Aprili: Utasoma vitabu vingapi?
Mkesha wa kuukaribisha mwezi mpya ndio huu. Kesho tutauanza mwezi mpya kwa siku iitwayo 'ya wajinga'. Masuala ya kuangazia kidogo: Ni kwa kiasi gani umepoteza muda mwingi pasi na sababu ya msingi? Soga. Stori zisizojenga. Kuwakatisha tamaa watu. Mabishano. Na kadhalika. Na kadhalika. Umesafiri kilomita ngapi mwezi huu? Hebu fikiria, kama ungeamua kuzitumia kilomita hizo kusoma, ungesoma vitabu vingapi? Kwa mwezi Machi, umeweza kusoma vitabu vingapi? Ni fedha kiasi gani umetumia kununua vitabu? Utasema hela hazitoshi. Hivi unajua ni shi'ngapi umeteketeza kwa kukwangulia vocha mwezi huu? Umekwangua vocha kusaidia kusambaza 'text messages' za mizaha! Umeona ulivyo na fedha? Haya. Hima na tuanze kuzitumia hizo hizo vitabuni mwezi huu! Na tusome. Mwezi Aprili uwe ni wa kusoma.