Mbinu za Kukabiliana na Sonona, Hofu Mahali pa Kazi
Tuchukulie unafanya kazi muhimu
inayotakiwa ndani ya masaa mawili yajayo. Wakati ukikimbizana kumalizia kazi
hiyo, umeme unakatika. Ofisi haina jenerata na huwezi kutumia kompyuta bila
umeme. Unajawa na wasiwasi lakini huna cha kufanya.
Unaangalia saa yako, dakika
zinayoyoma. Mara simu inaita. Mkubwa
wako wa idara anaulizia kazi. Anakujulisha uharaka wa kazi hiyo kwani kikao cha
wakurugenzi kinakaribia kuanza. Kijasho chembamba kinakutoka kwa mbali. Unakosa
amani lakini huoni unaweza kufanya nini. Hali kama hii inaitwa msongo wa mawazo
(stress.)
Dalili za sonona
Mara nyingi msongo wa mawazo ni
hali ya kupita inayochangiwa na msongamano wa majukumu, mahusiano mabovu kazini
na wakati mwingine changamoto za maisha nje ya kazi.
Hata hivyo, mazingira yanayozaa msongo
wa mawazo yakiendelea kuwepo kwa muda mrefu, huleta hali ya kukata tamaa na
maisha inayofahamika kama sonona (depression). Mtu mwenye sonona hujisikia
hatia, huzuni, hasira na kisirani na hivyo ni mwepesi kukwazwa na mambo
yanayoonekana kuwa madogo.
Mara nyingi hujiona hana thamani
kama watu wengine na hupoteza tumaini kwa sababu wakati mwingine huwa haoni
dalili ya mipango yake kufanikiwa. Usiku hapati usingizi shauri ya
mawazo mengi na hivyo huwa mchovu kazini, mvivu, huweza kusinzia na anaweza kusikia
maumivu ya mwili.
Tafiti nyingi zinaonesha kuwa
karibu nusu ya wafanyakazi duniani kote wameathiriwa na sonona inayoathiri
utendaji wao wa kazi, mahusiano yao na wakubwa wa kazi pamoja na wafanyakazi
wengine.
Vyanzo vya sonona
Kuna mambo mengi yanaweza
kuchangia sonona. Mosi, mazingira mabaya ya kazi. Unapofanya kazi kwenye
mazingira ambayo huna uhakika mambo yatakuwaje kesho, huna hakika sababu gani
itatumiwa na mwajiri wako kukuondoa kazini, uwezekano ni mkubwa unaweza
kujikuta na sonona.
Fikiria wafanyakazi wenzako
wanafukuzwa kazi hovyo bila kufuata utaratibu. Hali kama hii inaweza kuleta
tahayaruki kwa wafanyakazi wanaobaki na wakajikuta wakikabiliwa na sonona.
Pili, mahusiano mabaya na watu
kwenye eneo la kazi. Kutokuelewana na mwajiri wako, migogoro na wafanyakazi
wenzako, hayo yote yanaweza kukufanya ukawa na sonona.
Lakini pia, inaweza kuwa maisha
nje ya kazi. Hapa kuna migogoro ya ndoa, matukio mabaya katika familia, hali
mbaya ya uchumi, kuondokewa na wapendwa wetu, haya yote yanaweza kuchangia
sonona.
Aidha, maandalizi hafifu ya
maisha baada ya kustaafu yanaweza kuchangia hali ya sonona. Mfanyakazi anapoona
anakaribia kustaafu na akang’amua kuwa hajajiandaa kikamilifu na maisha mengine
nje ya mfumo wa ajira anaweza kujikuta akikata tamaa na maisha.
Vyovyote iwavyo, unapokuwa na
sonona usichukulie jambo hilo kwa wepesi. Mbali na kuathiri utendaji wako wa
kazi na hata kuhatarisha ajira yako, sonona inaweza kugharimu afya yako ya
mwili na akili. Mbinu zifuatazo zinapendekezwa kisaikolojia kukabiliana na
sonona.
Ongea na mnasihi
Kama tulivyoona, vyanzo vya
sonona ni maisha ya kawaida ambayo si ajabu kumpata mtu yeyote. Inashauriwa
waajiri kuwa na huduma ya unasihi kwa ajili ya wafanyakazi wao kila
inapohitajika. Hata kama huduma hiyo haipatikani kazini kwako, usiache kutafuta
msaada kwingineko.
Mnasihi atakusaidia kubaini
vyanzo vya tatizo ambao mara nyingi ni vigumu kuvibaini ukiwa tayari na sonona.
Inawezekana ikawa ni mtindo wako wa maisha nje ya kazi; mahusiano ya kifamilia;
kutokujiandaa mapema na mambo muhimu yanayohitaji fedha au pengine ni mtazamo
wako mbaya.
Ukiwasiliana na mnasihi mapema, kwa
pamoja, mnaweza kusaidiana kutengeneza utaratibu wa kukabiliana na mzizi wa
tatizo.
Ongea na mwajiri wako
Sonona inaathiri maisha yako ya
kazi. Kama tulivyotangulia kuona kwa ufupi, wakati mwingine unapokuwa na sonona
unaweza ukashindwa kufanya kazi kwa ufanisi. Usipojieleza mapema, hiyo inaweza
kuwa sababu inayoweza kutumika kukuondoa kazini.
Inashauriwa kuongea na mkubwa
wako wa kazi. Kama kwa mfano, umepewa kazi ya kushughukilia jukumu nyeti
linalohitaji uzingativu, pengine unahitaji kuwa mkweli kwamba unahitaji msaada.
Maneno yanayofanana na haya yanaweza kusaidia: “Ningependa kufanya kazi hii kwa
umakini, lakini najisikia kuzidiwa. Naomba kama kuna uwezekano nipate msaada wa
wenzangu zaidi,” au “Hali yangu ya kiafya si nzuri. Ninahitaji kupata msaada.”
Lonyamali
Morwo, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiSkills Business Consultancy ya Arusha
anafikiri tabia za waajiri zinaweza kuwa
sehemu ya ufumbuzi: “Nashauri mwajiri asiwe na tabia ya kuwachokoza na
kuwagombeza wafanyakazi. Utaratibu wa kufanya vikao vya mara kwa mara unasaidia
wafanyakazi kuongea na kutoa dukuduku na kero zao katika utendaji wa kazi.”
Jitengenezee mfumo kinga
Mtindo mzuri wa maisha unaweza kukusaidia
kukabiliana na sonona kabla hali haijawa mbaya. Mbali na kufanya mazoezi, kula
vizuri, kulala kwa wakati, ni vizuri kuwa na ratiba ya kupumzika.
Tafuta mahali palipotulia ukiwa peke
yako utazame vitu vinavyokupa amani na utulivu wa nafsi. Tangu nimeanza
utaratibu huu nimeona faida yake. Nenda ufukweni bila kazi isipokuwa kutazama mawimbi
ya bahari au kuona jua likizama; soma vitabu vinavyokupa matumaini; sikiliza
muziki mwororo. Pia kulingana na uwezo, unaweza kwenda mahali ukatazame madhari
ya kupendeza. Tabia kama hizi zinasaidia kupata utulivu wa nafsi.
Ikiwa unajisikia uchungu na wasiwasi,
wakati mwingine inashauriwa kupata muda wa kulia kupunguza msongo wa hisia
ndani yako. Usijizuie kuonesha hisia unapopita nyakati zinazokatisha tamaa.
Lakini pia ni vizuri kujenga
urafiki wa karibu na watu unaowaamini unaoweza kuwashirikisha mambo yako
binafsi. Unapojisikia kukata tamaa unahitaji kuwa na watu unaoweza kuzungumza
nao hata kama hawawezi kukusaidia mawazo. Mahusiano mazuri na familia yako ni moja
wapo ya kinga dhidi ya sonona.
Maoni
Chapisha Maoni