Rafiki yangu wa ujanani...

Nasikitika mwezi huu umekuwa mzurimbaya. Kwanza nilivinjari miji kadhaa hapa nchini nikakutana na watu wa namna mbalimbali. Hiyo ilikuwa nzuri sana kwangu kwa mwezi huu. Hata hivyo, uzuri huo ukasababisha ubaya mwingine. Sikuweza kuwa mwandikaji mzuri.

Hayo mawili. La tatu zuribaya, ni hili. Mara nyingine nimekuwa nikifuatilia mijadala mbalimbali kupitia simu ya kiganjani. Imenisaidia mara nyingi hasa nikiwa barabarani.

Bahati nzuri juzi nikiwa kwenye usafiri wa daladala kuna 'tukio la mzunguko wa kiuchumi' lilitokea, simu yangu niliyoipenda sana, ikawa imependwa zaidi na mtumiaji mwingine nisiyemfahamu. Bila shaka inamsaidia huko alipo japo hakuniarifu wakati anaichukua, lakini inavyoonekana aliihitaji kuliko mimi. Akaondoka na majina ya watu wangu kwenye simu yangu ambao nsingependa kuwapoteza.


Bahati nzuri wakati nakaribia kabisa kuipoteza simu hiyo, nilikuwa nimetoka tu kuwasiliana na rafiki yangu wa ujanani niliyepotezana naye kwa miaka kadhaa. Nilisoma naye madarasa ya upili, akinisaidia sana kusoma masomo ya Kiswahili na Historia (ambayo hata hivyo sikuweza kuendelea nayo).

Kwa hiyo baada ya kupotezana kwa miaka hiyo, bila kujua nani yuko wapi na anafanya nini, hatimaye akaweza kuwasiliana nami tena masaa machache kabla ya kuipoteza simu yangu kupitia kwa rafiki yangu mwingine niliyenaye hewani. Ni furaha iliyoje. Mwaihojo nashukuru sana.

Funzo muhimu. Si tabia nzuri kuachana na marafiki. Si tabia nzuri kudelete majina ya watu uliowahi kuchukua namba zao hata kama unadhani hawatakusaidia. Huwezi jua.

Huyu huyu unayemwona kama 'hasara' leo, anaweza kuja kufanyika 'faida' huko mbeleni. Tumepewa kujua ya leo, ya kesho ni ya mwenyewe.

Usipoteze marafiki wa zamani.

Maoni

  1. Kaka Bwaya kwanza pole kwa kupotelewa na simu yako uliyoipenda. la pili umeniwahi nami nilitaka kuandika hii habari nilipokuwa nyumbani nilikutana na rafiki yangu wa ujanani pia tulisoma shule moja darasa moja tulipoteana na kila mmoja alikuwa akimtafuta mwenzake. Ni kweli hizi simu mara nyingine zina faida. La tatu rafiki ni bora kuliko mwana sesele. Ni hayo tu

    JibuFuta
  2. Mwanasesele? yasinta una makuzi!

    Bwaya pole sana masaibu yaliyokukumba. Pili pongezi kwa kukutana/kuongea na rafiki zako 'wazee' (si ndio kiswahili cha 'old friends', au?). Kukutana na rafiki wa zamani kunakukumbusha mambo mengi ya zamani mabaya na mazuri, tena kwa haraka pengine kwa kasi ifuatayo kasi ya mwanga. Kingine kinachoweza kumkumbusha mtu zamani ni muziki. Muziki ni balaa katika kutanabaisha mambo ya awali. Pengine baadhi yenu mmewahi kutoa mchozi wa furaha, hata huzuni, msikiapo wimbo fulani uliopigwa miaka ilee ulipokuwa sehemu fulani na akina fulani mkifanya jambo/mambo fulani.

    Bwaya jaribu kuweka rekodi (ya dansi ama injili jinsi upendavyo) iliyotamba mkiwa na huyo rafiki mzee. utaona dunia inarudi nyuma. Kumbe wakati ukuta.

    Sasa naingia kwenye hili la simu. nashukuru tokea teknolojia hii ya simu itukumbe sijawahi kuibiwa/kupoteza simu. Lakini nimeshajiandaa kupoteza simu tayari (tena hii niliyonayo sasa naombea iibwe hata leo). Nimejiandaa hasa kwa hofu ya kupoteza namba na ndugu na marafiki 'wazee' kama Bwaya.

    Simu nyingi za siku hizi zina sehemu mbili za kuhifadhi majina na namba. moja ni kwenye chip ama simcard na nyingine ni kwenye simu yenyewe. hivyo unaweza kuona majina yanatokea mawili-mawili. Ukitoa chip yamabaki moja-moja. Nilichofanya mimi ni kutafuta simcard nyingine mpya (hajaleta sheria bado ya kujiandikisha ununuapo simcard) au ya zamani na kuirekodi majina yoote yaliyomo kweny simu yenyewe pindi nikiitoa simcard niitumiayo. ukiitoa hii simcard usiyoitumia mara kwa mara (kama flopy disk hivi)unaiweka sehemu nzuuri ambako hata nondo hawafiki. kazi ni kuiupdate mara kwa mara upatapo namba mpya. siku simu ikipendwa na wengine kuliko unavyoipenda wewe (Bwaya una makuzi na wewe!) aaah we wakachukua kale kasimcard na kukapachika kwenye simu nyingine kwa raha zako.

    Hapo vipi?

    JibuFuta
  3. Da! Hapa shwari, kaka Mwaipopo hiyo ni solusheni nzuri saaana! Nami nitaufanyia kazi ushauri huu haraka iwezekanavyo kwani hawa wanaozipenda hizi cm hawabishi hodi, wanajitokeza kama kifo vile.


    Pole sana kaka Bwaya kwa kupotewa na cm, na hongera pia kukutana na rafikiyo wa ujanani japo ni kwa njia ya cm.

    JibuFuta
  4. mie siinglii haya ya mwanasesele maana naona kuna makwinyanzi usoni kwangu

    JibuFuta
  5. Mwaipopo,

    Imebidi nikumbuke nyuma kuona muziki gani tulikuwa tunaupenda na huyu rafiki yangu, basi imekuwa poa sana.

    Kuhusu simu, asante kwa ushauri. Laiti ningelitambua hilo mapema pengine nisingekuwa naomboleza kupoteza namba za marafiki zangu wakongwe.

    Tatizo ni kwamba sikuwahi kuamini kwamba kuna siku kama hii ingetokea.

    Asante sana kwa ushauri mzuri.

    @Yasinta Mpangala na Kisima nashukuruni kwa kuniandikia.

    JibuFuta
  6. Duh!!! Unajua mara zote unapopata tatizo unaweza kulifanya ufanyavyo. Unaweza kulifanya likawa chanzo cha tatizo, ama kuamua kuwa sehemu ya suluhisho. Kwa hili naona inasakwa suluhisho.
    Nawashukuru nyote kwa ushauri. Kaka Bwaya. Kwanza kumbuka kuwa wakati huyo kaipenda simu yako, kuna wanaopenda maisha ya watu. Kwa hiyo tunashukuru kuwa kilichopendwa charejesheka. Lakini pia tujue kuwa aliyeipenda hiyo simu "atapendeka" kwa namna moja ama nyingine. Ama ataona anafanikiwa na ataendelea kuzipenda mpaka apendwe yeye na vyombo vya sheria, ama sheria za mikonon zitachukua mkondo wake.
    Usiwe na shaka. Namba utazipata kama ulivyozipata kabla hujawa nayo. Na nakutakia kila lililo jema

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging