Baada ya migomo mwaka jana...

Heri ya mwaka mpya. Bila shaka ulipata fursa nzuri ya kuupokea mwaka huu popote ulikokuwamo. Naamini si tu kwamba uliupokea mwaka kwa madebe na fataki, lakini pia ulipata fursa ya kuyaandika malengo na matarajio yako kwa mwaka huu tena. Kama hujafanya hivyo bado, hima, naufanye hivyo sasa.

Ningependa kuamini kuwa mwaka huu utakuwa wa kasi kubwa kwa blogu zetu. Naamimi mwaka huu wanablogu watakuwa pamoja zaidi kuliko ulivyokuwa mwaka jana. Naamini mwaka huu tutakuwa na mijadala tofauti tofauti zaidi kuliko ulivyokuwa mwaka jana. Wenye kujadili siasa watafanya kwa ufanisi zaidi. Wenye kamera zao watazitumia kwa ufanisi zaidi. Wenye kujadili mambo ya kijamii watafanya hivyo kwa moyo zaidi. Wale wa mambo ya falsafa na kila aina ya maarifa watafanya hivyo kwa bidii zaidi. Almuradi kila eneo, naamini kuwa litapata wabobezi. Ili kulifanya jukwaa la blogu kuheshimika zaidi. Blogu ziwe ukumbi muafaka kwa kila mwenye wazo na maarifa ya kuwashirikisha wengine.

Mwaka uliopita ulichukua sura ya watu kudai haki zao, iwe kwa njia za kistaarabu ama zile zinazoonekana kutumia miili zaidi. Zilionekana dalili nyingi za kile kinachoitwa ubeuzi. Katika maeneo yaliyoleta purukushani kubwa na ya kutetemesha, ni elimu. Wanafunzi walitikisa nchi kwa migomo. Malalamiko ya wanafunzi yalikuwa kuidai serikali yao kuwalipia gharama za masomo kwa asilimia zote. Ikumbukwe kuwa malalamiko haya yalikuwepo tangu awali utaratibu wa kupewa mikopo kwa madaraja ulipoanza kutumika kwa nguvu.

Ubaya wa sera hii umezidi hasa baada ya kubainika kuwa hapakuwapo na umakini katika kupanga madaraja ya mikopo hiyo. Vigezo zinavyotumika havieleweki kwa kiasi cha kushangaza. Wanafunzi walio ndugu wa damu kwa mfano, watokao familia moja kwa maana ya vigezo vinavyofanana, walijikuta wakipewa mikopo hiyo kwa madaraja tofauti.

Baada ya kugoma, serikali kama ilivyo kawaida yake, ilitumia nguvu nyingi. Vyuo vilifungwa kwa muda usiojulikana. Na leo hii, mbali na kupotezewa muda mwingi wa masomo, tunaambiwa wapo wanafunzi wa kike wanajiuza kutafuta namna ya kujikimu.

Hivi majuzi nikiwa hapa hapa Singida nilikutana na blogu hii hapa. Bado naicheki. Unaweza kuitembelea uweze kuamua mwenyewe kile hasa kinachofanyika mumo. Sijafikia mahala pa kuhitimisha ila kuna jambo nimeanza kulihisi.

Je, ni kweli wanafunzi walikuja na madai yao na hatimaye kugoma, kwa shinikizo la 'wanasiasa' kama inavyodaiwa na blogu hiyo?

Nakutakia utekelezaji mwema wa mipango yako kuanzia hivi sasa.

Maoni

  1. MIMI kwa upande wangu ninaona wanafunzi wakirudi chuoni wasikae kinywa kwani kukaa kinywa ni ishara ya kuwa hoja zao zilikuwa hazina ukweli.

    Iwapo kama watasimama imara na kuendelea kudai haki yao natumai watapata, kwani haki haishindwi hata kama serikali itatumia mtutu na bunduki, haki itabaki palepale. Hoja yangu ni hiyo wanablogu wenzangu.

    JibuFuta
  2. kaka Bwaya asante sana kwa blogu hiyo. Mimi niliwahi kuiona blogu hiyo kitambo sana ila naona KINYAA kama siyo KICHEFUCHEFU.
    Hoja kwanza sipendi blogu inayozungumzia ushabiki wa kisiasa bila kujua undani wa mambo au uhakika wa vyanzo, pili KINYAA changu ni matumizi ya lugha. kwanini kama blogu yako ni ya kiswahili unachanganya na kiingereza? ndiyo usomi au? mbona sote tupo hapo hapo mlimani lakini tunajali kama blogu ni ya kiswahili basi lugha yake isichanganywe iwe kiswahili fasaha na kama kiingereza basi iwe hivyo. Natamani sana kutapika nikiiona blogu hiyo na nitasema katika ukurasa wangu bila kificho nitamlenga moja kwa moja.

    Mgomo haukuwa wa Odong wala nduguze, mgomo ulihusu sera za uchangiaji. Niliwahi kuandika makala katika matoleo matatu ya gazeti la RAI 'TUNAGOMEA SERA AU MFUMO'? lengo likiwa kudurusu mambo kadhaa kuhusu migomo ya vyuo na uendeshaji wa nchi yetu. Mimi nasema tatizo letu ni mfumo wa kutuongoza kwani sera zipo kibao lakini mfumo gani ikiwa walishazika mwaka 1992 kuwa ujamaa ni uhayawani halafu ukwamuaji wa mabenki unafanyika kipindi hiki kwa sera za ujamaa.

    Blogu hiyo inasema kwamba alijiingiza katika siasa. Niliwahi kumwuliza mwandamizi mmoja wa chuoni pale ni kweli kwamba odong hakustahili kusoma eti hakuleta vyeti? nikamwambia ningekuwa Rais ningweatimua kazi Mukandala na Maboko wake kwani ni uzembe useme leo mtu kasoma miaka kadhaa eti hana cheti. Nani hajui kama Mkunadala ni mshauri wa mambo ya siasa kwa Kikwete? unafikiri kwanini alimchagua kuwa kiongozi wa UDSM? wanajua hapo ni mahala ambapo zinaanza chokochoko kwahiyo lazima wathibitiwe, yeye atasema fulani na fulani wakorofi. Sasa Julius Mtatiro alichochea mgomo lini? Kuna jamaa anaitwa Burton Gwakisa alikuwa waziri wa mikopo DUCE(chang'ombe) majuzi aliomba kuwania ubunge wa mbeya vijijini kwa tiketi ya chadema.

    Nisomapo blogu hiyo naharisha kabisa sina hamu nayo kwani ni propaganda tu zinaenezwa, mbona Gwakisa alishasema yeye ni mfuasi wa chama fulani, huyu ameitwa mara kadhaa ili kunyamazishwa na amesaini makubaliano kadhaa na uongozi wa chuo sababu tu anahamasisha kugoma kwa maslahi ya wote.
    UDSM ukiona wanashindwa kutatua wanakimbilia kuna kujiingiza katika siasa, wasemao hayo ni wapumbavu kabisa, hawajui undani wa mambo. Hata kama watasema leo kuwa siasa zimetawala nakwambia kuna mgomo hatari unakuja ambao utakuwa mkubwa kuliko huu, iwapo mambo yanayofanyika yataendelea kufanywa NABASHIRI HILO. Binafsi sina mpango tena na sitaki habari za elimu mpaka kichwa kitulie na kuona mwelekeo mzuri vinginevyo sirudi tena.

    Blogu hiyo inanichafua kwani inaonekana jamaa hawajui kiswahili wala kiingereza WIZI MTUPU!!!!!

    JibuFuta
  3. Katika maisha.....
    Tunao wapiganaji,
    Wasio choka kuhoji,
    Harakati ziso foji,
    Malengo kuyafikia.

    Katika maisha.....
    Tuna wanaharakati,
    Hata liwe varangati,
    Hawachoki kufight,
    Hakika hufanikiwa.

    Katika maisha.....
    Huwa kuna vibaraka,
    Hupenda kutuzunguka,
    Nia zetu kuvunjika,
    Tusiweze endelea.

    Katika maisha.....
    Tunapaswa tuyajuwe,
    Mema na mabaya yawe,
    Twataka tufanikiwe,
    Nasi tutafanikiwa.

    Ni hayo tu kaka Bwaya.!

    JibuFuta
  4. Bwaya,watawala wetu wana tatizo sugu la kukimbilia kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu.Kuhitimisha kwamba migomo vyuoni ni kutokana na shinikizo la wanasiasa ni mtindio wa tafakuri.Simple logic inaweza kubainisha kwamba mwanafunzi anayehitaji kuhitimu ndani ya muda stahili hawezi kushawishiwa kirahisi atende jambo (kama kugoma) litakalopelekea sio tu kuchelewesha muda wake wa kuhitimu bali pia kuathiri mwenendo mzima wa masomo yake.

    Lakini tunaweza kwenda mbali zaidi ya hapo.Kinachoitwa SHINIKIZO is in fact KUELEZANA HALI HALISI.Sioni dhambi kwa wanasiasa kuwaeleza wananchi chanzo halisi cha matatizo yao.Kwani matarajio yetu kwa wanasiasa ni yapi hasa kama sio kusaidiana nasi kuyatambua matatizo yetu na kutafuta njia sahihi za kuyatatua?Wanasiasa wanapojumuika na wanavyuo kujadili matatizo ya sekta ya elimu wanaishia kulaumiwa kwamba wanashinikiza migomo.I dont buy that b***shit.

    Tuliopita vyuoni enzi hizo tunafahamu namna elimu yetu ilivyokuwa politicized.Umoja wa vijana wa CCM ulikuwa taasisi muhimu kuliko serikali za wanafunzi,lakini wakati huo haikuwa DHAMBI wala SHINIKIZO kwa vile ulikuwa mkono wa chama tawala.

    Ni muhimu kutambua kuwa elimu ni miongoni mwa jitihada za binadamu kuyamudu mazingira yake,na wasomi (including wasomi watarajiwa vyuoni) hawawezi kuwa watazamaji tu pale wanapoona mambo yanakwenda mrama.Zaidi,hawawezi "kutulia" pale ubabaishaji unapoathiri jitihada zao za kujiendeleza kielimu.

    Tatizo la msingi katika suala zima la migomo vyuoni liko kwenye utekelezaji wa sera ya liberalization ya mfumo wetu wa elimu.Na tatizo hilo ni sehemu tu ya utekelezaji mbovu wa sera nzima ya liberalization,iwe kwenye siasa au uchumi.

    Again,kukimbilia kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu hakuwezi kuwasaidia watawala wetu kumaliza matatizo yanayoikabili nchi yetu.Kufunga vyuo na adhabu nyingine sio tiba ya matatizo yaliyopo,na pengine ni muhimu zaidi kuwa na kinga badala ya tiba za "zimamoto" ambazo zina madhara makubwa in long run.

    JibuFuta
  5. Bwaya Nipo majukumu kaka.Ukweli kazi ipo sana nimeangalia matatizo na migongano ya wanachuo inatia huruma.Siku hizi naona ukidai haki yako basi wanakuja watu na kudai madai yako yamekaa kisiasa.

    Ahsante sana Markus kwa kutanabaisha.

    JibuFuta
  6. Sina lakuongezea! Nipo nasikiliza lakini!

    JibuFuta
  7. Hizi ni dalili za chama kulichokuwa kikiitwa cha mapinduzi, kuishiwa. Nimesoma kwa makini maoni ya wachangiaji waliotangulia, na kwa kiasi kikubwa nakubaliana nao.

    CCM imechoka. Na huu ndio wakati wa kuking'oa madarakani. Wanachofanyiwa wanafunzi si stahili yao. Ni uonevu wa kutupa.

    Kusema kwamba eti wanatumiwa na wapinzani ni uchovu wa fikra.

    Mpka kieleweke

    JibuFuta
  8. Kaka Bwaya mara nyingi nakwepa sana mijadala inayohusiana na masuala ya vyuo vyetu vikuu.

    Kwani mtu akikuambia ujadili matatizo ya vyuo vyetu vikuu ni sawa na kuambiwa utembee juu ya jamvi la misumari, hujui ukajage wapi.

    Kwa hiyo naomba unisamehe, sitachangia chochote.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Kama sio utumwa ni nini hiki?