Unaanzisha mahusiano ya ndoa/mapenzi?

MAZUNGUMZO mengi yanayohusu maandalizi ya ndoa hujikita katika kufanikisha tukio la siku ya harusi. Na wakati mwingine wanaojiandaa kwa ndoa huandaliwa siku chache sana kabla ya tukio hilo. Kwa ujumla, suala la ndoa limerahisishwa kiasi cha kuonekana kuwa yeyote anaweza kukabiliana nalo kwa uzoefu pasipo maandalizi ya kutosha. Hata hivyo, pamoja na wepesi wa maandalizi halisi, na msisitizo uliowekwa na jamii katika 'siku ya harusi', ndoa nyingi huishia kwenye migogoro mingi muda mfupi baada ya tukio la harusi.

Pamoja na sababu nyinginezo, wengi tumeaminishwa kwamba hisia za mapenzi na mtu 'sahihi' ndiyo sababu ya kutosha kuanzisha ndoa. Imani hii si tu haina mwelekeo, lakini pia imejaa udanganyifu unaoweza kuwa sababu ya kukosekana uaminifu katika ndoa. Kama tulivyoona kwenye makala iliyopita, mazingira fulani fulani huweza kumfanya mtu kumpenda yeyote 'kimapenzi' lakini hiyo isiwe sababu ya msingi kukufanya uanzishe mahusiano ya kudumu. Tunapotumia sababu ya 'hisia za kimapenzi' tunajiweka kwenye hatari ya matatizo ya kimahusiano. Tuone.

Sababu za huanzisha mahusiano
Hapa zipo sababu nyingi zinazowasukuma watu kuingia kwenye ndoa. Tupo tunaotafuta heshima ya kukubalika kwenye jamii maana tunajua ndoa ni namna rahisi ya kupata heshima hiyo. Tupo tunaosukumwa na shinikizo la umri na hivyo tunaogopa kuonekana tumechelewa kuwa ‘watu wazima wenye heshima zao’. Tunaingia kwenye ndoa kwa sababu tu umri umeenda. Wengine tunatafuta usalama wa maisha. Bila ndoa sitaweza kufanya mambo fulani fulani hivyo ndoa huwa ngazi ya kunisaidia kufikia malengo.  

Kwa wengine wetu ndoa ni namna ya kutafuta mapenzi katika kukabiliana na hisia za upweke. Mioyo na nafsi zetu zinakosa upendo hivyo tunatafuta wa kutupenda.  Tukumbuke, kutindikiwa upendo ni sababu inayoongoza katika kuwashinikiza vijana kuanza mapenzi katika umri mdogo. Kwa kuwa mapenzi kabla ya ndoa ni jambo lisilokubalika kidini na kijamii, tunaamua kuolewa au kuoa ili tusiendelee kutenda dhambi. Tunadhani ndoa ni namna ya kuhalalisha tendo la ndoa.

Wengine wetu tunadhani ndoa ni mpango wa kuwamiliki watu wenye sura na maumbile fulani. Tunawatumia watu hao kama nyenzo za kupandisha hadhi zetu kwa wengine. Na wakati mwingine tunafikiri tukiwapata watu wa namna hiyo basi tutakuwa na uwezo wa kuwapenda kwa muda mrefu tukidhani msisimko wa kimapenzi huongoza mahusiano ya ndoa, jambo ambalo si kweli. 

Ingawa sura na maumbile yanaweza kuwa na nafasi wakati wa mwanzo wa mahusiano, mchango wake hupungua kadri muda unavyokwenda. Na kama urembo ungekuwa sababu ya kudumu kwa mapenzi na uaminifu wa ndoa, basi tusingesikia wanawake warembo wakiachwa na wapenzi wao kwa sababu mbalimbali ikiwemo uzinzi.

Hizi zote, pamoja na nyingine zinazofanana na hizo ni sababu zinazotumiwa na wengi lakini zote wa kiasi kikubwa ni batili. Haziwezi kutusaidia kuishi maisha ya ndoa yenye utoshelevu na uaminifu. Wanaoingia kwenye ndoa kwa kutumia sababu hizi, huishia kufikia malengo hayo mengine lakini sio ndoa yenye misingi ya kuaminiana na yenye utoshelevu. Ndio hao huja kusikika waksema, ‘walio ndani wanataka kutoka, walio nje wanatamani kuingia.’ Kwa nini? Kwa sababu waliingia kwenye ndoa kwa sababu nyepesi na batili bila kujiandaa ipasavyo, hatimaye wakagundua ndoa ni zaidi ya yale waliyofikiri ni ya muhimu. 

Sasa katika kutafakari cha kufanya ninapotaka kuanzisha uhusiano wa ndoa, yapo mambo matatu makuu ya kuzingatia. Jambo la kwanza ni mimi. Jambo la pili ni kwa nini. Jambo la mwisho ni nani. Yote matatu yanazunguka kwenye dhana moja: kushinda mapambano ya matakwa binafsi ya wanaopendana. Nitajadili jambo la kwanza na tatu kwa pamoja kisha nitahitimisha na la pili.

Tafsiri ya utayari wa kuanzisha mahusiano
Kama tulivyogusia hapo juu, wengi wetu tunatafuta mtu sahihi kuliko tunavyojitahidi kuwa watu sahihi. Na wakati mwingine mtu unajiuliza, kwa nini tunatumia muda mrefu kutafuta mtu sahihi kuliko kujiandaa kuwa mtu sahihi? Mtu sahihi na aliye tayari kwa mahusiano ni nani na yukoje? Ana sifa tatu kubwa; 1) ameshinda mapambano ya matakwa binafsi 2) anayo mambo ya msingi yanayomtambulisha na 3) anatambua kinachoongoza/sukuma maisha yake.

Ameshinda mapambano ya matakwa binafsi. Kwa hakika, ndoa msingi wake mkubwa ni kushinda ubinafsi.  Kwa lugha ya kibiblia, ndoa inanidai kuua nafsi na matakwa binafsi ili niweze kuwa mwili mmoja na mwenzangu. Kwa maana nyingine kifo cha matakwa binafsi huwezesha mchakato wa kufanyika kwa mwili mmoja.

Kwa lugha ya elimu nafsi, kufa kwa ubinafsi kuna maana ya kuweza kuishinda vita ya ego ili kuhusiana vyema na nafsi yangu mwenyewe kabla ya kuhusiana na mwingine. Kwa maneno mengine kobe mwenye amani, hutoa kichwa chake nje bila ya wasiwasi. Hofu ya kujulikana na kuathirika na mazingira humfanya arudishe kichwa chake ndani.

Mwanadamu anayeshinda matatizo ya nafsi, ni sawa na kobe mwenye amani na uhuru. Hukitoa kichwa chake nje pasipo hofu ya kukataliwa. Katika hali hii, anaweza kuhusiana kwa ukaribu na mtu mwingine bila kujilinda na hivyo kuongozwa na matakwa yake dhidi ya wengine.
Kobe mwenye uhuru hutoa kichwa nje bila wasiwasi. Hofu humfanya akirudishe ndani. Picha: petinfoclub.com

Kama lengo ni kuanzisha mahusiano yatakayojengwa juu ya msingi wa uaminifu na kuaminiana ninalazimika kuhusiana na mtu ambaye naye kadhalika ameshinda mapambano vya nafsi na kuwa tayari kutafuta matakwa ya mwingine. Sababu ni kwamba mtu anayehangaika na nafsi yake mwenyewe, kwa kutafuta mahitaji yake mwenyewe, hawezi kuhusiana kwa karibu na kwa utoshelevu na mtu mwingine. 

Maswali ya msingi katika kushinda matakwa binafsi ni je, nina mahusiano mazuri na nafsi yangu? Ninajionaje? Je, sitishwi na kufahamika kwa tabia yangu ya sirini? Je, sijihami kuzuia mtu mwingine asinifahamu kwa undani? Ninaridhika na vile nilivyo au bado ninahangaika kujielewa? Namna gani ninaweza kufikiria na kuyaelewa mahitaji ya mwingine? Ninajisikiaje nikikosolewa? Nina hisia za wivu usio wa lazima? Niko tayari kupokea mabadiliko au nina ubishi ninaposhauriwa? Ninaweza kumfanya mwingine awe na furaha bila kujali ninajisikiaje kwa kufanya hivyo?

Hayo yote ni maswali yanayonisaidia kuelewa kiwango cha mahusiano yangu na nafsi yangu mwenyewe. Maana ili niwe na utayari wa kuingia kwenye ndoa imara na yenye uaminifu, ni lazima niwe na nafsi iliyoshiba yenye uwezo wa kutoa kuliko inavyopokea. Yenye uwezo wa kutokudai kupendwa, bali kupenda. Yenye kusifu badala ya kudai kusifiwa. Isiyosubiri kufanyiwa, itenda. Isiyodanganya kwa hofu ya kukataliwa bali kusema kweli bila hofu ya matokeo ya ukweli huo. 

Ingawa ni kweli binadamu huwa na uwezo wa kuficha sura zao halisi hasa katika hatua za awali za mahusiano, bado kwa uangalifu naweza kubaini matatizo ya msingi yanayodhihirisha tatizo la nafsi kwa mtu ninayefikiri kuhusiana nae. Mfano rahisi wa tatizo la nafsi ni uongo. Mtu mwongo hafai kujenga ndoa yenye misingi ya uaminifu kwa sababu mwongo mara nyingi hulazimika kudanganya kama jitihada za kuficha sura yake halisi kwa matumaini ya kukubalika. Kwa kuwa udanganyifu ni lugha ya kutokuridhika na vile tulivyo, tunahitaji kutafakari kwa bidii tunapogundua chembechembe za uwongo kwa tunaowapenda. Matatizo mengi yanayojenga uchungu wa ndoa huanza na uongo. 

Anayo mambo ya msingi yanayomtambulisha. Mambo gani katika maisha yanabeba utambulisho wangu? Ninaamini nini kuwa ndio msingi wa maisha yangu? Maeneo yapi ninayoyaamini hayana mjadala? Masuala gani nayachukulia kuwa tunu zinazoongoza maisha yangu?

Kwa mfano, imani za kidini zinaweza kuwa msingi wa maisha ya wengi usio na mjadala. Dini zinaongoza mitizamo, imani na hata tabia zetu. Wakati mwingine tunaweza kuwa hatuelewi kwa nini tunaamini tunavyoamini, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba dini hizo ni tunu isiyojadilika kwa wengi wetu. Ni mambo ya msingi kiasi kwamba tunaweza kupishana na mtu anapojaribu kuyachokoza. Hapa hazungumzii mambo mepesi kama itikadi za vyama, ushabiki wa mambo fulani fulani yanayojadilika.

Ninapotaka kuhusiana na mtu tunayetofautiana mambo ya msingi katika imani, hata kama ninajisikia kumpenda kiasi cha kufa, ninakuwa najiweka katika uwezekano wa migogoro mikubwa hapo baadae. Ingawa ni kweli wapenzi wawili wakishinda ubinafsi, wanaweza kuishi na tofauti zozote zile katikamaisha, hata hivyo, imani zilizojikita ndani ya mtu zaweza kuhitaji gharama kubwa zaidi kuachana nazo na hivyo kuwa sababu ya migogoro mingi. 

Hivyo, ni busara kutumia hatua za awali kwa mazungumzo ya kina na ya mara kwa mara ili kuelewa angalau kwa ujumla imani katika mambo ya msingi yanayotawala maisha ya mpenzi wako. Mahusiano ya ndoa, kama tulivyosema ni zaidi ya hisia za mapenzi. Imani namaamuzi huwa kiungo muhimu cha mahusiano. Kwa kuwa imethibitika kwamba tofauti ya imani hizi za msingi ni sababu ya migogoro mingi ya ndoa/mahusiano, hekima ni kufikiri kwa bidii unapoanzisha uhusiano na mtu unayetofautiana nae imani na mambo mengine ya msingi. 

Anatambua kinachoongoza maisha yake. Wengi wetu tunayo malengo hata kama hajayajandikwa mahali. Wapo wenye malengo ya kuwa mabilionea wakubwa. Wengine wanataka kuleta mabadiliko fulani katika jamii. Wengine wanalenga kuwatumikia wengine kwa kujitoa kama sadaka kwa faida ya wengine na kadhalika. 

Malengo haya huwa msingi wa maamuzi ya kimahusiano katika maisha. Ni muhimu kuyaelewa kabla sijafanya maamuzi ya kuanzisha mahusiano ya kudumu na mtu mwingine. Hii itanisaidia kufanya maamuzi sahihi ya kupata mtu tutakayesaidiana kufikia maono/ndoto zetu pamoja. Maana wanasema, watu wawili wasipopatana hawawezi kwenda pamoja. Kutokwenda pamoja katika ndoa si jambo lenye afya.

Tunajua katika jamii kama yetu upo uwezekanao wa kuwepo watu wengi tu wasio na malengo yoyote katika maisha. Hii si siri na wala si jambo la kuonea haya. Hata hivyo, ikiwa ninakutana na mwenzi asiye na malengo yoyote katika maisha, mtu anayeamini maisha ni kula, kufua na kuvaa, basi ni vyema nilitambue hilo mapema ili jitihada za kutengeneza malengo ya pamoja zianze. Tunaambiwa pasipo malengo watu hupotea.

Wapo wapenzi hushindwa kuhusiana kwa karibu sana kwa sababu tu, mmoja ana malengo ya kwenda mbali wakati mwingine analenga kurudi kutoka alikokuwa. Ni sawa na kuwaweka watu wawili pamoja, mmoja akiwaza namna ya kuifikia dunia, wakati mwingine anashangaa kwa nini asumbuke na kijiji kizima. Hekima ni kujadiliana na kukubaliana mwelekeo wa pamoja.

Kwa nini ninahitaji ndoa/mahusiano?
Kama tulivyoeleza hapo awali, watu wanazo sababu mbalimbali za kuanzisha mahusiano ya ndoa. Sababu hizo kwa kiasi kikubwa hutegemeana na namna wanavyohusiana na nafsi zao wenyewe kama tulivyoona. Kwa mfano, ninapojiona sipendwi, mara nyingi nitaingia kwenye ndoa kwa matarajio ya kupendwa zaidi kuliko nikavyojitoa kupenda.  Wakati nikijaa upendo kabla ya kukutana na mtu yeyoye, nitakuwa ziada ya kutoa kwa mwingine kuliko ninavyotarajia kupendwa. Hivyo, ndoa kwangu itakuwa ni fursa ya kupenda kuliko kupendwa.

Kadhalika, katika malengo ya maisha. Mtu mwenye kuyatazama maisha kama fursa ya kuwa bilionea hawezi kuingia kwenye ndoa kwa kutumia sababu sawa na mwenzake anayeyachukulia maisha kama fursa ya kujitoa sadaka kwa ajili ya faida ya wengine na sio kutafuta utajiri. Tofauti hiyo ya mitizamo ya maisha huzaa tofauti ya sababu za kuingia kwenye ndoa. Na bahati mbaya, kutokufanana kwa sababu zinazowafanya waingie kwenye ndoa yaweza kuwa chanzo cha kukosekana kwa furaha ya ndoa. 

Ni kwa sababu hiyo washauri wa masuala ya ndoa wanafikiri kwamba kwa lengo la kuepusha migogoro isiyo na lazima kwenye ndoa, ni vyema kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya mbili kuu ambazo ni matokeo ya kufa kwa matakwa binafsi: 1) kujitoa kwa ajili ya faida ya mwenzangu  kwa gharama yoyote inayowezekana na 2) kujitoa kwa ajili ya kile ninachokiona ndilo kusudi la maisha yetu kama wapenzi.

Maana ya hayo ni kwamba kwa kuyashinda matakwa binafsi, nitaweza kuwa tayari kusikiliza na kuelewa mtazamo na mwelekeo wa mwenzangu, na kisha kuangalia namna tunavyoweza kwenda pamoja kwa kuhusianisha mitazamo na makusudi yetu kama wenzi. 

Hatua za kuchukua?
Vigezo vingine kama sura, umbile, elimu, uchumi, utaalam wa tendo la ndoa, rangi ya ngozi na mambo mengine kama hayo havijasahaulika. Nilivikumbuka vizuri lakini nilipanga nije nikwambie hapa mwishoni kwamba hayo yote hayana maana yoyote kwenye mahusiano yenye misingi tunayoizungumzia.Na badala yake, kiwango cha kushughulikiwa matakwa binafsi ndicho kigezo kikuu.

Sura na maumbo ya mwili yanabadilika. Ni vipaumbele kwa wanaodhani ndoa ni msisimko wa 'kifilamu'. Elimu haina mwisho unaweza kuipata wakati wowote na haiwezi kuathiri mahusuano. Pesa hutafutwa na kuisha. Haziathiri mahusiano yenye msingi wa kuaminiana na uaminifu. Ufanisi wa tendo la ndoa una umuhimu lakini unafundishika. Kudhani ni kipaumbele cha mahusiano ya ndoa ni kupotoka. Katika hayo, matatizo ya nafsi ndiyo yenye gharama kubwa zaidi na ndiyo asili ya ama matatizo mengi ya ndoa au furaha ya ndoa.

Ikiwa unahisi unalo tatizo la nafsi kwa dalili tulizozigusia hapo kwa ufupi, na bado unafikiri kuanzisha mahusiano ya kudumu na mtu mwingine, tafuta msaada. Hakikisha na huyo unayekusudia kuanzisha nae mahusiano naye amepona nafsi yake kabla hamjaenda mbali. Kwa watu wa imani, maombi yanaweza kumbadili mtu na kumfinyanga na kuua kabisa matakwa binafsi. Lakini pamoja na maombi, ni busara kupata ushauri maalum wa wanasihi wa ndoa kabla kujaingia kwenye mahusiano ya ndoa. Utamaduni huu ni mgeni lakini ni wa muhimu. 

Makala haya ni majibu ya swali la msomaji wa blogu hii aliyetaka kujua vigezo vya kuangalia anapotafuta mwezi wa maisha.
Christianbwaya [at] gmail [dot] com

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia