Unahusianaje na nafsi yako?

Huwa unajisikiaje ukijitazama kwenye kioo? Unaridhika na sura unayoiona? Vipi ukiangalia picha zako za hivi karibuni? Unaridhika na ulivyo? Umbo lako? Mtindo wa nywele zako? Rangi ya ngozi yako? Unajionaje?

Watu wengi tunapata shida sana kujikubali. Hatujipendi. Kila tunapojitazama, tunaona kasoro. Wachache wetu huziona kasoro hizo kama vitu vidogo visivyotupa tabu sana. Mtu aweza kujiangalia kwenye kioo, akaona kasoro ndogo, lakini akajipa moyo: "Ngoja nichane, nitapendeza". " Ngoja niende saluni, nikabadili mtindo". Akaziona kasoro na zisimsumbue.

Lakini wengi wetu huvunjika moyo kwa kudhani/amini kuwa kasoro hizo hazirekebishiki. Pengine rangi ya ngozi si nyeupe vya kutosha. Ama umbo letu halivutii, na mambo kama hayo. Kuvunjika moyo kwa namna hiyo, husababisha kujengeka kwa hisia hasi kuhusu nafsi ya mtu mwenyewe.

Jambo moja kabla hatujaendelea: Mahusiano mema na nafsi zetu hutokana na vile tujichukuliavyo. Mahusiano mabaya na nafsi zetu husababisha kujidharau, aibu, na hata kujichukia. Vilevile, mahusiano mazuri na nafsi zetu, huleta kujiheshimu binafsi, kujikubali na kujipenda. ( Kwa bahati mbyaa watu wengi tunayo mahusiano mabaya sana na nafsi zetu wenyewe, ingawa tunajitahidi sana kuhusiana vyema na nafsi za watu wengine)

Na ili kubaini vile tunavyojichukulia wenyewe, ni muhimu kufanya uchanganuzi wa namna tunavyojichulia sisi wenyewe, na namna tunavyohisi tunaonwa na wengine.

Tunavyojichukulia hutokana na vile tunajiona (iwe kupitia kioo, picha nk) na pia vile tunavyoamini tunaweza kufanya mambo fulani kwa ufasaha. Na ilivyo, ni kwamba matokeo ya kwanza tunayoyapata kupitia majaribio yetu, huwa na athari kubwa ya namna tunavyojichukulia. Mfano kijana, kwa mara ya kwanza, anampenda binti, anaanza harakati za kumshawishi awe rafiki yakle. Binti huyo " akimtolea nje", kijana huyo huweza kuvunjika moyo kiasi cha kuweza kujenga chuki na nafsi yake mwenyewe ikifuatiwa na uadui wa kudumu na viumbe hao wa kike, hasa kama matokeo ya jinsi hiyo yatamtokea kwa mara ya pili.

Hivyo, jinsi tunavyopata matokeo tuliyoyatarajia, ndivyo tunavyojenga kule kujisikia vizuri; matokeo tusiyoyatarajia yanapojitokeza mara kadhaa, ndivyo tunavyojenga mahusiano mabaya na nafsi zetu wneyewe.

Tunaweza kubaini tuonwavyo kwa kutathimini mwitikio kutoka kwa wengine ( hasa tunaowaheshimu). Watu wakitusema vizuri, mara nyingi tunajisikia watu wa maana. Tunapata changamko la nafsi. Ndio maana mara nyingi huwa rahisi sana kukubali sifa (hata zile zinazoitwa za kijinga), kuliko udhaifu wetu unaposemwa.

Hata hivyo mambo haya, kama nilivyopata kusema, yana hirizi yake katika maisha ya familia. Kama ulibahatika kuwa na wazazi wanakuosema vizuri, wanaonyesha kukujali, kwa kiasi kikubwa utakuwa mtu mwenye mahusiano bora na nafsi yako. Lakini kwa wale tuliozaliwa katika mikiki miki, bila shaka tuko kimikiki miki vivyo hivyo.

Kwa kuwa kuifahamu nafsi yako ni wajibu wako mwenyewe, nikupe kazi ifuatavyo:

1. Unajionaje?

Chukua karatasi, jielezee unavyojiona. Mwingine anauliza: Nijielezee? Ndio. Orodhesha ujuzi, uwezo, ufahamu, wasifu na kila kizuri unachodhani unacho. Mfano waweza kusema: " Nina uwezo mzuri katika (eneo hili)..." " Ninaujuzi (huu)...." Kwa lugha rahisi ifagilie nafsi yako kadiri uwezavyo. Hiyo insha itakayotoka hapo, itakuwa inaeleza namna unavyojiona mwenyewe, self-concept, kwa lugha ya msisitizo.

2. Wengine wanakuonaje?

Tathmini mahusiano yako na watu wengine. Angalia wanapohusiana nawe huonekana kuamini wanafaidi kipi cha maana. Halafu fanya vile vile ulivyofanya katika (1) hapo juu, lakini sasa jieleze, watu wengine wanaona nini kwako. Sentensi zako zianze na: " Watu wengine wanaamini nimejaliwa..." " watu huniafuata kujua (hiki na hiki)..." Andika mengi kama uwezavyo.

Maelezo yako hayo yatakupa picha ya wewe ni nani, self-perception, kwa msisitizo.

Maoni

  1. Heri ya mwaka mpya!
    Ni kweli kabisa wengi wetu huwa hatuchunguzi au kuzikagua nafsi zetu hata mara moja kwa mwaka. Hali hii husababisha wengi wetu kutokujipenda hata kidogo na kushindwa kabisa kuwapenda wengine.Tunasahau kabisa kuwa sisi binadamu ni wajibu wetu wa kwanza ni kujipenda sisi wenyewe na kuzikubali kasoro au mapungufu tuliyonayo,zipom kasoro ambazo zinaweza kurekebishika na zingine haziwezi kabisa kurekebishika.Sasa ni wajibu wetu kama alivyosema Bwaya ukichukua karatasi na kalamu ukarodhesha maeneo ambayo unayamudu na maeneo ambayo hujamudu iatkuwa rahisi sana kwako kujitambua nafsi yako na kuwaelewa wengine. wengi wetu tumezoea kuona kasoro za wenzetu wakati zetu hata hatuzijui.Tutenge muda wa kuzichunguza nafsi zetu.

    JibuFuta
  2. Nuru,

    Heri ya mwaka mpya na wewe. Ninathamini sana mchango wa mawazo kama yako.

    Nimegundua kuwa unayo mambo makubwa ambayo inabidi yasiishie tu kwenye kisanduku cha maoni. Yasibaki kwenye barua za wasomaji.

    Ningependa kusoma mawazo yako, na wasomaji wengine kuhusu namna ya kuchukuliana na udhaifu usiorekebishika ambao twaweza kukutana nao katika kujichunguza. Nini cha kufanya?

    Hilo ndilo nilililotaka kuligusia baada ya hili. Naamini mawazo ya wasomaji kama wewe, yatakuwa muhimu katika hoja hiyo inayofuata. Karibu.

    JibuFuta
  3. Nashukuru kwa kuthamini mchango wangu.
    Kwa jinsi ya ufahamu wangu nakubaliana na wewe kama mtu ukijichunguza kwa makini utagundua kuna sehemu una udhaifu.Sasa namna ya kukabiliana na huo udhaifu kwanza ni kukubali kuwa unaudhaifu au mapungufu, kinachofuta baada ya kukubaliana na huo udhaifu ni kuangalia upande mwingine au upande mzuri wa huo udhaifu.Labda nitoe mfano kidogo unaweza ukawa una udhaifu wa kukasirika mara kwa mara,sasa badala ya kuangalia upande mbaya wa hasira zako kuwa una waudhi watu basi lichukulie suala hilo ni kama huwa haupendi watu waingilie mipaka yako vilevile ili uwe binadamu kukasirika ni sehemu muhimu ya maisha.Pia Mkuu Bwaya hakuna katika maisha kitu kisichorekebishika ila ninavyofahamu mimi kuna kuamua kutokujirekebisha. Ni kama vile tunavyoamua kucheka au kukasirika. kwa hiyo pia kuna suala la maamuzi.Je ni rekebishe udhaifu wangu au la.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia