Tabia Tano Zitakazokupa Nidhamu ya Muda Kazini
Mafanikio
katika eneo lako la kazi, kwa kiasi kikubwa, yanategemea matumizi ya muda
ulionao kwa siku. Kile unachokifanya kati ya saa 6:00 usiku na saa 5:59 usiku wa
siku inayofuata, ndicho kinachoamua utekelezaji wa majukumu yako.
Sote
bila kujali aina ya kazi tunazofanya wala mahali tunapoishi tumepewa mtaji wa
saa 24 kwa siku. Tofauti, hata hivyo, ni namna tunavyoweza kutumia saa hizo kwa
tija.
Makala
haya yanakupa uzoefu wa watu ninaowajua wana shughuli nyingi lakini wameweza
kujijengea tabia ya nidhamu ya muda. Kwa
ujumla, wanatufundisha tabia tano muhimu.
Kuongozwa na malengo
Injinia
Sylvanus Kamugisha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Sylcon Builders Limited anasema mahali
pa kuanzia ni malengo ya mwaka uliyonayo:
“Vipaumbele vinatokana na malengo ya mwaka
niliyonayo. Mfano, mwaka huu nimeazimia kuwa mtu was ala. Kupunguza uzito kilo
20, kusoma vitabu 40 na mambo kama hayo.”
“Kwa
hiyo kwenye ratiba yangu ya siku pamoja na mambo mengine inaanza na dakika 15
za sala, baadae naenda kufanya mazoezi dakika 30 mpaka 45, baada ya hapo nasoma
kurasa 10 mpaka 15 za kitabu kilicho kwenye ratiba yangu na ratiba nyingine
inaendelea.”
Aidha,
namna unavyotafsiri malengo yako katika siku inayofuata ni muhimu kama
anavyoeleza Prosper Mwakitalima, Mkurugenzi wa Ubunifu wa Brand Exponential: “Nina
utaratibu wa kupangilia siku yangu, siku moja kabla. Kisha ninaandaa mambo ya
kutekeleza kesho kabla sijalala. Hii inanipa muda wa kuiona kesho kabla
sijalala.”
Erick
Mbogoro, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma naye anakubaliana naye: “Huwa
naandaa abstract schedule (ratiba) yangu kabla ya kuanza siku. Kwa hiyo nafanya
kazi kulingana na muda niliojipangia.”
Kujiwekea vipaumbele
Erasto
Kitia, Ofisa elimu vifaa na takwimu, Halmashauri ya Wilaya Singida, anasema lazima
kuwa na vipaumbele vya siku, “Jambo la kwanza lazima uyakubali na kuyaelewa
majukumu yako vizuri. Tengeneza mpango wa kuyatekeleza majukumu hayo kwa kuweka
vipaumbele na kuweka muda wa utekelezaji. Lakini muhimu sana kuwa na
uwajibikaji binafsi na nidhamu ya kazi.”
“Katika
kazi kuna mambo ambayo yakifanyika kwanza hurahisisha yajayo. Mengine yako
ndani ya kipindi fulani tu kikipita hayawezekani tena. Kwa namna hiyo unaweza
kujua kipi kianze na kipi kifuate,” anafafanua.
Dk
Mwemezi Rwiza, mhadhiri katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
(NM-AIST) jijini Arusha hupangilia vipaumbele kwa kuangalia uzito wa majukumu.
Anasema, “Ili kupangilia siku yangu, naangalia
uzito. Kama VC (Makamu Mkuu wa Chuo) ameita kikao ofisini kwake na pia kuna
muswada wa kukabidhi saa 10 jioni, nitaenda kwa VC kwanza. Naangalia pesa pia.
Kama ninaandika andiko la mradi na kuna kikao cha kamati ya miundo mbinu ya
chuo, kipaumbele change kitakuwa andiko la mradi.”
Orodha ya mambo ya
kufanya
Tumaini
Stephen, Mwanasheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hutunza muda kwa
kutengeneza orodha ya mambo ya kufanya kila siku: “Kila mwisho wa siku huwa
napanga vitu vya kufanya siku inayofuata. Huwa napanga vitu kuendana na
uhalisia wa muda nilionao na nahakikisha kila nilichopanga nakifanya ndani ya
muda niliopanga.”
Katika
kupanga vipaumbele vya siku, Tumaini Stephen ana utaratibu wa kuangalia uharaka
wa jambo. “Sisi watu wa mahakamani huwa tuna deadline (makataa) haswaa kwenye
kuweka vizuri nyaraka. Kama kesho ndio siku ya makataa na sijamaliza kuziandaa
hilo lazima liwe jambo la kwanza kesho.”
Dk
Rwiza naye anaunga mkono utaratibu huo, “Nahakikisha orodha hiyo ina uhalisia.
Siyo realistic (haiwezi kuwa na uhalisia) kusahihisha mitihani karatasi 15 za
wanafunzi halafu pia niwe na muda wa kupitia dondoo za andiko la miradi mitatu
tofauti.”
Kutengeneza ‘desturi’
ya siku
Bahiya
Abdi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, anasema kwake nidhamu ya
muda ni matokeo ya desturi ya siku aliyojijengea. Anasema, “Mimi ni mtu wa
routine (kufanya mambo yale yale kila siku.) Huwa nimeshapanga nini huwa
ninafanya kwa wakati fulani kwa vitu ambavyo kila siku lazima nivifanye.
Sipotezi muda kupanga nini nitafanya saa ngapi wapi kwa sababu nina vitu
ambavyo lazima nivifanye kwa wakati ule ule kila wakati.”
Lonyamali
Morwo Mkurugenzi Mtendaji wa MultiSkills Business Consultancy naye ana desturi
ya siku: “Nina majukumu matano ya kutekeleza kila siku. Naenda kazini, nasoma
vitabu, lazima nikae na familia na kukutana na marafiki na pia niwe na muda wa
kufanya kazi zangu binafsi nje na ajira. Kwa hiyo mimi huwa naamka saa 10
alfajiri na kuhakikisha hayo yote nimeyafanya kila siku.”
Kuongeza uzingativu katika
kazi
Moja
ya changamoto ya nidhamu ya muda ni kukosa uzingativu. Bahiya Abdi hukabilianaje
na changamoto hii? Anajibu, “Huwa sikubali kuwa disturbed (kusumbuliwa) wakati
nafanya kazi muhimu zinazohitaji umakini. Mfano, huwa naweka simu yangu mbali
ili isinipe vishawishi vya kuitumia kufanya.”
Dk
Rwiza, ambaye pia ana maelfu ya wafuasi
wanaofuatilia anayoyaandika kwenye mtandao wa Twitter naye hutumia mbinu
kama hiyo: “Huwa siendekezi sana inconveniences (mambo yanayoingilia shughuli)
zisizo na msingi. Kama nina kazi inayotakiwa mapema au niko na familia yangu
huwa ninazima simu na hata kuchomoa waya wa internet.”
Ushauri
Lonyamali
Morwo anamalizia kwa kutoa ushauri:
“Matumizi sahihi ya muda ndio siri ya mafanikio. Muda ni pesa na thamani
ya pesa ipo kwenye muda. Unapata mshahara kwa kutoa muda, unapata mazao
shambani kwa kutumia muda wako kuzalisha. Muda ukipita umepita na haurudi tena.
Tujifunze kutunza muda.”
Maoni
Chapisha Maoni