Mbinu za Kuchagua Kazi Itakayokupa Utoshelevu



Maamuzi ya kazi gani ufanye ni moja wapo ya mambo ya msingi yanayoathiri maisha ya mtu. Kazi iwe ya kujiajiri au kuajiriwa ndiyo maisha yako.

Muda unaoutumia ukiwa kazini unaweza kuwa mwingi kuliko muda unaoutumia ukiwa kwingineko. Maana yake ni kwamba unapofikiri kazi ipi uifanye kimsingi unafanya maamuzi yatakayoathiri mfumo mzima wa maisha yako.
Maamuzi sahihi yatakufanya uwe na utoshelevu zaidi, mtu mwenye  furaha na matumaini. Maamuzi mabaya, kwa upande mwingine, yanaweza kuwa sababu ya kukata tamaa na maisha.

Ni dhahiri kufanya maamuzi ya kazi ni changamoto kubwa kwa sababu mara nyingi ni rahisi kuongozwa na msukumo wa nje. Makala haya yanatathmini baadhi ya sababu unazoweza kuzitumia kufanya maamuzi yanayohusu kazi.

Uzingatie kile unachokipenda?

Ukimsikiliza kijana anayefikiri afanye nini baada ya masomo yake, mara nyingi sababu anayoitoa ni mapenzi aliyonayo na kitu fulani. Mfano, kijana anakwambia anataka kuwa mwanasheria, injinia, rubani, daktari kwa sababu hicho ndicho kinachomvutia.

Hata hivyo, changamoto ni kwamba mambo yanayotuvutia hubadilika kulingana umri. Kila hatua ya maisha tunayopita hutengeneza mahitaji mapya ya kimaisha yanayoweza kubadili mambo yanayotuvutia.

Kuna umri, kwa mfano, unaweza kujikuta unavutiwa na vitu visivyo halisi. Mashujaa unaowasikia kwenye vyombo vya habari, masimulizi unayokutana nayo mitaani, yanaweza kukufanya ukatamani kufanya kitu fulani kwa sababu tu umesikia kitu hicho kipo.

Hata hivyo, inawezekana baada ya muda kile kinachokuvutia leo kitabadilika. Mabadiliko hayo yanazingatia ukweli kwamba mahitaji yako kwa umri ulionao si sawa na mahitaji uliyokuwa nayo miaka kadhaa iliyopita.

Leo unaweza kufikiri unapenda kuwa rubani na kwamba kurusha ndege ndiyo maisha yako. Hata hivyo, shauku ya kuwa rubani inaweza kuwa imetokana na matamanio ya sifa tu ya kufanya kazi ya kipekee.

Kesho, kadri unavyokutana na uzoefu mpya, mvuto huo wa kurusha ndege unaweza kuhamia kwingine.

Kwa kuwa ni vigumu kujua utapenda nini kesho, kufanya maamuzi ya kazi ipi ufanye kwa kuangalia unapenda nini inaweza kuwa kosa la kiufundi.

Uige wanachofanya wengine?

Kwa namna fulani wapo watu wanaoathiri maamuzi yetu. Wazazi, marafiki, watu tunaowaona kwenye vyombo vya habari wana nguvu ya kujenga ushawishi fulani kwenye maisha yetu.

Kuna uwezekano mkubwa, mtoto wa mwalimu naye atakuwa mwalimu. Mtoto wa daktari anaweza kuwa daktari kama ambayo mtoto wa mwanasiasa naye anaweza kuwa mwanasiasa.

Pia, marafiki ulionao nao wana nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo yako. Unapoona wanafanikiwa kwenye eneo fulani la kimaisha, upo uwezekano na wewe ukatamani kujaribu eneo hilo.

Changamoto hata hivyo, ni kwamba kila mtu ana upekee wake. Si kila kinachofanywa vizuri na wengine basi na wewe unaweza kukifanya kwa uzuri ule ule. Maamuzi yetu ya kazi yakiathiriwa na yale tunayoyaona kwa watu wengine uwezekano wa kutokufanya vizuri ni mkubwa.

Ukubwa wa mshahara?

Nilipokuwa shuleni niliota kupata kazi itakayonilipa. Nilifikiri kazi yenye kipato kikubwa ndiyo mafanikio ya kazi. Ndivyo wanavyofikiri vijana wengi wanaoanza maisha.
 
Hata hivyo, utoshelevu wa kazi ni zaidi ya kipato. Ingawa ni kweli moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kujipatia kipato, ni dhahiri kipato si sababu pekee.

Wapo watu wengi wanaopata kipato kikubwa lakini bado wanalamikia kazi zao. Wengine wanaacha kazi zenye kipato kikubwa kwenda kufanya kazi tofauti ikimaanisha kuwa kipato kikubwa si sababu inayotosha kuridhisha nafsi zao.

Unapofanya maamuzi ya kazi ukilenga kuwa tajiri pekee, unaweza kuishia kuwa mtu mwenye huzuni. Pamoja na uzuri wa kuwa na fedha, bado kuna ukweli kwamba mafanikio yako kazini ni zaidi ya hitaji la kupata fedha.

Kugusa maisha ya watu?

Kulenga kugusa maisha ya watu ni kufanya kazi inayowanufaisha watu wengine. Kwenda mbele ya mahitaji yako binafsi na kutumia ujuzi na muda wako kuangalia watu wengine wanahitaji nini kutoka kwako.

Changamoto kwa kizazi chetu, hata hivyo, mara nyingi tunajiangalia sisi wenyewe na mahitaji yetu. Tunataka kufanya kazi zitakazotufanya tuwe bora kuliko wengine na hata kuwatumia watu kwa maslahi yetu.

Ingawa ni vigumu kufikiria mahitaji ya wengine kwa asilimia mia, unapojaribu kufanya hivyo kimsingi unajiwekea akiba ya kundi la watu linalokutakia mema.

Ufanye uamuzi gani?

Jambo la kwanza ni kujidadisi. Hapa nina maana ya kujaribu kujichunguza ili kujua kitu gani unakiona kwenye jamii ambacho wewe unaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.

Kwa vyovyote vile, ufumbuzi wa tatizo huhitaji ujuzi. Ikiwa unataka kuwatetea watu wanaonyang’anywa haki zao, kwa mfano, pengine ukiwa na ujuzi wa sheria au uandishi wa habari, itakuwa rahisi kufikia malengo yako.

Changamoto, kama tulivyotangulia kusema, kile unachofikiri unaweza kukifanya leo, si lazima ukifanye kesho kwa sababu maisha yanabadilika.

Hata hivyo, tofauti na mtu anayeamua kuwa mwanasheria ili awe tajiri au basi tu kuwa maarufu, wewe utajifunza sheria ili uweze kutatua tatizo fulani unaloliona kwenye jamii inayokuzunguka.

Kutatua tatizo la mtu mwingine, ni utoshelevu usiobadilika. Katika kila hatua ya maisha yetu, sote tunatamani kuwa watu wenye manufaa kwa wengine. Haya ndiyo matamanio ya kila mwanadamu anayejitambua.

Haitoshi kuwa na ujuzi fulani. Lazima kuutumia ujuzi huo kutatua matatizo halisi. Utumie ujuzi huo kufanya kazi itakayopunguza tatizo fulani unalofikiri linaisumbua jamii.

Hii ndiyo siri kubwa ya maamuzi bora ya kazi yatakayokupa utoshelevu. Kutatua matatizo halisi yanayowasumbua watu wa jamii yako. Nenda katatue tatizo ambalo pengine limepuuzwa na jamii. 

Kadri unavyotatua tatizo hilo, ndivyo thamani yako itakavyoongezeka, na ndivyo utakavyoendelea kufurahia kile unachokifanya.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?