wao. Bahati mbaya wahitimu hawa wanapoingia kwenye soko la ajira wanagundua, japo kwa kuchelewa, kwamba waajiri na kazi kwa ujumla zinahitaji ujuzi na sio maarifa.
Uboreshaji wa mafunzo
Tunapendekeza mambo makubwa mawili. Kwanza, tuanze na sifa za watu wanaopewa wajibu wa kuwaandaa vijana wetu vyuoni. Mojawapo ya sifa za mtu kuwa mhadhiri iwe ni ujuzi na uzoefu katika eneo husika la taaluma.
Mhadhiri wa uhasibu, kwa mfano, alazimike kuwa mhasibu kwanza kabla hajapewa jukumu nyeti la kuandaa wahasibu. Kwa namna hiyo, itakuwa rahisi kwake kutafsiri nadharia za kitaaluma na kuzioanisha na mazingira halisi ya kazi ambayo kwa hakika anayafahamu.
Badala ya kuwachukulia wahadhiri kama wazalishaji wa maarifa kupitia utafiti, pengine tuwe na watu maalum kwa kazi hiyo ili wahadhiri wajikite kufanya tafiti endelevu zenye mwelekeo wa kuoanisha kile wanachokifundisha darasani na mazingira halisi ya kazi.
Utaratibu wa sasa wa mafunzo ya vitendo unafanyika kwa mtindo wa kukamilisha ratiba za mihula badala ya kumwezesha mwanafunzi kujifunza katika ukamilifu wake.
Tunahitaji utaratibu mzuri wa kuyafanya mafunzo yanayotolewa katika vyuo vikuu kutumia mfumo wa uanagenzi. Tuimarishe uhusiano baina ya vyuo na waajiri ili iwe rahisi kwa mwanafunzi kuendelea na mafunzo kwa vitendo wakati wote wa masomo.

Hatua hizi, kwa pamoja, zitawasaidia wahitimu wetu kuwa na ujuzi ambao si tu utawawezesha kuajiriwa, lakini pia kuwawezesha kuutumia ujuzi huo kujiajiri wenyewe.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?