Acha woga, zaa mawazo

Leo naamkia uzazi. Uzazi wa mawazo. Mawazo. Mawazo.

Upo umuhimu mkubwa sana wa sisi kama binadamu kujielewa. Kujielewa kutatusaidia kutatua matatizo yetu mengi. Matatizo ya kiutamaduni. Kisiasa. Kijamii. Na kadhalika. Kulielewa ni muhimu sana.

Kujielewa ninakokuzungumza hapa ni kule kufahamu kuwa ndani mwako yapo mawazo ambayo usipoyagundua yatakufa na wewe. Wewe unayo mawazo muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya watu wanaokuzunguka. Bahati mbaya ni kwamba mawazo hayo yanakusubiri wewe uache woga. Useme. Ueleweke unawaza nini.

Mengi ya matatizo yetu hayako huko tunakodhani. Si unajua mara zote huwa hatupendi kuwajikia matatizo?

Chanzo cha matatizo yetu kiko katika fahamu zetu wenyewe. Lakini ajabu ni kwamba watu wengi tunajua sana kuzungumzia udhaifu wa wengine. Tunajua kuchambua hoja za wengine. Tunajua kupuuza vya wengine. Tunajua kulalamika. Kusononeka. Lakini kumbe kufanya hivyo hakuwezi kuleta mabadiliko ya kweli.

Hivi sasa wananchi wanalalama. Serikali imefanya hiki. Serikali. Serikali oooh. Serikali. Serikali uuuh. Serikali. Lakini wanasahau kuwa ni wao wenyewe ndio ndio "walioiajiri" serikali hiyo. Ubora ama udhaifu wake, wa kulaumiwa ni wao wenyewe.

Huwezi kulalamika leo wakati jana ulibadilishana kura kwa kopo la mbege. Ulikubali mwenyewe, kuuza haki yako kwa kutokujielewa wewe, unacholalamikia ni nini? Narudi kwenye hoja.

Ni rahisi sana kukosoa mawazo ya wenzetu, kuliko kuonyesha msimamo wetu kwa kuzalisha mawazo yetu wenyewe na kuyasimamia.

Hima tuamke. Tuzae mawazo.

Mawazo ni mawazo. Toa mawazo yako waziwazi. Sema unachofikiria. Zaa mawazo. Kwa sababu hakuna mwingine mwenye mawazo yanayofanana na yako. Usilalamike sana. Weka wazi mbadala ulionao. Usijidharau. Sema unachowaza, utusaidie.

Hapo tutaanza kuona tofauti.

Maoni

  1. Unajua chanzo cha uoga au mimi hupenda kuita hofu huwa ni malezi. Ukichunguza kwa makini utagundua kwa kiasi kikubwa malezi yametuathiri sana. Katika malezi huwa unalelewa kufanya mambo ambayo jamii au wazazi huwa wanayapenda au kuwafurahisha, na pindi ukijaribu kutaka kufanya jambo ambalo ni tofauti na mtazamo wao ndipo hapo unaanza kujengewa dhana nzima ya woga. Nakwambia utatishwa hadi inafika wakati unaamini ktk hofu au woga. Matokeo ya hali hiyo ni kufungwa kwa uwezo wa kufikiri na kujikuta kila unachotaka kukifanya unahisi kuwa ni woga.
    We angalia hata hilo suala la watu kulalamikia serikali ni kutokana na kule kuambiwa kama watabadilisha viongozi watingia kweny vita nao wakaamini lakini msingi ni hali ya kutishwa waliyojengewa.

    JibuFuta
  2. Nakubaliana na wewe Nuru. Kwamba woga wa kuonyesha wazi mawazo yetu unatokana na malezi tuliyopata. Kwamba wazazi wameshindwa kututia moyo na/au kutufanya tutiwe na moyo wa udhubutu kusema vile tulivyonavyo moyoni kwa jasiri. Kwamba ni kwa sababu hiyo tunapaki kusubiri kusikia wengine wanasemaje, tukosoe ama "tuedit".

    Kinachobaki hewani, na ndicho kilicho muhimu ni, tufanyeje kuondokana na woga ama hofu kama unavyopenda kuiita wewe? Tufanyeje ili tuweze kusema bila kujali kwamba tutaonekanaje kwa wanaotusikiliza?

    JibuFuta
  3. Nuru shaaban umesema kweli kabisa, sina la kuongeza.

    JibuFuta
  4. Njia pekee ya kuachana na hofu kwanza ni kujenga hali ya kujiamini. Na njia nzuri ya kujenga kujiamini ni kuwa na imani chanya au wengine husema positive thinking. Ukisha kuwa na mtazamo chanya hali ile ya hofu huwa inaondoka. Pili kuwa mkweli nayo husaidia sana hali ya hofu kuandoka. Kama haukitaki kitu au haukubaliani na kitu kwa mtizamo wako basi ni vizuri ukakisema wazi na ukamaanisha. Pia wengi wetu tumeingia katika hofu kwa sababu ya kutokuwa na maamuzi ambayo sio mazuri, tunapoamua jambo huwa hatupendi kujipa muda wa kulitafakari jambo hilo, ukiamua jambo lolote ukiwa uko kwenye furaha sana lazima utalikosea na baadaye kujutia maamuzi yako na kisha kuingia katika hofu au woga na vivyo hivyo ukiamua jambo ukiwa katika hali ya hasira matokeo ni hayo hayo Cha msingi ni kuamua mambo yte tukiwa katika hali ambazo ni za kawaida na zitztupa muda wa kuweza kuamua kwa kuujua ukweli ni upu. Kuliko kutoa maamuzi tukiwa kweny kuhemukwa.
    Watu wanapewa wali,fulana na kofia na wakati mwingine pesa siku moja kabla ya kupiga kula unategemea mtu huyo atakuwa na maamizi sahihi??
    Pia tuache kabisa tabia ya kujutia maamuzi yetu ambayo tumejafanya jambo hili nalo huwa linatuingiza sana kweny hofu na matokeo yake ni kuishi kwa hofu maisha yetu yote. Jambo kama umeliamua litekeleza kama likshindikana lirudie ukiona hauwezi achana nalo na ufikirie jambo jipya la kukupa moyo kuliko kufikiiria lile ambalo ulishinda kulifanya matokeo yake ni kuogopa kufanya hata mambo mengine kwa usahihi.
    Kwa jamii yetu watu wengi tumeathiliwa na haka ka ugonjwa ka hofu na mtu hayuko tayari kuanza kujiondoa katika tatizo hilo.
    Tuwaelimishe jamani kila tunapopata muda wa kukutana na watu hawa na wala tusichoke.

    JibuFuta
  5. Nuru, umesema kweli. Asante kwa mchango wako makini.

    Nina swali dogo: hofu haina faida? Je, ni katika mukhtadha upi inaweza kuhesabika kuwa sawa kukosa hofu?

    JibuFuta
  6. Kuzaa mawazo ni kazi kuliko kuzaa mtoto. Mnajua hilo?

    JibuFuta
  7. Ni kweli haina faida sana itakuweka katika maumivu yasiyokwisha na kukutia katika kujuta kwingi kila muda.
    Wakati tu utakapoweza kusimama wewe kama wewe bila ya kuwa na hofu ndio utakapo hesabika huna hofu.Au kwa lugha nyingine utakapo acha kuishi kwa mazoea au utakapo ondoa sauti za wazazi jamii na nyingine zilizopandikizwa kichwani mwako hapo tunasema utakuwa huna hofu.
    Alichosema Kulaba ni kweli kuzaa mawazo ni kaazi sana kuliko kuzaa mtoto.

    JibuFuta
  8. Wengine wana mawazo lakini hawayafanyii kazi. Hao vipi jamani? Ikitokea mtu kafanya anasema kama nilivyowaza?

    JibuFuta
  9. Kuwa na mawazo na kutokuyafanyia kazi ni uvivu. Uvivu huu utapeleka pabaya. Hatufanyi tunavyofikiri, ila tunaiga kwa wengine. Doreen umegonga.

    JibuFuta
  10. katika pita pita zangu mtandaoni, nimekutana na blog nyingi sana, mbaya na nzuri,kuhuzunisha,kuchekesha,na ninayo furaha sana kukutana na ya leo hii ya kuelimisha,kwa kweli mi ni mpenda saikology katika maisha yangu yote, napenda kujua mtu anawaza nin, mpaka mtoto je anawaza nin??sasa pia natoa pongezi sana kwa mmiliki wa blog hii na pia natoa taarifa kwamba nitakuwa nachangia sana mawazo yangu hapa na watanzania wenzangu duniani kote,kutokana na kupenda kwangu saikolojia najifunza mambo mengi sana katika maisha yangu,siwezi kuyataja yote ila nataka kuongezea kidogo point katika watoa maoni hapo juu,hususani dada nuru shaabani,kwanza kabisa namuunga mkono kwa yote aliyosema ila na mi nataka kuongezea tu,Hofu ina faida,hofu faida yake kubwa ni kimaadili, maadili ya mtanzania sio mabaya sana,pia katika hofu inaweza kupunguza ukimwi kwa kijana kuogopa kumtongoza binti,na pia hofu kwa wanafunzi ni nzuri sana kwa sababu inamuweka kwenye mazingira ya kusoma ili kuhofia kufeli,sasa pia cha kufahamu ni kwamba kwa nin tunapaswa kuwa na hofu na kwa nin hatupaswi kuwa nayo..kwa ujumla hofu ina madhara makubwa sana,watzanzania tumekuwa na uoga unaotupeleka pabaya sana,leo hii mtu anashindwa kujijua kabisa kama ana haki zinazomlinda,angalia tunashindwa kudai kuona hata katiba zetu na hali zetu kama mwananchi..angalia kwenye madaladala konda anapomuona trafki,hata kama hana kosa...naomba niishie hapo,kwa herini wadau wote,

    JibuFuta
  11. Nashukuru kutembelewa na watu wanaoacha maoni mazuri kama nivyi nyote. Karibuni sana, nawapenda wote.

    JibuFuta
  12. Nimekutana na blogu hii leo nimependa unayoandika kuelimisha. Kazi nzuri sana. Keep it up because it is up!

    Abdul

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?