‘Hakuna uhusiano wa elimu ya mzazi na ubora wa malezi’ –watafiti
IMEJENGEKA dhana kwamba kiwango kikubwa cha elimu anachokuwa
nacho mzazi kinaamaanisha ubora na ufanisi wa malezi. Katika nchi za ki-Magharibi
kwa mfano, ubora wa malezi kwa maana ya uelewa wa mahitaji ya kisaikolojia ya
mtoto umekuwa ukihusishwa na elimu ya wazazi inayokwenda sambamba na
uwajibikaji wa kimalezi. Hali inaonekana kuwa tofauti katika nchi zilizo kusini
mwa jangwa la Sahara.
Tafiti zilizofanywa kwa nyakati tofauti katika nchi za
Tanzania, Botswana, Naijeria na Lesotho zinaonesha kwamba hakuna uhusiano wa
moja kwa moja kati ya elimu, kipato wala mafanikio ya kimaisha ya wazazi na
ubora wa malezi ya watoto wao. Badala yake, katika hali ya kushangaza, wazazi wasio na elimu na wenye kazi zisizo na
hadhi ndio wanaoonekana kuwajibika zaidi kuliko wenzao wenye elimu ya kuanzia
Shahada na kuendelea.Watoto nchini Naijeria wakifurahia kuwa pamoja. Picha: naijamayor.com |
Aidha, tafiti hizo zinaonesha wakati wazazi wenye elimu
kubwa hawapati/hawana muda wa kukaa na kuwasiliana na watoto wao ipasavyo, bado
angalau hujitahidi kuweka mazingira ya kujifunzia nyumbani kwa maana ya vitabu,
televisheni, na vifaa vingine vya michezo kwa watoto. Kwa upande mwingine, wazazi
wasio na elimu wala kazi zenye hadhi, wameonekana kuwa na uhusiano na watoto, wakitumia
muda mwingi kuwafunza watoto tabia zinazokubalika katika jamii zao.
Hata hivyo,
wazazi hawa wameonekana kushindwa kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia
majumbani kwao kama wenzao wenye elimu.
Mazingira ya nyumbani
Watafiti karibu wote niliowataja mwisho wa makala haya wanakubaliana
kwamba bila kuzingatia elimu wala kipato cha mzazi, mazingira ya nyumbani pamoja
na mitazamo ya wazazi ndiyo hasa huathiri makuzi na malezi ya watoto. Wakati
mazingira ya nyumbani yakimaanisha hali ya upendo unaooneshwa na wazazi kwa watoto,
mahusiano ya wazazi wenyewe, mienendo ya wazazi, muda wanaoutumia wazazi nyumbani na upatikanaji wa vifaa vya
kujifunzia; mitazamo ya wazazi kwa upande mwingine ni matarajio ya wazazi kwa
watoto wao, jitihada za kuelewa na kujibu mahitaji ya kihisia ya mtoto, namna
ya kuwapa moyo na hata kuwaadhibu watoto.
Hata hivyo, matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kwamba wazazi wengi
wa Afrika huanza kujali, kufuatilia, kuelekeza na kuingilia shughuli za watoto
wao wanapofikia kipindi cha kubalehe. Sababu kubwa inayotajwa ni kwamba katika
kipindi hiki ndipo watoto huanza kuonesha tabia zisizowapendeza wazazi, ambazo
kimsingi huwa ni matokeo ya kupuuzwa kwa mahitaji ya kihisia tangu awali. Kabla
ya hapo, wazazi bila kujali elimu huamini hapana haja kubwa ya kuweka nguvu
katika kujenga tabia ya mtoto.
Maana ya matokeo haya
kwa wazazi
Barani Afrika, elimu ya darasani hamsaidii mtu kuwa mzazi
bora wala kutokuwa nayo hamkufanyi mzazi kutimiza wajibu wake. Kinachoonekana
ni kwamba ongozeko la elimu linaenda sambamba na ongezeko la majukumu mengine
ambayo wazazi hujikuta wakiyapa uzito kuliko malezi. Kwa upande mwingine,
kutokuwa na majukumu hayo huwa faida kwa mtoto ingawa changamoto inabaki kuwa uelewa
sahihi wa mahitaji ya mtoto.
Inavyoonekana, mabadiliko ya kijamii na kiuchumi tunayoyashuhudia
katika nchi zetu hizi, yanaleta changamoto mpya katika malezi. Wakati mzazi
msomi akiathirika kwa kutoa muda wake katika kukabiliana na changamoto hizi nje
ya familia, mzazi asiye na msomi naye anapambana na changamoto hizi hapo hapo
nyumbani kwa namna yake. Kwa namna moja
au nyingine, aina za kazi tunazofanya kama wazazi, mitazamo yetu na changamoto
nyinginezo huathiri namna tunavyojishughulisha na makuzi ya mtoto kihisia.
Pengine ni wakati muafaka sisi kama wazazi na walezi kuanza
kujenga utamaduni wa kuelewa hatua muhimu za ukuaji wa mtoto ili kutambua
mahitaji na matatizo ya watoto tangu mtoto anapozaliwa.
Kiungo cha tafiti na
watafitiwa?
Zimefanyika tafiti nyingi sana kuhusu mahitaji na matatizo
ya watoto barani Afrika. Kwa nini tafiti hizi haziwafikii walengwa? Sababu moja
kubwa ni kwamba tafiti nyingi hulenga kukuza maarifa ya kitaaluma pekee. Hufanywa kwa minajili ya watafiti kuwasiliana
wao kwa wao na sio kutumika moja kwa moja katika kutatua matatizo halisi. Hii
ndiyo sababu matokeo mengi huishia kupamba makabati ya maktaba za taasisi za
elimu bila kufahamika kwa umma.
Pamoja na changamoto nyingi, blogu hii inalenga kuwa kiungo
kati ya maktaba hizo na wazazi. Kwa majuma kadhaa tutafanya mapitio ya mahitaji
ya msingi ya kisaikolojia katika vipindi mbalimbali vya umri wa mtoto tangu
kuzaliwa mpaka miaka 20 kwa mgawanyo ufuatao: miaka 0 – 3, 3 – 6, 6 – 12 na 12
– 20. Lengo si kumwelekeza wala kumshauri yeyote nini cha kufanya, bali kujaribu
kueneza maarifa yanayopatikana lakini hayafiki yanakostahili kufika.
Makala haya yameandaliwa
kwa msaada wa maandiko, tafnifu na vitabu vya watafiti wafuatao: A. Blair, I.
Omari, T, Mwamwenda, D. Mbilinyi, A. Mbise, A. Oyewole na C. Nyinamuntu ambao
wote wana kauli katika elimu ya makuzi na malezi ya mtoto.
Maoni
Chapisha Maoni