Malezi yanayofanya mtoto amsikilize na kumwamini mzazi
TAFITI zinaonesha kwamba watoto wengi ni 'mayatima' wenye wazazi tunaoishi lakini hatupo kwenye maisha yao. Wazazi tupo lakini hatuna muda wa kujua hisia zao, fadhaa zao, maoni yao, hofu zao na hata
matumaini yao. Aidha, tafiti hizo hizo zinasema wazazi wengi tunatumia muda mwingi na
watoto wetu ama kuwaonya, kuwakosoa ama kuwapa hotuba/maagizo ya ‘fanya hivi,
acha hiki’ kuliko tunavyowasaidia kujenga mahusiano ya moja kwa moja kati yetu
na watoto.
Wazazi kwa upande wetu, tunajitetea kwamba maisha yamekuwa na pilika nyingi. Mambo yamebadilika hivyo yatupasa kutumia muda mwingi kutafuta pesa kujenga maisha ya baadae watakayoishi watoto wetu. Tunawavalisha, tunawalisha, tunawapeleka shule na kuhakikisha wanalala na kuishi kwa usalama. Katika jitihada zote hizo tunajikuta tukikosa muda wa kutulia na kujenga maisha ya sasa ya kimahusiano na watoto wetu ambayo kwa kiasi kikubwa huathiri maisha na mahusiano yetu na watoto wetu hapo baadae.
Wazazi kwa upande wetu, tunajitetea kwamba maisha yamekuwa na pilika nyingi. Mambo yamebadilika hivyo yatupasa kutumia muda mwingi kutafuta pesa kujenga maisha ya baadae watakayoishi watoto wetu. Tunawavalisha, tunawalisha, tunawapeleka shule na kuhakikisha wanalala na kuishi kwa usalama. Katika jitihada zote hizo tunajikuta tukikosa muda wa kutulia na kujenga maisha ya sasa ya kimahusiano na watoto wetu ambayo kwa kiasi kikubwa huathiri maisha na mahusiano yetu na watoto wetu hapo baadae.
‘Elimu ya kujitegemea’
inavyowaathiri watoto
Wazazi wengi tunasubiri watoto ‘wapate akili’ ili tuanze
dozi rasmi ya mihadhara ya maagizo, maelekezo, makanyo, maonyo na kadhalika, tukiamini mtoto hujifunza kwa mafundisho rasmi. Wakati mwingine tunaamini fimbo
ndilo jibu la tabia njema ya mtoto. Tunatumia na vifungu vya biblia, ‘Usimnyime
mtoto mapigo/fimbo’. Na tunawachapa kweli tukitarajia heshima na adabu.
Athari za mtazamo huu
ni kwamba katika kipindi muhimu kabisa cha mtoto kujifunza, tangu anazaliwa
mpaka miaka mitano, hatuwekezi vya kutosha. Tuko bize tukisaka maisha na kuwatelekeza
watoto kimahusiano. Wanapofikisha miaka mitano tunawapeleka boarding wakapate elimu bora ya
kimataifa itakayowasaidia kuzungumza kiingereza na sio kuwa binadamu atakayeishi na wenzake vizuri.
Tunasahau kwamba kipindi tunachodhani mtoto hajifunzi,
ukweli ni kwamba hicho ndicho kipindi sahihi na muhimu kujifunza kuliko kipindi
kingine chochote cha maisha ya mtoto. Ndicho kipindi mtoto anapojenga
taswira ya ilivyo dunia na wakazi wake, tabia na ubinadamu, imani na tunu
nyingine za msingi katika maisha.
Ni kipindi nyeti ambacho mtoto huhitaji mahusiano ya karibu kabisa na mzazi, ambaye naye shauri ya pesa, hapatikani. Kutokupatikana katika kipindi hiki muhimu, kumsikiliza mtoto na kuingiza kile tunachopenda kukiingiza katika moyo wa mtoto, huongeza umbali wa kimahusiano baina ya mtoto na mzazi.
Ni kipindi nyeti ambacho mtoto huhitaji mahusiano ya karibu kabisa na mzazi, ambaye naye shauri ya pesa, hapatikani. Kutokupatikana katika kipindi hiki muhimu, kumsikiliza mtoto na kuingiza kile tunachopenda kukiingiza katika moyo wa mtoto, huongeza umbali wa kimahusiano baina ya mtoto na mzazi.
Na bahati mbaya, umbali huu wa kimahusiano kati ya mzazi na mtoto huongezeka
kadri mtoto anavyopata akili. Hukua akiviamini na kuvitegemea vyanzo vingine
vya maarifa zaidi ya mzazi. Bila hata mtoto mwenyewe kung’amua, taratibu huanza
kukosa imani na wazazi ingawa hujitahidi kuwaridhisha akiogopa fimbo na kelele. Mtoto huanza kumwona mzazi kama mtu mwingine yeyote anayeweza kumpa chakula, mavazi na malazi isipokuwa faraja ya moyo.
Hapa ndipo wanetu huanza kujifunza zaidi kupitia televisheni, marafiki na watu wengine
kama walimu wanaokabiliwa na msongo wa mawazo ambao wakati mwingine hupanda mambo tofauti kabisa na mtazamo na matakwa ya sisi
wazazi. Yote haya hufanyika bila taarifa ya mzazi ambaye yuko bize kutafuta maisha ya mbeleni ya mwanae.
Mtoto huyu anapofikia umri wa kuanza kufanya mambo yake kwa
uhuru kwa kutumia elimu hiyo aliyoipata kwa mfumo wa kujitegemea tangu amezaliwa , tena
bila 'ukaguzi' wa mzazi, ndipo mzazi hukumbuka 'shuka asubuhi'. Huurejea wajibu wake na huanza jitihada za
kutafuta/kulazimisha urafiki na mtoto wakati ambao mtoto hana haja na urafiki
huo. Too late wanasema wazungu. Shughuli pekee inayoweza kufanyika kwa ufanisi katika kipindi hiki kizito ni
kulalamika, kufoka na kuadhibu, mahusiano ambayo kwa hakika huongeza umbali wa mawasiliano baina ya
mtoto na mzazi. Mzazi humwona mtoto ameasi, na mtoto humwona mzazi anajipendekeza na kumfuata fuata.
Tuyape malezi uzito
unaostahili
Ili kukwepa fedheha ya kulazimisha urafiki na mtoto hapo
baadae, tunashauriwa sisi kama wazazi tuyape malezi uzito unaostahili kuanzia pale
tunapofikiria kupata mtoto. Na kwa kweli malezi ndiyo fursa pekee ya mtu
kubadili maisha ya mtu mwingine vile apendavyo. Fursa hii huwezi kuipata hata
kwa mwenzi/mpenzi wako maana katika mahusiano ya ukubwani kinachotokea zaidi ni
kuchukuliana na sio kubadilishana tabia. Kwa hiyo kama kuna fursa pekee ya kubadili
mtu katika dunia hii ni malezi. Tuitumie.
Kupitia malezi mzazi anaweza kuwekeza apendavyo na kuumba
tajiriba itakayoongoza mwelekeo wa maisha ya mtoto. Hata biblia imelieleza
suala hili vizuri sana. Kwamba kile unachomfundisha mtoto kukifuata akiwa mdogo hatakiacha
maisha yake yote. Kuwekeza katika ufahamu wa mtoto katika hatua za mwanzo
kabisa za maisha yake huweka alama ya kudumu itakayoathiri mitazamo, imani na
hata tabia ya mtoto katika maisha yake yote ya mbeleni. Tulitambue hili tunafukuzana na mipangilio ya kutafuta pesa.
Tupatikane kwa
watoto, tuwasiliane na mioyo yao mapema
Hatuwezi kuwasiliana na moyo wa mtoto pasipo kupatikana. Kuwa
nao, kucheza nao, kutembelea nao, kuzungumza nao na mambo yanayofanana na hayo
huhakikisha tunaweka alama njema ya kudumu katika maisha ya mtoto. Kupatikana na
kuwasiliana na moyo wa mtoto ni muhimu kuanze tangu anapozaliwa au hata anapohesabu majuma tumboni mwa mama.
Watoto wanaoishi kwenye kitongoji cha Mathare, Nairobi. Picha: @bwaya |
Ingawa mfumo wa maisha ya sasa unatufanya tukose muda wa kuwa na
mtoto mmoja moja kibinafsi na kuhusiana kwa karibu na moyo wake, bado huu ni
wajibu wa msingi wa mzazi anayejitambua. Kwa kuelewa umuhimu wa mahusiano haya
ya mwanzo, na kuchukulia malezi kwa uzito, tunaweza kabisa kujenga utaratibu wa kuwa na muda maalum kwa
siku wa kumsikiliza mtoto mmoja moja. Hili likifanyika tangu mtoto anapozaliwa,
huongeza uwezekano wa sisi wazazi kuaminika kwa watoto na hivyo kuwa na nafasi ya
kujua yaliyoujaa moyo wa mtoto na kuchukua hatua stahiki kungali ni mapema. Je, tunafanya hivi? Tunawapa watoto wetu muda wa kufurahia mahusiano na sisi wazazi 'kibinafsi'?
Fikiria jambo hili. Ukiweza kutumia saa 1 tu kwa wiki, sawa
na dakika zisizofika kumi kwa siku kuzungumza kirafiki na mwanao mmoja mmoja, wakati
anapofikisha umri wa miaka 12/13 anapopevuka na kuanza kujiona mtu mzima, utakuwa
umekaa na mwanao kwa siku 27 tu! Fikiria. Wakati mtoto anaondoka nyumbani
kwenda shule ya bweni akapate ufunguo wa maisha utakuwa umekaa nae kwa takribani mwezi mmoja tu! Miaka
mingine yote ulimwacha akihusiana na televisheni na watu wengine usiowajua!
Hivi kwa jinsi maisha yalivyobana namna hii, wazazi tunapata
hata dakika hizo kumi kwa siku kukaa na wanetu na kuwasikiliza na kuwasiliana
nao kirafiki ukiacha kuonya na kuadhibu? Wengine tunaishi Dar es Salaam kikazi, watoto wako kwa bibi yao! Si ajabu hatufanikiwi kuwa na influence yoyote kwa watoto. Wakianza kufanya vitu vyao, tunaishia
kulalamika ‘watoto wa siku hizi wameharibika.'
Tuwe vile tunavyotaka
watoto wawe
Mtoto hujifunza kwa kiasi kikubwa kupitia kile kinachofanywa
na watu wake muhimu wanaomzunguka. Ni muhimu kufanya kile tunachotaka mtoto
akifanye. Tuwe na tabia na imani tunazotaka kuzihamisha kwa mtoto. Mathalani,
kama ninatamani mtoto awe msomaji wa vitabu, ni lazima nihakikishe ninajenga
mazingira ya usomaji nyumbani kwa kuonesha mfano mimi mwenyewe. Mtoto anakua akijua
maisha ni kusoma. Na sihitaji kumwandalia somo la ‘umuhimu wa kusoma vitabu’ ili ajenge tabia ya kusoma. Nafanya
ninachotaka afanye. Aone nikifanya ibada kama ningependa awe mwombaji na yeye. Niwe
na upendo kwake na mke wangu kama ninataka awe mtu wa upendo kwa watu.
Kadhalika, nikitaka atukane wenzake na siku nyingine
anitukane na mimi kimoyomoyo, niwe na tabia ya kumtukana yeye na kumwambia
maneno magumu. Nikinywa pombe mbele yake maana yake ninamwandaa kunywa pombe ukubwani
hata kama ‘sijamfundisha’ kwa maneno. Maana mtoto hujifunza kwa wepesi kupitia
yale ninayoyafanya mimi kama mzazi. Vinginevyo, nitakuwa na bahati
ikiwa mwenendo wangu utamwuudhi kiasi cha kumfanya aamue kuasi tabia zangu. Na hapo si ni mpaka ajue ninachofanya hakifai kwa binadamu wa kawaida?
Tuwapende watoto, wajisikie
kukubalika
Ninapompenda mtoto vile alivyo bila kujali alichokifanya
ninamfanya aelewe maana ya upendo na aniamini. Simpendi ili nimdai tabia njema.
Hapana. Nampenda hata anapokosea. Nampenda kwa sababu ni mwanangu apatie au akosee. Na wala si kumdekeza. Wakati
mwingine tunakosea kama wazazi. Tunawapenda watoto kama malipo ya tabia njema. Na
wakati mwingine hatufichi, tunawaambia waziwazi kuwa tutawapenda kama watafanya
tulichowaagiza kukifanya. Tutawapa zawadi wakifanya vizuri. Conditions.
Wanapokosea tunaonesha kuwachukia na wakati mwingine tunawatenga
kihisia. Tunawakomoa watoto, eti! Hatuadhibu tabia zao, tunawaadhibu wenyewe. Hali hii huwafanya watoto wawe
wanyonge na wajione hawakubaliki kama watu na mioyo yao hujisikia kubebeshwa deni
na mzigo wa kutekeleza msukumo wa nje wasioona mantiki yake. Hakuna binadamu wa
kawaida hufurahia shinikizo la namna hii na kwa kweli huwa ni vigumu sana mtoto
wa jinsi hii kufundishika. Adhabu zitaongeza usugu.
Ni kweli kuna nyakati watoto huwa watundu na mzazi hulazimika
kumfokea na kumwadhibu badala ya kufikiria kumjengea mtoto tabia anayoitaka. Lakini
ni vyema tukaelewa kwamba adhabu na mashinikizo yasiyotanguliwa na upendo na mazingira
ya kujenga tabia njema hayana matokeo chanya katika maisha ya mtoto.
Kiboko cha kweli anachokihitaji mtoto kujenga tabia njema ni upendo. Na wala kumpenda mtoto si kumdekeza kama tunavyoamini wazazi wengi tulikulia mazingira yaliyotindikiwa upendo. Hatukulelewa kwa upendo, tunahamishia magonjwa yetu kwa watoto. Samahani. Nilitaka kusema upendo halisi hujenga mazingira ya kupanda tabia zinazofaa bila kusubiri kuadhibu tabia zisizofaa zilizotokana na kunyimwa upendo.
Kiboko cha kweli anachokihitaji mtoto kujenga tabia njema ni upendo. Na wala kumpenda mtoto si kumdekeza kama tunavyoamini wazazi wengi tulikulia mazingira yaliyotindikiwa upendo. Hatukulelewa kwa upendo, tunahamishia magonjwa yetu kwa watoto. Samahani. Nilitaka kusema upendo halisi hujenga mazingira ya kupanda tabia zinazofaa bila kusubiri kuadhibu tabia zisizofaa zilizotokana na kunyimwa upendo.
Tushughulike na msongo
wa nafsi zetu kwanza
Kazi ya kulea inahitaji nafsi iliyotulia. Nafsi isiyotafuta
amani kwa kuumiza wengine. Ninapokuwa mzazi mwenye nafsi iliyosongwa na matatizo
siwezi kutekeleza ipasavyo jukumu nyeti la malezi yatakayomjenga mtoto
anayejitambua, anayejiamini na atakayekabiliana na changamoto za maisha ya
ukubwani. Nitajikuta nikimtumia mtoto kama dodoki la kufyoza ugonjwa
unaoisumbua nafsi yangu. Nitakuwa mwepesi, pasipo mimi kujua, kusema maneno
magumu yasiyolingana na umri wa mtoto. Nitajisikia kuridhika kumfanya mtoto alie
na kukosa amani. Nitaadhibu na kukemea kuliko ninavyowajibika kujenga imani,
mitazamo na tabia njema.
Ni muhimu sisi kama wazazi kushughulika na matatizo ya
nafasi zetu na kuhakikisha kwamba tunahusiana vyema na nafsi zetu ili tuweze
kujitoa kuwalea watoto wetu katika njia iwapasayo. Tukishashughulika na nafasi
zetu, kinachofuata ni kujiuliza, tungependa watoto wetu waweje watakapoanza
kujitegemea kimaamuzi? Kitu gani tungependa kichipue kwenye mioyo yao
kitakachoongoza maisha yao ya sasa nay a baadae? Maana upo ukweli kwamba malezi
yanachangia kwa kiasi kikubwa tabia tunazoziishi ukubwani. Kama tunapenda
kutumia fursa ya kuumba tabia njema kwa watoto wetu, hatuwezi kukwepa kufanya maamuzi
ya kulichukulia suala hili la malezi kwa uzito unaostahili. Malezi si kazi inayoweza kufanywa na yeyote. Tuyape uzito unaostahili.
christianbwaya@gmail.com
Nimependa hili somo nitarudi tena hapa...kuna kitu nafikiria
JibuFutaYasinta karibu sana. Tafadhali tushirikishe unachokifikiri tujifunze pamoja.
JibuFutaKuna hili jambo ambali huwa linanitatiza sana haya maisha ya siku hizi...yaani ile tabia ya kula chakula pamoja si mnakumbuka mlio na umri wangu jinsi ilivyokuwa na ule ni muda mzuri sana kwa familia kupasana habari zote za maisha. Lakini siku hizi kila mtu anakula kwa wakati wake...Hivi kwa nini tunapoteza utamaduni wetu?
JibuFutaNi kweli kabisa dada Yasinta. Utamaduni wa familia kula pamoja mezani unasaidia sana kujenga mahusiano na values/tunu za pamoja baina ya wanafamilia. Mnacheka, mnabadilishana habari nyepesi nyepesi na hivyo inakuwa rahisi kujua yanayoendelea kwa kila mwanafamilia.
JibuFutaLakini sasa, Yasinta, wazazi hasa sie akina baba tutapata wapi muda wa kula na familia/watoto wakati tuko bize na kusaka maisha mpaka saa tatu/tano usiku? Baba anayerudi nyumbani watoto wakiwa wamelala, na wa kwanza kuondoka (watoto wakiwa usingizini) atapata wapi muda wa kula na watoto?
Kadhalika, mambo kama kuzorota kwa mahusiano baina ya wazazi, mashinikizo ya kimaisha na hata kutokuyapa malezi uzito wake yanaathiri kwa kiasi kikubwa utamaduni huu muhimu katika kujenga mahusiano ya karibu kati ya wazazi na watoto wao.
Baba mwenye tatizo na mke wake anaweza kujikuta akikwepa meza ya chakula, kwa kisingizio cha 'mambo mengi' wakati kiukweli yuko baa anaharibu akili na vichwa vinavyofanana nae. Tunahitaji kubadilika. Turudishe utamaduni huu unaopotea kwa kasi kubwa.
Nimejifunza mengi kwa somo hili, bila shaka nimeongeza maarifa ya malezi bora.
JibuFutaASANTE,,,IMENISAIDIA
JibuFutaNimejifunza Mambo mengi hapa, kaka nashukuru inawezekana kwa namna moja au nyingne nimekua nikimjaza mwanangu sum kwa kumchapa viboko badala ya maelekezo na urafiki
JibuFuta