Unajengaje Uhusiano Mzuri na Viongozi Kazini?
Moja ya mambo yanayoweza kukusaidia kufanikiwa kazini ni namna unavyohusiana na mkubwa wako wa kazi. Huyu ni mtu anayekuongoza, anayetoa maelekezo ya nini kifanyike na wakati mwingine ndiye mwenye kauli ya mwisho kwenye taasisi, idara au ofisi unayofanya kazi. Kwa nafasi yake, kiongozi wa kazi ni mtu mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi yanayohusu kazi yako hata kama anaweza asiwe mwajiri wako moja kwa moja. Huyu ni mkuu wa ofisi, idara, kitengo, kampuni au taasisi unayofanyia kazi. Ndiye mtu anayekusimamia na kupokea taarifa za utendaji wako na labda kuzipeleka kwenye mamlaka za juu.