Evolution ni nadharia isiyo ya kisayansi

Wapo watu ambao waliweza kuitumia sayansi vibaya na kuidanganya dunia kwamba ‘maumbile’ (nature) ndio kila kitu. Kwamba kule kuyajua maumbile yanaongoza na kutawala mfumo wa ulimwengu (universe) ni sababu tosha ya kuyaamini maumbile yenyewe. [Mfumo kwa maana hii, ni uhusiano wa vipengele mbalimbali vya kimaumbile vinavyotegemeana kiasi kwamba pakitokea hitilafu katika kipengele kimoja, basi uhusiano wote unaathiriwa.]

Watu hawa ni mafisadi wa kisayansi. Na wengine wao nilishajaribu kuwasema zamani kidogo kuonyesha kwamba walitumia sayansi kutuhadaa sisi tutetemekao tusikiapo neno ‘...kwa uchunguzi wa kisayansi...’

Kabla sijaenda mbali, niliseme hili mapema: Sayansi ilivyo ni maarifa ya muhimu sana. Tupo tunaoamini kwamba bila maarifa ya kweli kweli ya kisayansi, tungeishi kwenye dunia tusiyoielewa vizuri (japo hatujafika mahali pa kuielewa kwa maana halisi ya kuelewa) na wala kuelewa namna dhana mbali mbali za kimaumbile zinavyofanya kazi. Kwa hivyo, maisha yetu yangekuwa magumu sana pasipo maarifa mengi yaliyoletwa na wanasayansi mahiri kama akina Newton, Faraday, Eisteen wachache kwa kuwataja. Sayansi ni muhimu katika kutujuza mwenendo wa vile tusivyoviona vinavyotawala maisha yetu katika universe.

Lakini wapo mafisadi waliotudanganya kwa kutumia kivuli cha sayansi. Watu hawa walidhani ili uwe mwana sayansi ni lazima usiamini katika Mungu (jambo ambalo nadhani ni la kipuuzi kuliko upuuzi wenyewe.) Wengi wao walijidanganya kwamba kule kuwa mwanasayansi kwa maana ya kuwa na maarifa ya kufahamu yasiyofahamika kwa wengi, basi maana yake ni kwamba huhitaji kuwa na habari na Mungu. Walikuja na imani zao, wakazijengea hoja kwa matumizi ya data zinazokubalika katika sayansi,na hatimaye maarifa mazima yakafuata mkondo wa imani (soma dini) zao.

Nitoe mfano wa Charles Darwin, binadamu ambaye amejipatia umaarufu na wafuasi dunia nzima kwa kuaminika kuwa ameweza kueleza kwa nini viumbe vilivyopo havijaumbwa bali vilipitia mabadiliko ya muda mrefu ya kimaumbile yaliyojiongoza yenyewe kwa nguvu ya maumbile. Unaweza kusoma maelezo haya mafupi kupata mwanga wa mshumaa kuhusu dhana ya mabadiliko ya kimaumbile (evolution.)

Ukitazama kwa makini mawazo ya watu wanaoamini (kwa hakika si kuelewa) dhana hizi za Darwin, utaona kwamba hayakuanza wa uchunguzi wa kisayansi, bali kwa imani.
Kwa mfano wanakwambia, uhusiano wa kimaumbile uliopo baina ya viumbe unaonyesha kuanzia kwa kiumbe mmoja wa kale. Ili kuelewa wanachosema watu hawa, fikiria mti ulivyo. Kwamba matawi yaliyopo kwenye mti yote yameanzia kwenye shina moja (ancestor) ambalo limegawanyika katika matawi na hatimaye kwenye vijitawi vidogo vilivyoishia na majani. Hii ni kusema kwamba viumbe wa sasa ni matokeo ya mabadiliko endelevu yaliyokuwepo kwa viumbe wa kale.

Mabadiliko yanayowakumba viumbe waliopo, husababisha kupotea kwa kiumbe huyo (extinction) ama kutokea kwa viumbe wengine ambao hawakuwepo awali (speciation). Mtiririko huo wa kubadilika umetufikisha hapa tuliko leo. Kwamba sisi kama binadamu hatukuwepo wakati fulani, ila tumebadilika kutokana na viumbe tuliokuwa tumekaribiana kimaumbile na kuwa tulivyo hivi leo. Na viumbe hao waliokuja kubadilika kuwa sisi, nao hawakuwepo wakati fulani, ila tu wamebadilika vivyo hivyo kutokana na viumbe fulani waliokuwepo nyakati hizo (mamilioni ya miaka) na kugeuka kuwa viumbe wengine kabisa baadae.

Sasa kwa vile mabadiliko haya yanaonekana kuchukua miaka mingi sana kutokea kwa ukamilifu unaonekana, basi kisayansi hubidi mabaki ya viumbe wa kale yatumike katika kujifunza mwenendo mzima ulivyokuwa na kupata mtiririko unaoeleweka. Mabaki haya huitwa fossil, na yametokana na kiumbe husika kufa na kugandamizwa kwenye miamba inaojijenga hatua kwa hatua kwa miaka mingi.

Watu hawa wanaongozwa na imani ya Ki-Darwin, wanadai kwamba masalia ya miaka tofauti tofauti ya viungo vya viumbe wa jamii moja yakikusanywa na kuchunguzwa huonyesha uhusiano nilioueleza kwa kifupi hapo juu kwa dhana ya mti. Hata hivyo, mara nyingi pamekuwepo na kile kinachoitwa ‘the missing link’ ambapo hubidi kubashiri zaidi kuliko ushahidi wa hali halisi.

Lakini tafiti zilizofanywa na watu wengine, zinaonyesha kwamba mabaki hayo hayana uhusiano wa kimti (phylogenic relationship) yanayoshabikiwa sana na wanasayansi wanaoamini katika U-darwin. Kwa mujibu wa tafiti za wanasayansi hawa wengine, kila mabaki ya kiumbe (fossil) yanajitegemea na hayaonyeshi uhusiano unaoelezwa na wenzao (wa Ki-Darwin)! Yaani hakuna uwezekano wa kiumbe mmoja wa kale kubadilika kuwa kiumbe mwingine mpya. Hili linakubalika kwa sababu hata wanasayansi wa Ki-Darwin hukumbana na kile nilichokiita ‘the missing link’ katika michoro yao.

Huu kwa hakika ni ushahidi kwamba madai kuwa viumbe wamebadilika (evolved) ni uongo unaoaminiwa kwa sababu tu za hamu ya mwanadamu hujitenga mbali na mwenye viumbe kwa matumizi ya sayansi.

Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3