Umuhimu wa Kusema Hapana kwa Ngono Kabla ya Ndoa
PICHA: eskimi.com |
Majuzi niliwaambia wanafunzi wangu wakitaka
kuwa na ndoa bora hapo baadae, lazima wajifunze kuacha ngono kabla ya ndoa. Kusikia
hivyo, walicheka mithili ya watu waliosikia kichekesho kipya cha mwaka. Sikushangaa.
Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, wastani wa umri wa kijana kuanza ngono ni
miaka kati ya 14 na 15. Wanafunzi wangu walikuwa na kati ya umri wa miaka 21 na
23.
Wangali
wakicheka, niliwakaribisha kutazama video ya utafiti wa Profesa Walter Mischel wa Chuo Kikuu cha Stanford uliopima subira
ya watoto wa miaka minne. Video hiyo iliwaonesha watoto waliogawiwa vitu vitamu
viitwavyo marshmallow ili kuona kama wangeweza kujizuia kula hata katika
mazingira ambayo walikuwa na uhuru wa kufanya hivyo.
Mtafiti aliwaambia
watoto wangeweza kula pipi hizo kama wangetaka lakini kama wangesubiri mpaka
atakaporudi wangepata ‘marshmallow’ zaidi kama takrima ya kujinyima. Mwisho
wa video hiyo, watoto wachache tu ndio walioweza kujizuia wakati zaidi ya nusu
ya watoto walishindwa kujizuia.
Kipimo cha kujizuia
Video hiyo ilizima
ghafla kicheko cha wanafunzi wangu. Nilichukua kipaza sauti na kuwakaribisha
kutafakari kile walichojifunza kwenye utafiti huo. Baada ya kusikiliza maoni
yao mengi, niliamua kuhitimisha: “Hawa watoto tunaowaona hapa walifuatiliwa na Mischel
kwa miaka mingi baadae. Mischel aligundua jambo la ajabu kidogo. Wale walioweza
kungoja walikuwa na mafanikio makubwa shuleni na hata katika maisha kwa ujumla.
Walioshindwa kungoja waliishia kuwa watu wasio na mbele wa nyuma.”
Ukumbi wote wa
mhadhara ulikuwa kimya. Wanafunzi walikuwa wakifuatilia niliyokuwa nikiwaeleza.
Niliendelea, “Uwezo wa kujizuia ni tabia inayohitajika sana kwenye maisha.
Kuanzia kwenye taaluma, biashara, kazi, imani, na hata kwenye ndoa. Bila
kujifunza kujizuia huwezi kupata mafanikio yoyote.”
“Kuna mambo unaweza
kuyafanya kama kijana usione matokeo yake lakini yakakujengea mustakabali mbovu
kwenye maisha ya baadae ya ndoa. Mfano kufanya ngono holela kabla ya ndoa.
Ngono ikiwa tabia, hutaiacha ukiwa kwenye ndoa. Usipoweza kujifunza kujizuia
sasa ukiwa kijana na kufanya maamuzi magumu ya kusema sitafanya ngono kabla ya
ndoa, itakuwa vigumu kwako kuwa mume au mke mwaminifu ikiwa utafanikiwa kuingia
kwenye ndoa.”
Kutofautisha
upendo na tamaa
Wanaume wengi huchanganya kumpenda
mwanamke na kumtamani. Ingawa upendo unazo chembechembe fulani za tamaa ndani
yake, kwa kiasi kikubwa, upendo una uwezo mkubwa wa kujizuia kuliko tamaa. Mwanaume
mwenye upendo wa dhati, hatangulizi hisia bali maamuzi. Upendo humfanya awe na
uwezo wa kutokufanya mapenzi na mtu ampendaye.
Kwa upande mwingine, mwanaume mwenye
tamaa hufikiri akimpenda mwanamke lazima afanye nae ngono. Mtu huyu anayeongozwa
na hisia kuliko maamuzi, anapofanikiwa kufanya ngono na mwanamke huyo, msisimko
huo wa kimapenzi aliokuwa nao awali huzimika. Hali hii inapotokea, hujikuta akipunguza
mawasiliano na hatimaye uhusiano wake na mwanamke huzorota.
Ngono
hupunguza kujiamini
Pamoja na starehe yake, ngono inapofanywa
holela na mtu msiye na makubaliano naye, inapunguza kujiamini kwako. Fikiria msichana anayetoa mwili wake kwa
mwanaume kama ishara ya kumpenda. Kinyume na matarajio yake, mwanaume hupoteza
msisimuko naye hasa anaposhiriki ngono wakati hana mpango naye. Katika
mazingira hayo, ni rahisi uhusiano huo kufifia na hatimaye kumfanya msichana
huyu aliyeamini anapendwa kuanza kujisikia kukataliwa.
Mazingira kama haya huwakuta wasichana
wengi wanaojikuta wameachwa na rafiki zao bila kutarajia. Kuachwa huwafanya
wawe na wasiwasi na uzuri na sifa nyingine walizonazo. Wengine huanza kujichukia
na kuamua kujirahisisha kwa wanaume wengine kama njia ya kujiaminisha kuwa bado
wanapendwa. Hali kama hii hupunguza sana kujiamini kwa mwanamke.
Ngono
hufanya usiaminike
Mnapokubaliana kufanya ngono na mtu
mtakayefunga naye ndoa, kwa haraka haraka inaweza kuonekana ni ishara ya
kuaminiana. Kwamba ameweza kuutoa mwili wake kwa ajili yako, inaweza
kutafsirika kama kiwango cha juu cha mapenzi.
Hata hivyo, kisaikolojia, hali ya
kutokuaminiana katika ndoa ina uwezekano mkubwa wa kuanzia hapa. Mwenzako
huanza kuwa na wasiwasi na uaminifu wako unapokuwa na watu wengine. Ikiwa uko
kwenye ndoa na unajiuliza kwa nini mwenzako hakuamini, upo uwezekano mkubwa
mlifanya kosa la kukutana kingono kabla ya ndoa.
Ushauri
Mbali na ngono kuongeza uwezekano wa kuambukizwa
magonjwa ya zinaa, mimba zisizotarajiwa na kukuvurugia mipango ya maisha,
ukiweza kujifunza kusema hapana kwa ngono kabla ya ndoa, utapunguza uwezekano
wa kuingia kwenye ndoa na watu wasiokufaa. Hata kama ulishaanza, bado una
nafasi ya kusema hapana tangu leo. Heri ya mwaka mpya 2018.
Makala haya yalichapishwa awali na gazeti lako pendwa la Mtanzania. Unaweza kufuatilia safu ya Saikolojia kwenye gazeti hilo kila Alhamis kwa makala kama haya.
Makala haya yalichapishwa awali na gazeti lako pendwa la Mtanzania. Unaweza kufuatilia safu ya Saikolojia kwenye gazeti hilo kila Alhamis kwa makala kama haya.
Maoni
Chapisha Maoni