Nilipozungumza na blogu ya Maneno Matamu: “Kiswahili ni alama ya Uafrika wangu.”
Yafuatayo ni mahojiano yangu na blogu ya Maneno Matamu kuhusu, pamoja na mambo mengine, suala la lugha za Kiafrika na nafasi ya blogu katika kukuza lugha hizo katika enzi hizi.
Ulianza kuandika blogu mwaka 2005. Uliamuaje kushiriki katika mtandao wa Internet namna hii?
Nakumbuka nikiwa mwanafunzi nilikuwa mfuatialiaji mzuri wa makala za mwandishi maarufu, Ndesanjo Macha (ambaye sasa ni Mhariri wa Global Voices eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara).
Yeye ni mwanablogu wa kwanza wa Kiswahili. Na kwa kweli niilivutiwa sana na aina yake ya uandishi, mijadala aliyokuwa akiiendesha kwenye blogu yake pamoja na matumizi mazuri ya lugha. Kwa hiyo hamasa ya kublogu ilitokana na blogu yake.
Blogu kwangu niliiona kama fursa nzuri na rahisi ya kujadili masuala ninayoyaelewa vizuri ya kiutambuzi na sayansi. Mule niliona ingekuwa rahisi kupata jukwaa la kubadilishana mawazo na watu bila kikwazo chochote na pia pasipo kulazimika kuonana nao.
Si tu ninaelimisha kama ninavyofikiri, lakini ninaelimishwa na wasomaji wangu. Jambo hili ni gumu kupitia magazeti na vyombo vingine vikuu vya habari. Kwa hiyo uhuru wa kusema ninachokifikiri ulikuwa ni hamasa muhimu ya kuanza kublogu mwaka 2005, nikiwa mwanafunzi.
Kwa sasa bado nafanya juhudi za kupangilia ratiba yangu vizuri ili niweze kublogu kwa ufanisi zaidi.
Unapenda kusema kwamba wewe ni mpenzi wa Kiswahili. Hii lugha, ina maana gani kwako?
Kiswahili ni lugha yangu. Naichukulia kama zawadi ya Mungu kwangu na jamii yangu. Nakiheshimu kama utambulisho wa utamaduni wangu.
Unajua tuna bahati mbaya sana sisi Waafrika hatujali vitu vyetu wenyewe. Kwangu mimi Kiswahili ni alama ya Uafrika wangu. Ni nyenzo ya kuwasilisha kwa urahisi sana mawazo yangu kwa jamii yangu. Ni kipimo cha uelewa wangu kwa maana kwamba kama siwezi kueleza dhana fulani kwa Kiswahili, basi najichukulia kama sijaielewa bado.
Kiswahili ni hifadhi ya elimu. Ni urithi. Na ndio maana mimi ni kati watu wanaoamini kwamba kati ya matatizo makubwa yanayoukabili mfumo wa elimu nchini mwangu [Tanzania] ni uamuzi wa kutumia lugha za kigeni kuwafundishia wanafunzi wetu.
Pamoja na mapungufu yake, bado Kiswahili kinaweza kusaidia sana kuongeza uelewa wa wanafunzi wetu kuanzia ngazi za chini mpaka Chuo Kikuu. Inawezekana isipokuwa tu kama sisi ni aina ya watu wasiopenda vya kwao tunaong’ang’ania vya watu ambao nao hatuna hakika kama wanapenda vyetu.
Je, unaongea lugha zingine, isipokuwa Kiswahili?
Ndio. Naongea Kinyaturu kwa ufasaha. Hii ni lugha ya mama yangu na amekuwa na jitihada za kuhakikisha tunawasiliana kwa lugha hii. Ni utambulisho wa jamii yetu ndogo ya wanyaturu, wenyeji wa eneo la katikati ya nchi. Nakiheshimu.
Vilevile naongea Kiingereza kwa kuwa tu najua kimetawala ustaarabu wa vitabu na mimi ni mpenzi mkubwa wa kusoma. Ila sikipendi na wala sijivunii nacho.
Kama mwanablogu, unaonaje kuhusu umuhimu wa kutumia lugha za kiafrika?
Mtandao wa intaneti umekuwa ni maktaba ya maarifa. Tukitumia Kiswahili tutakuwa tumesaidia kuhifadhi lugha yetu na kuipa nafasi ya kuwa nyenzo ya maarifa kwa jamii ya wasemao Kiswahili.
Ni muhimu sana sisi wenye fursa ya kutumia mtandao tukachangia maarifa haya mtandaoni kwa Kiswahili. Kufanya hivyo kutasaidia kuongeza matumizi ya teknolojia katika jamii zetu maana watu wetu hawatalazimika kujua lugha za kigeni ili kujifunza na kuhabarishwa mtandaoni.
Dunia inabadilika. Itakuwa ni aibu kwa lugha yetu yenye mamilioni ya wasemaji kukosa nafasi inayostahili mtandaoni na siku moja tukajikuta tumo kwenye kundi la lugha zinazopotea.
Kila mmoja wetu achangie. Na hii ndiyo sababu niliamua kushiriki mradi waSwahili Lingua. Ninajivunia kuchangia benki ya maarifa na habari mtandaoni kwa kutumia lugha yangu mwenyewe. Najua ninawarahisisha wasiojua lugha za kigeni kupata maarifa na habari hizo kwa lugha yao wenyewe.
Je, una ujumbe wa kutuma kwa wasomaji wetu?
Hakuna heshima kubwa kama kutambua asili yako. Natoa wito kwa sisi Waafrika kujielewa na kuthamini utamaduni wetu. Kati ya vielelezo vya kujielewa ni namna tunavyothamini na kukuza lugha zetu tulizozaliwa nazo.
Soma makala halisi kwenye blogu ya Maneno Matamu, au tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza Blogger Christian Bwaya: “Swahili is a sign of my africanness”
Maoni
Chapisha Maoni