Tunawezaje kutunza muda katika mazingira haya?

Unaamka asubuhi na mapema. Unagusa tepu ya maji uoge, lahaula, yamekatika. Unaokoteza matone machache, unafanikiwa 'kupiga paspoti' kuondoa harufu ya kikwapa.

Chai. Umeme haupo. Luku imekata. Hivyo umepanga kwenda benki kisha intaneti, halafu ununue luku, na kupita pita panapowezekana siku hiyo.

Shughuli ya kwanza, benki. Kwenda ilipo benki ni shughuli inayohitaji uvumilivu. Unamaliza masaa mawili njiani. Foleni ndefu.

Hatimaye unafika benki. Kwenye mashine ya kuchukulia fedha, foleni ndefu. Unangoja kwa karibu saa moja ili kuifikia. Bahati mbaya, unapokaribia unasikia malalamiko, mashine 'imezira' kazi. Hujui ufanyeje.
Unaenda kujaribu kwingine, unafanikiwa baada ya kama saa moja. Ishakuwa saa saba, hujatia chochote kinywani.

Unaamua kwenda kula. Hotelini wanasema chakula ulichoomba bado kiko jikoni bado, wameamua kutumia mkaa umeme (wa dharura) umekatika. Kwa vile ilivyo joto, unaamua kukingoja badala ya kuungulia juani. Unamalizia saa kamili ukiwa pale. Bahati unakula.

Basi, unaenda kwenye mkahawa wa intaneti, unakalia kompyuta moja. Baada ya robo saa, umeme huo umekatika. Huna cha zaidi, unaondoka ukilalamika.

Unaelekea kwenye luku, nako kafoleni flani. Nusu saa inakatikia pale.

Wakati ukiyaendea yale mengineyo, hewala, unakutana na rafiki zako wa siku nyingi. Hukupanga kukutana nao. Wananogesha michapo mpaka unasahau ulikokuwa unaenda.

Giza linawatenga unaamua urudi nyumbani. Barabarani foleni ni ile ile ya asubuhi. Saa tatu usiku, unafika nyumbani.

Unabahatisha maji unaoga. (Ungewahi usingeyakuta, yamerudi saa mbili). Unaweka luku, unaingia jikoni. Unajipikilisha tambi na tusamaki tuwili.

Wakati vikichemka, unachukua kitabu usome, mara mwaa! Umeme 'wa dharura' umechukuliwa na wenyewe. Hujala.

Kwa kukata tamaa unapanda kitandani ulale huku ukijaribu kufikiri ulivyoshindwa kutekeleza ratiba yako kwa leo. Kausingizi kanakuchukua huyooo unalala. Siku imeisha. Kesho, panapomajaliwa, yatakuwa yale yale.

Maoni

  1. Hapa naweza seama nina bahati mbaya. Tena bahati mbaya sana kusimama foleni kwote halafu mashine haifanyi kazi. ha ha ha ha .

    JibuFuta
  2. ndio maana nitahama jiji hili muda mfupi tu ujao niwaachie kero na nikaishi kwa vibatari na kuchimba shimo kuweka fedha zange na kukojoa kwenye kopo usiku ili nimwage asubhi

    K L L

    JibuFuta
  3. Jana kutwa nilikuwa nikizunguka mjini, nilichokuwa nikikitafuta sikukipata, mara kutahamaki giza hilo, nikakimbilia kwenye kiota changu kujipumzisha, hakika tunapoteza muda bila kujua...

    JibuFuta
  4. Kila siku naamka saa kumi na moja alfajiri nafanya mazoezi kidogo kisha nachungulia net na kusoma ujinga wa wenzangu kwenye blog, baada ya kupata stafutahi mida ya saa moja asubuhi naenda kazini. Duh! foleni, napoteza saa nzima kutoka mikocheni mpaka mjini.

    Natoka ofisini jioni ya saa kumi na moja, foleni tena!!, loo nafika nyumbani saa kumi na mbili kasoro, napumzika kidogo baadae natembea hadi ufukweni kunyyoosha miguu na kufanya mazoezi mafupi,halafu narejea nyumbani na kumsaidia mama kuandaa chakula cha jioni, kisha nakaa kwenye net tena kupitia blog hee!! mara saa nne usiku hiyo, nimechoka na siku imeisha.....

    JibuFuta
  5. Digna,

    Kutunza muda katika mazingira yetu kunaingiliwa na namna huduma zinavyotolewa pamoja na utamaduni. Tunayeyusha masaa mengi katika kungoja huduma hizo. Tunayo safari ndefu kuweza kuutunza muda.


    Koero, sehemu kubwa ya muda wangu wa ziada nautumia kusoma na intaneti. Mazoezi sijayapa bado nafasi. Nitaanza.

    JibuFuta
  6. Ili wananchi
    waitumikie nchi
    yao "kizalendo" rerikali haina budi
    kuhakikisha kuwa inatoa huduma zilizobora na kwa wakati, hii ni pamoja na kuhakikisha hata mashirika binafsi yanatoa huduma bora na kwa wakati muafaka.
    Hii itasaidia kutenga muda mwingi wa kufanya kazi za kimaendeleo na za kujenga taifa.

    JibuFuta
  7. Nuru Shabani30/3/09 11:59 AM

    Suala la muda bongo bado ni tatizo kila kona.Ukienda idara binafsi hawajali muda,idara za serikali ndio usiseme ni kasheshe.

    JibuFuta
  8. Ndugu Nuru naomba tuwasiliane e-mail yangu.

    JibuFuta
  9. Udosini muda wa asubuhi huwezi kuongea na mtu akiwa anakimbizana na rupia,akishakula kalamati na chapati zao kuanzia saa 8 ukitaka huduma utalia.Muda huo kila kitu kinaanza kwenda nyuma ya muda.

    No hurry in Africa!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging