Ujuzi wa kanuni za maumbile haumkani Mungu

TUMEKWISHA kuona mifano ya upotoshaji uliofanywa na baadhi ya ‘wanasayansi’ ambao kimsingi walioongozwa na imani kuliko uhalisia. Tukaona kwa ufupi sana nafasi ya sayansi katika kutambua (sio kuvumbua) kanuni za maumbile ambazo kimsingi zilikuwepo kabla ya maarifa haya hayajakuwepo. Hapa tunaendelea pale pale kwa mifano zaidi.

****************
Sayansi kwa kuzichunguza kanuni hizo, imeweza kuyabadili maisha ya mwanadamu kwa namna mbalimbali. Kwanza maarifa hayo yameweza kutusaidia kuvumbua nyenzo muhimu zilizotuwezesha kufanya mambo ambayo hapo awali hatukuwa na uwezo nayo.
Pamoja na manufaa yote tuliyoyapata kwa maarifa haya ya sayansi, bado yapo maeneo ambayo kusema kweli sayansi imeharibu. Kwanza, kwa matumizi mabaya ya maarifa hayo yamefanya maisha ya viumbe yawe ya wasiwasi zaidi kuliko ilivyowahi kuwa katika kipindi cha nyuma. Kwa mfano, kwa maarifa yaliyopo, zimetengenezwa silaha ambazo kwa kweli kichaa mmoja akipandwa na hasira asubuhi moja na akakosekana wa kumdhiti anaweza kuiteketeza sayari ya dunia kwa muda mfupi sana.
Lakini vilevile, maarifa ya sayansi hayajaweza kwa hakika kuwa na maelezo makamilifu katika baadhi ya maeneo. Moja wapo ya maeneo hayo, ni kuhusiana na mwanzo wa uhai.

Awali ya yote, ieleweke wazi kwamba sayansi haijaweza kukubaliana na uwepo wa mwasisi wa uhai na vyote vilivyopo katika ulimwengu (universe). Najua maarifa hukua. Vipo vyumba vya maabara ambavyo usiku na mchana hutumiwa kutafiti mambo yasiyojulikana. Natambua uwezekano wa kisichofahamika leo, kueleweka vyema kesho. Hata hivyo, kwa sababu siku zote zimekuwepo jitihada za makusudi kujaribu kutafuta maelezo mbadala kuhusu chanzo cha uhai ambacho kwa hakika kimejidhihirisha vyema mpaka sasa; na kwa sababu siku zote wapo wanadamu amabo wanatafuta kumkana Mwasisi huyo kwa gharama yoyote kwa kujaribu kuthibitisha (pasipo shaka) kwamba uhai ulijitokeza wenyewe bila muasisi yeyote; basi ni jambo lililo wazi kwamba hata ungekuwepo ushahidi wa moja kwa moja kisayansi kuliko ilivyo sasa, kwamba Muasisi ndiye kafanya vyote hivyo, ujinga wa kumkana usingefikia tamati yake asilani.

Sayansi inasema nini kuhusu chanzo cha uhai?

Sayansi, ambayo msingi wake mkubwa ni ushahidi, kwa kudhani kwamba kila kitu ni lazima kielezeke kwa ushahidi –inayo maelezo rasmi (ambayo angalau kwa sasa yanachukuliwa kuwa kweli tupu) kuhusu chanzo cha uhai.
Uhai wenyewe maana yake ni kule kuwepo, kwa maana ya kuweza kutenda vitendo kwa hatua anuani kutegemeana na mtiririko wa uwepo wa hali hiyo. Kuwepo, ambayo ni sifa ya uhai wenyewe, ni lazima kuhitimishwe na kifo. Uwepo usiohitimishwa na kifo, si uhai. Ni sawa na jiwe ambalo lina sifa ya kuwepo, lakini uwepo huo hauhitimiki kwa kifo.
Kisayansi, uhai huu ‘uliibuka’ kutokana na vitu visivyo hai. Vitu hivi (hewa,radi nk) viliungana hatua kwa hatua ndani ya maji (baharini) na mwishowe, baada ya miaka mingi sana viliweza kutengeneza kiasili kiitwacho DNA. Kiasili hiki, ambacho ndicho msingi wa uhai wa kiumbe yeyote, ndicho kilichoongoza ‘mapinduzi’ kuelekea katika mradi wa kuunda chembechembe hai ya kwanza rahisi ambayo nayo baada ya miaka mingi iliweza kubadilika kuwa chembe chembe hai iliyobora zaidi.
Msomaji atakuwa ameona kwamba kule kudai kwamba uhai umeanza na vitu visivyo hai, ndio msingi wa kujaribu kukwepa kuwapo kwa Nguvu iliyokuu ambayo inaweza kuaminiwa kuwa designer wa uhai huo.

Aidha, seli hizo (kwa mujibu wa nadharia inayokubalika sasa katika sayansi), baada ya miaka mabilioni baadae ziliweza kubadilika zenyewe kwa kuongozwa na mabadiliko yaliyopo kwenye mazingira na kuwa kiumbe rahisi, ambaye naye baadae alibadilika by chance (kwa kubahatisha bila mwelekeo maalumu) na kuwa utitiri wa viumbe waliopo sasa. Kwa lugha rahisi ni kwamba kisayansi viumbe wote wametokea (by chance) kutokana na viumbe wengine. Hakuna wakati ambao viumbe wote waliopo leo, waliwahi kuwapo kwa wakati mmoja.

Kwa maoni yangu, maelezo haya ni kujaribu kukwepa ukweli ambazo unafahamika kwa kila mwanasayansi asomaye elimu ya viumbe hai.

Hapa ninayo mifano michache rahisi sana ambayo ninadhani inaweza kutufanya tufikirie zaidi ya ushahidi wa kisayansi.

Mabadiliko yanayotokea kwenye mwili wa kiumbe, ambayo baadae yanasababisha kutengenezwa kwa mbegu za uzazi ambazo nazo hubadilika na kuwa kijusi baada ya kuungana; kwa hakika ni mabadiliko ambayo huwezi kusema ni ya kutokea hivi hivi tu kama tunavyoambiwa na maprofesa wetu.
Tuchukulie mfano ambao wengi tutakuwa na habari nao. Ukizungumzia namna mbegu za kiume zinavyofanyika kwenye mwili wa mwanaume, utashangaa. Chembechembe hai maalumu ambazo ziko kwenye korodani hupitia mabadiliko ambayo yameratibiwa kwa ustadi mkubwa kupitia vinasaba vilivyomo kwenye chembechembe hiyo isiyoonekana hata kwa darubini za kizamani. Pamoja na udogo wake, seli hizo hubadilika bila makosa na kutengeneza vipengele vingi ambavyo kimoja kikikosewa mbegu nzima haiwezi kufanya kazi.
Kwa upande wa mwanamke hali ni ile ile.
Baada ya kukamilika, inashangaza namna ambavyo viumbe hao wawili wanajikuta wakikutana kimwili ili kuzikutanisha mbegu hizo. Kinachoshangaza ni namna ambavyo, ili mtoto afanyike ndani ya mwanamke ni lazima kitendo cha kuingiliana kimwili kiwe katika kipindi fulani cha mabadiliko ya mwili wa mwanamke!
Kumbuka kwa kadri yai linavyotengenezwa kwenye mwili wa mwanamke, mawasiliano huwepo ambako tumbo la uzazi nalo huandaliwa (ili isije ikatokea kwamba mimba imetungwa wakati mji wa mimba haujajiandaa!) Huu ni uratibu wa namna ya ajabu sana.
Mbegu hizo zikishakutana, mabadiliko yanayotokea kwenye kijusi hicho hatuwezi kuyaeleza kwa maelezo rahisi. Namna seli (ambazo awali zilikuwa zinafanana) zinavyogawanyika na kuwa seli tofauti na nyingine, ni jambo ambalo halina mfano wake! Ukweli ni kwamba kuna namna ambayo inathibitika kwamba hayo yote yanafuata mwongozo fulani pasipo makosa. Ni kama mjenzi anayefuata ramani iliyochorwa na mchora ramani. Hiyo ni kusema kwamba kila seli inajua inatakiwa iwe nini na kwa wakati gani, baada ya nini kuwa kimekamilika! Ajabu sana! Seli inayotakiwa (sio kujitakia) kuwa kwa mfano moyo, ni lazima iwe moyo na sio kiungo kingine.
Hapo hatujazungumzia namna ambavyo kijusi (kitoto) hicho kinavyohifadhiwa tumboni mwa mama ili kisidhurike mpaka kitakapozaliwa. Hayo yote yanatokea kwa utaratibu ambao kwa kweli ni upumbavu kudhani kwamba yanatokea tu kwa sababu tu eti ya nature.

Nimetoa mfano huo kuonyesha kwamba ni makusudi ya kijinga sana kudhani kwamba eti kwa sababu tu tunatafuta kuamini kwamba ‘we just evolved’ tunakataa kuuona ukweli kwamba yule Designer (mbunifu wa yote haya) yu halisi.



Nitatoa mfano mwingine baadae.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Haiba ni nini?