Ndivyo walivyoboresha Elimu?

CCM inajigamba sana kwamba imepanua elimu katika nchi yetu. Katika ilani yake ya uchaguzi, CCM inatuambia kwamba shule za Sekondari zimeongezeka kutoka 1745 mwaka 2005 mpaka shule zipatazo 4102 mwaka jana. Kwamba wanafunzi wanaosoma sekondari katika nchi yetu, wameongezeka kutoka 401,598 mwaka 2005 kufikia 1,401,559 hivi sasa! Kwa mtu anayehesabu mafanikio kwa kuangalia vitu na idadi, haya yanaweza kuonekana kuwa ni mafanikio makubwa sana kuwahi kufikiwa katika nchi yetu.

Lakini tukitazama aina ya hao wanaoitwa wanafunzi wanaodaiwa kuwa mashuleni kwa wingi, utashangaa! Katika wanafunzi hao ni asilimia 17.8 tu ndio hufaulu kwa daraja la I. II na III. Umati mwingine unaobaki (yaani asilimia 82.2) wanaishia kupata daraja sifuri na lile la IV. Kwa maana nyingine, kwa kila wanafunzi 10 wanaofanya mtihani wa Taifa, ni wanafunzi wawili tu hupata angalau daraja la III. Hiyo ni elimu ya Sekondari hata baada ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari.

Ukija kwenye elimu ya msingi ambayo nayo iliundiwa “mkukuta” uitwao MMEM, hali ndio mbaya zaidi. Mwaka huu tunaambiwa zaidi ya wanafunzi milioni moja walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Na kwa vile ni wakati wa kampeni, hiyo ilikuwa habari kubwa. Ili kujua hao wanaodaiwa kuwa “ni ongezeko kubwa la wahitimu wa elimu ya msingi” wanamalizaje elimu hiyo ya msingi, tuangalie matokeo ya utafiti.

Taasisi ya Uwezo imebaini kwamba asilimia 49.1 ya wanafunzi wanaohitimu Elimu ya Msingi, hawajui kusoma wala kuandika Kiswahili cha msingi! Yaani kwenye wale milioni moja walimaliza elimu ya msingi mwaka huu, laki tano waliingia darasani kuchochora mistari (maana hawajui hata kusoma)! Nilidhani baada ya kutangazwa utafiti huu, ingekuwa bora nchi iingie katika maombolezo ya siku tatu!

Na kwa kweli ingekuwa ni uungwana kwa CCM kusitisha kampeni zao ili watuombe radhi watanzania kwa kutuharibia mustakabali wa watoto wetu. Watueleze wana mpango gani na hao nusu ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba wakiwa wajinga? Je, CCM ina mkakati upi wa kushugulika na hiyo asilimia 82.2 inayoishia kukwama kidato cha Nne? Au ni kuwajengea Machinga complex kwa kila mkoa?

Hii ni dhuluma kwa watoto wa masikini. Watoto ambao wazazi wao zaidi ya milioni 1.5 ni 'toleo jipya' la mafukara wapya wanaoishi chini ya Tsh 570 kwa siku! Ni ajabu kwamba CCM kinaendelea kupiga kampeni kama kawaida! Na kweli, kwa nini kisifanye hivyo wakati kinajivunia asilimia 80 ya wananchi “wanaokikubali”?

Maoni

  1. Ndiyo maana mimi huwa sipendi takwimu zisizo na maana.

    Unaponiambia eti uchumi (au sijui GDP)umekua kwa asilimia 7 mwaka huu lakini maisha ya watu masikini yamezidi kuwa magumu, hata kama uwe mchumi uliyebobea namna gani, takwimu zako na kukua kwako huko kwa uchumi hakuna maana yo yote.

    Ni yale yale. Takwimu nzuri zinazong'ara kuhusu elimu lakini ukiangalia vizuri ni "mazingaombwe" tu. Kama nusu ya wahitimu hawawezi hata kusoma na kuandika Kiswahili (si Kiingereza!) wamehitimu nini? Ni kweli wanastahili kuitwa wahitimu?
    Kuna anayejua hawa wasiojua kusoma na kuandika wanakwenda wapi? Halafu kesho na kesho kutwa wakiwa vibaka tunaanza kuwachoma moto na kuwabanika kama ndafu (http://matondo.blogspot.com/2010/09/kibaka-akiona-cha-moto-abanikwa-kama.html)!

    Ukweli ni kwamba elimu ndiyo msingi mama wa maendeleo na hakuna njia ya mkato kwani hakuna nchi hata moja ambayo imeweza kujikwamua kimaendeleo bila kuboresha mfumo wake wa elimu. Sijui ni kwa nini tunafikiri kwamba sisi tunaweza kuwa tofauti.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?