Ni usalama wa Taifa au ni ubaguzi wa rangi?

Tuko ndani ya uwanja wa ndege wa Sao Paulo, Brazil. Ni usiku, tunangoja usafiri wa kwenda Dubai, kama lisaa limoja lijalo. Nimekamata kitabu changu nasoma. Ni kitabu cha rafiki yangu kanigawia nionje yaliyomo. Yeye naye kakaa zake kimya anasoma kitabu changu pia. Saa nyingine tunafunika vitabu, tunazungumza mawili matatu, tunaendelea kupekua pekua. Ni katika kuongoja tu usafiri.

Faizul, Deo, Bijoy, na mimi jijini Sao Paulo. Picha: Dr Awab

Mara wanatufuata watu wawili waliovaa kiraia.
Mmoja kajazia, kajichora tatuu mkononi, kavaa viatu vinavyompyaya. Mtu wa mazoezi. Mwingine mdogo dogo tu, ila shida yake hasemi kiingereza. Kwa hiyo ni "mpole fulani hivi".

Baunsa anatuonesha kitambulisho chake. Ni askari wa Kibrazil.
"Ninaomba kuona hati yako ya kusafiria tafadhali?"askari bonge ananiambia, mwenzie akimsaidia kwa macho. Nilisita kidogo, nikijiuliza inakuwaje aje kwangu wakati nilikuwa na wasafiri wengine. Ndicho nilichomwuliza. Baada ya kudai kuwa anafanya hivyo akilinda taifa lake, sikuona sababu ya kubishana. Najua dunia inatishwa siku hizi. Ugaidi, madawa ya kulevya na mambo kama hayo. Kwa hiyo nikawapatia hati yangu bila tabu.
Baada ya kuipekua, mmoja wao (aliyeonekana kujua jua kimombo, yule bonge) akaniuliza maswali kadhaa ambayo bila shaka lengo lake likiwa ni kujua nimekuwa Brazil kwa muda gani, kwa sababu gani, naondoka saa ngapi na bla blaa. Tuliwapatia ushirikiano wa kutosha. Basi wakanirudishia hati yangu na kuondoka.

Sie tukaendelea na hamsini zetu, kwa kujadili tukio hili. Mjadala wenyewe ukiwa ni iwapo tendo hili linazo chembe za ubaguzi wa rangi ndani yake.

Baada ya kama dakika kumi hivi, wale jamaa wakarudi tena tulikokuwa tumekaa, safari hii wakitokea kwenye sehemu ya ukaguzi (getini) ambako tungekaguliwa kama lisaa limoja lijalo.
"Mista, una mzigo wowote unaosafiri nao?" Jamaa niliyekuwa naye, akawaondolea uvivu. "Mbona mmerudi tena kama watu wenye mashaka na sisi? Tuambieni sababu…hali hii inaweza kutufanya tushindwe kukaa vizuri na abiria wenzetu…"

Jamaa wakadai wamekuwa wakitusoma na kwamba tunaonekana kupanga kitu wasichokijua. Na kwamba walipokuja tuliwatazama kwa macho yasiyoeleweka.

"Mnatufanyia hivi kwa sababu ya rangi zetu?" akahoji mwuungana mwenzangu huku akiweka kitabu kwenye kiti pembeni.
"Hapana. Ninafanya hivi kulinda nchi yangu" kakasirika kidogo, makunyanzi yanaonekana usoni mwake. Du kajazia, anatisha.
"Sasa kama ni kulinda nchi yako, kwa nini mmetufuata sisi moja kwa moja tena mara mbili na sio hawa wenzetu…nieleze?" Swahiba wangu kapandwa na hasira na yeye.
"…ninachofanya ni kazi yangu...kuilinda nchi yangu"
"Hebu twende huku…" amri yenye mfano wa ombi.

Haya. Mguu kwa mguu wa mkaguzi.
Wakaongea kilugha chao huku kompyuta ikisumbuliwa, kilugha tena, hati yangu inaendelea kutazamwa na wale jamaa "wanaolinda nchi yao". Yule dada anawajibu kilugha, sielewi, ila ni kama anawahihishia kwamba "huyu dogo ni dakika chache anaondoka zake"
"Nashukuru, hakuna tabu tena." askari akadai huku akinirudishia hati yangu.
"Tafadhali naomba kujua shida ni nini hasa?" nauliza nikiwa na hasira. Unajua saa nyingine si vizuri kuzungumza ukiwa na ghadhabu kama niliyokuwa nayo.
"Yameisha Mista…tafadhali endelea na shughuli zako"
Sioneshi kuridhika na majibu yake. Narudia swali lile lile. Shida hasa ilikuwa nini?
"Tulikuwa na wasiwasi na jina lako. Tulidhani ni la kike…na wewe mwenyewe ni mwanaume, kwa hiyo hatuk…." akajibu askari aliyejazia.

Basi bwana. Nikaona ya nini kubashana na watu bwana. Mie hapa naondoka saa moja ijayo nawaachia nchi yao.

Moyoni nikiwaza: Hivi huu ni usalama wa Taifa au ni ubaguzi wa rangi? Ni rangi ya ngozi yangu ndiyo inayoleta mashaka? Au ni "taratibu zetu za kulinda watu wetu"?

Hata hivyo, hiyo haikufanya nihitimishe hoja ya ubaguzi wa rangi. Labda wewe msomaji utanisaidia kulijua hili kama umewahi kuishi Brazil na hasa hasa Sao Paulo. Hii ndiyo Brazil.

Maoni

  1. Kaka kwanza niseme pole kwa usumbufu huo.

    Lakini pia nadhani umepata nafasi ya kuwafahamu watu wa upande mwingine wapoje. Suala la ubaguzi tumewahi kulijadili sana. Lakini ubaguzi ni ubaguzi tu.

    JibuFuta
  2. Pole sana kwa yaliyokusibu..

    JibuFuta
  3. Pole Mkuu! Sijawahi kufika Sao ila navyofahamu pamoja nakuwa wanawatu weusi ubaguzi upo Brazil.

    Freddy Macha angeweza kusaidia kwa hili kwakuwa kawahi kukaa hapo mtaani.

    JibuFuta
  4. tena ukiendelea kubishana au ukionyesha hasira ndio wanahakikisha kuwa una njama. ukiwa umevaa hii jezi nyeusi halafu unaonekana kijana inaweza kuwa tabu.

    JibuFuta
  5. Pole mwayego....wanasema msafiri kafiri

    JibuFuta
  6. Mambo mengine yanachangiwa zaidi na historia. sina uhakika kama ndio huo tunaita ubaguzi wa rangi. KWA MFANO HATA NYUMBANI AKIPITA KIJANA ALIYEVAA KIAJABU AJABU(nadhani unanielewa) KATIKA MITAA YENU, LAZIMA UTAANZA KUJIULIZA USALAMA WA VITU VYAKO. Kwa sababu tu vibaka wengi wanavaa na kuonekana katika muonekano huo.

    Biashara ya kusafirisha madawa ya kulevya Brazili ni maarufu sana. na waafrika wengi wanatumika kusafirisha. INAWEZEKANA PIA IMECHANGIA KWA KUWASHUKU NA SI WATU WENGINE

    Ni sawa na US, matokeo mengi ya ualifu yanafanywa na Blacks. ndio maana polisi wanakuwa na mashaka zaidi na blacks kuliko wazungu. Najua ubaguzi upo. Ila si mara zote wanapofanya kazi nio yao ni ubaguzi moja kwa moja

    JibuFuta
  7. @ Fadhy, Maistara na Faustine asanteni sana

    @ Mtakatifu, asante kwa dondoo ya Fredy, ndo nimekumbuka kuwa huku palikiwa kwake miaka fulani. Anaweza kuwa anajua zaidi

    @ Anony na Mengji, itabidi tuanze kubadili mitizamo ya hawa jamaa. Isionekane ukiwa mweusi basi lazima uwe suspected

    JibuFuta
  8. Pole sana.Mlikuwa mnaonekana kupanga vitu wasivyovijua?Mngekuwa mmefuga madevu msingondoka hapo.

    JibuFuta
  9. Edigio umenichekesha. Karibu sana baada ya kimya cha muda mrefu.

    JibuFuta
  10. Kaka Bwaya pole sana. Mie ninamtizamo tofauti nafikiri ni watu wanalinda nchi yao na siyo ubaguzi wa rangi .Kazi yao ndivyo ilivyo inahusisha kukagua na kuuliza maswali.Tutaendelea kukutana na matukio haya safarini muhimu ni kukumbuka kuwa dunia imebadilika umdhaniaye siye ndiye.Kwa ufupi si ubaguzi ila kazi yao ndiyo inavyofanyika na ni kwa usalama wa wasafiri.

    JibuFuta
  11. Brazili elite wengi ni watu Weupe ambao wametokana na Walowezi Weupe na wana damu ya kibaguzi sana watu weusi bado hata leo Brazil wanabaguliwa, NA NI KITU KAMA KIMEJENGEKA MAMBO YOTE YA KIHUNI HUFANYWA NA WEUSI TOKA WIZI, UJAMBAZI NA MADAWA YA KULEVYA, NA WANAFANYA HIVYO KUTOKANA NA KUKOSA NAFASI KATIKA JAMII

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging