Kwa Nini Wanawake Wenye Mafanikio Wanaogopwa?
UPO ukweli kuwa wanaume wengi
wanawaogopa wanawake wenye mafanikio. Hawa ni wanawake wenye kiwango kikubwa
cha elimu, fedha, umaarufu au hata madaraka katika jamii. Hoja ya wanaume wenye
mawazo haya ni ugumu wa kuwaongoza wanawake wanaowazidi kama alivyonieleza Godfrey,
mwalimu wa sekondari jijini Arusha:
“Mwanawake akipata kitu anakuwa
jeuri sana. Hawezi kukusikiliza tena na atataka awe huru kufanya mambo yake
bila kuingiliwa.” Kwa mujibu wa Godfrey, uwezo wa kifedha na mafanikio kwenye
maeneo mengine ya maisha mara nyingi humfanya mwanamke asiwe na utayari wa kuwa
chini ya utawala wa mwanaume. “Huwezi kuishi na mwanamke anayejiona yuko juu
yako na ukabaki salama. Hatokuwa tayari kukupa nafasi ya kuwa na sauti kwenye
nyumba.”
Hitaji kubwa la wanaume wengi
ni mamlaka. Wanaume wanapoingia kwenye uhusiano na mwanamke wanakuwa na shauku
ya kuwa na sauti inayosikika bayana kukidhi dhana ya kichwa cha familia. Ili
sauti hii iweze kusikika bara bara uwezo wa kifedha, kielimu, kimadaraka na
hata umaarufu unakuwa na nafasi yake.
Kwa maana hiyo inapotokea mwanamke
ameshindwa kuwa chini ya mamlaka yake, mwanaume huanza kujisikia hayuko salama
kama anavyoeleza Dickson, karani wa benki mjini Moshi:
“Niliwahi kuwa na dada mmoja
mwenye Masters wakati huo mimi nafanya shughuli zangu ndogo ndogo za
kiujasiriamali na elimu yangu ya Diploma. Kaka nilikoma kuringa. Mule ndani
tulikuwa na bunge lisiloisha. Kila ninachosema, bi mkubwa lazima apinge. Masters
ikawa inashindana na Diploma sikuweza kuvumilia.”
Inavyoonekana kuna ukweli kuwa mwanamke
anapokuwa na mafanikio anakuwa na nguvu saidi. Hii si kwa wanawake pekee. Hata
wanaume nao wanapofanikiwa wanakuwa na nguvu zaidi katika jamii. Hadhi yao
katika jamii inaongezeka na wanasikika zaidi kuliko watu wasio na mafanikio.
Lakini je, kwa nini mwanaume
atishwe na sauti ya mwanamke? Je, haiwezekani mwanamke awe na sauti sawa na
mwanaume na mambo yakaenda? Silas anajibu, “Lazima mwanamke awe chini ya
mwanamke. Iko hivyo tangu kuumbwa kwa dunia. Ukijaribu kupora mamlaka ya
mwanaume umepora uanaume wake.”
Kwa upande mwingine tatizo linaweza
lisiwe mafanikio ya mwanamke bali kutokujiamini kwa wanaume kama anavyoeleza
Irene: “Wanaume wengi hawajiamini. Wanajitutumua tu kwa mabavu na ukali lakini
wamejaa wasiwasi. Kwa nini utishwe na mafanikio ya mwanamke kama unajiamini?”
anauliza Irene ambaye ni mhasibu wa shirika la moja la umma na kuendelea, “Kwa
nini utake kuwa juu ya mwanamke? Kwani ukiwa sawa na mwanamke unakosa uanaume
wako? Haya ni mawazo yaliyopitwa na wakati.”
Kwa mujibu wa Irene, si wakati
wote tatizo linakuwa ni mwanamke mwenye mafanikio. Wakati mwingine hizi huwa ni
hisia tu ambazo zikiaminiwa hugeuka kuwa kweli. Inavyoonekana wanaume wengi
wana nafsi zilizo na umaskini wa hadhi na hivyo wanatumia mahusiano yao na
wanawake kushibisha njaa waliyonayo.
“Umewahi kujiuliza kwa nini
wanaume wengi wanapenda kuoa wanawake wanaowazidi? Maprofesa wengi wanaoa darasa
la saba. Mtu kusoma kote anaishia kuoa housegirl. Unafikiri ni kwa nini?”
aliniuliza Balibate. Hoja yake ni kuwa wanaume huvutiwa na wanawake dhaifu ili
waweze kuwatawala kwa urahisi.
“Mwanaume wa kawaida yuko radhi
aoe mwanamke asiye na mbele wala nyuma tena bila kipato chochote ili iwe rahisi
kumtawala. Nafikiri suala hili limekaa kimazoea zaidi kuliko kimaumbile. Tumelelewa
tukiaminishwa uanaume ni jinsia bora zaidi kuliko kuwa mwanamke.”
Kama anavyoeleza Balibate, wanaume
wengi huficha udhaifu wao kwa kuvutiwa na wanawake dhaifu. Jitihada za kujihami
na fedheha ya kuonekana yeye ni mtu asiye na mamlaka humfanya aogope kuwa na
mwanamke anayeweza kumzidi.
Tunachoweza kujifunza ni kuwa
kuna ukweli kiasi fulani kuwa shida ipo. Wanawake wenye mafanikio huwa ni tishio
kwa baadhi ya wanaume. Ipo haja kwa wanawake kuchukua hatua za kuondoa tishio
hili. Wanawake wasiogope kufanya wajibu wao kama wanawake kwa kutambua mahitaji
ya kisaikolojia ya wanaume. Mwanamke waepuke kutumia mafanikio yao kushindana
na wanaume.
Lakini pia wanaume, kwa upande
mwingine, wanahitaji kujitambua na kuelewa kuwa hawawezi kuwa imara zaidi kwa
kutumia mbinu za kizamani. Siku hizi wanawake wengi wanakwenda shule. Nafasi
yao kufanikiwa imekuwa kubwa sawa na wanaume. Wanaume wakubali kuwa wanawake
nao wanaweza kuwa na mafanikio. Mawazo kuwa uimara wa wanaume utegemee udhaifu
wa wanawake yamepitwa na wakati. Muhimu ni wote, mwanaume na mwanamke
kujitambua na kutambua wajibu wao.
Maoni
Chapisha Maoni