Mtoto ni nani?
Sheria na mikataba mbalimbali inayozungumzia huduma na haki
za mtoto, inamtambulisha mtoto kama mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya
18. Hata hivyo, kutumia umri kama msingi wa tafsiri ya utoto hakuwezi kutusaidia
kujua kwa nini mtu mwenye umri huo aitwe mtoto. Katika makala haya, ningependa tumtazame
mtoto kwa kuangalia mitazamo tofauti katika jitihada za kumtofautisha mtoto na
mtu ‘mzima’ bila kutumia idadi ya miaka kama msingi mkuu.
Mitazamo mbalimbali ya dhana ya utoto
Kiufahamu/kiakili
Mtoto, kwa maana hiyo, ni mtu asiye na uwezo wa kutambua
mtazamo tofauti na alionao yeye. Mtu asiyefikiri kwamba mtu mwingine anaweza
kufikiri tofauti na yeye. Sababu kubwa hapa ni kwamba ufahamu wake bado
unaumbika na kwa kiasi kikubwa hauna tajiriba inayokidhi kulitazama jambo kwa
nyanja kadhaa kwa wakati mmoja.
Mitazamo mbalimbali ya dhana ya utoto
Mosi kabisa, kuna mtazamo wa ukuaji. Hali ya ukuaji wa mwili
inayosababisha mabadiliko yanayoendana na upevukaji, mabadiliko ya homoni,
uelewa wa mtu na kadhalika huweza kuchukuliwa kama kigezo cha kumtofautisha
mtoto na mtu mzima. Mtoto tunamtazama kama mtu mwenye viungo viteke vinavyoendelea
kukua, wakati mtu mzima ni yule asiyefikia kimo cha upevukaji.
Mabadiliko yanayoongoza ukuaji wa mtoto yanaweza kupimwa na
njia za kisayansi ili kuelewa maendeleo ya jumla yanayofanana kwa watoto wote
bila kujali wanakoishi na athari nyinginezo za kimakuzi. Ingawa kigezo hiki
hakizingatii ukweli kwamba kila mtoto ni mtu tofauti na watu wengine wa umri
wake, bado kwa kutumia wastani wa yale yanayoonekana kuwa ‘kawaida ya watoto wa
umri fulani,’ tunaweza kuwachukulia wengine wenye tofauti na kawaida hiyo kuwa
na ukuaji usio wa kawaida.
Kadhalika, tafsiri ya mtoto inaweza kuathiriwa kwa kiasi
kikubwa na historia, tamaduni na mienendo ya jamii. Uelewa wa nini kinamfanya
mtu ahesabike kuwa mtoto na wakati gani watoto hukoma kuitwa watoto na kuingia
kwenye utu uzima, unatofautiana katika jamii zetu. Ndio kusema utoto ni dhana inayoweza kuumbwa kwa
namna mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yenyewe na sio lazima iwe
mahitaji ya mtoto mwenyewe.
Katika jamii nyingi za ki-Afrika kwa mfano, matukio fulani yanaweza
kuchukuliwa kuwa mpaka wa utoto na utu uzima. Kuna mila kama jando/unyago, ndoa
na kadhalika vinavyotazamwa kama kivuko cha utoto kwenda utu uzima. Pia zipo imani/mila
za kidini zenye matukio ya namna hiyo kama kipaimara, sakramenti ya kwanza na
kadhalika. Haya yote ni matukio yenye ‘uwezo’ wa kumvusha mtoto kwenda utu
uzima bila kueleza ni mambo gani hasa yanamfanya mtu aonekane ni mtoto au mtu
mzima.
Aidha, mtazamo mwingine wa kumwangalia mtoto kwa jicho la
mahitaji yake ya kimsingi na namna tunavyoweza kuyajibu mahitaji hayo. Mtazamo
huu unatumika na mashirika, taasisi na watu wenye kufikiri namna ya kutoa
huduma za ustawi wa watoto kisera na kisheria. Hawa wanatumia mahitaji ya mtoto
kupanga kile wanachotaka kukifanya kwa mtoto na hivyo kuamua nani ni mtoto na
nani siye.
Kwa mfano, watetezi wa haki za watoto huweza kumchukulia
mtoto kama mtu yeyote mwenye umri fulani asiye na uwezo binafsi wa kujitetea na
hivyo kuhitaji kulindwa na unyanyasaji au ukiukwaji wa haki zake fulani fulani.
Kadhalika, kuna mashirika kama yale yanayowatafutia ufadhili watoto wanaoishi
kwenye mazingira magumu. Kwao mtoto anaweza kuwa mtu yeyote anayemtegemea mtu
mwingine katika kupata mahitaji yake bila kuzingatia sana umri. Mtoto anaweza
kuwa hata baba wa miaka 25 almuradi bado yuko kwenye orodha ya wanufaika wa ‘mradi
wa kuwasaidia watoto.’
Uwezo unaowapambanua watoto kwa ujumla
Katika mipaka ya makala hii, tutajaribu kuangalia tafsiri ya
mtoto kwa kutumia mtazamo wa yale anayoweza/asiyoweza kuyafanya kama matokeo ya ukuaji wa mwili. Kiujumla, tunaweza kusema mwili wa huyu anayeitwa mtoto unaendelea
kuumbika na kuongezeka kwa kasi kufikia umbile na umbo kamili linalochukuliwa
kuwa la mtu mzima. Huyu ni mtu anayejifunza kuutumia na kuufanya mwili wake
umwezeshe kukabiliana na changamoto za kimazingira. Ukuaji huu wa mwili unaenda sambamba na ukuaji wa uwezo mahsusi katika maeneo makuu matatu; kiufahamu, kimaadili
na kimahusiano, vyote vikimtambulisha mtoto bila kujali sana umri wake.
Kiufahamu/kiakili
Kwa ujumla, watoto si watu waliozidiwa akili na watu
wanaoitwa watu wazima bali ni watu wanaofikiri na kuyatazama mambo tofauti na
mtu mzima. Mtazamo huu wa kitoto hubadilika kadri ukuaji wa mwili unavyoendelea
kutokea si kwa maana ya kuwa bora kuliko ulivyokuwa awali bali kuwa tofauti na
ulivyokuwa ili kumsaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Mtoto hazidiwi ufahamu na mtu mzima. Picha: Sayuni Philip |
Fikra za mtu huyu anayeitwa mtoto zinaishia katika kile kinachoonekana,
kwa maana ya kutokuwa na uwezo wa kutafakari yasiyoonekana au kutegemea
yanayoonekana ili kufikiri. Ndio kusema mtoto kiufahamu anahitaji kuona kitu
halisi ili kuweza kufikiri.
Kimaadili/kiroho
Kimaadili/kiroho
Kadhalika, mtoto anatambua mema na mabaya lakini kwa kutumia
sababu tofauti na zile za mtu mzima. Mfano wa sababu zinazotumika na mtoto
kutofautisha jema na baya ni matokeo ya kilichofanyika, namna mahitaji yake binafsi
yalivyokidhiwa, kufikia matarajio ya jamii inayomzunguka kwa maana ya kuiga
yanayofanywa na yanayoonekana kukubalika na wale wenye mamlaka.
Kwa mfano, jema kwa mtoto ni lolote lenye matokeo yenye
kumnufaisha yeye. Kitendo anachokifanya na kinachomletea matokeo mazuri kwake
huo ndio wema. Ubaya kwa upande mwingine, ni lolote lile linalofanywa na
mwingine au analolifanya yeye lisilo na matokeo yenye manufaa kwake au
lisilokubalika na wanaomzunguka.
Tunaweza kusema kwamba mtoto anaweza kutenda jambo
pasipokujua athari za anachokifanya almuradi tu anachokifanya kinamletea
manufaa fulani kwake. Kwa kutambua kwamba mtoto hufanya bila kutafakari athari
kwa upana wake, sheria kwa kutumia kigezo cha umri, zinamlinda mtoto hata
anapofanya jambo lenye uhalifu ndani yake.
Tofauti na mtoto, mtu mzima anachukuliwa kuwa yule
anayeongozwa na dhamira yake na sio matarajio ya wengine katika kutanguliza
ustawi wa watu wengine zaidi yake yeye. Kwa kutumia tafsiri hii, maana yake mtu
mwenye miaka 35 anayefikiria na kutanguliza ustawi wake mwenyewe na kuongozwa
na matarajio ya wengine bila kutafakari kwa mapana athari za anachokifanya ni
mtoto ingawa anawajibikia matendo yake kisheria.
Kihisia/Kimahusiano
Kihisia/Kimahusiano
Mtoto ni mtu anayetumia hisia zaidi kama namna ya
mawasiliano yake na watu wengine ingawa hana uwezo wa kuelewa wala kudhibiti
hisia zake zinapohitilafiana na hisia za wengine. Anakasirika kusema ametishwa.
Analia kusema hajaridhika au anahitaji. Pamoja
na kuwasiliana kwa kutumia hisia, mtoto hana uwezo wa kuelewa hisia za wengine
na kujua kilicho nyuma ya hisia fulani ingawa hali hii hubadilika kadri
anavyokua. Ni kwa sababu hiyo, mtoto huhusiana na wanaonufaisha/wanaompa faida ya
moja kwa moja mfano mama, dada na kadhalika. Hali hii huendelea kubadilika
kadri anavyokua.
Kinachofanya mahusiano yake na wengine kuwa ya upande mmoja,
yaani yanayomnufaisha yeye ni kutokuwa na uwezo wa kufikiri mahitaji ya wengine.
Anadai kula yeye bila kujua anayempatia chakula amekula ama la. Analia kudai msaada
bila kujua anayeombwa msaada naye anaweza kuomba msaada kwa mwingine. Kimahusiano
tunaweza kusema anaamini wengine wanayo majibu ya mahitaji yake na yeye ni
mnufaika asiyewajibika.
Tunaweza kumsaidiaje mtoto?
Kwa ujumla tunaweza kusema mitazamo inayojaribu kumtambua mtoto
inatofautiana na wakati mwingine kupingana kulingana na mahitaji ya
anayetafsiri. Wakati sayansi inaweza kutupa sifa za mtoto pasipokujali amekulia
katika mazingira gani, jamii husika nayo inaweza kuja na tafsiri yake
inayoendana na mazingira yake kumwumba mtoto.
Yapo mazingira ambayo mtoto huonekana kama mtu asiye na hatia na ambaye hukosea kwa
kutokuelewa. Kwamba utoto ni umri wa kutokuhukumiwa kwa matendo yake na hivyo
ni wajibu wa jamii kumlinda mtoto na mabaya ya watu wazima, kumsamehe
anapokosea na kumrudisha kwenye mstari wa jamii kwa uangalifu ili hatima yake
aishi kwa furaha na amani.
Lakini yapo mazingira ya kijamii yanayomtazama mtoto kama
mtu anayezaliwa na uovu na uhalifu wa asili. Mtazamo huu ndio unaotufanya
wakati mwingine tuamini kwamba watu wazima wanayo mamlaka ya kuwastaarabisha na
kuwaadhibu watoto wanapokosea kwa sababu hukosea kwa makusudi shauri ya asili
ya uhalifu iliyo ndani yao. Ubatizo wa watoto kwa baadhi ya imani za kidini ni mfano
wa matambiko yanayokusudia kung’oa asili hii ya uovu inayoaminika kuambatana na
mtoto tangu anapozaliwa.
Vyovyote iwavyo, mtoto anachukuliwa kuwa tofauti na mtu mzima. Mtoto
kwa ujumla anaonekana kuwa mtu anayehitaji kusaidiwa kukabiliana na changamoto
za dunia kwa kuelewa mahitaji yake. Na kwa kuangalia tafsiri hizi, tunaweza
kuona kwamba mtoto anaweza kuwa mtu yeyote pasipo kujali umri wake ingawa kwa
mtazamo wa kisaikolojia, mara nyingi sifa za utoto huishia katika umri wa miaka
12. Huyu ndiye mtu ambaye kuanzia makala inayofuata kutaanza kuusaili uwezo na mahitaji yake kiumri.
christianbwaya@gmail.com
Napenda kuchangia kidogo hili suala. Ajabu ni kwamba hata mimi, na mvi zote hizi, bado najitambua na kujitambulisha kama mtoto kwanza katika familia yetu. Dhana hii ya "mtoto" wa fulani hafutiki hata ukawa mzee wa miaka 80.
JibuFutaKatika blogu zangu miezi ya hivi karibuni nimeandika kuhusu mazungumzo yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Lakini huyu mzee tunayemwita mtoto ana umri wa miaka 87.
Nakushukuru sana Profesa Mbele kwa kuipanua dhana ya 'mtoto'. Nakumbuka hata babu yangu hujirejea kama 'mtoto wa tatu' katika familia yao. Kumbe kijamii suala si umri kwa maana ya idadi ya miaka wala uwezo. Ni namna linavyoumbwa na tamaduni na mazoea yetu. Shukrani sana :)
JibuFutaIngiza maoni yako...tuwalinde Watoto,nipo kasulu kigoma
JibuFutaDhana ya mtoto inapotafsiriwa lazima kuzingatia vigezo au muktadha ambapo unatumia kuitafsiri dhana hii Kwan hata mtu mzima akienda Kwa wazazi wake bado ni mtoto, na haya katika sehemu za ibada unapofanya ibada bado wew ni mtoto Kwa muumba wako, kwaiy dhana ya mtoto lazima ifasiriwe kulingana na muktadha husika mfano katika Sheria mbalimbali za umoja wa mataifa haya Sheria za nchini mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18 kwaiy kigezo cha umri na Sheria kimetuka kufasiri dhana ya mtoto Kwa muktadha huo.
JibuFutaAsante sana Profesa kwa kula ya dhana hili. Nadhani dhana hili la mtoto tunakumbana nayo katika maisha na kamwe hatuwezi kuliacha au kulifuta. Hii ni kwa sababu utakua mtoto wa mamako mzazi milele.
JibuFuta