PICHA: Shutterstock Katika makala yaliyopita tuliona mbinu tatu unazoweza kuzitumia kuelewa mambo unayojifunza. Kwanza, ni ‘njaa’ inayokusukuma kuelewa. Unapokuwa na ari ya kuelewa jambo, mara nyingi, utahamasika kulielewa bila kutumia nguvu nyingi. Pili, tuliona ni muhimu kutengeneza picha kubwa ya jambo unalojifunza kabla hujaanza kujifunza undani wa mambo madogo madogo ndani ya picha hiyo. Kwa mfano, unaposoma aina za vyakula, lazima kwanza uelewe vyakula. Uelewa wa jumla wa vyakula utakurahisishia kazi ya kuchanganua aina zake kwa sababu tayari unayo rejea utakayoitumia kuelewa zaidi. Mbinu ya tatu ni kukihusisha kitu unachokisoma na mambo unayoyafahamu tayari. Unaposoma aina za vyakula, kwa mfano, lazima uwe unafikiria vyakula mbalimbali unavyovifahamu katika mazingira yako. Unapojaribu kuhusianisha kile unachokisoma na maisha yako ya kila siku, unaurahisishia ubongo wako kazi ya kupokea kuliko kuingiza kitu kipya kisichohusiana kwa vyovyote vile na kile