Tumetengwa na Watu ili Tuunganishwe na Teknolojia?
PICHA: The Brown Daily Herald |
Ukisoma
gazeti au kitabu, kuna mahali utakutana na ishara kuwa umefika mwisho hivyo
utaliweka gazeti au kitabu chini, na kuendelea na mambo mengine. Vivyo hivyo
unapoangalia filamu, unapofuatilia kipindi au taarifa ya habari kwenye radio au
televisheni. Kuna mahali utafika utakutana na ishara kuwa sasa umefikia mwisho.
Kipindi kimeisha, taarifa unayofuatilia imeisha, basi unapata nafasi ya kufanya
maamuzi ya ama usibiri kingine au uendelee na mambo mengine.
Mitandao haitupi fursa hiyo. Wabunifu wa mitandao hii wameitengeneza kwa namna ambayo hukutani na mwisho. Mitandao hii, hasa ya kijamii, ni kama 'maporomoko' ya habari mpya kila sekunde yanaitwa 'streaming', 'TL' na majina mengine. Kadri unavyofuatilia habari moja, ndivyo unavyoletewa 'mafuriko' ya vingine vipya. Hukutani na ishara kuwa sasa umekaribia kufika mwisho, kapumzike. Matokeo yake unaweza kujikuta muda wote unaunganisha habari moja kwenda nyingine.
Hali hii inaathiri sana mfumo wa maisha yetu. Kwanza, tunakosa muda wa kutulia. Hatupati muda wa kutafakari mambo bila kuingiliwa ingiliwa na gharika ya habari mpya zisizo na undani. Habari zenyewe siku hizi inabidi ziwe fupi kadri inavyowezekana kwa sababu hakuna mtu anaweza kufuatilia kitu kwa zaidi ya sekunde kadhaa.
Kule kwenye mtandao wa Twita, kwa mfano, kinachoandikwa ni sharti kiwe na herufi zisizozidi 140, video za WhatsApp na Instagram hazipaswi kuzidi dakika moja na kadhalika. Haya yote yanathibitisha kuwa watu sasa hivi hatuwezi kufuatilia kitu kimoja kwa muda mrefu. Tunavutiwa na vitu vingi kwa wakati mmoja. Tumekuwa kizazi cha nusu nusu nyingi. Hatuna uzingativu.
Matokeo yake hata kwenye maisha yetu ya kawaida, uzingativu umekuwa adimu. Mazungumzo ya kawaida, kwa mfano, huendelea wakati kila mtu akiendelea kugusa gusa kioo cha simu. Mnaweza kuwa watu wengi, lakini kila mmoja yuko 'busy' duniani. Roho i radhi, lakini vidole na uzingativu vi dhaifu.
Pili, shauri ya kukosa utulivu wa nafsi, tunajikuta tunakosa furaha. Kadri unavyotumia mitandao hii muda mwingi, tafiti zinasema, ndivyo unavyojisikia kusongwa na mawazo. Kimsingi msongo wa mawazo ndio unaofanya watu wawe watumiaji wazuri zaidi wa mitandao. Ni namna fulani ya kujiliwaza.
Nimefanya maamuzi na ninayasimamia. Kwamba sitagusa gusa simu wakati ninazungumza na mtu. Ikiwezekana, simu ikae mfukoni wakati wote wa mazungumzo na ikibidi izimwe kabisa ili nizingatie ninachokizungumza na mwenzangu.
Pia, sitakaa mezani kula au kufanya kazi, niwe mwenyewe au nikiwa na watu wengine huku nikiendelea kugusa gusa simu kufuatilia mafuriko ya habari za kila sekunde ambazo wakati mwingine zisihitaji. Nimeipiga marufuku nafsi kufikiri eti bila kuishi kwenye gharika hii ya habari mpya kila sekunde basi maisha hayaendi. Najua si kazi nyepesi. Nafahamu kuwa kwa enzi hizi za mafuriko ya habari, maamuzi haya yanaambatana na maumivu fulani. Lakini hakuna namna nyingine. Je, unadhani nitafanikiwa? Je, unaweza kuungana nami katika hili?
Maoni
Chapisha Maoni