Tuzo kwa wataalamu je?

TUMEKUWA tukishuhudia, si mara moja, vyombo vya habari vikitangaza 'tuzo' za kuwaenzi wasanii wetu. Ni habari njema kwamba utolewaji huo wa tuzo hushabikiwa mno na hadhira ya Watanzania kiasi cha kuweza kuyashawishi makapuni makubwa makubwa kudhamini tuzo hizo kifedha. Hilo ni jambo jema.

Laiti kasi hii hii tunayoiona katika usanii ingesambaa kwenye maeneo mengine.

Hivi ingekuwaje kama tungeamua kuwaenzi na watu wengine walioweza kuonyesha juhudi za kufanya tafiti muhimu za kitaaluma?

Ingekuwaje kama serikali ingekuwa na, kwa mfano, siku maalumu ya kuwapa tuzo wasomi waliobobea ama wataalamu walioweza kuleta changamoto muhimu kwenye jamii?

Ingekuwaje kama makampuni makubwa makubwa haya haya tunayoyaona kwenye 'usanii' nayo yangeamua kushabikia wanazuoni?

Tungekuwa na kwa mfano, tuzo ya mtafiti bora wa mwaka; ama daktari bora wa mwaka; ama mwanasayansi bora wa mwaka; ama mwalimu bora wa mwaka; ama mwandishi bora wa vitabu wa mwaka; na kadhalika na kadhalika. Si ingekuwa poa?

Kufanya hivyo si tu kwamba ingewapa moyo watu hao ambao mchango wao muhimu haujulikani kwa sisi tunaoitwa watu wa kawaida (tuliowengi); bali pia ungeihamasisha jamii kuthamini mchango wa wataalam pia! Ingewafanya wanafunzi kuuona ufahari katika taaluma hizo kama wanavyouona katika 'usanii' na 'siasa'.

Kusema hivyo haimaanishi kwamba napingana na wanaowapa wasanii tuzo. Hata kidogo. Na wafanye. Ila ninachotaka kusema ni kwamba tunaweza kufika mahali tukawa na tuzo hata za mwanasiasa bora wa mwaka, wakati hatufanyi hivyo kwa maeneo mengine ambayo umuhimu wake hauonekani kuthaminiwa sana.

Nadhani umenielewa.

Maoni

  1. Kaka Bwaya,

    Naona kama wazo hili limechelewa....
    Ni kweli kabisa nadhani huu ni wakati muafaka wazo hili kufanyiwa kazi.
    Hivi ni nani mwenye namba ya simu ya Dr. Slaa tumtwangie huko Bungeni kama akiliwasilisha hili wazo linaweza kupata baraka za Wabunge wetu.......

    Naomba kuwasilisha...

    JibuFuta
  2. Moe Ibrahim(tajiri mwenye pesa kweli kweli) anayechagua Raisi bora kila mwaka hapa barani Afrika na kumpa dola nyingi tu mpaka kufa kwake.

    Huwa najiuliza,
    ingekuwaje kama angewekeza pesa hii kwenye elimu? Kwa nini aitoe kwa watu ambao hawatakaa wahjue shida hata kama asingewapa?

    Kwa nini asisaidie yatima barani Afrika?
    Kwa nini asiwekeze kwenye vitengo vya utafiti?
    Kwa nini asiwe na utaratibu wa kutoa tuzo kwa mwalimu, daktari, watafiti, wabunifu n.k bora wa mwaka hata wa kila mwezi?

    Pengine wale wanaotoa tuzo hizi wanategemea kwa upande mwingine kufaidika.

    JibuFuta
  3. Ni wazo nzuri na mimi naona bado alijachelewa. Kwanza tujiulize hizo tuzo kama za wasanii bora wa mwaka zinatolewa na nani? Nani ni mwanzilishi wa tuzo hizo? Na fedha anazitoa wapi kufanya hivyo? Utagundua kuwa ni mtu mmoja alipata wazo kama lako. Akaliweka sawa katika maandishi na kutafuta wadhamini wa tuzo hizo. KAMA UMEPATA WAZO HILI UNAWEZA KULIFANYIA KAZI, KISHA UKAPIGA HODI TBL, ZAIN NA MAKAMPUNI MENGINE UKAFANIKISHA.

    JibuFuta
  4. Kisima amesema kweli. Tuzo hizi huwa hata hazina lengo la kumnufaisha mpewaji. Lengo ni mtoaji na faida (soma biashara) zake. Ndio maana Mo Ibrahim anawapa matajiri (maraisi) fedha wasizozihitaji kwa kazi ambayo kimsingi ni kiini macho.

    Ndio maana mashirika ya pombe yanawatumia wasanii kutangaza pombe zao kwa sababu watanzania wanapenda wepesi wepesi na usanii una wateja wengi.

    Nchi za kibongo zina safari ndefu kuliko tunavyofikiri.

    Heko Kisima.

    JibuFuta
  5. Kama huyo Mo ni mfanyabiashara na "anagawa" pesa, basi yawezekana wanaoamini hivyo hawajui tafsiri ya biashara na pia siri ya mafanikio yake. Tuzo za wataalamu zinastahili kuwepo lakini kwa kuwa wenye kuzitoa ni wenye nia, uhitaji, ulafi na uroho wa umaarufu na faida ya "kesho" hawaoni haja ya kuwekeza kuliko na umuhimu wa kudumu ilhali matunda yake yataonekana miaka michache ijayo. Wengi wao wako kwenye biashara zainazodumu kwa muda mfupi na ndio maana kwao ni UMAARUFU kuliko UHALISIA wa tuzo hizo.
    Amani kwenu

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?