Shule zisizo na elimu zifungwe!?


Ivan D. Illich ni mwanafalsafa aliyezaliwa mjini Vienna mwaka 1926. Katika kitabu chake cha Deschooling Society, Illich anazishambulia taasisi ziinazohodhi wajibu wa kuelimisha jamii. Anasema; “…kwenda shule (tofauti na kuelimika) imekuwa ndio utaratibu wa maisha…shule zimeshindwa kukutana na mahitaji ya mtu mmoja moja, na mbaya zaidi zinaendeleza uongo ule ule kwamba yale yanayoitwa maendeleo yanayotokana na uzalishaji, utumiaji na faida ndicho kipimo cha ubora wa maisha ya mwanadamu.

“…Vyuo Vikuu (shule) vimegeuka viwanda vya kutengeneza vibarua kwa ajili ya matajiri, vikiwapa raia vyeti kwa ajili ya kutoa huduma, wakati huo huo vikionekana kuwanyang’anya leseni wale vinavyowadhania kuwa hawafai (waliofeli).” Tafsiri ni yangu.

Illich anatoa mapendekezo ya kukomesha mfumo huu wa baadhi ya watu kujipa wajibu wa kuwaelimisha wengine wakati wao wenyewe hawajielimishi. Haoni haja ya kuwa na majengo yanayoitwa shule ambayo kazi yake inaonekana kuishia kutengeneza watumwa wa soko huria.

Ni kitabu kizuri sana. Nilikisoma kwa lazima kama sehemu ya hicho kinachoitwa ‘elimu ya mtihani’ na kwa kweli nimeendelea kukisoma kwa hiari. Kama unataka kuelewa udhaifu mkubwa wa “kukiritimbisha” elimu ndani ya majengo yanayoitwa shule, kitafute ukisome.

Kilichapishwa kwa mara ya mwisho mwaka 1971, na Calder & boyars Ltd. ISBN 0 7145 0879 9

Maoni

  1. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta
  2. Nakumbuka nilisikia fikra za Ivan Illich nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu Dar, 1973-76. Fikra hizo ndizo ilitakiwa zitawale katika jamii yetu. Wengine wenye fikra za kimapinduzi ambazo zingetufikisha pazuri ni kama Paulo Freire, Frantz Fanon, Walter Rodney na Julius Nyerere. Lakini wa-Tanzania watakubali kuacha vijiwe, ulabu, na sherehe, washike vitabu? :-)

    JibuFuta
  3. @Profesa Mbele,

    inasikitisha kwamba pengine fikra za watu uliwataja hazitawali jamii yetu kwa sababu hatuzisomi.

    Nilianza kumsoma Freire, Illich na wenzie miaka ya 2000, karibu miaka 30 baada yako! Ni wazi nahitaji kujua zaidi.

    JibuFuta
  4. Ndugu Bwaya, haya yote ni masuala ya kufikirisha. Kila suali, tukilitafakari, linazua masuali zaidi.

    Badala ya sisi tuliosoma vitabu hivi zamani kujitapa kwamba tulishavisoma, suali ni kwa nini, katika miaka yote hii, hatujaweza kuleta mwamko mpya kati ya kizazi kipya, hasa ukizingatia kuwa baadhi yetu ni walimu.

    Nyerere niliyemtaja aliandika sana na alitoa hotuba nyingi sana, ambazo hao walioko madarakani walikuwa wanazisilikiza muda wote na kuzipigia makofi. Leo hakuna hata mmoja wao anayesimama kwenye mkutano wa hadhara na kuchambua fikra za Mwalimu.

    Badala yake, hao watu wanaleta vitu vya ajabu kabisa, ambavyo ni tofauti na aliyowafundisha Mwalimu Nyerere. Kwa mfano, alifundisha umuhimu wa elimu, na yeye mwenyewe aliweka mfano kwa juhudi zake za kujielimisha. Alikuwa anasoma sana, na papo hapo alikuwa anakuja Chuo Kikuu kupambana na wasomi kwa hoja.

    Leo, hao tunaowaita viongozi wanatoroka midahalo.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?