Ubabe wa dini wa kuhodhi maarifa isiyonayo

Dini kama msamiati, inaeleweka. Lakini tafsiri rasmi naweza kusema ni vigumu kuipata maana inategemeana mara nyingi na matakwa, maoni, makusudi ya huyo anayetafuta maana.

Wapo wanaotafsiri dini kwa kuhusisha na dhana ya Mungu kama msingi mkuu wa dini. Wengine wanatafsiri dini kwa kuihusisha na masuala ya ‘kiroho’ yaani spirituality, hisia na imani. Wengine wanaposikia dini mawazo yao yanakimbilia kwenye ‘vyama vya ushabiki wa kiroho’ yaani makanisa, misikiti, mahekalu na vitu kama hivyo.

Inachekesha kwamba neno tunalolitumia mara zote, eti linatusumbua kulitafsiri. Sababu ni kwamba tafsiri sahihi yapaswa kuwa ile itakayotuwezesha kuzikusanya ‘dini’ mbalimbali kwa pamoja. Mkusanyiko huu hauwezi kufanywa kwa matumizi ya tafsiri ya dini fulani tu.

Kwa maana hiyo, tunaweza kuzikusanya dini zote kwa kusema kwamba ni jumla ya imani zinazohusiana na vile tusivyoviona kwa macho, zinazojaribu kuleta majibu juu ya mikanganyiko ya maisha ili kuleta namna fulani ya matumaini ama ridhiko la mwanadamu. Kwa hiyo kwa kusema hivyo dini ni namna mwanadamu anavyo anavyojishughulisha na mahitaji yake yasiyoonekana.

Ieleweke kwamba mifumo rasmi ya imani (hapa namaanisha beliefs) yenye lengo la kumfanya mwanadamu aabudu, atukuze ama ajitoe kwa kile kinachoonekana kuwa chenye nguvu na uwezo usiopimika, ni kipengele tu cha dini na kamwe si maana ya moja kwa moja ya dini.

Ni kweli kwamba dini mara nyingi imeeleweka kama aina fulani ya taasisi, labda kwa sababu dini nyingi zimejikuza kuwa taasisi, lakini si kweli kwamba dini ni taasisi. Wala si kweli kwamba unapozungumzia dini basi moja kwa moja unazungumzia uhusiano wa mtu na Mungu. Maana hii hailipi kwa mikhutadha fulani fulani nitakayoibainisha huko mbele ya safari.

Dini kuu za dunia hii, ambazo nyingi zimejitengeneza kuwa taasisi kubwa kubwa, zimekuwa kinyume kabisa na sayansi. Ugomvi huu kati ya dini na sayansi umekuwepo tangu siku nyingi na kwa kweli ni wa kijinga. Baadaye nitajaribu kuurejea ugomvi wa suala la asili ya uhai na viumbe ambapo hapo pia tutaona namna ugomvi huu unavyoendekezwa kwa sababu za kimaslahi zaidi.

Hebu kwa sasa nikupe mifano midogo midogo.

William Harvey aligundua uwepo kwa moyo katika mwili wa binadamu baada ya utafiti wa muda mrefu. Kabla yake, dunia haikuwa na habari kama kuna kitu kinachofanana na moyo kinachosukuma damu ili kusambaza hewa ya oksijeni.

Harvey akaandika kitabu kuonyesha dunia maajabu ambayo hapo awali yalikuwa ndoto. Cha kusikitisha, sijui ni ulevi wa kuhodhi maarifa ama ni nini, viongozi wa dini moja kuu duniani, aliagiza Harvey atundikwe msalabani pamoja na kitabu chake kifuani mwake! Harvey akadhalilishwa akisemekana kuleta upotofu ulio kinyume na "imani". Akauawa kwa amri ya dini ili na maarifa yake yaoze nae kaburini.

Leo hii kila mwanadamu mwenye akili timamu hawezi kupuuza alichokifanya Harvey. Maarifa yaiyomgharimu heshima na maisha yake, leo ndiyo ufahamu rasmi wa kila mwenye "dini".

Msomaji atakumbuka kilichompata Galileo. Kwa kutumia periskopu alijionea duniara ya dunia. Alichokiona kilikuwa tofauti na kilichokuwa kinaonwa na ulimwengu wote unaobaki. Galileo aliuawa kwa kudaiwa kuleta maarifa yaliyo kinyume na neno la Mungu. Kosa lake lilikuwa kuona kile ambacho dunia haikioni.

Mifano ni mingi sana. Yote ikionyesha namna woga wa kijinga wa dini ulivyokuwa unaisababishia kiwewe cha kupambana na maarifa ambayo kimsingi hayakuwa na athari yoyote na maudhui ya kidini.


Labda msomaji anaweza kujisemea "lakini hizo zilikuwa ni enzi zile bwana." Jibu langu ni hapana. Dini haijawahi kubadilisha staili ya woga wake. Ilivyokuwa miaka hiyo ndivyo ilivyo leo hii. Kwa mfano hivi sasa kuna suala la kondomu ambalo ni uthibitisho wa imani zilisizo na matendo. Dini kuu ulimwenguni (ambazo angalau zinathubutu kusema misimamo yao hadharani) zinakataza "mashabiki wake" kutumia kondomu, iwe kujikinga na magonjwa ya zinaa wala kwa shughuli nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na kupanga uzazi.

Msimamo huu ni wa ajabu kwa sababu, kisayansi kondomu imethibitika kunusuru kwa maisha ya mzinzi kwa asilimia fulani. Ni kweli si asilimia mia moja, lakini angalau imethibitika kusaidia kwa asilimia fulani zinazozidi hamsini. Maana yake, angalau inapunguza tatizo kwa kiasi fulani miongoni mwa waasherati.

Hoja inayotumiwa na dini ni kwamba eti kondomu haisaidiii kumlinda mtumiaji kwa asilimia mia! Watu hawa wanasahau kwamba hata unapokula huwezi kuwa na uhakika wa kushiba kwa asilimia mia moja. Watu hawa wanaona bora kufanya ngono zembe uwe na uhakika wa kuambukizwa kuliko kukingwa kwa asilimia kadhaa! Yaani kwao, bora mzinzi afe kuliko kuokolewa japo kwa vijiasilimia hivyo. Hii haiwezi kuwa akili ya kawaida kwa mtu anayeamini katika kutunza uhai wa binadamu mwenzie.

Watu hawa wanasema, ukisema tumia kondomu maana yake, unahimiza ngono. Haya tukubali hata kama ni hoja iliyo upenuni mwa upuuzi. Lakini ajabu ni kwamba watu hawa hawa hata kwenye ndoa ambapo wenzi wanataka kupanga uzazi, eti kondomu ni marufuku! Yaani kuzuia muunganiko wa yai la mama na mbegu za baba ni kitu kisichokubalika? Kuamua idadi ya watoto unaotaka kuwa nao ni dhambi? Kwa aya ipi? Eti enendeni mkaijaze dunia! Kuijaza dunia maana yake mayai yote ya mama ni lazima yarutubishwe kuwa mtoto? Mayai yaidi ya 400?

Kama mkristo anaweza kumwaga mbegu zake nje ili zisirutubishe yai la mama, kwa nini basi asizimwagie tu kwenye kondomu (kitu kile kile)? Hapo utaambiwa dhambi!

Hizi ni juhudi za wazi za dini kujifanya inahodhi maarifa yote na mwishowe huishiaga na machozi. Hakuna ulazima wowote wa dini kutaka saa zote kupambana na sayansi, mpambano ambao mara zote huishia kwa sayansi kuja kukubalika baadae.

Kwamba sayansi ambayo ni maarifa yanayotokana na bashiri za kimantiki zinazoibua ushahidi wa kuthibisha bashiri hizo, haiwezi kuwa na ugomvi wa kudumu na dini ambayo tafsiri yake ndiyo tuliyoanza nayo hapo juu. Tafadhali irejee, unipe maoni yako.

Itaendelea…

Maoni

  1. Mada iliyotafitiwa kwa kina na kuandikwa kwa ustadi wa hali ya juu.
    Bwaya, kipaji kikubwa ulicho nacho ni ufundi wa mpangilio wa makala zako.
    Pamoja sana.

    JibuFuta
  2. Kama alivyosema Fadhy. Big up Bwaya

    JibuFuta
  3. Nimeisoma nimeielewa. Umeandika katika lugha nzuri na mpangilio mzuri. Ila linapofika swala la Imani, ninakuwa mzito sana kuchangia. ILA NIAMINI DINI INAKUWA NA INABADILIKA. Mahubiri niliyokuwa nayasikia nikiwa mtoto ni tofauti kabisa na ninayosikia sasa hivi. WALOKOLE NILIOWAONA MIAKA YA 90 NI TOFAUTI NA WA SASA. Mahubiri ya MOTO hautayasikia tena kwenye makanisa zaidi ya RC.
    Soon makanisa yote yata support matumizi ya condom na mambo mengine mengi yatakayoendana na mazingira ya wakati huo...

    JibuFuta
  4. Duh!!
    No comment. Nadhani wewe na walionitangulia wamenena

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?