Mwalimu Anavyoweza Kukuza Uelewa wa Mwanafunzi
PICHA: Sunday Adelaja |
Dhima kuu ya elimu iliyo bora ni kuzalisha raia wenye sifa ya
udadisi. Hawa ni raia wanaofikiri kwa makini, wanaohoji mazoea, wasioridhishwa
na majibu yaliyozoeleka na wenye ari ya kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili
jamii yao.
Hatua ya kwanza ya mwanafunzi kuwa mdadisi ni kuelewa kile
alichojifunza. Mwanafunzi asiyeelewa maudhui ya somo, hawezi kuwa na fursa ya
kufanya udadisi.
Yapo mambo kadhaa yanayoweza kuifanya elimu ikuze udadisi. Mosi,
ni mtalaa wenye ubora. Mtalaa ni mkusanyiko wa mambo yote, ndani na nje ya
darasa, yanayomwezesha mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaomsaidia
kujitambua kibinafsi na kuitambua jamii anamoishi.
Mtalaa ni mwongozo wa jumla, wenye malengo mapana ya kumwuumba
raia mwenye sifa fulani zinazokidhi mahitaji ya jamii husika.
Kimsingi, mtalaa ni matamanio ya jumla ambayo, ili yawe na
maana, lazima yakutane na vipaji binafsi vya mwanafunzi kumfanya atambue wajibu
alionao katika jamii sawa sawa na vipaji alivyonavyo.
Pamoja na ukweli kuwa mtalaa unahitaji kumwekea kijana
mazingira ya kutambua vipaji vyake na nafasi aliyonayo katika jamii, kazi kubwa
inabaki kuwa kwa mwalimu.
Mwalimu
kama mtafsiri wa maudhui
Mwalimu ndiye mwenye wajibu wa kutafsiri malengo mapana ya
mtalaa na kuyaoainisha na mazingira halisi anayoishi mwanafunzi. Bila mwalimu,
mwanafunzi ataishia kupata maarifa na ujuzi wa jumla usiomsaidia kuona mchango
wake mahususi katika jamii.
Ili mwalimu aweze kufanya kazi hiyo nyeti lazima awe na sifa
fulani. Sifa ya kwanza na muhimu ni kuwa na weledi na ari ya kumjengea
mwanafunzi uwezo wa kudadisi. Bila mwalimu mwenyewe kuwa mdadisi haiwezekani
kutarajia matokeo tofauti na vile alivyo yeye mwenyewe.
Ndio kusema, haitoshi kuwa na mtalaa bora kwa maana ya kuwa
na malengo mazuri yanayogusa matatizo halisi ya jamii. Tunahitaji kuwa na
utaratibu mzuri wa kusimamia utekelezaji wa mtalaa tukilenga kumsaidia
mwanafunzi kujenga shauku ya kujifunza, kiu ya maarifa na njaa ya kudadisi.
Katika makala haya ninalenga kuonesha namna gani
mwalimu aliyefuzu anaweza kutumia maudhui ya mtalaa huu kujenga tabia ya
udadisi kwa wanafunzi wake.
Uzoefu wa Opportunity
Education
Ninatumia uzoefu wa Shirika lisilo la Kiserikali
liitwalo Opportunity Education Foundation linalofanya shughuli zake hapa nchini
kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na
Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa (TIE).
Shirika hili linaendesha mradi unaoitwa Next
Generation Learning (NGL) ambao kimsingi unajaribu kuboresha mbinu za
kufundisha maudhui ya mtalaa wetu. Mradi unafanya kazi ya kutafsiri maudhui ya
mtalaa wetu katika lugha inayorahisisha uelewa.
Kazi hii inafanywa na walimu wa shule zetu
waliopata mafunzo maalum kuandaa mfululizo wa masomo yanayoandaliwa kutokana na
mtalaa wetu na mazingira yetu.
Sambamba na kutafsiri maudhui ya mtalaa wetu, NGL
wametengeneza mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji wanaousimamia wao wenyewe
kwenye shule teule. Mradi huu ambao tayari umeshaonesha mafanikio, unatumia
kanuni kuu tano ambazo naamini mwalimu yeyote anaweza kuzitumia.
Katika makala haya, tutagusia kanuni mbili kuu
ambazo ni kuoanisha maudhui yanayofundishwa darasani na maisha halisi anayoishi
mwanafunzi na pili, kuchochea shauku ya mwanafunzi kuuliza maswali.
Kuoanisha
maudhui na maisha
Tumekuwa tukifundishwa maudhui ambayo kwa kweli
wakati mwingine hatuelewi tutayatumia wapi. Nakumbuka, kwa mfano, nikiwa kidato
cha V kwenye somo la Fizikia tulifundishwa hesabu ndefu za namna ya kutafuta
muda utakaotumiwa na tone la mwisho la maji kudondoka kwenye bomba la maji
linalofungwa.
Hatukuelewa kwa nini ilikuwa ni lazima kusumbua
akili kufanya hesabu hizi ngumu zisizotatua tatizo lolote kwenye maisha yetu ya
kila siku.
Ufundishaji wa namna hii, kwa hakika, ulitukatisha
tamaa sisi mwanafunzi kama wanafunzi kujifunza kitu ambacho hatuoni faida yake
katika maisha yetu ya kila siku.
Mradi wa NGL umeonesha mfano wa namna tunavyoweza
kuondoa hitilafu hii. Kupitia uandaaji wa mfululizo wa masomo yanayotafsiri
mtalaa kwa lugha nyepesi (quests), mwanafunzi anasaidiwa kuelewa kwa nini
anahitaji kujifunza kile anachotakiwa kujifunza.
Kupitia mfumo wao wa ujifunzaji, NGL wanajaribu
kufikiri namna gani kile kinachofundishwa darasani kinaweza kugusa maisha ya
kawaida ya mwanafunzi. Mwanafunzi anapoona uhusiano wa moja kwa moja kati ya maudhui
anayojifunza na maisha yake ya kila siku anakuwa na ari kubwa ya kujifunza.
Anachojifunza mwalimu hapa ni kwamba ni muhimu
kutafuta namna ya kuhusianisha somo lake na maisha ya mwanafunzi.
Mwanafunzi anapoelewa kwamba kile anachojifunza
kinahusiana na maisha yake ya kawaida, inakuwa rahisi kwake kupanua uelewa wake
kuliko pale anapojifunza kitu asichojua kitamsaidiaje.
Kwa mfano, mwalimu wa Kemia anapofundisha somo la
mada (matter) anahitaji kufanya kazi
ya ziada kumsisimua mwanafunzi aone namna maarifa ya mada yanavyoweza kumsaidia
katika maisha yake ya kila siku.
Kuchochea
maswali kwa mwanafunzi
Walimu wengi hawafundishi kuchochea uelewa. Kazi
ya walimu imekuwa ni ‘kuhubiri’ maarifa na mwanafunzi anachukuliwa kama mtu ‘mtiifu’
anayesubiri kupikiwa kila kitu na mwalimu. Kazi pekee ya mwanafunzi inabaki ‘kumeza’
kile anachoambiwa. Hana fursa ya kuuliza wala kuhoji.
Aidha, shule zetu ‘zinazofaulisha sana’ kimsingi
zinajitahidi kuhakikisha mwanafunzi anafahamu kwa hakika nini cha kukariri.
Walimu wa shule hizi wanafanya bidii kubwa kuwaimbisha wanafunzi kile
wanachojua kitaulizwa kwenye mtihani.
Mradi wa NGL unajaribu kukabiliana na changamoto
hii. Mwanafunzi anajengewa uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu hicho
anachojifunza badala ya kutegemea majibu yaliyopikwa na mwalimu.
Msisitizo hapa ni kumfanya mwanafunzi awe na
uwezo wa kuibua maswali ya msingi yanayochochea udadisi wake katika masomo. Mwanafunzi
anayewekewa mazingira ya kujiuliza maswali na kushiriki moja kwa moja katika
kutafuta majibu, anakuwa na uwezo wa kudadisi kuliko mwenzake anayeshiriki
‘kumeza’ maarifa.
Kwa hivyo, mwalimu lazima afanye kazi ya kuibua
maswali yanayohusiana na kile anachokifundisha ili wanafunzi waweze kujifunza
kwa mfumo wa kutafuta majibu wao wenyewe. Mradi wa NGL unatuthibitishia kuwa
mwalimu akiwezeshwa anaweza kutafsiri mtalaa huu unaodaiwa kuwa haufai kuibua
kiu ya kutafuta majibu.
INAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni