Nchi yetu inatengeneza aina gani ya wasomi?

IMEKUWEPO mijadala mingi kuhusu mfumo wetu wa elimu. Mijadala hiyo inatokana na watu wengi kuamini kwamba elimu yetu ina hitilafu kubwa. Elimu yetu ni wazi kuwa bado haijaweza kukidhi vigezo vya haki vya elimu ya kweli.

Elimu ya kweli, kwa hakika inabadilisha maisha ya watu wake. Elimu ya kweli haitufanyi tujidharau. Elimu ya kweli haitufanyi tujipuuze sisi wenyewe pamoja na utamaduni wetu. Elimu ya kweli haitufanyi tuwe dumavu, watu wasiofikiri zaidi ya mtihani. Kwa hivyo, kwa wengi wetu mfumo wetu wa elimu, kwa hakika, hauna ubavu wa kutosha kutuletea uhuru wa kweli wa fikra na maendeleo.

Mfumo wetu wa elimu unahitaji kubomolewa. Tukiisha kuubomoa, tushiriki kuujenga kwa upya.

Tangu awali, mwanafunzi wa ki-Tanzania hajengwi kusoma zaidi ya mitihani. Mwanafunzi wa ki-Tanzania hatengenezwi kuchambua mambo, badala yake anajazwa 'maarifa' kiasi cha kushindwa kuyapambanua. Kwa hiyo unakuta purukushani kubwa madarasani inakuwa ni namna ya kupata alama A ni si vinginevyo.

Zamani zile nilidhani pengine mambo yangebadilika kwa elimu ya juu. Lakini ni bahati mbaya kwamba sivyo ilivyo. Nisahihishwe katika hili. Kwamba elimu ya chuo kikuu nayo inaendeleza 'ugonjwa' ule ule. Ni nadra sana kupata fursa ya kuelimika kwa maana halisi ya kuelimika. Labda kwa bahati sana unapokutana na mwalimu anayelazamika kwenda nje ya somo ili kutoa elimu isiyopatika ndani ya somo.

Walimu hawaweki mazingira ya kweli ya kujifunza. Wanamtegemea mwanafunzi kuyameza maarifa yao. Matokeo yake wanafunzi wajikuta wanasoma (wanakariri) kwa ajili ya mitihani, ndani ya mabano ya mwalimu husika kupitia viandikwa vyake. Ndio maana baada ya kuhitimu, ni wanafunzi wachache sana huweza kujisomea.

Sifanyi jaribio la kubeza elimu yetu. Lakini pia nisingependa kunafikika. Hivi tunapata wapi uthubutu wa kuwabeza wanafunzi wanaosoma katika baadhi ya nchi zinazosifika katika maendeleo ya teknolijia? Tunawezaje kuwaita 'shalo' na sie kujiona 'dipu' eti kwa sababu wanaweza kutokuvijua vile tunavyovijua hata kama wanao ujuzi mkubwa kivitendo?

Yupi msomi, mwenye kila aina ya maarifa kichwani yenye faida zaidi darasani (mtanzania), ama ni yule mwenye maarifa machache yaliyo mahususi kivitendo?

Hivi elimu yetu inazalisha wasomi ama makasuku wa nadharia? Tunahitaji mjadala wa dhati katika hili. Kujielewa kunaanzia katika aina ya elimu tunayoipata.

Maoni

  1. Ni ukweli unaouma lakini pia wa lazima. Bongo tunasomea mitihani na muhimu ni kufaulu. Tunasahau kuwa kufaulu na kuelimika ni mambo tofauti. Unaweza kufaulu kukariri desa, lakini mwishowe 'ufaulu' huo usikupe tija yoyote.
    Siku hizi kila mtu anasifia ongezeko la ufaulu wakt ukweli ni kuwa ufaulu huo hauendani na kufanuka kwa maarifa.
    Ushauri wangu: serikali iangalie upya namna ya kuboresha mitaala. Mitaala ya sasa imeshaonyesha udhaifu katika kutubadilisha. Tutafute namna ya haraka ya kutafuta suluhisho. Mtindo wa kutumia muda mwingi kudhibiti wanafunzi hauna faida. Sana sana tunazalisha mafisadi watarajiwa.

    JibuFuta
  2. kaka Bwaya nikunukuu:

    "Tangu awali, mwanafunzi wa ki-
    Tanzania hajengwi kusoma zaidi ya mitihani. Mwanafunzi wa ki-Tanzania hatengenezwi kuchambua mambo, badala yake anajazwa 'maarifa' kiasi cha kushindwa kuyapambanua. Kwa hiyo unakuta purukushani kubwa madarasani inakuwa ni namna ya kupata alama A ni si vinginevyo"

    Maelezo haya yamenikuna sana.
    Kuna kitu kinaitwa solving, ukienda kwenye hizi sijui ni shule au niziiteje, zinazowaandaa wanafunzi wanaotaka kurudia mitihani ya kidato cha nne au cha sita. Badala ya kufundishwa wakaelewa, wanafundishwa kujibu maswali ya mitihani, hiyo imeenea hata kwa hizio shule zinazotangaza kufundisha kidato cha kwanza mpaka cha nne kwa miaka miwili, wanasoma kujibu mitihani tu, na sio kuelewa wanachofundishwa.
    nakubaliana na wewe, inabidi mfumo wetu wa elimu ubomolewe, kisha ujengwe upya.

    ngoja niwape nafasi na wengine watoe maoni yao.

    JibuFuta
  3. Mimi nafikiri kabla ya kuubomoa mfumo huu wa elimu, kuna haja ya kuangalia kama kuna mambo yoyote ambayo kwa namna moja ama nyingine yanachangia hali hili ya tatizo la mfumo duni wa elimu.


    Kwa sababu bila kufanya hivi nionavyo ni kwamba mfumo wa elimu unaweza kubadilika na kutokana na visababishi vya mfumo wa zamani ambao haukuwa mzuri bado vitakuwepo, hii itaweza kusababisha hata mfumo huu mpya kuonekana hauna maana.

    Kwa mfano,wanafunzi waliowengi wanafahamu kuwa elimu ndio njia pekee ambayo itamsaidia kuwa na maisha bora hapo baadae na njia pekee ya kuifaidi elimu ni kufaulu mitihani ili kusonga mbele hadi ngazi za juu za kielimu na hatimaye kufanya kazi akiwa amekaa ofisini "ful kiyoyozi" "muziki wa taratibu" na kuitwa "bosi".Njia ya pekee ya kufaulu mitihani ikiwa ni "kukariri" viandikwa kutoka kwa wale waliopitia kwenye mfumo huu wa kukaririshwa.Njia nyingine wanayoitumia katika kufaulu mitihani ni kuiba mitihani inayotarajiwa kufanywa. Hapa napata picha ya kwamba "malengo ya wanafunzi husika ni tofauti na malengo ya elimu inayotolewa"


    Kulingana na mawazo yetu sisi watanzania,muhitimu wa digrii ya biashara anaweza kuchekwa sana kama atafungua duka lake na kulisimamia yeye mwenyewe kisomi.Hapa utaona jamii inavyochangia mfumo duni wa elimu tulionao.Namaanisha hivi,wanaotakiwa kufanya kazi za nguvu ni wale wenye elimu ndogo na wale wasio na elimu kabisa.Pia utaweza kugundua kuwa kwa wale waliobahatika kuingia darasani,wale walioishia madarasa ya chini ndio wanaanza kutumia elimu yao kivitendo zaidi na katika hali ya kiuhalisia.
    Ninawaomba watz walioko ughaibuni wajaribu kutupa japo kwa ufupi kuhusu mfumo wa elimu wa huko na je malengo ya elimu ya huko yanafuatwa vizuri na wanafunzi wenyewe?

    Kweli mfumo wa elimu haujakaa vizuri, lakini malengo ya elimu mwayaonaje? Je yanasema kinachotakiwa ni mwanafunzi kufaulu mitihani?

    Anayetaka kugombea uraisi wa tanzania ni lazima awe katika ngazi ya elimu ya kuanzia kiwango cha "shahada ya kwanza" hili lina mchango wowote kwa mfumo wa elimu tulionao? Ingekuwaje kama kungekuwa na vigezo ambavyo vinamlazimu mgombea kuonyesha chochote alichoifanyia jamii?


    Inashangaza sana wizara ya elimu kutangaza kuwa kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi kimeongezeka na hivyo elimu imefanikiwa na kwa upande mwingine tunasikia kwamba mtanzania wa leo anaishi kwa kiwango cha chini ya dola moja kwa siku. Hapa unaonaje? Ni kweli elimu itakuwa imefanikiwa?

    JibuFuta
  4. Kweli kabisa mfumo wetu wa elimu sio mzuri sana,mm naona bora tuuboreshe,kuliko kuubomoa.ni hayo tu.

    JibuFuta
  5. Naomba niwe na mtizamo tofauti kidogo.Kwanza,sidhani kama ni wanafunzi wa Kitanzania pekee wanaosoma kwa ajili ya kufaulu.Kwa bahati nzuri wiki hizi mbili tatu hapa chuoni wanafunzi wako busy na mitihani yao...I wish ningeweza kupiga picha mbili tatu kuonyesha lundo hili la binadamu kutoka nchi na asili mbalimbali linavyohangaika kusoma kwa bidii zaidi muda huu KWA AJILI YA KUFAULU.Kwa mwanafunzi,KUFAULU KWANZA,kisha matokeo ya kufaulu huko yatategemea mambo kadhaa "huko uraiani".Tatizo haliko Tanzania pekee bali kwenye mfumo mzima wa elimu ya kimagharibi ambayo iliipiga teke elimu yetu ya asili baada ya ujio wa ukoloni.Huo ndio uchumi wa soko,ambao kwa kiasi kikubwa unazingatia mashindano na survival of the fittest.

    Baba wa Taifa alichukizwa na alichokiona kwenye mfano halisi wa mfumo wa elimu ya kimaghaibi katika kipindi cha ukoloni.Baada ya uhuru yakafanyika majaribio kadhaa ikiwa ni pamoja na kwenye Education for Self-Reliance...kwa kifupi,dhamira ilikuwa kubadilisha mentality kuwa elimu ni kwa ajili ya kupata ajira bora.Nafasi haitoshi kuelezea namna matarajio bora ya Mwalimu yalivyoishia kuwa ndoto nzuri ambayo haikutimia ipasavyo.Dhamira ya kuwa na wahitimu (wa shule ya msingi au sekondari) ambao watakuwa nyenzo muhimu katika kuleta mapinduzi ya kilimo ilipelekea "mapinduzi mengine" kama UPE...matokeo yake sote tunayajua.

    Tunaweza kujilaumu au kulaumiana katika mambo flani pasipo kuangalia forces flani ambazo kulingana na mfumo tulionao (sio wa elimu) bali wa dunia kwa ujumla,sisi tunabaki kuwa watekelezaji wa matakwa ya hao wenye nguvu (inajirudia tena,survival of the fittest).Hivi katika mfumo huu hatari wa samaki mkubwa kumla dagaa tunaweza kweli kuwa na maamuzi ya mwisho na kile tunachokiita CHETU?

    Tunaweza kutaka wanafunzi wetu waelimike badala ya kusomea mitihani,lakini wakifanya hivyo wataishia kufeli.Na kibaya katika mfumo huu wa mbwa kala mbwa (dog-eat-dog)kuwa na kinachokutofautisha na mwenzio ni kinga na nyenzo muhimu,ndio maana wengi wanahangaika na kupata maksi nzuri au vyeti pasipo kujali sana kama vinaendana na uelewa wao.

    Nadhani tunachoita tatizo la kimtzamao wa kitanzania ndio hali halisi ya mfumo hatari wa kimagharibi,mfumo ambao mtu ni muhimu kuliko utu,sifa (credentials) zinafunika umuhimu wa wajibu,nk.Ujamaa ulikuwa na uzuri wake lakini ndio hivyo tena...hatuna budi kuishi kulingana na sheria za sasa za mchezo huu hatari.

    JibuFuta
  6. Naanza kwa kunukuu "Ndio maana baada ya kuhitimu, ni wanafunzi wachache sana huweza kujisomea."
    Jaribu kutembelea maktaba zetu kama hauta kutana na wanafunzi wamejazana wakikariri manake sio kusoma,nenda sehemu wanazouza magazeti utashanga kuona watu wanasoma vichwa vya habari baadaye wanaondoka,hawanunui magazeti.Hudhuria matamasha ya vitabu watu hawaendi kununua vitabu.Tembelea majumbani kwa watu vitabu utakavyovikuta ni vile vya mashuleni tu na ni kwa sababu kuna wanafunzi wanavitumia.
    Kwa kweli nchi hii inapoenda kwa upande wa elimu ni kubaya sana.
    Mfumo wetu wa sasa umekuwa wa kumfanya mtu atake kufaulu zaidi kuliko kuelewa.Waalimu wanawafanya wanafunzi waamini kusoma ni vitabu vya shule tu,nje ya hapo ni kupoteza muda.Mimi ninaamini kama hautasoma vitabu mbalimbali maarifa au uelewa utatoka wapi?Nenda vyuo vya elimu ya juu,sasa huko ndiyo balaa,ni madesa kila kukicha na walimu ambao wengi wao nia madokta na maprofesa wamekuwa ni mabingwa wa kuwakaririsha wanafunzi,nitatoa mfano,Mhadhiri anaingia darasani na kuanza kusema "My friend I am very sliperly,if you try to catch me this way I go this way so be very careful,if not you your very best friend will go".Hebu jaribu kufikiria kama ni wewe unayesoma somo la huyu mwl itakubidi uanze kusoma kwa kufaulu na sio kuelewa.Ipo mifano mingi sana ya namna hii katika taasisi zetu zinazotoa elimu.
    Najua tunaweza kujisifu kwa kiwango cha wanafunzi kufaulu je,hao waliofaulu wanaoufahamu wa kutosha?
    Wengi wa wasomi wakitoka makazini ndiyo utawakuta wamejazana na baa au kwenye makumbi ya starehe,wiki nzima hwana hata muda wa kupitia kurasa moja ya kitabu kupata maarifa.
    Mimi ninaamini kama tungekuwa na wasomi wenye ufahamu nchi yetu ingekuwa inapiga hatua mbele.

    JibuFuta
  7. Kisima, nchi yetu katika kuandika malengo imefanikiwa sana. Malengo huandikwa kwa lugha nzuri inayovutia. Ukiyasoma kwa juu juu, utadhani walioyaandika walishaondoka siku nyingi kwa jinsi ambavyo utekelezaji wake hauna uhusiano na lugha tamu ya malengo hayo.

    Kwa hivyo, sidhani kwamba tatizo liko kwa wanafunzi wenyewe. Tatizo liko kwenye mfumo wenyewe. Wanafunzi wanasababishwa kudhani kwamba elimu ni kufaulu mtihani. Kila kitu darasani kinawaambia hivyo. Kuanzia namna ya ufundishaji, mbinu za kutathimini uelewaji wa mwanafunzi na hata namna tunavyoyachukulia matokeo yaliyoandikwa kwenye karatasi.

    Unakuta kinachotaminiwa ni kilichoandikwa kwenye cheti na sio alichonacho mwenye cheti juu ya mabega yake.

    JibuFuta
  8. Kaka Evarist,

    Asante kwa maoni yako safi. Yameleta ladha nzuri zaidi.

    Labda nikuulize: Pamoja na wanafunzi hapo kuonekana kusomea mtihani zaidi (jambo ambalo halikwepeki katika maisha ya shule) je, unadhani namna wanavyofundishwa, wanavyopimwa uelewa, namna wanavyoyatumia matokeo ya mitihani hiyo (vyeti) inafanana na hapa nyumbani?

    Tungependa kupata tofauti za msingi unazoziona.

    Kwa mfano ikiwa walimu wanafanya kama alivyoeleza Nuru Shabani hapo juu kwamba wanaonekana kuwa na kiu ya kuona wanafunzi wakitaabika kuwaelewa, kuwafanya walazimike kusoma 'madesa' yao kuliko vitabu, ama namna wahitimu wa elimu hiyo ya wakoloni wanavyoishia uraiani ( wanaendelea kupenda kusoma au ndio inakuwa basi tena?). Vilevile jinsi wanavyopimwa (mitihani) na kadhalika.

    Tunaomba msaada wako.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?