Ukitaka Mwenzako Akuamini, Jifunze Kutanguliza Mahitaji Yake
PICHA: Merriam-Webster |
WIKI iliyopita nilitoa mifano michache
ya namna ubinafsi unavyoweza kuwa na manufaa katika kutusaidia kupambana na hatari
zinazotishia usalama wetu –kimwili na kisaikolojia. Nilisema ubinafsi pamoja na
ukakasi wake unalenga kutusukuma kupata mahitaji yetu ya msingi. Jambo hili
liliwahi kuelezwa na Abraham Maslow.
Kwa mujibu wa Maslow, unahitaji
‘kushibisha’ ule ubinafsi unaoishi ndani yako kwanza ili upate nguvu za kupanda
ngazi ya juu kabisa ya ustawi wa mwanadamu. Maslow anasema wakati huo ‘unaposhibisha’
ubinafsi wako, muda mwingi utautumia ‘kupambana na hali yako’ kuliko kujali
ustawi wa watu wengine. Utakuwa na marafiki unaowatumia ‘kushibisha’ ubinafsi
wako. Utatamani kupendwa kuliko kupenda. Utatarajia kupewa kuliko kutoa.
Hata hivyo, Maslow anasema, kadri njaa
hiyo ya kukidhi mahitaji yako binafsi inavyoshibishwa, ndivyo unavyopanda ngazi
kuanza kujali mahitaji ya watu wengine. Katika hatua hii, Maslow anasema,
mwanadamu hujiona anacho kitu cha kumpa mwingine. Furaha yake huanza kutegemea namna
anavyoweza kugusa maisha ya wengine kuliko anavyonufaika kibinafsi. Ikiwa hivyo,
kwa mujibu wa Maslow, basi unakuwa umefikia hatua ya juu kabisa ya kupevuka kama
binadamu aliyestawi na kufanikiwa.
Urafiki kati ya watu wawili waliofikia hatua
hii ya ustawi wa nafsi una nafasi kubwa ya kuleta utoshelevu mkubwa kwa sababu
kuu mbili. Kwanza, kila mmoja anakuwa na nguvu ya kuvaa viatu vya mwenzake akitaka
kuelewa mahitaji yake. Mazungumzo yao, kwa mfano, hujaa usikivu na uzingativu
kuliko kuongea na kutaka kusikika.
Mnasihi maarufu Carl Rogers aliuita uwezo
huu, empathetic understanding, yaani kuvaa viatu vya mwenzako ili kuelewa kile anachojaribu
kukisema. Hii ndiyo sifa ya mtu anayetanguliza mahitaji ya mwenzake. Hata pale mtu
huyu anapokuwa hakubaliani na mtu, bado ni rahisi kwake kuvumilia. Uvumilivu ni
tabia ya mtu anayetambua upande wa mwenzake.
Niliwahi kukutana na
Evans (sio jina lake halisi) aliyekuwa na mgogoro na mke wake. Evans alikuwa na shida ya mawasiliano na mke
wake aliyekuwa amezira kwa hasira kwa majuma kadhaa. Mara nyingi walipojaribu
kuzungumza, Evans aliniambia, waliishia kugombana. Ukuta mkubwa wa mawasiliano
ulikuwa umejengeka kati ya Evans na mke wake.
Katika mazungumzo
yetu, niligundua Evans alikuwa na tatizo la kutokusikiliza. Muda mwingi katika
mazungumzo yetu, Evans alishika shika simu yake kufuatilia kilichokuwa
kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii. Wakati mwingine alipiga simu bila hata
kuomba radhi. Hakuwa na utulivu. Nilihisi hiyo ndiyo tabia yake hata anapokuwa
nyumbani. Nilimwomba kukutana na mke wake pia kama sehemu ya kutafuta ufumbuzi.
Alinikubalia.
Mke wake alithibitisha
hisia zangu. Alalamika namna Evans alivyo mwanaume mbinafsi asiyejitambua. Alitoa
mfano kuwa mara zote walipozungumza, Evans alishikilia msimamo wake. Evas hakupenda
kusikiliza upande wa mke wake. Wakati mwingine alifanya maamuzi yanayopendelea
upande wake bila kuzingatia mke wake alifikiri nini. Ilikuwa dhahiri mke wake
alikuwa amechoshwa na tabia ya Evans kujitanguliza mwenyewe.
Evans alihitaji kujifunza
tabia mpya ya kumtanguliza mke wake. Evans alihitaji kujifunza kuwa msikivu na
kuvaa viatu vya mkewe. Tulifanya zoezi la kusikiliza kwa uzingativu.
Tulijifunza umuhimu wa kuacha kutumia simu, tabia ya kuangalia wapita njia,
kupiga miayo, na kujenga tabia ya kufuatilia anachokisema mwingine kwa vitendo.
Haikuwa kazi rahisi lakini hatimaye Evans alielewa. Evans alijifunza namna
tabia yake ya kujitanguliza ilivyochangia tatizo kinyume na mawazo aliyokuwa
nayo awali.
Evans alirudi
nyumbani kufanyia kazi tuliyojifunza. Alianza kujifunza ‘kumpa masikio’ mke
wake na kuelewa mtazamo wake. Evans alianza kutanguliza hisia za mke wake
badala ya kuweka mbele hisia zake. Haikuwa rahisi mwanzoni. Lakini aliposimamia
tabia hiyo mpya kwa muda, taratibu mke wake alianza kumwamini. Moyo wake
ukaanza kufunguka kwa Evans. Nilipokutana na Evans majuma kadhaa baadae
aliniambia, “Kumbe kumtanguliza (mke wangu) kumenisaidia kupata nilichokitaka.”
Evans aliaminika kwa sababu alijifunza kumtanguliza mke wake.
Hiki ndicho
ninachomaanisha ninaposema ndoa bora hujengwa kwa uwezo wa kumtanguliza
mwenzako. Ingawa kwa haraka haraka inaweza kuonekana ni utumwa wa namna fulani,
lakini mwisho wa siku, unapomtanguliza mwenzako, wewe ndiye unayenufaika kwa
kumfanya mwenzako naye asukumwe kufikiria mahitaji yako.
Evans angeendelea
kusisitiza jinsi alivyo sahihi kwa mipango na tabia yake badala ya kufikiri mke
wake naye anawaza nini, asingeweza kubomoa ukuta wa mawasiliano uliokuwa
umejengeka kati yao. Kwa maana nyingine, kutanguliza mahitaji yake kungemnyima
hitaji lake la kuwa karibu na mke wake.
Nimalizie kwa kukuuliza,
mara ngapi umeshindwa kujua mwenzako anahitaji nini kwa sababu muda wote
umekuwa ukitanguliza kile unachokitaka? Je, kwa kutanguliza matakwa yako,
umekuwa ukijanga uhusiano wako na mwenzako? Pengine unahitaji kujifunza
kumtanguliza mwenzako. Kwa kufanya hivyo mwenzako atakuamini kama ilivyotokea kwa
Evans.
Makala haya yalichapishwa kwenye safu ya SAIKOLOJIA, kwenye gazeti la MTANZANIA. Unaweza kufuatilia kila Alhamis.
Makala haya yalichapishwa kwenye safu ya SAIKOLOJIA, kwenye gazeti la MTANZANIA. Unaweza kufuatilia kila Alhamis.
Maoni
Chapisha Maoni