Je, Kazi yako Inakuza au Inadumaza Wito Wako?
Inawezekana
unafanya kazi ambayo hukuwahi kufikiri kama siku moja ungeifanya. Labda
unadhani hukuchagua vizuri kipi cha kufanya, au pengine mazingira
yalikulazimisha kushika kilichokuwa kinapatikana.
Kwa upande
mwingine, inawezekana pamoja na kuipenda kazi yako, unahisi kuna namna fulani
ya udumavu. Hupati fursa za kupanda ngazi kiutendaji na umeanza kujihisi unapoteza
wito wako.
Vyovyote iwavyo, bado
kuna tumaini. Unaweza kabisa kufanya kazi unayojua fika haiendani na wewe,
lakini hatua kwa hatua, ikakutengenezea jukwaa zuri la kuumba vizuri wito wako.
Hapa ninakuletea
uzoefu utakaokusaidia kujitathmini na pengine kuchukua hatua muhimu katika kuchochea
ule uwezo wa pekee ambao Mungu ameuhifadhi ndani yako.
Unafanya kazi yenye staha?
Mratibu wa
Ukuuzaji wa Ujuzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Dar es Salaam, Bw. Albert
William Okal anaeleza namna gani mazingira yako ya kazi yanavyoweza kukuza wito
wako:
“Hakuna kitu kama
uchaguzi mbaya wa kazi. Kila kazi unayofanya inaweza kuwa sahihi kwako ikiwa tu
mazingira yake yanawezesha kukuza ujuzi. Ukiweza kujifunza namna nzuri ya
kufanya kazi yako, ukagundua aina ya majukumu unayoyafanya kwa ufanisi zaidi,
unaweza kabisa kuigeuza kazi usiyoipenda kuwa na tija badala ya kukimbilia
kubadilisha kazi (tafsiri ni yangu.)”
Okal anafafanua,
“Tukichukulia wito kama uwezo wa kukuza ujuzi na uzoefu wa kazi, maana yake lazima
tufanye kazi kwenye mazingira yanayotufanya tupate utoshelevu."
"Nafikiri mtu
anayefanya kazi inayompa uhuru wa kutumia maarifa na ujuzi wake; kuheshimiwa na
kutambuliwa kwa juhudi anazoweza kazini; nafasi ya kujifunza na kujiongeza,
mazingira yanayompa nafasi ya kufanya makosa na kumruhusu kujifunza kupitia
makosa hayo, uwepo wa ujuzi stahiki kwa ajili ya kazi hiyo; hayo yote kwa
pamoja yanaweza kuwa fursa ya mtu kuboresha wito wake.”
Uzoefu wa Bw.
Okal unatufunza mambo mawili makubwa. Kwanza, hata kama unafanya kazi
unayoamini haikuwahi kuwa chaguo lako, huna sababu ya kukata tamaa. Kazi yako
ya sasa inaweza kuwa daraja la kukuza ujuzi wako na kukufikisha kule unakotaka
kwenda.
Hilo, hata hivyo,
linategemea ubora wa mazingira ya kazi. Mbali na juhudi zako binafsi, mwajiri
naye ana wajibu wa kukupa ushirikiano na msaada wenye lengo la kukuwekea
mazingira bora ya kazi.
Ndio kusema kazi
yoyote inayokupa uhuru wa kubuni mambo mapya, kujifunza na kutumia ujuzi mpya,
inaweza kukusaidia kuendelea kujitambua na hivyo kuufikia wito wako.
Unajifunza ujuzi mpya?
Wakati mwingine
unaweza kukata tamaa kwa sababu wenzako wanabadilisha kazi mara kwa mara na
wewe umeendelea na kazi hiyo hiyo kwa muda mrefu. Je,hiyo inaweza kuwa na maana
ya udumavu kazini?
Albert William Okal ana
mawazo tofauti: “Aina ya majukumu unayofanya sambamba na nafasi unayopata ya
kujifunza na kukuandaa kwa majukumu makubwa zaidi inaweza kuwa sehemu ya kukua
kazini. Mwalimu, kwa mfano, anaweza kuendelea kuwa mwalimu lakini majukumu yake
yakawa yanabadilika kadri anavyojifunza ujuzi mpya. Kutoka kuwa mwalimu asiye
na majukumu, anaweza kuwa Mkuu wa Shule, Mkaguzi wa Shule au Afisa Elimu. Huyu
huwezi kusema amedumaa kikazi.”
“Lakini pili, ni
muhimu ufanyaji kazi nao uboreshwe. Unaweza kufanya kazi hiyo hiyo lakini ukajifunza
ujuzi mpya wa namna ya kutekeleza majukumu yako. Hapo huwezi kusema kazi yako
imekudumaza. Mfano mfanyakazi aliyekuwa anasambaza mizigo kwa mguu, anapofikia
hatua sasa anatumia baiskeli au pikipiki kufanya majukumu yale yale, hiyo pia
ni ishara ya ukuaji. Kigezo cha tatu, kwa maoni yangu ni tija ya kipato. Kazi
inayokukuza lazima iende sambamba na ongezeko la kipato.”
Ndio kusema, kwa
mujibu wa Bw. Okal, unapokuwa kwenye mazingira ambayo namna yako ya kufanya
kazi haibadiliki, muda unaenda unatumia njia zile zile kufikia malengo yale
yale, tafsiri yake inaweza kuwa udumavu kazini.
Unatumia
vipawa vyako?
Kwa upande wake, Lonyamali Morwo Mkurugenzi Mtendaji wa
MultiSkills Business Consultancy ya Arusha, anafikiri kazi inayokukuza lazima
ikuwezeshe kutumia vipawa vyako:
“Kila mtu amezaliwa na kipaji fulani. Sote kwa namna moja au
nyingine kuna kitu tumeitiwa kukifanya. Swali kubwa tunalohitaji
kulijibu ni ikiwa tunafanya kazi kufuatana na vipawa vyetu au basi tu tumelazimishwa
na mazingira tunayojikuta nayo kazini?” anauliza na kuendelea, “Ukitaka
kufanikiwa katika maisha ni lazima kutambua kipawa chako. Haijalishi unafanya
kazi ya kuajiriwa au umejiajiri, suala la muhimu ni je, unapenda unachokifanya?”
Bw. Morwo anaamini
maswali matatu yanaweza kutusaidia kujitathmini. Anasema: “Ni muhimu kujihoji.
Je, ninachokifanya ndicho nilichoitiwa kufanya? Je, ninachokifanya ndicho
ninachokipenda? Je, kinachokusukuma ndani yako ni nini, kipawa ulichonacho au
wajibu uliopewa na mwajiri?” Kinyume na hapo kazi unayofanya inaweza kuwa inadumaza
wito wako.
Ushauri
Lonyamali Morwo anashauri, “Lenga kujenga kipawa chako kupitia kazi
unayofanya. Fanya kitu unachokipenda na chenye msukumo wa kutoka ndani ya nafsi
yako. Ukifanya kitu kisichotoka ndani yako utafanya kwa uzito kumridhisha
aliyekuamuru ukifanye na hiyo itakuwa ni kutimiza wajibu.”
Kwa upande wake, Albert William Okal anasema huna sababu ya
kuhama hama kazi kukuza uwezo wako: “Jipe muda kukaa kazini ulete tofauti
inayoonekana hata kama hupati kipato kikubwa. Epuka kuacha kazi ndani ya muda
mfupi kwa kisingizio cha kutafuta maslahi zaidi. Kwa namna hiyo utakuwa
unajijenga kiuwezo na ufanisi wako utaongezeka (tafsiri ni yangu).”
Tunajifunza thamani ya uzoefu na ujuzi kazini. Kadri
unavyopata ujuzi mpya kazini ndivyo unavyojitambua vizuri zaidi. Ukijitambua na
kujituma, kazi yoyote unayoifanya sasa ina nafasi ya kukujenga kwa maana ya
kukujaza uwezo mpya utakaokusaidia kuufikia wito wako.
Maoni
Chapisha Maoni