Utangulizi wa hoja: Tumetokea wapi?

Kujielewa ninakokuzungumzia, kunahusisha na uelewa wa mambo kadhaa yanayoaminika kuongoza maisha ya viumbe katika ulimwengu ( pamoja na dunia) tunamoishi. Kwamba sisi binadamu tulitokea wapi na tunatafuta nini hapa duniani. Huko ni kujielewa.

Ulimwengu na viumbe vilitokea wapi? Swali kama hili si rahisi sana, pamoja na umuhimu wake katika kujielewa.

Yapo mawazo mengi yanayojaribu kutafuta uhalali wa fikra kadha wa kadha kuhusu chanzo hasa cha ulimwengu wenyewe pamoja na uhai na maisha ya viumbe hai na visivyo hai katika ulimwengu huu.

Mawazo haya yanaweza kuganywa katika makundi makubwa mawili: Wanaoamini zaidi pasipo ushahidi, na wanaojaribu kutumia akili zao katika kutafuta ushahidi wa mambo haya. Wale wa kwanza, kwa wingi wa idadi, ni wanadini. Wale wa pili, ni wanasayansi.

Mwanadini, anatafuta kujenga imani zaidi hata kama haielezeki. Mwanasayansi anatafuta ushahidi unaoelezeka.

Katikati ya hao wawili, wapo wengine ambao kazi yao ni kuhoji uhalali wa mahitimisho yanayowekwa na wenzao hao, kwa kujenga hoja. Hoja dhidi ya imani na pia hoja dhidi ya sayansi kwa lengo la kupata mtitiriko wa kimantiki utakaowawezesha kufanya uamuzi wa wapi pa kuegemea. Katika kufanya hivi, husababisha wawili hao ( dini na sayansi) kutafuta njia bora zaidi ya kuboresha nadharia zao.

Watu wa dini (hapa nikimaanisha imani) wanaamini kuwa kila kilichopo ( vinavyofahamika na vitakavyofahamika) chanzo chake ni Mungu. Mungu ni nani, majibu yanatofautiana kati yao kulingana na imani walizonazo. Wanasayansi wengi mpaka sasa wanajaribu kutupa mwangaza ( ama kutuingiza gizani zaidi?) kuhusu matumizi ya akili zetu ili kubaini yalikotokea haya yote tuliyoyataja awali.

Tutakachotaka kukifanya, ni kuangalia wapi ni wapi katika kujua yupi yu sahihi kati ya pande hizi mbili.

Niliahidi kumjadili Charles Darwin, na ndicho nitakachokifanya, baada ya kuanza na mtazamo jumla wa hawa wanaitwa wanasayansi ili tuelewane vyema. Kazi hii itafanyika ( hata kama ni kwa mwendo wa kinyonga) alimuradi agenda ikamilike.

Swali la kwanza: Mwanasayansi ni nani? Bila shaka anafanya sayansi: Je, sayansi ni nini? Hapo ndiko tutakakoanzia wakati wowote kuanzia sasa.

Karibu tujadiliane, tutofautiane, tuelewane, tujielewe.

Maoni

  1. Tuko nawe!Tunasubiri zaidi uendeleze kutupa chakula cha ubongo....

    JibuFuta
  2. Simon,

    Hii inaweza kuwa sumu ya ubongo vile vile.

    Asante sana kwa ushirikiano wako mkubwa.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Heri ya mwezi mpya!