Ujumbe wa wiki hii

NAANDIKA makala hii kwa moyo wa upendo, mtu unayempenda ni lazima umwambie ukweli. Ukimficha ukweli unakuwa humpendi; ni kweli ukweli unauma na mara nyingi hatupendi kabisa kusikia ukweli; hata hivyo hakuna wa kutengua kwamba msema kweli ni mpenzi wa Mungu.

Kwa vile Mungu hatukutani naye uso kwa uso, bali tunakutana naye kupitia kwa binadamu wenzetu; ni haki kusema kwamba msema kweli ni mpenzi wa watu?

Naandika kutoa ushauri na hasa maoni yangu ambayo ni ya nia njema kwa taifa letu la Tanzania.


(Picha ya Kijiji cha Mjengwa)
Hii ni aina ya barua ya wazi kwa wale wanaotamani kuendelea kutawala wakati miaka ya kustaafu inakaribia. Labda kuna haja ya kuongeza miaka hii ya kustaafu. Miaka sitini ya sasa watu wanakuwa bado wana nguvu na kutaka kuendelea kutumika au kula “utamu” wa uongozi.

Kwa vile sasa hivi umri huu haujasogezwa mbele, kuna haja kuwakumbusha ndugu zetu ambao bado wana “Ambition” ya kutaka kuendelea na mbio hizi za hata kukalia viti muhimu kama urais na uspika, kwamba nyuma yao kuna vijana wengi, wenye mtizamo wa kisasa wa kuiona Tanzania ndani ya Afrika, ndani ya Afrika ya Mashariki na ndani ya dunia nzima ya leo inayojibatiza kijiji kimoja.

Kaulimbiu ya CCM ya Ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, si ya kubahatisha. Ina maana yake; ni bahati mbaya kwamba wale wanaoiimba, wanafanya hivyo kama Kasuku, lakini wangetumia muda wao kutafakari wangetambua kwamba sasa ni wakati wa kizazi chetu kustaafu na kuwachia njia vijana wanaokuja kwa kasi ya kutisha.

Hakuna haja ya kusubiri kusukumwa kama walivyosukumwa baadhi ya wazee na kuangukia pua kwa aibu kubwa. Mtu mwenye hekima anapisha njia mapema, ili heshima yake ibaki pale pale na kubaki na nafasi iliyotukuka ya kushauri na kuelekeza.

Hakuna haja ya kusubiri kuzomewa na kugomewa hadi kufikia hatua ya kukulazimisha kujitoa. Hakuna haja ya kusubiri kufanyiwa maandamano na vikao vya kukujadili kama unafaa au hapana. Ni kweli kwamba Watanzania ni wasahaulifu; wengine hawakumbuki yaliyotendeka jana.

Lakini si kweli kwamba wote ni wasahaulifu; wachache hao wanatosha kuchochea moto kiasi cha kukufanya kujuta ni kwa nini hukujikalia kimya na kufanya mambo yako.

Vidonda bado ni vibichi, hata watoto wadogo bado wanaimba Richmond na wengine kwenda mbali na kuibatiza Rich Monduli. Atakaye kuambia hili limesahaulika, atakuwa hakupendi.

Kwa vile umekubalika kwa mzee wa kimila, tosheka! Washauri na kuwaelekeza ndugu zako huko na kuingia kwenye mtandao wa wazee mashuhuri ndani ya taifa letu.

Nakubali kabisa kwamba tulifurahi pamoja, tukadhalilishwa, tukaonewa na kusikitika pamoja, sasa tusonge mbele: Ushindi ni wetu! Sina matatizo na hili. Na kama ushindi wenyewe unalenga kumhudumia Mtanzania na kumsaidia kupiga hatua kuelekea maendeleo;

Kama hautakuwa ushindi wa kujilipiza kisasi, kuchota rasilimali kiasi cha kutosha na kuwatajirisha marafiki, ndugu na jamaa. Labda mimi ningesema hivi: Tulifurahi pamoja, tukadhalilishwa, tukaonewa na kusikitika pamoja, sasa tupumzike!

Tusifikiri kwamba bila sisi hakuna kitakachofanyika. Tutoke kwenye ndoto na malengo haya ya kutaka kufika tulikolenga miaka mingi bila ya mafanikio. Sote tuna malengo, lakini si yote yanafanikiwa.

Hata hivyo tunamshukuru Mungu, na kutosheka pale tulipo! Hata wale waliostaafu na kupumzika wana mchango mkubwa katika kuliendesha taifa letu la Tanzania. Si lazima mtu uwe rais, waziri, waziri mkuu au spika wa Bunge, ndio utoe mchango wa maana.

Binafsi ningeifanya kauli mbiu hii mpya iwe hivi:Tulifurahi pamoja, tulisikitika pamoja na sasa tusonge mbele hadi ushindi, na kuishi ya maisha ya hekima, busara na ushauri zaidi ya kuwa kauli mbiu ya siasa za kiwendawazimu.

Siasa zisizo soma alama za nyakati na kukubali mabadiliko yaliyosukwa na Vision, historia na bidii ya kufanya mabadiliko hayo; siasa za ili liende, heshima na utukufu na kuendelea kuutukuza umasikini kana kwamba sisi tuliumbwa tumelaaniwa.

Kaulimbiu mpya inahitaji watu wapya, mazingira mapya na ‘vision' mpya inayochimbuka ndani ya historia ya Taifa letu; historia inayokusuta pale unapotaka kujichanganya kuendeleza ndoto zako zisizo tekelezeka.

Labda hapa kuna ulazima kusisitiza nililolitaja hapo juu kwamba tusifikiri kwamba bila sisi hakuna kitakachofanyika. Kuna hatari ya kuwa na kiburi hicho cha kibinadamu. Mimi nina mfano hai wa maisha yangu.

Kati ya mwaka 1985 hadi 1998 kule Bushangaro, Karagwe, tulijaribu kuunda Jumuiya ya Mkamilishano. Tulifanya kazi kwa karibu sana na marehemu Askofu Christopher Mwoleka.

Mimi na baadhi ya mapadri waliounga mkono mradi huu wa kujenga jumuiya ya watu wanaoishi pamoja kama familia, tulifikiri bila sisi jumuiya hiyo haiwezi kusonga mbele. Tulikataa kwenda kusoma zaidi masomo ya Theolojia, ili kujipatia digrii ya uzamivu.

Kila wakati tuliogopa kuondoka tukifikiri tukitoka kila kitu kita kufa. Pamoja na malengo yetu hayo yaliyokuwa yamejawa na kiburi cha kibinadamu, Jumuiya hiyo ilikua mbele ya macho yetu, tukiwa hatuna uwezo wa kuitetea, baada ya Askofu mpya kuja na sera zake za namna ya kufanya mambo.

Kiburi chetu kikayayeyuka na kutambua kwamba bila sisi mambo mengine mengi yanaweza kuendelea kama yanavyoendelea hata sasa bila sisi kuwepo.

Siwezi kusema hatukufanya kazi. Tulifanya kazi ya kufa na kupona. Tulibatizwa jina la wachapa kazi. Ukweli ni kwamba wakati ulifika wa kutuweka pembeni na wengine wakaendelea.

Inawezekana hawafanyi vizuri kama ambavyo tungelipenda sisi kufanya, lakini maisha yanaendelea.

Wanasema yule anayetamani Uongozi, anakuwa anatamani kitu bora. Uongozi kwa maana ya uongozi ni kuwa mtumwa wa wengine, ni kuwa mtumishi wa watumishi. Hivyo anayetamani kuwa hivyo, anakuwa amechangua fungu lililo bora.

Lakini pia ni muhimu kwamba wale unaotaka au kutamani kuwaongoza wakukubali na kukupenda vinginevyo, itakutesa wewe na kuwatesa wale unaotamani kuwaongoza.


Na Padre Karugendo, Tanzania Daima Jumapili tarehe 3/10/2010

Maoni

  1. Celebritynudes [url=http://hotnudcelebs.blogspot.com/2010/08/garth-grows-her-own-vegetables.html] naked pics[/url] Naked celebrity

    JibuFuta
  2. Greetings folks, I am fresh right here and I'd like to say hi there to you. I'm truly savoring looking at what you might be talking over on this community forum. I have found many strategies which made it easier for me personally quite definitely.
    -------------------------------------
    [url=http://bernardapilkey.fotopages.com/?entry=2126419][color=#000000]radio music[/color][/url]

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?