Je, majina yetu hayawezi kubeba falsafa zetu?

KUNA hili suala la majina yetu. Inafahamika wazi kwamba tunapozaliwa, mara nyingi shughuli ya kwanza kabisa inayofanywa na wazazi, ni kutupatia majina 'yao' wanayojisikia kuwa yanatufaa. Tunajikuta kama ambavyo tunarithi dini za wazazi wetu bila kuhoji, na majina nayo tunayabeba mazima mazima.


Majina haya mara nyingi tunayapewa bila tafakuri ya kina. Wazazi wanaamua tu wengine ni kwa sababu ya matukio ya wakati huo mtoto anazaliwa bila kujali atakavyojisikia mtoto pale atakapojielewa yeye mwenyewe ukubwani.


Kwa mfano, mtoto anaitwa Matatizo, au Masumbuko, ama Shida na majina kama hayo. Mtoto huyo anapokuja kubaini kuwa jina alilopewa na wazazi wake halikuwa na nia nzuri ndani yake na hivyo kuleta hisia za ubashiri wa aina ya maisha atakayoishi, hapo ndipo mparaganyiko huanzia.

Na wengine hupewa majina mazuri, lakini ni ya kigeni, yasiyo na uhusiano na utamaduni wetu. Ni majina yanayoitwa ya dini, na pengine tunayafurahia lakini kimsingi yakawa kielelezo cha utumwa wa mawazo tuliyonayo. Kumbe majina hayohayo yangeweza kuwa katika lugha zetu na kuonesha kuwa tu watu tunaojiamini na kuupenda utamaduni wetu.


Ninachojaribu kuhoji ni hiki: hivi kwa nini watoto wasiachwe bila majina rasmi mpaka pale watakapojichagulia majina yao kwa hiari yao wenyewe?
Najua kuwa majina si zaidi ya alama ya utambulisho. Majina yanatutofautisha na watu wengine. Hata hivyo, majina haya yanapoleta mgogoro wa kisaikolojia na kiutamaduni, nadhani kuna haja kamilifu ya kuliangalia suala kwa upana zaidi.

Ikiwezekana watoto watambulike kwa majina ya mpito mpaka watakapojielewa wao wenyewe na kujichagulia majina yao yenye kusadifu falsafa zao wenyewe.

Kwa nini majina yetu yasingebeba falsafa zetu wenyewe na wazazi wakabaki kuwa washauri?

Maoni

  1. NI KAZI NJEMA ULIYOITAFAKARI NA KUILETA KATIKA KIBARAZA CHA CHAKULA CHETU CHA KILA SIKU KWA MAONI YANGU NADHANI KAMA INGEWEZEKANA KUFUANYA UTARATIBU HUO TUNGEFANYA LAKINI KUNA WENGINE HUWA WANAJIITA MAJINA MENGINE TENA HASA HAWA WASANII.

    NIMEFURAHI MJADARA MZURI WA KUFIKIRIKIKA ZAIDI.

    JibuFuta
  2. Ahsante sana kaka Bwaya kwa mada hii,
    Mada kama hii iliwahi kujitokeza shuleni wakati nikiwa kidato cha sita.

    Nakumbuka ulikuwa ni mjadala mzito, lakini baada ya kusigana sana kwa hoja mbalimbali tulikuja kugundua kwamba kwa kiasi kikubwa majina tuliyonayo yanaakisi maisha tuliyo yetu.

    Kwa mfano naomba mniwie radhi kwa kutaja majina wazi wazi, kwani bila kufanya hivyo sidhani kwamba maoni yangu yatakuwa na maana.

    katika utafiti wangu, kuna wasichana watatu wanaoitwa Shida ninao wafahamu vizuri tu, ambao wanaishi maisha yenye utata mkubwa, mmoja aliwahi kufeli mara kadhaa kidato cha pili na mpaka sasa yuko mtaani na maisha yake si mazuri sana, mwingine sijui back ground yake ameolewa lakini anaishi kwenye ndoa ngumu ajabu, huyu wa tatu alifukuzwa shule akiwa kidato cha tatu kwa kupata ujauzito, na mpaka sasa anao watoto watatu kila mmoja na baba yake, maisha yake kwa ujumla anayajua mwenyewe,

    Yuko kijana mwingine namfahamu anaitwa Mateso, huyu naye anateseka sana, amesoma kiasi chake lakini hana kazi anazurura tu mtaani,niliwahi kumuuliza kwa nini hatafuti kazi akanijibu kwamba hana bahati ya kupata kazi na kila akipata haichukui muda anatimuliwa, nilipomuuliza sababu akadai kwamba majungu ndiyo yanayomuangusha. Kwa mujibu wa maelezo yake anadai ana damu ya kunguni.

    Labda watu wa utambuzi kaka Kamala na Kaluse watujuze,je kuwa na damu ya kunguni kuna maanisha nini? hiyo ni changamoto kwao,

    Naomba niishie hapa ili wadau wengine nao wachangie.

    JibuFuta
  3. Nimeipenda hii. Nakubaliana na ndugu hapo juu. Watu wenye majina yanayofanana hata mienendo yao hushabihiana.
    Pia nawafahamu watu wenye majina mazuri na mambo yao yanakuwa mazuri.
    Hivi Fadhili, wanakuwaje? Msaada kwenye tuta niongeze kujitambua.
    Ni hayo tu!

    JibuFuta
  4. Kiutambuzi hakuna jina baya wala zuri, bali kinacholeta hicho kinachoitwa jina baya ni tafsiri zetu.

    Kaka Fadhy na dada Koero, kumbukeni tu kwamba, kitu chochote kinapopewa tafsiri na jamii na kuaminiwa, moja kwa moja kinachukuwa nafasi.

    Labda niseme kwa lugha nyingine kwamba jamii ndiyo inayoyapa majina nguvu kutokana na tafsiri iliyoko vichwani mwetu, kwani kila kinachoaminiwa na jamii huwa.

    Mbona kuna majina ya baadhi ya makabila ambayo ukiyatafsiri kwa lugha nyingine, inaweza kuwa ni matusi, je ni nini mustakabali wa wenye majina hayo?

    JibuFuta
  5. tehe

    wahaya wanakamsemo kao/ketu kwamba 'eibara liba liita nyinalyio' tukiwa na maana kuwa jina baya humuuwa mwenye nalo. ni kweli kwamba mtu akiitwa jina baya, pale anapoitika hukubalina na huo ubaya na hivyo kuwa hivyo. kuna wenye majina ya kimalaya na kipepo kutoka kwenye biblia na hivyo huandamwa na vitu/tabia hizo na ndio maana situmii jna langu la bibliani

    wakurya, wahaya nk, huwa wababe na hasa wanaume kutokana na majina yao kuwa ya kibabe, kwa mfano lutatinisibwa, lutabasibwa.

    hata hivyo, ukiwa na jina baya hata kama huelewi maana yake ila jamii inayokuita jina hilo inaelewa maana hiyo mbaya, unaweza kuathiirika kwani kila huitwapo na jamii, hurejea ubaya na hivyo kukutumia nguvu hiyo ya ubaya na yaweza kukukamata kutokamna na ukubwa/wingi wa nguvu ielekezwaya kwako.

    JibuFuta
  6. Wachangiaji,

    Asanteni kwa maoni. Mnaonaje imani kuwa yapo majina ya kidini?
    Wakati sisi tunaamini kuwa Omari ni lazima awe mwislam, kwa wenzetu jina hila limaanisha huyo ni mwarabu.

    Imefika mahala sisi waswahili tunaamua dini ya mtu kwa kuangalia jina lake! Petro hata kama hajawahi kukanyaga kanisa kwa miaka kadhaa, kwetu anaonekana mkristo kwa sababu tu ya jina. Je, huu sio uzembe wa kiutamaduni?

    JibuFuta
  7. Mie najielewa tuu kwa kuwasoma wapendwa. Asanteni sana. Lakini pia niulize hili. Umeshawahi ku-search maana ya jina lako? Nilifanya kisha nikatafuta prints zake na kuna tofauti kiasi hasa nyie wenye majina ya "kizungu". Sasa sijui ni maana ipi iathiriyo jina lako?
    Ni swali tu

    JibuFuta
  8. La kwangu lina maana ya Mkristo. Vipi hapo?

    JibuFuta
  9. Ndesanjo alishawahi kuongelea kwanini aliacha kutumia jina alilobatizwa nalo gregory kipindifulani , kwa kinamna topiki hii ikagusiwa.Mimi kama Simon nishawahi kukosa kimwana niliyempenda Zanzibar baada yakustukia naitwa Simon na kustukia ni Mkristo. Sijabadili jina kwa sababu moja kubwa kuwa naamini siwezi kukana kuwa nilivyo ni mchanganyiko wa yote yaliyotokea mpaka kufikia wazazi wangu wakaniita Simon Mkodo Heriel Kitururu. Mtu yeyote anayeniita Mkodo najua moja kwa moja tulicheza naye utotoni kwa kuwa jina hilo liliisha umaarufu nilipoa anza shule ya vidudu na kisiri kuna kipindi cha utotoni nilikuwa siwaambii watu kuwa jina langu jingine ni MKODO kwa kuwa kuanzia mpaka dada yangu walikuwa namchezo wa kunitania kwa kulibadilisha kutoka MKODO kuwa MKOJO.:-)

    Mimi naamini jina kama laana yenyewe haikulaani kama hujilaani. Ni kama tu tatizo kwa wengine ni changamoto kwa mwenye tatizo kutatua tatizo ingawa kwa wengine tatizo ni chanzo cha mwongezeko wa tatizo.

    Tatizo la umasikini linaweza kuwa changamoto ya kujitoa umasikinini kitu ambacho jina SHIDA kinaweza kukusababishia uamuekuepuka shida. Sijui lakini ningeathirikaje kama ningeitwa MAKABURI, ingawa Simon lenye maana JIWE sioni kama linanisaidia hata kuopoa ngoma.:-)

    JibuFuta
  10. Nimependa falsafa yako Simon.

    Jina lako la Mkodo naona linakuja vizuri zaidi. Tunaomba ruhusa ya kulizindua kabisa kwa shughuli za kiblogu. Unaonaje?

    JibuFuta
  11. Mkodo! Hilo jina hata mimi nimelipenda,
    Unajua majina ya kibantu yana utamu wake katika kuyatamka.

    majina kama Koero, Bwaya Mkodo, Kamala Lutanisimbwa, Mpangala, Mtanga, Mubelwa Bandio Mutwiba na majina mengine nimeyasahau

    JibuFuta
  12. Jamani uhondo umenikosa huu lakini sijachelewa au vipi. Mimi naitwa
    Markus Mapambano Frank Honorius Mpangala. Niliwahi kuzua zogo nyumbani baada ya kuanza kulikana jina la Markus, nikaanza kujiita Mapambano Mpangala au wakati mwingine kutumia majina ya babu yangu Ngachipanda Nganyanyuka Mpangala. Nilihoji mantiki lakini mzee wangu hakunipa jawabu alitazama na kutulia akasema najua unajitambua lakini ukipenda badili sina neno. Duh nikaamua kutulia tu, bora liweliwe tu maana sina hamu nalo hata kama halijanikosea ati la yule mmisionari wa Bavaria ujerumani?

    Nakubali utmbuzi wa Kaluse jamani ni tafsiri zetu, lakini siku hizi tunasafirisha hata majina Bongo mara utasikia Cruz????

    hata hivyo majina yetu saaaaaafi saaaana! Ndiyo maana kuna Koero, kamala,bwaya,kaluse,ngonyani,mwaipopo,............. nimweka deshi jaza jina lako la kibantu.

    Lakini ni kweli majina yanatafsiri falsafa fulani?

    JibuFuta
  13. Mada hii imenivutia sana kaka Bwaya.Mimi itanibidi niwaulize wazazi walitumia vigezo gani mpaka kunipatia jina.

    Napita tu kaka Bwaya,najipanga vizuri, !

    Karibu kwenye kibaraza changu,naamini hutatoka bure!

    JibuFuta
  14. Markus, bora tukuitwe mapambano. Naona kama linaelekea elekea falsafa zako. Au sio?

    Kisima karibu sana kaka.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?